JINSI YA KUJENGA MITANDAO MIZITO

Katika dunia tunayoishi sio ajabu kukuta mzee wa miaka 60 akimuamkia kijana wa miaka 26, “ shikamoo bosi” au kukuta mtu mzima wa miaka 55 akibebeshwa mkoba na bosi wake wa miaka 30 ! Ndio ilivyo, dunia yetu tuliyopo thamani au nguvu ya mtu inapimwa kwa kuangalia mtu huyo ni ‘nani’ katika jamii au eneo husika. Hivyo, kabla haujaomba mtu akuingize katika ‘mtandao’ fulani, jiulize wewe ni ‘nani’ hasa au hao waliopo katika mtandao watakutafsiri wewe kama nani.

Hata kama utaweza kutumia nafasi ya mtu mwingine kuingia katika mtandao, bado hautoweza ku enjoy mtandao husika, na utajiona mgeni kila siku, hivyo basi, kuna haja ya kutambua jinsi ya kujijengea mtandao wako mzito, kwani kama inavyosemwa na wengi "hapa uniani hapa kuna mambo mengi yanayoweza kukusaidia kupata utakacho, lakini zaidi ya yote ni ‘ Wewe unamfahamu nani’, nani hasa wapo kwenye mtandao wako.
Ili kujenga mtandao wako imara ni muhimu kufahamu tabia za jumla za watu. Zifuatazo ni pointi chache muhimu  ambazo hautakiwi kuzisahau kuhusu tabia za watu:-

Watu hufuata palipo na mafanikio: Kwa kawaida watu wengi hupendelea kujihusisha na watu au asasi zilizofanikiwa kuliko zile ambazo hazijafanikiwa, au ndio zipo kwenye maandalizi ya ‘kutoka’. Ndio maana timu za soka kwa mfano zinaposhinda mashabiki hufurahia na kujitokeza kwa wingi kuwalaki wachezaji, lakini timu hiyo hiyo inapofungwa na kuendelea kufungwa, mashabiki hawajitokezi hata kwenye mechi tuu, na wengine huamia timu nyingine hata kama kuhamia huko ni ‘kwa mkopo’. Pia jifunze kwa wasanii, wanapokuwa wachanga, hakuna watu wengi wanaojitokeza kama mashabiki wao, ila wasanaii wanapokuja kuvuma, basi unakuta ‘mashabiki hawatoshi’, ndio maana si ajabu Lady Gaga ana fans wa Facebook zaidi ya milioni 55. 
Hivyo, usiwe na ndoto za mchana za kujenga mtandao mkubwa wa watu wa kukunufaisha kama wewe mwenyewe hauonekani machoni mwa watu hao kuwa ‘mtu wa mafanikio’. 
Mafanikio yako sio lazima yawe kama ya timu ya soka, au wasanii, bali inaweza kuwa ni aina ya kazi uliyonayo, aina ya kampuni au asasi unayofanya kazi, cheo chako ulichonacho, familia utokayo, aina ya watu unaojuana nao,  nchi unayoishi, au hata mkoa unaoishi, eneo katika mji unaoishi, n.k.  Ni muhimu watu wafahamu jinsi wewe ulivyo mtu wa mafanikio ili waweze kukubali katika kuunda mtandao wao. Ndio maana kuna msemo usemao “Mwenye vingi ataongezewa, na mwenye vichache hata vichache hivyo atanyang’anywa”.

Watu hufuata wanapoamini:  Haitoshi tuu kuwa mtu wa mafanikio ili uweze kuvutia mtandao wa mafanikio, kwa sababu watu huongozwa na imani waliyonayo kwa mtu au asasi wanayoifuta. Bali watu wanatakiwa wakuamini. Imani hiyo hutokana na taswira wanayoijenga kuhusu wewe. Hivyo sio tuu uwe mtu wa mafanikio, lakini zaidi sana uonekane kuwa kweli ni wa mafanikio hata machoni mwa watu husika. Ndio maana kuna msemo usemao “ Cha muhimu kwa watu sio unasema wewe ni nani,bali kile ambacho wao wanaona kuwa wewe ni nani”. Hivyo unaweza kusema mambo mengi, ukajitangazia sifa kadha wa kadha na kujiweka karibu na watu ‘mashuhuri’ lakini mwishoni watu wanataka kuona wewe ni nani kweli kweli.

Watu ni wabinafsi kwa asili:  Watu kwa asili huangalia maslahi yao kwanza kabla ya kuangalia maslahi yako au ya wengine, na hivyo hufuata pale wanapoona wananufaika, haijalishi ni kwa kiwango gani mtu au asasi amegharimika kuonyesha anajali, kama wao hawajanufaika,hilo sio tatizo lao. Hivyo basi wewe mwenyewe ni lazima uwe na malengo ya kile unachotaka kufikia, ujue aina ya watu unaotaka kuwa nao katika mtandao wako, na utumie nguvu kuwafikia hao tuu. Na zaidi sana usipoteze muda kuwaridhisha watu wote , hata wale ambao umeona kweli wanaoweza kukusaidia katika mtandao wako.

Hitimisho:
Tumeona kutokana na maelezo ya hapo juu kuwa siri kubwa ya kuwa na mtandao mzito ni wewe mwenyewe kuwa kwanza mtu ‘mzito’. Kuna njia nyingi za kuwa mtu mzito, iwe kupitia kuajiriwa au kujiajiri. Kinachojenga hasa mtando mzito ni uwezo wako wa kuleta manufaa kwa wengine, iwe kupitia ujuzi wako, mahusiano yako, hekima yako, kufahamika kwako n.k. Ni lazima watu wajue ‘upekee’ wako kwao, ni muhimu wa amini katika upekee huo, na ni muhimu wauhitaji huo upekee wako.
 Zaidi sana, uwezo wa kufanya mawasiliano bora, na kuwa na upeo na busara vitakufikisha mbali katika kujenga mtandao wa watu ambao kweli watakunufaisha. Na kama tayari unahisi unao mtandao mkubwa, jiulize unanufaikaje na huo mtandao, je una mipango ya kunufaika kutokana na huo mtandao wako?
Share:

1 comment: