JINSI YA KUTUMIA RASILIMALI CHACHE KUPATA MAKUBWA MAISHANI ?

Bila shaka unatamani kujiona ukipiga hatua kufika mbali. Na pengine wewe ni kama mamilioni ya watu wanaojirudisha nyuma wao wenyewe kwa kujiambia kuwa hawawezi kwakuwa wana mapungufu fulani au hawana rasilimali fulani.
Hata hivyo umesikia pia kuwa ni muhimu kuanza na ulicho nacho kabla ya kusubiria kupata hizo rasilimali unazodhani unazihitaji ili “utoke”. Utafanyaje katika kutumia rasilimali ndogo ulizo nazo ?Unahitaji kufanya maamuzi yenye manufaa kila mara unapotumia rasilimali zako , hii inajumuisha pia namna unavyotumia muda.  
Dhumuni la makala hii basi ni kukupa mwanga wa jinsi ya kufanya maamuzi yenye manufaa ili ufaidike na kupiga hatua kubwa hata katika upungufu wa rasilimali ulizonazo.

Maana ya gharama
Neno gharama sio tuu kutoa fedha, ila gharama ni chochote unachohitaji kukitoa ili upate unachohitaji. Hivyo mfano basi kama ili kupata soda unahitaji kulipa elf mbili, maana yake ni kuwa itabidi unahitaji kutoa elfu mbili ili kupata soda. Ingeweza pia kuwa ili kupata soda unahitaji kutoa shati , hivyo bei ya soda au gharama ya soda katika hali hiyo ingekuwa ni shati.

Wasemavyo wachumi kuhusu kufanya maamuzi
Wataalamu wa uchumi wametupatia kanuni nzuri sana ya jinsi ya kufanya maamuzi. Kanuni hiyo wanaiita gharama ya kuwa na nafasi ya kufanya hicho unachotaka kufanya (kwa kizungu opportunity cost).
Ipo hivi: 
Kurahisisha kuelewa hii kanuni chukulia kua una vitu viwili tuu unavyohitaji kufanya na hakuna jinsi ya kufanya vyote kwa pamoja kwa kutumia rasilimali zilizopo. Hapa kumbuka kuwa hata muda ni rasilimali.  
Tuchukulie hivyo vitu viwili ni kuangalia TV kipindi ukipendacho cha michezo, na kitu kingine ni kusoma makala fulani itakayokuelemisha na kukuongezea maarifa fulani.
Ukiamua kusoma hiyo makala , maana yake unaacha kuangalia TV kwa muda huo. Hivyo basi unapata nafasi ya kusoma kwa kugharimia  kuangalia TV.  
Yaani gharama ya kusoma kwako ni kuangalia TV.

Muongozo wa kufanya maamuzi  yenye faida
Kiuhasibu :Faida = Mapato – Gharama
Tukichukulia muongozo huu tujiulize jee ni wakati gani basi maamuzi ya uchaguzi wa lipi la kufanya yatakuwa maamuzi ya faida ?
Bila shaka maamuzi ya faida kwakutumia kanuni ya kiuchumi tuliyosoma hapo juu ni kuwa , ni pale ambapo gharama ya kupata nafasi ya kufanya hilo unalotaka kufanya ni ndugu kuliko hilo unalofanya.  Kwa maana rahisi ni kuwa kama ukijiuliza je lipi kati ya unalotaka kufanya na lile au yale unayohitaji kuacha kufanya , lipi kati ya hayo lina athari zaidi kwako kama likiachwa kufanywa kwa muda huo unaohitaji kufanya.  Kama ukifanya jambo ambalo halina athari sana kuliacha, ukafanya ambalo lina athari kubwa endapo litaachwa basi , hapo unafanya maamuzi yenye faida. Kinyume cha hapo maamuzi yako ni ya hasara.

Mfano halisi wa kufanya maamuzi yenye faida
Tufanye majumuisho ya mada hii kwa kuchulia mfano rahisi  wa maamuzi.
Mfano wa kwanza :
Unahitaji masaa mawili kusoma mada fulani ambayo itakupa mwanga na kuboresha uwezo wako pengine wa kufikiri, au wa kishule , kijamii n.k. Wakati huo huo unahitaji kuutumia muda huo kuangalia TV kipindi ukipendacho cha muziki kama kiburudisho.
Katika hali hii:
Gharama ya kuangalia TV ni kuacha kusoma
Gharama ya kusoma ni kuacha kuangalia TV.
Bila shaka kuacha kuangalia TV ukasoma hauingii sana gharama, kuliko kinyume cha hapo yaani kuacha kusoma badala yake uangalie TV.  Kwani kuacha kusoma kunakufanya uwe hatua kadhaa nyuma katika kujiletea ufahamu ambao utaboresha maisha yako, hata hivyo kuacha kuangalia TV hakukunguzii kitu zaidi tuu ya ‘kupitwa’ na burudani.  Kitu ambacho unaweza kufanya wakati wowote kwa muda wa ziada.

Hitimisho:
Kama ulivyoona hapo juu ili kuweza kufanya maamuzi sahihi ni muhimu kufanya ulinganifu wa yale unayochagua kuyafanya na yale ambayo unaacha kuyafanya. Hivyo basi hakikisha mara  kwa mara unakuwa na orodha ya mambo ya kuamua kufanya.  
Orodhesha kwa maandishi mambo yote unayotakiwa kuyafanyia maamuzi , na uyapangilie kuendana na “hasara” ya kutofanya, ukiweka yale ambayo yana mbele yale ambayo yana hasara kubwa endapo hautoyafanya kwanza, kisha kuhitimisha na yale ambayo hayana hasara kubwa kuyaacha kuyafanya kwanza.
Mpangilio huu wa maamuzi sio tuu kwa mambo unayotaka kununua, zingatia mpango huu hata katika namna unavyotaka kutumia muda wako. 
Mfano jiulize ipi ina faida zaidi kutumia muda wako kwa Facebook ukisoma posts za marafiki na kupost vitu visivyo na msingi, au utumie muda huo kufanya yale ambayo haswa yatakuingizia kitu cha msingi katika maisha yako. Kwani pengine ni wewe huyo huyo unayesema hauna muda wa kutosha kufanya mambo ya msingi, au hauna internet ya kukuwezesha kutumia rasilimali nyingine kibao zilizopo mtandaoni.



Share:

0 comments:

Post a Comment