Wajasiriamali ni watu muhimu sana katika jamii, kwa sababu nyingi kama
vile kuongeza ajira, kuongeza bidhaa na huduma, kuboresha maisha ya watu
kupitia bidhaa na ajira n.k. Mjasiriamali ni mtu mwenye kuthubutu
kuanzisha shughuli ya uzalishaji, kuboresha utendaji wa namna fulani.
Wajasiriamali huamini katika 'ndoto' zao , na hukubali kujishughulisha
kwa shughuli zozote wanazodhani zitapelekea 'ndoto' zao kufanikiwa, huku
wakiamini pia kuna uwezekano wa wanayoyafanya yasifanikiwe. Hata hivyo
hatari hiyo ya kutokufanikiwa, haiwafanyi kuacha wanayolazimika kufanya.
Makala hii inadokeza mambo unayoweza kufanya kwa ajili ya mtoto ili kumuandaa mtoto kuja kuwa mjasiriamali.
1. Kujifunza 'kutengeneza' fedha: Msaidiie
mtoto kadri anavyokua na kupata ufahamu wa kutosha awe na utamaduni wa
kujiingizia kipato. Mfano unaweza kumpa kazi ambazo akifanya kwa kiwango
mnachokubaliana unamlipa fedha. Muweze pia kushiriki shughuli ndogo
ndogo za ujasiriamali kama vile kukaa dukani (kama mna duka), kupeleka
bidhaa kwa wateja wako, n.k Hii itamsaidia kujenga ufahamu kuwa fedha
inapatikana kwa mabadilishano ya bidhaa/huduma na ataanza mapema kujenga
ufahamu wa mbinu, matatizo na michakato ya kijasiriamali. Pengine
vinaweza visimsaidie sana akiwa mtoto, ila kadri anavyokuwa, ataweza
kuunganisha 'uzoefu' wake.
2.Nidhamu ya fedha: Mtoto
anapaswa kuelimishwa kuhusu matumizi ya fedha, ajue na kuweka akiba. Pia
kwa nidhamu ya fedha, inapasa mtoto asizoeshwe kupewa fedha kirahisi
rahisi, kwani hii haimjengi kufikiria kuhusu 'kutengeneza' fedha, badala
yake anazoea 'kudaka', hivyo kumuandaa kuwa muajiriwa wa kudumu.
3. Ulimwengu wa biashara:
Ni vizuri kumpatia mtoto ufahamu wa mambo yanavyoenda katika ulimwengu
wa biashara, mfano aone vile unavyojadili bei, ajifunze kuhusu huduma
kwa wateja, na unapoona hayo unakuwa unampa maelekezo mtoto. Mfano,
unapokuwa naye na ukapatiwa huduma mbaya toka kwa mfanyabiashara fulani,
mueleze mtoto kuwa hivyo sivyo sahihi katika ulimwengu wa biashara.
Muweze mtoto kutembelea maeneo ya uzalishaji kama vile viwandani.
We are what we repeatedly do.- Aristotle
Sisi huwa vile ambavyo mara nyingi tumezoea kufanya.
4. Chochea ubunifu wake:
Watoto karibu wote wana aina fulani za ubunifu. Msome mtoto wako, na
mpe moyo kwa kila jambo analofanya la ubunifu. Mfanye atambue kuwa
unamuamini, na pia mueleze kuwa anaweza kufanya lolote analodhani
anataka kufanya la kiubunifu. Msaidie ikibidi kununua vifaa, kumpeleka
safari mbalimbali, n.k ili mradi awe huru kubuni. Hapa unamjengea uwezo
wa kujiamini.
Imagination is more important than knowledge.-Albert Einstein
Kufikiria/mawazo ni bora kuliko ufahamu
5. Mawasiliano na mtoto: Watoto wanatabia ya
kuamini zaidi wazazi au walezi wao. Hivyo una nafasi kubwa ya kumjenga
mtoto kuwa mjasiriamali kwa kufanya nae mazungumzo ya mara kwa mara.
Mfundishe kuwa na mikakati. Muulize anapenda kufanya nini, muulize
anapanga kufanya nini katika muda wake wa mapumziko, n.k. Pamoja na
ugumu wa maisha unaowafanya wazazi na walezi wengi kukosa muda na
watoto, hakikisha unatenga muda kwa ajili yake, kwani wewe ni mchochezi
mkubwa wa namna maisha yake ya baadae yatakavyokuwa.
6. Mwezeshe kujisomea:
Bila kusahau , tambua ubunifu ni nguzo kubwa katika ujasiriamali, na
ili kuwa na ubunifu, mtu anapaswa kuwa na taarifa /ufahamu mkubwa wa
mambo kwani ufahamu huo ndio unamuwezesha kutambua yapi yanawezekana na
yapi hayawezekana, na hapo ndipo anapokuja kuona 'gap' iliyopo ili
kuziba hiyo 'gap'.
Hivyo basi , mjengee mtoto mazoea ya kujisomea. Muwezeshe ajue lugha vema hususani lugha ya kiingereza.
Hitimisho:
Haijalishi
aina gani ya fani mtoto atakuja kufanya kazi hapo baadae, awe
mwanamichezo, mwanasheria, mhandisi, mhasibu, daktari , n.k, uwezo wa
kufikiria kijasiriamali, uwezo wa kutaka kuzalisha zaidi, ni muhimu
kwake na kwa jamii. Na zaidi sana, ajira atakayopata hapo baadae
itamsaidia kujiingizia kipato ambacho kitamuwezesha kukusanya mtaji wa
kujiajiri.
Kuna msemo mzuri toka kwa Peter F. Drucker:
“This defines entrepreneur and entrepreneurship - the entrepreneur always searches for change, responds to it, and exploits it as an opportunity.”
Hivyo kumsaidia mtoto kuwa mjasiriamali kuna faida kubwa zaidi kuliko kumuacha hivyohivyo. Anza sasa.
0 comments:
Post a Comment