Wataalamu
wa uchumi na historia wanasema, dunia tuliyonayo sasa sio tuu kwamba inakumbwa
na machafuko mengi, ila ni dhahiri kuwa machafuko haya yataendelea kwa muda
mrefu. Hivyo basi ni muhimu tujifunze njia za kujiimarisha ili tuweze kupita
salama katika machafuko haya:-
1. Uhuru wa fikra: Kama kuna nyakati ambapo unahitaji uwezo wa
kuiona dunia kama ilivyo na sio kama unavyotaka iwe, basi ni sasa. Ni muhimu
kuboresha ufahamu wako wa mambo mengi ya kimsingi ya kimaisha kama vile mapenzi,
biashara, tabia, teknolojia , mbinu za kutatua matatizo, lugha, na zaidi
sana maswala ya kiroho.
Uhuru
wa kifikra utakuwezesha uweze kujitawala vema, kwani kimsingi wewe ndiye mtu wa
kwanza kabisa unayeweza kuleta mabadiliko makubwa na maendeleo kwa maisha yako,
kwakuwa unayo nguvu ya utashi, kufanya
maamuzi au kuacha watu waamue mambo kwa ajili yako.
2. Kuwa mzalishaji: Katika machafuko haya,
bidhaa na huduma mbalimbali zitakuwa
adimu, na kwa wazalishaji wachache watakaoweza kuzalisha kwa ufanisi wataweza
kujikuta wakiendesha maisha vizuri.
Hivyo pamoja na kuwa mtumiaji wa fedha zako kwa mambo ya burudani,
unahitaji kuhifadhi fedha zako kwa namna ambayo fedha zako hazitopoteza thamani
zake, na wakati huo huo, ukifanya utafiti wa aina ya bidhaa au huduma ambazo
utakuwa ukizalisha, ili nawe unufaike na mazingira tuliyonayo. Kuendelea kuwa muingizaji wa kipato (kwa njia
ya ajira pekee) na kuwa mtumiaji zaidi ya mwekaji akiba, si jambo la busara,
hasa katika hali ngumu ya kiuchumi na kijamii tuliyonayo.
3. Kuboresha mtandao: Kwakuwa unahitaji kutambua fursa nyingi kwa
kadri inavyowezekana na kwakuwa wewe ni mzalishaji, unahitaji sana kujenga
mtandao mkubwa na mtandao wenye manufaa ili kuweza kutambua fursa mbalimbali
kupitia mtandao wako, na pia kuweza kuuza bidhaa zako kupitia mtandao huo. Soma
zaidi kuhusu jinsi ya kujenga mtandao wa watu ‘wazito’ katika makala yetu hii
(bofya) JINSI YA KUJENGA MTANDAO WA VIGOGO
4. Kaa tayari kwa kusafiri: Fursa zinaweza kutokea popote pale, hivyo kuwa
tayari kusafiri nje ya mkoa uliopo sasa, na zaidi sana nje ya nchi. Hakikisha
una passport halali na isiyoisha muda wake, na tambua taratibu za kusafiri nje
ya nchi, kama vile mambo ya visa, na
gharama za maisha kwa nchi tofauti. Bofya makala kuhusu SAFARI YA BONGO -AFRIKA KUSINI, upate picha ya mambo ya msingi katika kusafiri nje ya Tanzania.
5. Mipango ya muda mrefu: Tambua kuwa hali
hii ngumu ya maisha ni swala ambalo litaendelea kwa muda mrefu, hivyo ni muhimu
kujipanga wewe na familia yako. Kama una watoto au una mpango wa kuwa na
watoto, basi ni wakati wa kufikiria pia namna ya kuja kuwawezesha watoto wako
wawe na ujuzi wa uhakika, na kuwa wawe wazalishaji. Hakikisha unajitengenezea ujuzi na uzoefu
uliokomaa katika jambo fulani au mambo kadhaa tofauti, ili uweze kuja kuuza
ujuzi na uzoefu wako huo katika soko gumu la huduma tunalokumbana nalo.
6. Kuwa mwepesi wa kubadilika: Mambo mengi
yanabadilika kwa haraka sana, ufahamu uliokuwa nao jana , mbinu ulizotumia siku
za nyuma hata kama zilifanikiwa,
inawezekana kabisa zisifanikiwe kwa sasa, na kwa kadri mambo yanavyozidi
kubadilika. Ushindi wa kipekee unakuja pale unapoweza kuwa mwepesi wa
kubadilika, kwa kubuni njia mpya na bora za kukabiliana na mazingira
unayokumbana nayo.
0 comments:
Post a Comment