Pengine wewe ni mfugaji, au tuseme una ujuzi fulani mfano kupendezesha watu saluni au kutengeneza mavazi , na labda ushajaribu kufanya hicho kitu unachokipenda lakini haujaona matokeo ya kukuridhisha. Basi makala hii inakuhusu wewe na wengine wote wa aina yako ambao wanataka kuingia katika ulimwengu wa biashara ila wanatatizika kwa kukosa elimu sahihi ya ujasiriamali.
Ili ulifanye wazo lako liwe biashara kweli itakayokulipa na itakayodumu kwa muda mrefu kumbuka yafuatayo:
Dhamiria haswa kujiingiza katika hilo jambo:
Kama wewe mwenyewe una wazo tuu na unafanya kama vile kujaribu ila hauna uhakika bado kama kweli hicho ndicho kitu unachotaka kufanya basi jirekebishe. Biashara inahitaji kujituma kweli kweli na kukabiliana na mapito magumu. Hata hao waliopata mafanikio si kwamba siku zote yatakua sawa. Angalia mpira wa miguu hata wachezaji wenye uwezo mkubwa sana kama vile Messi na Ronaldo sio kwamba kila shuti wanalopiga golini huwa wanafunga. Ila kwakua wamejizatiti kushindana na kutaka kushinda, ndio maana mara nyingi hutoka uwanjani na wakiwa wamefunga goli walau moja.
Amua mapema una lengo la kupata zaidi ya fedha
Ni kweli kuwa biashara ina raha pale unapoingiza fedha, lakini ukiingia katika kufanya biashara kwa lengo tuu la kupata fedha, tena wengine hujiwekea kabisa eti nataka nipige zangu kama milioni ishirini hivi halafu nifanye kitu kingine, huko si kufanya biashara bali ni kuganga njaa. Elewa biashara ni kama mtoto wako anayezaliwa. Inabidi uifikirie biashara yako kama kiumbe ambacho kitahitaji kuwa na maisha yake. Ukipangie namna gani kitakua, namna gani kitapata mahitaji yake, na wewe kama mzazi utakua unanufaika humo humo lakini heshimu uwepo wa biashara yako kama kitu kinachojitegemea. Sio kwamba eti biashara yako uichukulie kama ndio tiketi yako ya kufanya mambo yako unayotamani wewe, halafu usiiwazie biashara mema.
Hicho ndicho kinachowakuta wengi wasiofikiria vema kwamba biashara ni zaidi ya fedha, matokeo yake ni kula mtaji kwa kutumia fedha za biashara kwa mambo yao binafsi kama kujenga nyumba au kulipa madeni binafsi.
Usikubali kubabaisha babaisha mambo
Kama unaamini katika wazo lako na umeamua kweli kuitengeneza biashara yako ifike mahali pazuri basi jua kuna gharama za msingi lazima utaingia. Tukirudi kwa mfano wetu wa biashara yako kama mtoto wako, jinsi utakavyoingia gharama kubwa katika kumkuza ndivyo utakavyoongeza fursa za kufanikiwa kwake. Mfano mtoto aliyeenda international school ataweza English haraka zaidi kuliko aliyepelekwa shule za uswahili .
Hivyo basi na wewe usitafute njia za mkato katika kuboresha biashara yako. Kama inakubidi kuingia gharama fulani, basi ingia gharama mfano kumlipa mtaalamu wa mambo ya marketing na mambo ya uhasibu ili akupangilia muundo ulionyooka wa biashara yako kifedha na kimarketing ufanye hivyo.
Usiwe na chanzo kimoja cha mapato
Unaweza kuwa kweli na lengo la kufanya biashara kubwa ila matatizo ya kifedha ya kifamilia yakakurudisha nyuma kwani inaweza kukubidi utumie fedha za biashara kufanya matumizi binafsi. Hata kama hautosumbuka na mambo ya kifamilia , bado utambue kuwa biashara si jambo lililonyooka. Sio kwamba siku zote utakua na mafanikio. Hivyo basi jitahidi sana uwe na vyanzo tofauti tofauti ili uweze kuisaidia biashara yako pale itakapoyumba kujiendesha yenyewe kama yenyewe.
Uwe na watu wa karibu wanaoelewa vema mwelekeo wa biashara
Hapa nazungumzia washirika wengine ambao mtaanzisha nao na kuendeleza biashara waelewe vema muelekeo wenu upo vipi. Pia jitahidi upate na wafanyakazi au wasaidizi ambao kweli wana sifa za kuzalisha na kutenda shughuli nyingine za biashara kiufanisi.
Narudia tena, usikubali njia za mkato ukaajiri watu ili mradi tuu. Na usikubali kuwa mbabaishaji wewe mwenyewe kwani wateja na watu ambao utafanya nao kazi wataliona hilo na hivyo nao kutoipa kipaumbele biashara yako.
Uutafute mzani sahihi wa shughuli zote za msingi za biashara yako
Usijikite tuu kwenye kutengeneza bidhaa bora, ukasahau kutafuta wateja. Au ukatafuta wateja halafu bidhaa zisiwe bora. Au ukayafanya vizuri hayo mambo ya wateja na bidhaa ila ukazembea katika kuwajali watendaji wako na mambo ya usimamizi wa fedha.
Mfano haitopendeza uanze kuingiza fedha nzuri ila watendaji wanaokusaidia kuingiza hizo fedha hauwalipi kwa kiwango cha kuridhisha. Hata kama watu hawatokukuambia itafika wakati utajikuta upo matatani kwani watu wana kikomo cha uvumilivu.
Ufanye nini sasa ili uanze biashara na ukuze biashara ?
Hayo maelezo ni ya jumla ili kukuamsha na kukutia moyo wewe mwenye ndoto ya ujasiriamali. Karibu tuzungumze upate ushauri makini unaoendana na wewe mwenyewe na wazo lako la biashara. Tutakusaidia kuchambua wazo la biashara, sisi ni wataalamu wa masoko na mambo ya fedha, hivyo tutakusaidia kupanga mchanganuo wa biashara vema kabisa, na utapata mbinu za kukuza biashara yako hatua kwa hatua.Tuwasiliane kwa WhatsApp +57 301 297 1724 au email: john.myungire@gmail.com
0 comments:
Post a Comment