SABABU 4 KWANINI RAFIKI ZAKO NI HATARI ZAIDI KULIKO ADUI ZAKO

Pamoja na ukweli kwamba rafiki ni muhimu katika maisha, makala hii inachambua namna nne (4) ambapo rafiki wanaweza kuwa hatari zaidi ya adui zako. Kinachoelezwa katika makala hii ni kuwa uhatari wa rafiki upo katika namna urafiki unavyoendeshwa. Jisomee mwenyewe:-

1. Kioo: Mara nyingi tunajikuta kuwa tunaamini zaidi mtazamo wa rafiki zetu kuhusu sie, kuliko vile utashi wetu unavyotuambia. Tunafanya mambo mengi kwa imani na ufahamu tuliojijengea kichwani kuwa kufanya hivyo ndio kunakotarajiwa na rafiki zetu. Kwa kifupi, yale yanayoonekana kuwa yanafaa machoni mwa rafiki zetu –iwe mavazi, lugha, matumizi ya fedha, hata aina ya mwenza wa maisha, ndio hayo tunayojitahidi kuyafanya. Hivyo kama rafiki zetu wana mtazamo usio chanya, basi tunajikuta tunaelekea pabaya pia.

2. Tunajiweka watupu mbele zao: Kwakuwa tumewapa ‘kitambulisho’ cha kuwa wao ni rafiki zetu, tunajihisi tupo salama kuelezea mambo yetu ya msingi kimaisha kama vile habari za familia, biashara, masomo, na hata mapenzi. Tena kuna nyakati tunadiri hata kuwaambia siri zetu. Hali hii ya ‘kujiweka mtupu’ mbele yao ni hatari kwani taarifa tunazo ‘share’ nao zinaweza kutumika kutuangamiza, si umewahi kusikia “Information is Power” ? Kwa sababu hii ni rahisi kwa marafiki kutudhuru kama mwanamuziki Shaa alivyoimba katika wimbo Shoga.


3. Ushindani: Kwakuwa rafiki ndio watu wa karibu zaidi kwetu, na kama tulivyoeleza hapo juu mara nyingi wao ndio kioo chetu, tunajikuta tukijiingiza kwenye ushindani nao kwa kusudia au bila kutarajia, kwakutaka kuwa kama wao au  zaidi yao. Na wao pia kwa kukusudia au bila kukusudia kwakuwa wanatufahamu vizuri nao wanajikuta wakianzisha ushindani ili kuwa kama sisi au zaidi yetu. Hali hii ya kutaka ushindani kati yetu, ukizingatia kuwa tumekwishajiweka  ‘watupu’ mbele za rafiki zetu, inafanya rafiki hao kuwa ni hatari zaidi ya hata adui zetu wa sasa.
Wakati mwingine ushindani wa marafiki zetu hujidhirisha waziwazi kama mwanamuziki Nyota Ndogo alipokeza kwenye wimbo Watu na Viatu.
 
4. Dhambi ya kutenga watu: Tunaposisitiza kutazama binadamu wenzetu katika makundi mawili ya adui na rafiki, twaweza kujikuta tukiwapa umuhimu na thamani kubwa rafiki, na kuwatenga maadui. Kutenga huku kutaendelea kwani ndani ya hao unaoona rafiki, unaweza chambua zaidi na zaidi na kuona kumbe baadhi sio rafiki, ni maadui. Kutenga huku mara nyingi hufanyika wazi wazi, hivyo kumfanya rafiki kujihisi wa kipekee, nap engine kutumia nafasi hii kukuumiza, bila wewe kutambua kwa haraka, kwani ni unajua huyo ni mmoja wa watu wako.

HITIMISHO:
Ni jambo zuri sana kuwa na rafiki, na rafiki ni muhimu sana. Hata hivyo, ni jukumu lako kusimamia vema urafiki wako na watu wengine. Haitoshi tuu kuwa na rafiki wema, bali unapaswa kujua namna ya kuishi na hao rafiki wema. Endelea kuwa na maamuzi binafsi, tafuta uhuru wa fikra na usiogope kuwa na mtazamo tofauti na rafiki zako.
Nimalizie makala hii kwa nukuu hizi:

“ Tunaweza kuwamudu adui zetu, Mungu tulinde dhidi ya Rafiki Zetu” – Martin Luther
“ Nilimuomba Mungu aniondolee maadui, nikaanza kuona rafiki wakipungua”- Meek Mill.
Share:

1 comment: