Kuna
sababu mbalimbali kwanini mtu atake kuajiri, badala ya kuajiriwa, mfano
kipato kidogo anachopata katika kazi husika, hitaji la kutaka uhuru
zaidi binafsi wa kufanya kazi, hitaji la kuweza kutoa ajira kwa wengine
na zaidi sana kuweza kutumia vema kipaji na uwezo wa kuzalisha ambao
katika kazi ya sasa mtu hapati nafasi ya kufanya hivyo.
Kujiajiri
ni jambo linalohitaji maandalizi ya muda mrefu na kuna mambo ya msingi
kuyafahamu, haiwezekani tuu , ukaacha kazi na kusema ok, acha nijiajiri.
Makala hii inachambua mambo ya msingi ya kujiandaa na kuyafahamu kabla mtu hajaamua kuacha kuajiriwa.
Mkakati ni muhimu: Wazo au ndoto isiyo
na mkakati wa kuitimiza ni upuuzi yaani ndoto hiyo au wazo hilo halina maana, hivyo basi ndoto yako ya
kujiajiri siku moja, ni lazima iwekewe mkakati wa kuifanikisha ikiwa ni pamoja
na muda hasa wa lini utaitimiza hiyo ndoto.
Katika kuweka mkakati huu wa
kutimiza ndoto yako, fanya utafiti wa kina kuhusu mipango yako binafsi ya
maisha, mtazamo wako kuhusu maisha, mpenzi/mke wako, familia yako, na hali ya
jamii kwa ujumla inavyoenda kama vile mabadiliko ya hali ya kisiasa,
teknolojia, na uchumi.
Tengeneza malengo ya aina ya shughuli unayotaka kuifanya
ukiacha kuajiriwa, na pima uwezekano wa shughuli hiyo kufanyika kweli na kama
itakulipa. Utambue pia aina ya watu na rasilimali nyingine utakazozihitaji, na
jinsi utakavyozipata.
Unahitaji fedha: Ndio, unahitaji kiasi
cha fedha za kutosha kununua vifaa na malighafi za kutengenezea bidhaa yako.
Pia unahitaji fedha za kuwalipa wafanyakazi wako, na zaidi sana , unahitaji
fedha za kuendesha maisha yako na familia yako , kwa kipindi fulani kabla ya
biashara kuanza kukulipa mshahara. Hivyo kabla haujaacha kibarua chako,
hakikisha umetengeneza bajeti ya kutosha na una akiba ya kutimiza mahitaji ya bajeti
yako. Usingependa uache kazi halafu uanze kuwa omba omba kwa rafiki na jamaa,
au uanze kujuta.
Network ni muhimu: Kumbuka katika
kujiajiri kwako, utahitaji wateja, washirika, wafanyakazi na hata washauri
mbalimbali ili mambo yako yaende vizuri. Hivyo, wakati ukiwa umeajiriwa ndio
wakati wako muafaka wa kutengeneza na kupanua wigo wako wa watu unaowafahamu na
waliokaribu nawe.
Kumbuka
kuendeleza mawasiliano kwani watu hawapendi kuona wewe unataka
kuwatumia tuu kisha unawatupa. Endeleza mawasiliano walau hata kwa
salamu tuu. Zaidi sana, heshimu watu wote, hata usiowafahamu au wale
unaodhani 'sio watu muhimu'.
Jenga taswira
nzuri kwa jamii kwa lugha fasaha, picha na matukio mengine, usifanye watu wakufikirie vibaya.
Usipitwe na wakati: Hakikisha kuwa
unafuatilia taarifa za matukio, dili na watu wanaohusiana na aina ya shughuli
unayopanga kuifanya wakati utakapojiajiri. Hii itakusaidia kupata uzoefu na
kusoma alama za nyakati, na pengine kutambua fursa nyingine zaidi.
Endelea
kujifunza zaidi kuhusu kazi yako, watu na jamii kwa ujumla kwani kujiajiri kunahitaji
uzoefu zaidi, na zaidi sana uwezo wa kupambana na changamoto nyingi ambazo
nyingine haujawahi kukutana nazo kabisa, ila taarifa za awali na kujua jinsi
mambo yanavyoenda kwa ujumla katika jamii vitakufanya ushinde changamoto.
Maana halisi ya biashara: Baada ya
kuacha kuajiriwa, hautarajii kuwa mtu wa ‘kuganga njaa’ yaani kufanya biashara
ili mradi tuu hela iingie, lakini haujui mwelekeo wa biashara yako upoje, na
wala hakuna mkakati wa kuikuza na kuimarisha biashara husika.
Biashara inahusu
kutimiza mahitaji ya watu, kwahiyo ili mradi utakuwa na uwezo mkubwa wa
kutimiza mahitaji ya watu, na kuendelea kuhamasisha watu zaidi kuja kwako uweze
kutimiza mahitaji yao , basi biashara itakua, na itaendelea kuwa endelevu.
Kinyume cha hapo, ushindani utakutoa katika biashara kwani wateja watakambilia
kwa wengine. Biashara sio tuu kupata wateja, ni vile kuweza kuendelea kupata
wateja na kuendelea kupanua biashara.
Inabidi uipende shughuli husika
unayoifanya, na uweze kutimiza mahitaji ya wateja kupitia biashara husika.
Muda
wako mwingi utautumia katika shughuli yako mpya utakayojiajiri hivyo, kama
ambavyo kazi uliyonayo pengine ‘inakuboa’, hakikisha ajira yako binafsi ‘haikuboi’.
Umuhimu wa wafanyakazi:
Watendaji wa
shughuli husika za biashara yako utakayoianzisha ni muhimu wawe wenye
ujuzi na
uzoefu wa kutosha wa kufanya shughuli husika, na uweke mikakati ya
kuwapatia
nyenzo zote muhimu za kufanyia kazi ikiwemo teknolojia na mazingira
mazuri ya
kazi. Hivyo basi wakati unajiandaa kujiajiri tilia maanani hili katika
bajeti
yako ya kuajiri. Usingependa wafanyakazi wao wajisikie vibaya kama vile
wewe
ulivyojisikia vibaya katika ajira yako fulani (pengine ajira yako ya
sasa). Muda huu ambao umeajiriwa, ndio muda pia muafaka wa kusaka
'vipaji'- yaani watu ambao utafanya nao kazi utakapojiajiri.
Inakuhusu wewe : Mafanikio yako katika
kujiajiri yanategemea mambo mengi ila zaidi sana yanakutegemea wewe. Je, nini
hasa sababu yako ya kutaka kujiajiri?
Ni kweli una bidhaa au huduma haswa ya
kupeleka sokoni itakayokufanya iendeshe maisha yako na kuiendeleza biashara
husika au ni hasira tuu za jinsi bosi wako anavyokuchulia hapo ofisini kwako,
au kwakuwa mshahara uliopo sasa haukutoshi. Je, mipango yako mingine ya maisha
ipoje?
Ndoto zako za kusoma, au kuishi sehemu tofauti tofauti, pengine mkoa
mwingine tofauti na uliopo sasa, au pengine hata nchi husika. Je, yote hayo
yanaathiri vipi mipango na mikakati yako ya kujiajiri, bila kusahau msukumo
toka kwa familia yako.
Ndoto sahihi: Ni kweli kuwa upo sahihi
kufikiria au kuota kufanya biashara kubwa na yenye mafanikio sana, lakini
kumbuka mafanikio hayaji kwa usiku mmoja, na hata kama yatakuja kwa usiku
mmoja, inahitajika kazi ya muda mrefu kuyafanya yawe endelevu.
Hivyo basi,
usingoje wakati ‘muafaka’ wa wewe kuwa na kiasi kikubwa cha fedha au kwamba ‘umeyaset’
vema mambo yote.
Anza kidogo kidogo, kubali kufanya makosa, na tambua kuwa hata
kama utafanya uchambuzi na uchunguzi wa kutosha kuhusu soko, jamii na
teknolojia, hali halisi unayoenda kukumbana nayo inaweza kuwa tofauti na ile
uliyojifunza wakati wa uchambuzi au uchunguzi wako kwakuwa hicho unachoenda
kufanya ni kipya hakikufanyiwa uchambuzi, bali unakifanya kutokana na uchambuzi
uliofanya hapo awali.
Kuna mtu mwingine atakuja kutumia makosa au mafanikio yako kupanga
mambo yake.
Maneno Mazuri.
ReplyDeleteShukran kwa ushauri wako.
ReplyDelete