ILIVYO KUSAFIRI KWA BARABARA DAR- JOBERG (AFRIKA KUSINI)

Hakuna shaka kuwa Afrika Kusini ndio nchi iliyoendelea zaidi katika bara la Afrika. Pengine ungependa kuitembelea ili kujionea ilivyo hasa mji maarufu wa Johannesburg. Makala hii inachambua mambo kadhaa unayoweza kukumbana nayo kama utasafiri kwa njia ya barabara hususani kwa njia ya kupanda mabasi kutoka Dar es salaam hadi Johannesburg aka Joberg aka Egoli. Mojawapo wa sababu za kusafiri kwa basi  ni kujionea kwa macho nchi nyingine kama vile Zambia, Msumbiji, au Zimbabwe. Wengine hufikiria swala la kupunguza gharama ya nauli kwa kupanda  basi badala ya kupanda ndege ambayo ni gharama zaidi. Makala hii inaangalia safari ya Dar-Joberg kupitia Harare, Zimbabwe.

Siku za kusafiri:  Safari nzima kutoka Dar es salaam mpaka Joberg ni ya siku nne(4). Siku nne hizo ni kama ifuatavyo, kutoka Dar- Harare, Zimbabwe siku tatu, na kutoka Zimbabwe mpaka Joberg ni siku moja. Kumbuka kuwa sio kwamba siku zote hizo basi litakuwa likitembea. Kuna muda wa mapumziko ya msosi, kuchimba dawa, na masaa kadhaa ya kusubiri abiria wagonge mihuri ya viza kwani basi likifika mpakani husimama na kuwataka abiria wote washuke ili waweze kukaguliwa. 
Wakati mwingine abiria hutakiwa kushusha mizigo yao yote, hata iliyopo kwenye buti ili ikaguliwe. Hivyo muda mwingi hupotea wakati basi halitembei.

Nauli: Kwakuwa hakuna basi la moja kwa moja kutoka Dar es salaam mpaka Joberg, tarajia kulipa nauli ya Dar es salaam – Harare, Zimbabwe, halafu kutoka Zimbabwe unapanda basi lingine la moja kwa moja hadi Joberg. Hata hivyo unaweza amua kupanda Dar  - mpaka Lusaka, halafu kutoka Lusaka ukaamua kupitia nchi nyingine mfano ukaingia kwa Afrika Kusini kwa boda ya Msumbiji. Makala hii inajadili njia ya kupitia Harare Zimbabwe.
Kutoka Dar – Harare, Zimbabwe waweza lipa kwa fedha za kitanzania au kwa dola, kuendana na makubaliano yako na watu wa mabasi pale Ubungo Bus Terminal. Nauli ya Dar – Harare ni kati ya Dola za Kimarekani 80 -100. Wakati nauli ya Harare, Zimbabwe mpaka Joberg, Afrika Kusini ni kati ya Dola za Kimarekani 50-100 kutegemeana na msimu wa mwaka, kwani wakati wa sikukuu bei hupanda sana. Hivyo kwa hesabu za haraka haraka kwa makadirio ya juu, nauli kutoka Dar-Joberg ni jumla ya Dola za Kimarekani 200 ila inaweza kuwa hadi Dola za Kimarekani 150. Kumbuka hii ni nauli ya kwenda tuu.

Fedha za kigeni: Nchi tofauti zina sarafu tofauti hivyo jiandae kutumia sarafu tofauti kufanya manunuzi ya mahitaji yako ukiwa nchi husika. Mfano kwa nchini Zambia utatumia KWACHA, ukiwa Zimbabwe, sarafu kuu ya kutumia ni Dola ya Kimarekani, wakati utakapoingia nchini Afrika Kusini sarafu kuu ni RAND.
Unaweza kusafiri na kiasi chako cha kutosha cha fedha za kigeni za nchi tofauti kama tulivyotaja hapo juu, au ukaamua kuenda kununua kiasi cha fedha za kigeni unachohitaji utakapofika katika nchi husika. Mfano ukiwa Lusaka Zambia, utaweza kununua KWACHA kwa wauzaji wa fedha za kigeni hata pale pale kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Lusaka. Sio tuu KWACHA, waweza nunua pia hata Dola za Kimarekani. Waweza pia fanya manunuzi ya fedha za kigeni ukiwa Harare, Zimbabwe au hata Joberg katika maduka ya mabadilishano ya fedha za kigeni.

Vyakula na Gharama zake:  Katika nchi zote utakazotembelea tarajia kukuta vyakula unavyovifahamu kama vile ugali, wali, chipsi, kuku na nyama , hivyo usiogope sana kwamba hautopata misosi unayoipenda (Hata hivyo radha na mapishi vinaweza kuwa tofauti na vya bongo). Vinywaji pia vipo vya kawaida, kama soda na bia, hata hivyo pamoja na ukweli kuwa safari ni ndefu,  hauruhusiwi  kunywa bia ukiwa kwenye basi. Nchini Zimbabwe unaweza kupata msosi mzuri kwa kuanza Dola za Kimarekani 8-15, pia waweza lipa kwa RAND ukiwa Zimbabwe. Nchini Zambia unahitaji walau KWACHA 35000. Ukiwa Afrika Kusini , msosi wa kawaida unaweza kupata kwa RAND30 na kuendelea. Kumbuka msosi hapa unajumuisha na kinywaji pia.
Menu katika mojawapo ya mgahawa nchini Zambia

Mambo ya Uhamiaji:Kati ya mambo yanayochosha katika safari ya Dar- Joberg ni kuvuka mipaka ya nchi ambapo utatakiwa kuonyesha hati ya kusafiria (passport) ili igongwe muhuri wa viza. Kwanza kuna mpaka wa Tanzania na Zambia, halafu  kuna mpaka wa Zambia na Zimbabwe, na hatimaye kuna mpaka wa Zimbabwe na Afrika Kusini. Ni lazima uwe na passport halali ya nchi yako ili uweze kuionyesha  igongwe muhuri wa VIZA, na zaidi sana inabidi uwe na kadi ya chanjo ya homa ya manjano.  Pia tambua kuwa ukifika mipakani  kuna muda mrefu wa kusubiri mpaka passport yako ipate kugongwa muhuri. Unaweza kujikuta umesimama kwenye foleni ya mpakani kwa muda hata wa Masaa Matatu! Pia tarajia vurugu au hali ya kutokuwa na subira ya wasafiri wengine wakati wa kusubiri. Kwa bahati nzuri hakuna malipo kwa mtanzania kuingia au kutoka nchini Afrika Kusini, isipokuwa usizidishe siku 90 za kukaa kwako nchini humo.

Mambo ya Lugha: Lugha inayotumika sana na abiria wengi kutoka Dar es salaam mpaka Zambia ni Kiswahili kwani wengi wao ni Watanzania au watu kutoka Zambia ambao wanajua jua kwa kiwango walau kidogo jinsi ya kuzungumza kiswahili. Unapoingia Zimbabwe hali inaanza kubadilika kwani wengi hapo huzungumza Kiingereza kama lugha kuu ya Mawasiliano. Hata hivyo ukiwa stendi kuu ya mabasi utaweza kuona waTanzania wengine waishio Zambia au wafanyao kazi kwenye mabasi kutoka Tanzania kama vile Tawqa na Falcon. Kutoka Zimbabwe mpaka Joberg , lugha kuu ni kiingereza, hata hivyo si ajabu kusikia abiria wengi wakizungumza lugha nyingine zaidi ya kiingereza, mfano Kishona au Kindebele kwani tarajia abiria wengi kuwa ni Wazimbabwe wanaoenda Afrika Kusini. Mambo ya lugha yanaanza kubadilika zaidi utakapoingia Afrika Kusini, kwani yapo makabila mengi, na kuna lugha 11 maalum kwa mawasiliano, kiingereza ni mojawapo tuu ya hizo lugha rasmi.
Wenyeji wengi hutumia lugha zao asili ambazo pia ni lugha rasmi kama vile ki Xhosa, ki Zulu, ki Tswana, ki Afrikans, kiSutu, n.k.

Ukiingia Afrika Kusini: Ni mwendo wa masaa karibu nane hadi kumi kutoka ‘BODA’ ( mpaka) wa Afrika Kusina na Zimbabwe mpaka kufika Mji Mkuu wa Afrika Kusini Pretoria. Kutoka Pretoria, unatumia kati ya nusu saa hadi dakika 45 kufika Joberg.  
 Ukiwa Joberg unaweza bado kutembelea miji mingine mingi maarufu nchini Afrika Kusini kwa kutumia basi, mfano kutoka Joberg- Durban ni masaa Sita hadi Saba. Kutoka Joberg – Cape Town, ni zaidi ya Masaa 24. Kutoka Joberg kwenda Port Elizabeth ni  wastani wa masaa 20. Huduma ya malazi katika nyumba za wageni ni kati ya RAND 250 hadi R400 kutegemeana na eneo.  
Na nyumba za wageni nyingine unaweza kuhitajika kushare room na wageni wengine, yaani unaweza kulipa R250 na kuwekwa katika chumba ambacho mpo wageni wawili au watatu jumla. Kuna hoteli pia ambazo bei zake ni juu zaidi, pengine kuanzia R400 kwenda juu. 
Share:

19 comments:

  1. asnt kwa ku2pa mwanga

    ReplyDelete
  2. Safi saana kaka! sisi tunaopanga kusafiri inatupa mwanga..... wengine fanyeni hivi ktk ishu mbalimbali ili tufumbuane macho!

    ReplyDelete
  3. Shukran kaka, mimi birthday nafsi nimeongeza kitu katika uelewa wangu. Na je vipi kuhusu kupanga chumba gharama zake, na ke vipi kuhusu suala la kazi? Na inakuwaje kama mtu anahitaji kuishi kuho au kutafuata kazi

    ReplyDelete
  4. thanks bro, na gharama za nauli kwa basi kutoka hapo jors hadi capetowwn zime kaaje..??

    ReplyDelete
  5. Umetupa elimu ya usafiri na umetufungua wengi wetu akili na macho.
    Kwa xaxa vipi kuhusu kupanga chumba kwa mwezi bei na maeneo gani yenye bei nafuu?
    Ubarikiwe sanaa

    ReplyDelete
  6. Hii ndio maana halisi ya blog unapost kitu cha kuelemisha na kufundisha pia na kujuza tusio jua ongera sana

    ReplyDelete
  7. Naomba kujua nauli ya Tanzania Hadi Botswana au ya Botswana to Tanzania

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kaka akijibu nitafute, namimi ntaka nijuwe nauli ya uko Botswana

      Delete
  8. Kupanga chumba kwa mwezi ni kiasi gani kiongozi

    ReplyDelete
  9. Naomba unitumie namba yako kaka

    ReplyDelete
  10. Na kutoka Johannesburg mbaka bongo inafika shilingi ngapi sasa hiv

    ReplyDelete
  11. Ghalama ya passport kusafilia bei gani hapa Tanzania

    ReplyDelete
  12. Ahsante umenifungua, akili kwa kiasi fulani,napenda kujua je? Nikiwa pasport yangu nasafiri kwenda South natakiwa niambatanishe na nini?..ili nisisumbuliwe ?

    ReplyDelete