KANUNI 3 ZA MSINGI ZA MAWASILIANO SAHIHI NDANI YA FACEBOOK NA WHATSAPP

Je ulijifunzaje kutumia Facebook na WhatsApp? Wengi wetu tumejikuta tuu bila maelekezo maalum ya mtu yeyote tumejifundisha kutumia mitandao ya kijamii, na pengine tulipokwama kidogo ndio tuliuliza kwa watu walio karibu yetu.
Kutokujifunza vema kutumia mitandao ya kijamii , na ukichanganya na ukweli kuwa watu wengi hawana ujuzi wa kutosha wa mawasiliano yenye tija –effective communication, basi mitandao hii ya kijamii imekua ikidumaza uwezo wetu wa kujenga mahusiano endelevu na yenye manufaa na watu wengi.
Makala hii inakupa kanuni tatu za msingi katika kutumia Facebook na WhatsApp ili uwezo kujenga mahusiano bora badala ya kubomoa. Kumbuka anayekupatia muda wake ili wakati mnafanya mawasiliano katika mitandao ya kijamii anakupa jambo la msingi sana, kwani maisha ni muda, hivyo tumia muda huo wa mawasiliano vema kwa kufuata kanuni hizi.

1. Matumizi ya viashiria hisia (Emoticons):

Ingawa kuna maana zilizokubalika kwa ujumla za viashiria hisia , bado kuna watu wengi sana hawajui tafsiri yake, hivyo si ajabu ukatumia kialama fulani halafu kikatafsiriwa sivyo na mtu unayewasiliana nae.
Mfano mzuri alama hii hapa chini ya mikono miwili  inaweza kutafsiriwa kama ahsante, wengine kama alama ya kutoa heshima kwa mtu na wakati mwingine mtu anaweza elewa kama vile unaomba kitu.

Kwa mahusiano ya kibiashara, au kikazi au kwa mahusiano na mtu aliyekuzidi umri au mwenye ‘kilemba ‘  cha juu kama vile mkwe, ni bora ufanye mawasiliano yako bila kutumia hivyo vialama vya kuashiria hisia.
Na kama unawasiliana na watu wa rika lako , marafiki au mpenzi hakikisha unafahamu kama wanaelewa au kupenda matumizi ya hivyo vialama, ili  kujiweka katika nafasi ya usalama wa kutofanya mawasiliano ya kuudhi, au kutafsiriwa tofauti.

2. Subira ni muhimu wakati unasubiri majibu ya chat:
Kuna watu wanakera, amekuandikia meseji ukamjibu,ila upo bize , anaanza kukutumia meseji za viulizo na pengine meseji za hasira kuwa mbona upo kimya. Hata kama unamuona mtu yupo hewani, haina maana kuwa basi ni lazima aendeleze mawasiliano nawe bila kupumzika hususani kama mnachozungumza si cha haraka au ulazima.
Hata hivyo kwa mazungumzo rasmi au ya umuhimu sana mfano biashara, au mtu anaomba msaada wa kujibiwa maswali fulani, ni busara kama utajiona upo bize , basi umtaarifu kwani katika aina hii ya mawasiliano, mtu huyo atakuwa akisubiria kwa hamu au haraka majibu yako.
Ila kama ni mawasiliano tuu ya ‘kupoteza muda’ au utani au yasiyo na mada au mpangilio maalum, watu wengi hujibu kwa ‘manati’.

3.Kuwa rafiki kabla ya kuomba msaada: 

Wewe mara kibao ukiwa online hata meseji humuandikii mtu achilia mbali kama ni kwa FB basi hata kulike au kucomment posts za rafiki, na kibaya wengine hata hawajibu meseji walizotumia ingawa Facebook au WhatsApp inaonyesha wazi kuwa uliiona au kuisoma meseji. 
Halafu siku ya siku una shida wewe, ndo unakuja hewani kwa meseji cha kwanza wengine hata salamu hawana , wanataja shida yao. Au wengine salamu huambatana na ombi wanalotaka kutimiziwa.

Watu wengi hupenda kusaidia marafiki, hivyo ingawa ukweli ni kuwa huwezi fanya mawasiliano na marafiki wote ulionao katika Facebook au WhatsApp , jitahidi kabla haujafikiria kuomba msaada wa mtu , basi umemkumbuka siku si nyingi. 
Watu hawapendi kujisikia ‘wakitumiwa’ na wengine. Hata salamu ya mara moja moja inatosha kuonyesha unajali na kuwa unafaa kusaidiwa au kusikilizwa pindi utakapokua na shida.
Share:

1 comment: