UJUMBE "MKALI" WA VALENTINE DAY HUU HAPA

Kuna wakati utasikia mtu anasema "aah mie kwa kutafuta dili ni mshenzi kweli kweli".
Lakini wakati mwingine neno mshenzi linaweza kuchukuliwa kama ni tusi.
Au chukulia mfano wa neno GIFT kwa kiingereza linamaanisha zawadi ila kwa kijerumani (Nukuu toka BBC Language) linamaanisha SUMU.
Ninachotaka kusema ni kuwa kumbuka MANENO tunayotumia, ni sisi binadamu ndio tunaamua yamaanishe nini. Na kuna wakati tafsiri :-
1. Inaweza kutumika vibaya ili kujenga picha ya kitu unachodhani ni sawa kumbe neno limebeba maana nyingine. Mfano mzuri ni neno KUPENDA linapotumika katika mahusiano ya mwanamke na mwanaume. Wengi wamekuwa wakilitumia sivyo ndivyo. Kwani wengine wamekuwa wakisema NAKUPENDA wakati wakimaanisha NAKUTAMANI.
Mtu huyo ana "take advantage" ya maana halisi inayofahamika ili kumrubuni mwingine. Au pengine tuseme ni kama neno GIFT kwa kiingereza na kijerumani ni tofauti hivyo huyu jama inawezakana maana yake ya UPENDO ni tofauti na ile tunayoifahamu sote kuwa:- Upendo ni kuwa kwako tayari kufanya yaliyo mema na bora kwa ajili ya mwingine. Upendo katika maana hii hauna maana ya nini unataka kupokea kutoka kwa mtu mwingine bali ni nini unataka kutoa kwa mtu mwingine.
Hata hivyo unapopenda inakuwa ni kama deni kwa unayempenda kwa kuwa:-
Unajisikia kujitoa kwa mwingine, basi furaha yake ni ya muhimu zaidi kwako. Na kwa sababu unataka kujitoa kwake basi unaona HAJA ya kuwa karibu na mtu huyo. Sio kwa sababu tuu ya uzuri wake, mali zake n.k bali ni kwa sababu ya kuwa wewe unataka kujitoa kwake.
--Hata hivyo UPENDO sio lazima utokee mara tuu mnapokutana na mtu, yawezekana baada ya kufahamiana vya kutosha, au baada ya tukio fulani hisia ya upendo ikaja. Upendo Haulazimishwi wala Hauigizwi. Mwisho wa kuigiza upendo ni AIBU.
--Ni kweli kuwa kwa mwanamke na mwanaume kuna hisia za kimwili, na hisia hizo ni muhimu katika kujenga uhusiano. Hapa neno uhusiano sio sawa na UPENDO.Hata hivyo sio kila hisia ya mapenzi ni Upendo.
2. Umesikia mtu akisema HANA MUDA ? Kesho tutaangalia maana ya msemo huu na kwanini ni ya kupotosha. Usikose TAFAKARI YA KESHO.
Share:

1 comment: