Baada ya
makala yangu ndani ya gazeti la Mwananchi la Februari 11, 2016, yenye kichwa
cha habari MBINU ZA UHAKIKA ZA KUPATA AJIRA-1 , nimepokea barua pepe kadhaa za
wasomaji wa gazeti hilo wakipenda kujua zaidi namna ya kupata kuingia katika
soko la ajira endapo kama ndio tuu wametoka vyuoni.
Katika
makala hii naelezea mbinu za kupata ajira mapema mara tuu baada ya kutoka
masomoni.
Ni kweli
kuwa waajiri wengi huhitaji wafanyakazi wenye uzoefu. Hivyo kufahamu namna ya
kupata kazi mara tuu baada ya kutoka chuo huna budi kuelewa kwanini waajiri
wanataka uzoefu na mambo mengine wanayoangalia halafu wewe uwe tayari
kuwashawishi hata kama haujawahi kuajiriwa sehemu fulani.
Maana ya uzoefu wa kazi na kwanini waajiri wanataka uzoefu wa kazi
Waajiri
wengi hutaka kuajiri watu ambao tayari wana uzoefu wa kazi kwa kuwa zoefu wa
kazi unamfanya muombaji kazi awe tayari anaelewa kivitendo:
- Masuala ya msingi ya sehemu za kazi kama vile uwajibikaji, kujieleza, kupangilia maisha yao ili kusiwe na muingiliano wa maisha binafsi na mambo ya kazi
- Matumizi ya vifaa mbalimbali vya kazi kama vile simu, kompyuta, na baadhi ya mashine maalum kwa kazi maalum
- Namna ya kushirikiana kikazi na kufanya mawasiliano na washirika katika sehemu ya kazi kama timu.
- Umuhimu na namna ya kuonyesha huduma kwa mteja
- Namna ya kuwajibika katika miradi ya kampuni , na ikibidi kuongoza watu wengine na kuandika ripoti
- Uelewa wa muundo wa usimamizi wa sehemu za kazi na kuheshimu mgawanyiko wa madaraka na namna ya kuwajibika kutegemeana na nafasi yako ya kazi.
- Zaidi sana anaelewa utofauti uliopo kati ya matumizi ya aliyochosomea darasani na namna ufahamu wake unavyoweza kutumika katika ulimwengu halisi, na kwamba anaweza kuhamisha toka zana za darasani kuwa vitendo na anaweza kwa tafakari makini kujua kikomo cha aliyojifunza darasani na nini afanye katika hali halisi anayokumbana nayo kazini.
Baadhi ya mambo
niliyotaja hapo juu pengine umewahi
yasoma darasani kama mambo ya organization structure, communication skills, n.k
ila kuna utofauti kati ya kusoma darasani na kuyaishi katika sehemu halisi ya
kazi.
Unapotoka chuoni unakuwa na
ufahamu wa hayo mambo pamoja na uelewa wa shughuli ya fani yako kama vile
uhasibu, uhandisi, usimamizi wa mifumo ya kompyuta n.k lakini sio haswa haswa
kivitendo.
Je ufanyaje ili umshawishi muajiri kukuajiri
mara tuu baada ya kutoka chuoni ?
Kwakua
muajiri anachotaka ni mtu aliye tayari kutumika katika kuleta uzalishaji katika
kazi na atayeleta mchango katika shughuli husika, basi usitegemee kupata tuu
ajira bila kuweza kumuaminisha kuwa wewe
unafaa katika hilo.
Elewa kuwa
uzoefu wa kazi sio lazima uwe uliajiriwa
katika ajira rasmi kwa miaka kadhaa. Kwa ambao bado mpo vyuoni, mnaweza
kushiriki katika vyama, vikundi au kujitolea kufanya shughuli fulani katika
mazingira ya kazi kama vile asasi zisizo za kiserikali -NGOs au hata katika
makampuni bila malipo.
Pia unaweza
wewe mwenyewe kuanzisha shughuli ukishirikiano na watu wengine , shughuli
ambayo mtajenga mazingira ya kazi mfano kuwa na asasi isiyo ya kiserikali –NGO,
au hata kikundi kisicho rasmi sana lakini chenye shughuli rasmi zinazogusa
utoaji huduma au utengenezaji wa bidhaa fulani.
Shughuli
nilizotaja hapo juu kwa ajili ya wanafunzi zaweza pia kufanya na watu ambao
wamekwisha maliza chuo na hawana uzoefu
wa kazi. Hata kufundisha kunaweza kukuletea uzoefu fulani.
Uwepo wa
teknolojia unakufanya uweze kujishughulisha katika mambo mengi sana ya msingi
ya kukuongezea maarifa na uzoefu wa hicho ulichosomea kiasi kwamba utakapokua
unaandika barua yako ya maombi ya kazi utaweza jieleza kwa ufasaha na kuonyesha
kuwa wewe pamoja na kumaliza tuu chuo, umekomaa tayari kwa kuanza kazi.
Kumaliza
kwako tuu chuo kusikukatishe tamaa kwani una fursa kibao za kujishughulisha nje
ya ajira rasmi kiasi kwamba ukawa na uzoefu au kukaribia uzoefu unaohitajika na
waajiri wengi hivyo ukiwa unaomba kazi ukajieleza uzoefu ulionao.
Kwa wale
mliopo mavyuoni , ni wakati muafaka kabla ya kumaliza chuo kujishughulisha na
shughuli zitakazowaweka karibu na mazingira ya kazi kama nilivyotaja hapo juu.
Hitimisho:
Unahitaji
uzoefu na kuna fursa nyingi za kujipatia uzoefu wa kazi sio lazima katika ajira
rasmi. Ukishajipatia uzoefu kama nilivyoeleza hapo juu, jieleze vema katika
barua yako ya maombi ya kazi.Usiogope kujieleza kwani kujieleza kwako vema ni moja ya viashiria kuwa wewe ni mtu unayejielewa na kujua namna gani unavyoweza kuwa wa msaada kwa muajiri.
Soma pia
makala hii kuhusu namna ya kuandika barua ya maombi ya kazi ili ujue namna ya
kujielezea uzoefu ulio nao. BOFYA HAPA NAMNA YA KUANDIKA BARUA YA MAOMBI YA KAZI
0 comments:
Post a Comment