ZIFAHAMU KOMPYUTA ZA KUVAA MWILINI

Makala hii inachambua teknolojia inayoibukia kwa kasi ambapo watu wataweza kutumia kompyuta ambazo zitakuwa zimevaliwa mwilini mwao. Lengo la makala hii ni kukuonyesha msomaji jinsi maisha yetu na mazingira kwa ujumla yanavyotarajiwa kubadilika. Chukulia mfano wa maendeleo ya teknolojia yaliyoleta uwepo wa BLOGS na Mitandao ya kijamii, yamewezesha kurahisisisha upashanaji habari. Tuangalie sasa teknolojia hii ya kompyuta za kuvaa.
Kampuni ya Google wapo mbioni kutoa sokoni kwa mara ya kwanza aina ya kompyuta inayovaliwa machoni . Kompyuta hiyo yenye umbo la miwani kama uonavyo pichani hapo juu, inajulikana kwa jina la Google Glass, na itakuwa ikiendeshwa kwa kutumia program ya Android.

Katika siku za hivi karibuni Google ilitangaza nafasi za watu kutoa oda ya miwani hiyo, ambapo bei yake ilikuwa $1500, hata hivyo kwa sasa Google imesitisha kupokea maombi hayo, ambapo wakazi wa Marekani tuu ndio walipewa nafasi ya kuwasilisha maombi.

Miwani hii ya Google, ambayo ni maendeleo makubwa katika teknolojia ya kompyuta zinazovaliwa mwilini, inadhihirisha jinsi ambavyo wanasayansi walivyodhamiria kufanya matumizi ya kompyuta na internet yawe kila mahali na zaidi sana watu watumie kompyuta bila kutumia mikono yao.  Miwani hiyo ya Google inawezesha mtumiaji kuona vitu, au watu kwa muonekano ang’avu, na pia anaweza kuiamlisha miwani ifanye matendo kama vile kupiga picha, kutuma ujumbi, ku search taarifa fulani, kushare picha au ujumbe kwa mitandao ya kijamii, na hata kupiga simu, yote hayo yanafanyika kwa njia ya sauti tuu. ( Jionee video hapo chini inavyoonyesha jinsi Google Glass inavyoweza kutumika).

Wachambuzi wa habari za teknolojia wanatabiri kuwa teknolojia ya kompyuta zinazovaliwa mwilini itashika kasi kwa siku zijazo kwani tayari Apple na Microsoft wapo kwenye michakato pia ya kuandaa aina zao za  kompyuta za kuvaa.  Kwa mujibu wa gazeti la Uingereza la  The Guardian la Novemba 27,2012, Microsoft wapo mbioni kutengeneza miwani yao ambayo itakuwa na ubora zaidi kuliko Google Glass, kwani wanadhamiria kufanya miwani hiyo iweze kurekodi na hata ku play back, matukio ambayo mtu atakuwa anayoona.

Wakati Microsoft wakijiandaa kuingia katika soko la Miwani ya kuvaa, kampuni ya Apple inasemekana ipo kwenye mchakato wa kutengeneza kompyuta ya kuvaa mkononi kama saa, inayoenda kwa jina la iWatch. Hata hivyo  kampuni ya Apple yenyewe haijatangaza bado aina hasa ya kompyuta ya kuvaa, ingawaje wadadisi wengi wanatazamia kuona Apple ikitoa kompyuta za kuvaa mikononi. Katika makala yake ya Machi 4, mwaka huu wa 2013, website mashuhuri kwa habari za teknolojia CNET, wametaja aina nyingine za kompyuta za kuvaa zinazotarajiwa kutoka Apple kama vile iTV, na iGlass.

Kumbuka makala tuliyoiwasilisha hapa Mbuke Times kuhusu Internet ya Kila Kitu “ Internet of things”,  maendeleo haya ya kompyuta za kuvaa mwilini , yanakuja kutumia internet ya kasi kubwa zaidi ya LTE.
Share:

0 comments:

Post a Comment