‘IDEAS’ 7 ZA JINSI YA KUANZISHA BLOGU ZENYE MVUTO

Ukifuatilia sana fani ya blogging nchini kwetu Tanzania, utagundua changamoto kubwa iliyopo ni katika ubunifu na uandishi wa taarifa za kuweka katika blogu. Tatizo la ubunifu linajionyesha wazi kwa utitiri wa blogu zenye mwelekeo mmoja kwamba nyingi ni blogu za habari za matukio ya kila siku, na kwamba habari zenyewe nyingi ni ‘copy & paste’.
Imefikia hatua sasa, watu wengi kuchukulia kuwa blogging ni jambo la kama vile mzaha mzaha tuu,na kwamba mtu yoyote yule ili mradi anajua kutumia computer ,ataweza kufungua blogu yake na kuwa ana copy na ku paste habari toka vyanzo mbalimbali na kuweka kwa blogu yake.
Hata hivyo, bado kuna uwezekano mkubwa wa watu wanaotaka kuanzisha blogs wakatumia ubunifu kidogo kuboresha blogs zao kwa kuleta upekee wa taarifa wanazoweka, na la msingi sana tutazame thamani ya taarifa tunazoweka kwa wasomaji wetu.
Tanzania ni yetu sote, na kwamba blogs zina mchango mkubwa kama chombo cha habari kuelimisha na kuelekeza jamii kwenye muelekeo sahihi. Ni kweli kuwa picha za utupu, na habari za udaku ‘zinauza sana’ lakini tukumbuke  kuna mambo mengine mengi tuu ambayo tungeweza kuandika kama bloggers na kutoa mchango kwa jamii yetu.
Kuna msemo unaosema “ Be change you want to see” Yaani wewe mwenyewe uanze kwanza kufanya mabadiliko kabla ya kudai mabadiliko  yatokee tuu.
Zifuatazo ni baadhi ya ‘ideas’ ambazo zinaweza kutengeneza blogs zenye ‘kuuza’ (kuleta wasomaji wengi) na pia zikaleta mchango chanya katika jamii.  UPO HURU KUTUMIA ‘IDEAS’ HIZI KUTENGENEZA BLOGU YAKO


1.Fursa kwa wajasiriamali :  Waweza anzisha blogu mahsusi kwa fursa motomoto kwa wajasiriamali wa sasa na wale wanaotaka kuwa wajasiriamali. Blogu hii haitojihusisha na makala kuhusu ujasiriamali (maana wapo wengi wanaandika kuhusu hilo) badala yake itajikita katika kuweka taarifa motomoto za upatikanaji wa mafunzo ya ujasiriamali, mikutano, semina, mikopo, na asasi mbalimbali zinazosaidia wajasiriamali. Waweza pia weka links za blogs zinazohusiana na ujasiriamali ili kufanya blogu hii iwe nyumbani kwa wajasiriamali.

2. Shule za Kata: Habari nyingi zinaandikwa kuhusu shule za kata. Ili kuleta upekee blogu yako hii itajikita kueleza mafanikio , changamoto na jinsi shule za kata zinavyojitahidi kujikwamua. Takwimu na picha ni muhimu sana kwa blogu hii. Pia unaweza onyesha program mbalimbali za maendeleo zinazosaidia shule za kata. Kuhoji wanafunzi wa shule husika, na kuonyesha maisha ya shule za kata. Lengo ni kusaidia wazazi na walezi kutambua mazingira na maendeleo ya shule wanazopeleka watoto wao, au wanazotarajia kupeleka watoto wao. Maana wapo wengi mtoto toka Form 1 hadi Form 4, hawajakanyaga shule anaposoma mtoto.

3.Picha Uwanjani: Kuna blogu nyingi zenye habari na michezo na burudani.  Ili kuleta upekee, blogu yako hii itakuwa ni ya picha tuu. Tena picha kali zaidi , ikisindikizwa na Facebook page, yenye kusheheni picha za matukio mbalimbali ya burudani na michezo. Si unajua kuwa picha inatoa maneno maelezo zaidi ya Maneno ? Ndio hivyo, hakikisha picha unazoweka zinabeba ujumbe au taarifa fulani, ambayo hautoelezea kwa maneno ila mtazamaji atajionea mwenyewe. Kumbuka kutaja vyanzo vya picha ambazo haukupiga wewe mwenyewe.

4.Nukuu zetu: Unakumbuka nukuu kama vile “…ukitaka kula ukubali kuliwa”?. Basi waweza tengeneza blogu maalum ya  nukuu toka Tanzania. Waweza zigawa katika makundi ya Siasa, Jamii, Teknolojia, Uchumi, Michezo, Elimu, n.k. Usisahau ile nukuu ya Tanzania ni muungano wa visiwa vya Zimbabwe, Pemba na Tanganyika. Kumbuka kupata nukuu sahihi, na ikiwezekana utaje kabisa nani alitoa maneno hayo. Blogu hiyo ya nukuu zetu, itaburudisha na kuelimisha pia, na kutukumbusha wapi tunatoka, na wapi wapi tutarajie kuenda.

5.Skonga:  Blogu hii itakuwa maalum kwa wanafunzi na wazazi. Ni kama vile shule, ila shule ya mtandaoni, ambapo Matokeo mbalimbali ya Form 4, 2, QT, FORM4, yatawekwa. Msaada kwa wanafunzi kwa njia ya ‘materials’ ya kujisomea yataweka, na makala zenye kujaa mbinu za kusoma, changamoto za maisha ya kishule, habari motomoto zihusuzo elimu zitawekwa humu. Mambo mengine ya maisha ya kishule kama vile majina ya walimu, ambayo wanafunzi huwatunga yatawekwa humu. 

6.Wakali wa Bongo: Badala ya kuandika habari za watu maarufu na mashuhuri kama udaku, blogu hii ya wakali wa Bongo, itajitofautisha kwa kuangalia maisha ya watu hawa katika muonekano chanya. Blogu itachambua changamoto wanazokumbana nazo, nini wamejifunza kuhusu mafanikio, na wanafanya nini kuendelea kubaki kuwa na mafanikio. Pia blogu itaangalia wakali wengine waliopo katika jamii lakini hawajapata kuwa mashuhuri kama vile wanafunzi waliofaulu kwa viwango vya juu kabisa katika masomo yao. Itaangalia pia biashara zinazotamba Tanzania, Shule zinazotamba na zilizowahi kutamba kama vile TAMBAZA, wanasiasa, na asasi zisizo za kiraia. Blogu hii itanogeshwa na mahojiano na wahusika, picha, na historia mbalimbali. Unataka kuanza blogu hii ? Embu fuatilia na kuandika ukali wa shule ya TAMBAZA.  Enzi hizo TAMBAZA ilivyosifika kwa fujo lakini pia kwa ubora wa wanafunzi.

7.Mkali wa Facebook:  Blogu hii ni mahsusi kwa mambo yanayovutia kuhusiana na Facebook. Mambo kama vile picha zilizopata ‘likes’ nyingi (zisiwe picha za mtu binafsi), status kali, au comments zenye mvuto zaweza kuwekwa humo. Mambo mengine ni taarifa za kiufundi kuhusu applications mbalimbali zinazopatikana Facebook kama vile BranchOut, na mambo mapya ya matumizi ya Facebook yanayoletwa na kampuni ya Facebook kama vile Timeline.
Share:

14 comments:

  1. Nimependa makala yaani ni nzuri sana inabidi nizifanyie kazi. Ni kweli hapa tanzania watu wanapenda sana news blogs ila nyingine wanaona ni ngumu kuandika makala nahisi.

    ReplyDelete
  2. Ni kweli broo umesomeka vizuri

    ReplyDelete
  3. Elimu ninayoipata sikuwahi kufikiria kabla kiukweli umenifumgua macho kuanzia sasa nitafanyia kazi haya mawazo nashukuru saana kaka

    ReplyDelete
  4. Heshima kwako mkuuu, mimi binafsi najifunza vitu vingi sana

    ReplyDelete
  5. Mimi nataka kupata blog nitakayoitumia kualika watu watumie au watembelee company

    ReplyDelete