Dale Carnegie aliwahi kusema “Kinachokufanya
uwe na furaha Sio kile ulicho nacho, au vile ulivyo, au wapi ulipo, au kipi
unafanya, bali ni vile unavyofikiria kuhusu hayo yote”. Hata hivyo miongoni
mwetu , tumejikuta tuna wakati mgumu wa kujisikia na furaha kwakuwa tumetilia
mkazo kufanya mambo kwa ajili ya kuonekana mbele za wengine.
Haijalishi namna gani ‘unauza sura’-yaani
unatafuta kuonekana kuwa upo ‘juu’ iwe kwa kujibadili jina, kujidai kwa mavazi,
mali kama nyumba au gari, kwa cheo, au kwa watu unaowafahamu, hayo yanaweza
kuashiria upo kwenye mkumbo wa hali hii mbaya ambayo ukiitafakari kwa undani
utagundua kuwa ina chembe chembe za utumwa wa kifikra.
Kuuza sura au kujidai kama ninavyojadili katika
makala hii ni ile hali ya mtu kutaka kuonekana yupo ‘wa hadhi ya juu’ mbele za
wengine, kwa lengo kuu la kutaka tuu kuwa juu kama njia ya kukubalika mbele ya
jamii au kama njia ya ‘kupata heshima’ toka kwa hao anao walenga.
Kuna matendo mengi ambayo mtu anaweza akawa
anatenda akatafsirika kama ‘anauza sura’ ingawa si kweli anauza sura, kwakuwa
hana lengo la kutafuta heshima kama heshima, bali kuna malengo mengine ya ziada
kama vile malengo ya biashara – kutangaza bidhaa, au kujenga jina lake kwa
kutafuta umaarufu n.k.
Kuuza sura tunakokuzungumzia hapa kunaleta
mambo yafuatayo:-
1.Tunasahau nini hasa tunahitaji: Tunapotilia mkazo kujionesha kuwa sisi ni bora zaidi ya wengine
kwa sababu za ‘kujidai’ tunajikuta tunaweka mkazo zaidi katika namna vile
wengine wanategemea sisi tuwe, au tuseme tunaweka mkazo kwenye mambo yanayoonekana
au kukubalika na wengi kuwa ‘ni matawi ya juu’. Hali hii inaweza kutufanya
tusiweke mkazo katika tafakari ya mambo ya msingi ambayo sie wenyewe binafsi
haswa tunahitaji. Mfano, badala ya kutilia mkazo mahitaji ya familia yako ya
sasa, na hapo baadae kama vile elimu, afya n.k unaweza ukawekeza sana kwenye
vitu vya kifahari ili na wewe uonekane upo ‘juu’. Ndio maana si ajabu, kusikia
msanii maarufu aliye ‘tesa’ , akiombewa msaada wa kugharimiwa gharama za
matibabu! Au kijana aliyeonekana miezi michache iliyopita ‘akitesa’, sasa
amekuwa ombaomba misaada kwa watu mbalimbali.
2.Tunajiweka katika hali ya kujikataa: Kwa kuwa tayari tumeshakubali kuwa utimilifu wa
furaha yetu ni kuwa ‘juu’ zaidi ya wengine, au kupata hisia kuwa wengine
wanatuona tupo juu, tunajikuta tunajikataa sie wenyewe pale tunapoona kuwa
hatujafikia viwango. Ndio maana si ajabu kusikia mtu akisema anaishi Masaki,
wakati kiukweli kwao ni Tandale. Kwa hali hiyo hiyo, ndio maana si ajabu
kumkuta mtu akipiga picha kwa nguo za kuazima, au kwa namna ya ubora zaidi
itakayo ng’arisha muonekano wake na kuiweka Facebook ili hali, katika muonekano
halisi hayupo hivyo.
3.Akili inapumbazika: Mambo mengi yanayotumika na watu kutafuta kuonekana wapo juu, huwa si mambo halisi, bali ni mambo ya mpito,
ambayo pengine watu hufuata mkumbo na kuyatumia isivyopaswa. Mfano, kuna wakati
watu walitumia Flash Disks, kama kitu cha kuonyesha ‘wapo juu’, wengi walikuwa
wanazibeba bila matumizi, na wakati huo huo, lengo la Flash Disk halikuwa
kuonyesha ‘status’ ya mtu.
Mfano mwingine ni simu za mkononi , kuna wakati
ilikuwa kuwa na simu ya mkononi ni kuwa ‘upo juu’. Hali kadhalika, siku za hivi
karibuni kuwa na gari kumeonekana kama ni jambo la kuuza sura. Cha ajabu zaidi
hata kuweka status na kuwa na likes nako kumechukuliwa kama sehemu ya
kutengeneza ‘heshima’.
Viwango vya elimu pia vimekuwa vikitumika
katika kutafuta ‘status’ wakati ki uhalisia, elimu ina kazi nyingine tofauti na
hiyo ya ‘kutia adabu’ watu wengine. Utakuta kwa mfano, mtu akitafuta digrii, au
Masters au akifanya uchaguzi wa jina la chuo, sio kwa sababu kuu ya manufaa ya
uchaguzi husika bali ni kwa kuangalia namna ambavyo ‘status’ yake itatafsirika, kuwa na yeye
‘yupo juu’.
Wengine huko Facebook, wamefikia hatua ya kuwa
na majina ya ‘ajabu’ kama sehemu pia ya kuleta heshima mbele za wengine- majina
kama DE VOS SHIZO NIZO, na kuweka picha za wasanii mbalimbali ni sehemu pia ya
kuuza sura !!
4.Tunasahau uwezo wetu mkubwa:Kwakuwa tunajikita kwenye kutafuta ‘ujiko’ au ‘heshima’ za bandia, na
kwakuwa tunajisahau kufuatilia mambo haswa ya msingi tunayohitaji katika maisha
yetu, tunasababisha Uwezo wa kuleta mabadiliko tulionao katika dunia hii kuwa
umebanwa na mazingira tuliyonayo. Badala ya kufikiria ‘nje ya boksi’ tunajikuta
mtazamo wetu wa maisha unajikita tuu ndani ya ‘boksi’ tulilomo, yaani ndani ya
mazingira tuliyonayo – kwa kuangalia wenzetu wana nini, wamefanya nini,
wanafikiria nini kuhusu sisi, na wanatarajia nini kuhusu sisi.
Hitimisho:
Makala hii haina lengo la kumaanisha kuwa kuwa
kufanya mambo makubwa na mazuri kwa ajili yako kama vile kununua nguo nzuri,
gari , nyumba , kupiga picha nzuri, kusafiri au kuishi maeneo mazuri ni vibaya,
badala yake inapongeza kufanya mambo kama hayo, kwa manufaa ya mtu binafsi, na
sio kuvutwa na kutaka kuvutia watu wengine.
Mwanasayansi na mwanahistoria Paul Rosenberg wa
Freemanperspective.comkatika makala
yake ya The contentment Revolution anasema:kuwa bora kwako si lazima
kuwe na maana wengine wapo chini yako. Rosenberg anaendelea
kusema kuwa kama tutajitahidi kufanya mambo kwa sababu yanatupendeza sisi,
tukawaza zaidi nini tunahitaji basi ni wazi tutajikuta tunapunguza machungu
yasiyo ya lazima ( mfano, machungu ya kujisikia upo chini ya watu wengine), na
hata kupunguza hasara ya fedha, muda na mambo mengine tunayopoteza ili tuu
kuwafanya watu wengine watuone kuwa eti sie tupo juu!.
Nimalizie kwa nukuu hii:
“Usiharibu kile ulichonacho, kwa kutaka kile usicho nacho”. Epicurus“Do not destroy what you have, by desiring what you don’t have”. Epicurus
0 comments:
Post a Comment