UMEKOSA AJIRA NA HAUNA MTAJI?: FANYA HAYA 7 UBADILI MAISHA YAKO

Makala hii inalenga kuibua tafakari ya namna bora ya kutafuta ajira na kuanzisha shughuli binafsi za kijasiriamali. Ingawa ni kweli kuwa kuhitimu ngazi fulani fulani za elimu ni jambo la msingi katika kupata ajira au kuwa na shughuli imara za kijasiriamali, wengi wamejikuta ngazi zao za elimu haziwasaidii kukabiliana na changamoto za ajira na ujasiriamali.

1. Boresha uwezo wako wa ufasaha wa lugha : Lugha ndio msingi mkuu wa mawasiliano. Jikite vema katika Kiswahili fasaha, na kiingereza kinachofuata kanuni sahihi katika kuongea na kuandika. Haijalishi una kiwango gani cha elimu, fanya bidii kuboresha uwezo wako wa kuandika vema na kuongea. Tumia hata internet kutafuta namna bora za kuboresha uwezo wako wa kuongea na kuandika kwani ‘broken’ english haitokufikisha popote, na Kiswahili kisichofuata kanuni hakitokufanya watu wakuchulie ‘serious’ katika maamuzi yao ya kufanya kazi nawe, iwe kibiashara au kiajira.

2. Jikite katika ujuzi fulani: Kama unataka kuitegemea elimu yako kuzalisha huduma au bidhaa fulani, ni lazima basi uwe kweli na ujuzi wa uhakika katika jambo fulani, na  sio tuu kuwa na cheti. Tafakari kwa umakini katika vyeti ulivyo navyo, ni mambo gani haswa unaweza kuyafanya kwa ufasaha, jikite katika hayo, ili kuwa na ujuzi imara utakaokupa heshima na kukubalika mbele ya wateja wako watarajiwa. Zaidi sana kumbuka, unaweza kujifunza ujuzi mpya usiokuwepo katika vyeti vyako.

3. Jitangaze : Kupitia mtandao wako, kupitia mikutano mbalimbali unayohudhuria iwe ya kifamilia, kidini, marafiki au vikundi vingine, hakikisha watu wanatambua uwepo wako , na kuwa wanajua kuwa unao ujuzi fulani. Zaidi sana sio tuu wajue unao ujuzi fulani, bali wajue pia kazi ulizokwisha fanya kupitia ujuzi fulani ulio nao. Watambue pia kuwa upo unapatikana kama utahitajika kwa ajira au kibiashara. Mitandao kama Facebook, inaweza pia kutumika kujieleza uwezo wako.

4. Jenga mtandao wa watu mbalimbali: Kuwa karibu na watu mbalimbali ili uweze kujifunza mengi toka kwao, na pia watu hao wanaweza kuwa wa msaada mkubwa kwako kama wateja wako, au wasambaji wa bidhaa fulani unazohitaji. Pia watu katika mtandao wako wanaweza kukusaidia kupata mtaji wa kuanzia ujasiriamali wako. Hata hivyo kumbuka, watu wamsingi katika kujenga nao mtandao wanahitaji kukutambua wewe kama mtu muhimu kwao pia, hivyo jiweke kama mtu muhimu kwa kuonyesha uadilifu, ujuzi wako, na heshima kwa wengine. Soma zaidi jinsi ya kujenga mtandao imara bofya hapa

5. Kuwa mbunifu: Tambua kuwa kinachowafanya watu kununua bidhaa fulani ni kwakuwa wanaamini bidhaa hiyo itakidhi hitaji lao. Hivyo basi tumia muda wako kuangalia matatizo au changamoto katika jamii na jinsi unavyoweza kuleta suluhu za changamoto hizo. Sio lazima uzalishe bidhaa mpya kabisa, hata kusaidia kuleta huduma adimu sehemu fulani, kusaidia kuboresha utendaji kazi wa watu kwa huduma za kiakili unazoweza kutoa kama ushauri, ni moja ya ubunifu unaoweza kufanya. Kumbuka ubunifu si jambo la haraka, unahitaji muda kusoma mazingira, fani na watu, kisha utafakari namna unavyoweza kutumia ufahamu wako wa mazingira, ujuzi mbalimnbali, na tabia za watu, ili kuleta huduma au bidhaa itakayohitajika na watu.

6. Fikra sahihi:  Kila mmoja wetu ana njia ya kipekee ya kufikia mafanikio yake maishani. Ingawaje ni kweli kuwa ajira na biashara zinatuingizia kipato cha kujikwamua kimaisha, hakuna kanuni moja ya namna gani utaingia katika ajira au biashara ili ufanikiwe kama fulani. Hivyo basi , usijilinganishe na watu wengine, kubali kuwa maisha yako ni ya kipekee, fikiria hali uliyo nayo kuwa ni ya kipekee na inahitaji suluhu ya kipekee. Hivyo tafuta njia yako ya kipekee ya kujiajiri kwa kuangalia hobbies zako, mtandao wako,  ujuzi wako n.k. Pengine hata kutokupata kwako kazi ni kwa sababu unawaza kupata ajira kama fulani na fulani walivyopata, au unawaza aina fulani ya kazi ndiyo ‘itakayokutoa’ kimaisha. Kumbuka kuna baadhi ya watu wana degree mbili na hawana kazi nzuri zaidi ya watu wenye degree moja, na kuna watu waliishia darasa la saba tuu, ila wana kipato kizuri na maisha bora.

7. Ota kwa usahihi na ujiamini: Hata kama unahisi hali yako kimaisha sio nzuri, bado unahitaji kuweka picha kubwa ya maisha yaliyo bora hapo baadae. Kuota sahihi ni kufikiria kwa umakini nini hasa unapenda kufanya, nini hasa unatamani yawe mafanikio yako, na zaidi sana kuota huku kunakuwezesha kujiona kabisa umefikia hali husika unayoitamani kwani unaamini na kujiamini kuwa zipo njia za kufikia huko. Kuota na kujiamini ni muhimu kwani ndiko sikuzote kutakako kusukuma kuendelea na unachofanya hata kama unapitia magumu, ndio wahenga walisema “palipo na nia, pana njia”.  Ukiota vema na ukajiamini, hautokaa tuu bure bure, ukilalamika ajira ngumu, au hauna mtaji, badala yake utatafuta mbinu za ziada, na kuwa mbunifu kwakuwa unakitu kinachokusuma kukifikia katika maisha yako, na hasa ndoto hiyo ikiwa inajumuisha kuleta mabadiliko katika maisha sio tuu, mabadiliko kwa maisha yako peke yako, bali kwa jamii pia.
Share:

5 comments: