IFAHAMU KAMBI YA WACHAWI GAMBAGA-GHANA


Ujumbe mkuu wa mwaka huu wa Siku ya Wanawake duniani ni Tutokomeze Ukatili Dhidi ya Wanawake.  Pamoja na kuwa wanawake wana mchango mkubwa sana katika jamii, wamekuwa ndio kundi kubwa linalopata shida na kudhurumiwa katika jamii zetu. Makala hii inakupa maelezo ya kweli kuhusu wanawake wengi, wao wazee na vikongwe huko nchini Ghana wamejikuta wakitengwa na jamii na kuwekwa kwenye kambi maalum maarufu kama kambi ya wachawi. Hii ni baada ya kukimbia kipigo na kunusurika kuuawa.

Huko kaskazini mwa nchi ya Ghana, kuna kijiji maarufu kiitwacho Gambaga, ambacho kinajulikana kama Kambi Maalum ya Wachawi, kwa kuwa wanawake wanaoshukiwa kuwa ni wachawi toka maeneo mbalimbali ya Ghana hususani vijiji vya karibu na Gambaga hukimbilia kwa Chifu wa Gambaga kwa kujisalimisha. Kama malipo ya fadhila ya usalama wao, huamrishwa kuwa vibarua wa Chifu wa Gambaga.

‘Kambi’ hiyo ilianzishwa na Imam mmoja aliyekuwa akipita eneo karibu na Gambaga na kushuhudia wanakijiji wakimuadhibu kwa lengo la kumuua, mwanamke aliyesadikiwa kuwa ni mchawi. Imam huyo aliwaomba wanakijiji waache kumuadhibu mwanamke huyo na wakambidhi mwanamke huyo kwake yeye Imam, ambapo Imam aliahidi ‘kumkabidhi’ mchawi huyo kwa Mungu, hivyo nguvu za uchawi zingeisha. Kwakuwa Imam aliheshimika sana na wanakijiji hao , alikabidhiwa mwanamke huyo mchawi na yeye Imam akaenda kumkabidhi kwa Chifu wa eneo la Gambaga kwa makubaliano kuwa Imam na Chifu wa Gambaga wangeshirikiana kuwabadili wanawake hao wachawi ili wawe raia wa kawaida.

Chifu wa Gambaga, maarufu kama Gambarana ili kutambua kama kweli mwanamke anayeshukiwa kuwa mchawi ni mchawi kweli au ni uzushi, huchinja kuku na kuangalia namna ambavyo kuku huyo anakufa. Kuna namna ambayo kuku akifa basi ujue mwanamke husika ni mchawi kweli na namna nyingine ya kufa kwa kuku ambayo huashiria kuwa mwanamke husika amezushiwa tuu.

Kuna sababu za tofauti kwanini wanawake hao hushukiwa kuwa ni wachachi, wengine huambiwa ni wachawi kwa sababu tuu  eti waliongea na mtu kisha baadae huyo mtu akaanza kuumwa, au tuu mwanamke husika ni muongeaji sana. Wengine ni kwa sababu tuu wameonekana katika ndoto usiku. Wengine uchawi wao ni kwakuwa ni wanawake wazee au vikongwe, na kwamba wanaishi peke yao kwa kuwa ni wajane au watoto wao wameenda kuishi mbali zaidi nao. 

Cha kusikitisha zaidi ni kuwa hata watu wa familia moja au ukoo mmoja huweza kumshuku ndugu yao uchawi na kisha kuamua kumuadhibu kwa kipigo kikali. Wanawake wanaobahatika kuepuka kipigo, ndio ambao hukimbilia kwa Chifu Gambarana huko Gambaga.

Baadhi ya ndugu wa wamama hao waishio katika kambi ya Gambaga kwa kuona aibu ya ndugu zao kuwa kwenye hiyo kambi ya wachawi, huamua kuenda kuwachukua ndugu zao na kwenda kuwaua kimya kimya ili kuondokana na ‘aibu’ ya uchawi katika familia au ukoo.

Makala hii imeandikwa kwa uchambuzi toka website mbalimbali, na video ifuatayo iliyoshinda tuzo ya Documentary bora kuhusu ukatili wa wanawake katika tuzo za Black International Film Festival za mwaka 2010.
Share:

0 comments:

Post a Comment