SABABU 7 KWANINI UENDELEE KUAJIRIWA BADALA YA KUJIAJIRI

1.Hauna Wateja Makini: Unashidwa kueleza kwa ufasaha wateja unaolenga hasa ni akina nani-yaani ni kundi gani la watu, na kwanini watu hao watanunua bidhaa yako. Haitoshi tuu kusema kwa mfano, utaanzisha kampuni ya mambo ya IT, au Advertising, lakini hauna maelezo ya kina akina nani hasa watanunua bidhaa unazotaka kuuza. Haitoshi kusema kwa mfano, “wateja wangu ni watu wote na asasi zinazohitaji huduma za IT, au Advertising,  inabidi uwe na uchambuzi wa kina aina gani ya watu na asasi zinazoweza kweli kuhitaji bidhaa zako, na kwanini unadhani watakuja kununua bidhaa zako. Kumbuka sio lazima uwe na majina ya asasi au watu unaotazamia waje wanunue kwako, ila kuwa na mtazamo wa kina wa tabia na wasifu wa kipekee wa wateja wako watarajiwa ni jambo la msingi.

2.Hauna Bidhaa Ya Kipekee:  Ili kuhakikisha unapata kipato cha kuridhisha na kuwa na biashara endelevu, inakupasa uwe na bidhaa ya kipekee katika kujiajiri kwako. Kama hauwezi kueleza kwa kifupi walau kwa sentensi tano, upekee wa bidhaa na uendeshaji wa biashara yako, ni dalili kuwa kujiajiri kwako hakutokuwa na tija.

3.Una haraka ya mafanikio:Mtazamo wako mkuu ni kujenga biashara yenye kukua ‘chap chap’, na pengine kwakuwa una mtazamo huu, una amini kuwa namna pekee ya wewe kuanzisha biashara yako ni kuwa kwanza na mtaji mkubwa wa kifedha. Ingawaje ni kweli kuwa fedha nyingi ni muhimu katika kuanzisha na kuendeleza biashara, mtaji mkubwa si wa lazima kwa kila aina ya biashara, na kwanza njia bora ya kuanzisha biashara ni kuanza kidogo kidogo. Hata biashara kubwa kama kampuni ya Apple inayotengeneza simu za iPhone – ilianzia tuu kwenye kachumba kadogo ka gereji, kampuni ya kompyuta ya DELL-inayotengeneza kompyuta aina ya Dell, ilianza kwenye kachumba kadogo ka bweni la chuo, tena kwa mtaji wa $1000 tuu !.

4.Hauna Mtandao wenye tija:Ni wazi kuwa watu watakaotoa mchango mkubwa katika mafanikio ya biashara yako ni wale ambao unamfahamiana nao kwa karibu, kupitia mtandao wako. Haitoshi tuu kufahamiana na watu wengi, bali watu hao wengi wakufahamu pia haswa haswa wakufahamu kwa mazuri na uwezo wako katika mambo makubwa, ni rahisi hapo baadae kupata humo katika mtandao wako, washirika wa biashara, wateja na hata wasambaji wa bidhaa na huduma kwa biashara yako. Na kama inavyosemwa: “ Katika dunia tuliyopo sasa, sio tuu una nini na una jua nini, bali je unamfahamiana na akina nani ?”

5.Hauna mkakati maridhawa wa kifedha:Biashara utakayoianza itahitaji fedha na pia wewe binafsi na familia yako mtahitaji fedha. Kwa kuwa ni muhimu kuweka tofauti mambo ya biashara na mambo yako binafsi, ni unatakiwa uwe na mkakati wa maridhawa wa kifedha wa matumizi na mapato yako binafsi na  yale ya biashara.Hata kama unafikiria kuwa biashara itakuingizia fedha za kujikimu na kusukuma maisha, je mapato kuchukua kwako huko fedha toka kwa biashara kutaathiri vipi mwenendo wa biashara, ambayo ndiyo itakuwa chanzo kikuu cha ajira yako?

6.Hauna Ufahamu wa kutosha kuhusu biashara uitakayo:Ufahamu wa biashara utakayo kuianzisha ni muhimu kwani utakuwezesha kujua kama kweli inalipa au la, na pia kujua mbinu za kuiboresha na kuifanya endelevu kwa siku za usoni. Ufahamu wa kutosha wa biashara utakuwezesha kutafakari pia kwa undani wateja gani hasa unawalenga, washindani gani hasa utakabiliana nao, na pia changamoto na matatizo ya biashara husika kabla haujaingia kuianza.

7.Hauna mvuto wa kutosha kwa biashara uitakayo kuanzisha: Unahitaji kusikia kitu kama wito au mvuto wa kipekee wa kitu unachotaka kukifanya kama biashara ili kweli uweze kukifanya kwa uendelevu , kwani kutakuja nyakati ambapo biashara haitaingiza kipato cha kutosha, utapitia changamoto na matatizo mengi, na wakati huo, kitu kitakachokupa msukumo wa kipekee wa kuendelea na kuwaongoza hata washirika na wafanyakazi wako muendelee na biashara, ni kule kupenda (wito) wako na hiko unachotaka kukifanya kama biashara.
Share:

0 comments:

Post a Comment