MUDA MUAFAKA WA KUANDIKISHA KAMPUNI TANZANIA NA JINSI YA KUANDIKISHA

Picha na BRELA.
Una wazo la biashara, una ndoto ya kufanya mambo makubwa. Unataka kuanzisha biashara ya ukweli au tayari unayo biashara na unafikiria kupanua zaidi biashara yako na wazo linalokujia ni kuwa na kampuni. Kabla ya kuanza kufikiria kuandikisha kampuni tilia maanani yafuatayo.

Gharama kabla ya kuandikisha kampuni
Ili kuandikisha kampuni unahitaji nyaraka fulani za kisheria ziitwazo Memorandum and Articles of Association.  Nyaraka hizi hueleza madhumuni ya kampuni , na kanuni za jumla za uendeshaji wa kampuni kama vile nani anafaa kuwa mkurugenzi wa kampuni , vikao vya kampuni, mgawanyo wa hisa za kampuni, muongozo kuhusu mikopo ya kampuni, n.k.
Kwakuwa hizi ni nyaraka za kisheria unahitaji muongozo wa mwanasheria wa jinsi ya kuandikisha. Hivyo utaingia gharama za kumpata mwanasheria wa kukufanyia hivyo.

Gharama za kuandikisha kampuni
Unahitaji si chini ya Tshs. 177200  kama gharama za kuandikisha kampuni kwa wakala wa usajili  wa biashara -BRELA.
Yaani : Gharama kuendana na kiasi cha mtaji wa biashara Tshs. 95000
Kuingiza masijala taarifa za kampuni yako Tshs.  66000
Ushuru wa nyaraka za mikataba ya kampuni (Memorandum and Articles of association) stamp kwa  kila nakala ni 5000 hivyo kwakua unahitaji walau nakala 3 basi jumla ni 15000
Ushuru wa stamp kwa fomu maalum fomu 14b Tshs. 1200
Jumla Tshs. 177200.

Hata hivyo hii ni gharama ya chini kabisa ya kusajili kampuni na BRELA kwani katika hela niliyotaja hapo juu tumechukulia kuwa kampuni utakayosajili utasema kuwa mtaji wake hautazidi Tshs. Milioni moja ndio maana utalipia tshs.95000.
Hata hivyo mtaji wa milioni moja hautoshi kufanya mambo mengi ya kampuni hivyo jiandae kulipa Tshs. 175000 kama mtaji wako utakua zaidi ya milioni moja  hadi milioni 5. Na ikizidi hapo ni kama ifutavyo:
Mtaji wa zaidi ya milioni 5 ila usizidi Tshs. milioni 20… kuandikisha tuu mtaji ni Tshs. 260000. Katika hii jumlisha hizo gharama nyingine za ushuru na kuweka taarifa masijala ya BRELA kama ilivyooredheshwa hapo juu.
Mtaji wa zaidi ya Tshs.  milioni 20 ila usizidi milioni 50… kuandikisha tuu mtaji ni 290000. Katika hii jumlisha hizo gharama nyingine za ushuru na kuweka taarifa masijala ya BRELA kama ilivyooredheshwa hapo juu.
Mtaji ukiwa zaidi ya Tshs. milioni 50 kuandikisha tuu mtaji ni Tshs.  440000. Katika hii jumlisha hizo gharama nyingine za ushuru na kuweka taarifa masijala ya BRELA kama ilivyooredheshwa hapo juu.

Kucheki  mchanganuo huo hapo juu kwa website ya BRELA  bofya hapa.

Gharama baada ya kuandikisha kampuni                  
Ukifanikiwa kuandikisha kampuni utapewa cheti cha uandikishaji wa kampuni , ambacho ni kama vile cheti cha kuzaliwa cha mtu hai. Kampuni inatambuliwa kisheria kama “mtu” anayejitegemea. Hata hivyo kama walivyo watu wengine wowote, ili kufanya biashara unahitaji leseni. Hivyo itabidi kutafuta leseni kwa KILA AINA YA BIASHARA unayotaka kufanya. Yaani kama unataka kuuza vileo, basi uwasilishe maombi ya vileo.
Ukitaka kuongeza biashara nyingine nayo pia inahitaji leseni. Hivyo ingawa ni kweli kua kampuni inaweza kuwa na biashara hata mia, ila kila biashara ni lazima iwe na leseni yake ya biashara.
Unahitajika kulipia leseni na  kutegemeana na aina ya leseni unayohitaji, inawezekana ukahitajika kutimiza masharti fulani ya kupata leseni husika hivyo utahitajika kuingia gharama za kufanikisha kutimiza hayo masharti.
Kabla ya kupata leseni, unahitaji kuandikisha kampuni yako kama mlipa kodi na kupewa namba ya utambulisho wa mlipa kodi –TIN.   Cheti cha TIN hutolewa bure, hata hivyo ,  itabidi kufanya makadirio ya kodi ya awali ya kampuni , na kulipa hiyo kodi kabla ya kukabidhiwa hiyo TIN.
Malipo ya kodi inategemea na aina ya biashara, mahali ilipo biashara yako n.k.
Kisheria kila kampuni inahitajika kuwa na ofisi. 
Hivyo utahitajika kuwa na ofisi, na kutegemeana na ukubwa wa ofisi na mahali ofisi ilipo itakupasa uingie gharama fulani ya pango.
Kila kampuni inahitajika kuwasilisha taarifa  maalum kwa BRELA kila mwaka. Taarifa hiyo inaitwa Annual Returns. Na kwa mujibu wa website ya BRELA, malipo ya Annual Returns ni Tshs.22000/=

Wakati gani ni sahihi kuwa na kampuni ?
Sababu kubwa ambayo watu hutoa kwanini wanaandikisha makampuni ni kwakua wanadai ni rahisi zaidi kupata tenda ukiwa na kampuni kuliko ukifanya biashara kama mtu binafsi.
Ingawaje ni kweli kampuni zina nafasi kubwa kuaminika kwakuwa ni limited liability, hata hivyo kuna masharti mengi ya aina gani ya kampuni inaweza walau kushiriki katika mchakato wa tenda. Mfano utahitajika uthibitisho kuwa kampuni ina usajili wa mlipa kodi – yaani kuwa na TIN, na uthibitisho kuwa imelipa kodi- Tax Clearance. Na wakati mwingine inaweza kuhitajika hadi Annual Returns.
Kwa maana rahisi ni kuwa kama unapanga kuwa na kampuni kwa malengo ya kuwa upate tenda kwa urahisi , basi hakikisha kuwa mbali ni kuisajili hiyo kampuni, una uwezo wa kugharimia gharama zote za kuifanya iendane na mahitaji yote ya nyaraka za kisheria, na taarifa za kiuongozi.
Hitimisho
Watu wengi husema hivyo kuwa eti watu hawapendi kufanya kazi na watu binafsi hivyo wanahitaji kufanya na makampuni. Hata hivyo, embu fikiria kama unakuwa na kampuni ambayo haifanyi kazi kama inavyohitajika , basi ni kama tuu hauna kampuni. 
Mfano kama wanataka kampuni ziwasilishe maombi ya tenda, basi watahitaji documents ambazo kwa kuwa una kampuni tuu ili mradi kampuni kwakuwa hauna mtaji wa kutosha kuunda kampuni kama inavyohitajika na pia kuwa na mtaji wa kuendesha biashara bora, maana yake kampuni yako haitakuwa kampuni ambayo itaaminika na kupewa tenda.
Ni muhimu basi kama una wazo la biashara na unataka kuanza biashara, tumia fedha zako kwanza katika kujaribu biashara husika, wekeza Zaidi katika gharama za kutengeneza au kuwa na bidhaa zenye ubora , na pia tumia fedha za kutosha kujitangaza . Hapo baadae utakapokuwa na uhakika kuwa biashara inalipa na una mtaji wa kutosha kulipia gharama zote za kuirasimisha biashara yako kama kampuni ndio ufanye hivyo.

NB: Huwa nasaidia watu katika mchakato mzima wa kuandikisha kampuni , toka kuandaa document zinazohitajika hadi ushauri wa namna ya kuongoza kamuni. Kama unahitaji muongozo binafsi wa namna ya kuandikisha kampuni, wasiliana nami kwa whatsapp +57 301 297 1724
Share:

4 comments:

  1. Inachukua mda gan mpka kukamilka usajil huo

    ReplyDelete
  2. +57 301 297 1724 hii namba pia km ipo nyingne unayotumia iweke tu maana hyo siioni whatsup

    ReplyDelete
  3. Thanks for sharing, nice post! Post really provice useful information!

    FadoExpress là một trong những top công ty vận chuyển hàng hóa quốc tế hàng đầu chuyên vận chuyển, chuyển phát nhanh siêu tốc đi khắp thế giới, nổi bật là dịch vụ gửi hàng đi đài loan uy tín, giá rẻ

    ReplyDelete