MBINU RAHISI YA KUJIFUNZA KUJITAMBUA

Tafakari yetu leo inahusu WEWE NI SEHEMU YA MFUMO ?
Karibu kila kilichoumbwa duniani ni sehemu ya kingine , kwa hiyo tuseme hata sisi binadamu ni mfumo. Lakini kabla sijaingia kwa binadamu embu tuangalie mfano rahisi wa MLANGO.

Wewe unapoutazama mlango mara nyingi unaangalia mlango kama mlango pekee lakini, mlango huo hauna maana kama hakuna kuta mbili kushoto na kulia kwake. Huo mlango pia usingekuwepo kama kusingekuwepo ardhi au sakafu hapo chini. Mlango wenyewe tuu umeundwa na vitu vingi kama kitasa au komeo, pia kulihitajika misumali n.k. Hata hivyo wewe bado unapozungumzia mlango akili yako moja kwa moja huangalia tuu Hicho ambacho sote huwa tunasema mlango ila kiukweli MLANGO ni jumla ya vyote vinavyofanya nyumba au chumba chako kijihifadhi kwa kuzuia kuingia kwa urahisi.

Wewe pia tunapokuangalia haraka haraka tunakuona wewe tuu, lakini wewe ni jumla au matokeo ya walezi wako, mke/mume wako, elimu uliyoipata, unachokula na kunywa, marafiki n.k. Ndio maana kama ukiishi eneo tofauti, ukawa na marafiki tofauti, ukapata elimu tofauti , ukawa na mpenzi/mke/mume tofauti, pengine wewe wa leo sio yule utakayekuwa wa wakati ujao.

--Kwa nini nimeleta tafakari hii ? Ni kwa sababu kama ukijitambua kuwa wewe ni sehemu ya MFUMO basi utajitahidi kuangalia namna vingine vinavyounda mfumo vinavyosababisha wewe kuwa hivyo ulivyo. 
Pengine ni aina ya mambo unayojifunza, aina ya siasa unayofuata, yale unayosoma na kuamini, pengine ni aina ya marafiki ulio nao, pengine ni mazingira unayoishi, n.k. 
Je kwa kiwango gani upo makini na kuvitumia vitu vingine au watu wengine katika mfumo wako ili uwe mtu bora zaidi ? 
Tafakari , chukua hatua ya KUJITAMBUA ZAIDI.
Share:

0 comments:

Post a Comment