Ninaamini kuwa lengo la mwanzilishi wa biashara lina nafasi
kubwa sana katika ku ‘shape’ biashara husika itakavyokuwa, kwakuwa lengo hili ndio huweka picha ya akilini vile
mtu alivyo tayari kujitoa kwa ajili ya biashara yake : wateja wake, wafanyakazi
na uzalishaji wa bidhaa.
Makala hii inachambua aina kuu nne (4) za malengo ambayo
watu huwa nayo wanapoanzisha biashara:-
1. Kuongeza kipato cha ziada: Wenye lengo hili pekee hujikita kwenye
kuanzisha biashara hususani biashara za msimu, ili mradi kipato kipatikane.
Mara nyingi huwa hawana mchanganuo wa kina wa biashara husika, na hawajali
mambo ya msingi katika usimamizi wa biashara kama vile kuboresha huduma,
kuboresha teknolojia wanazotumia katika biashara husika, kuwa na wafanyakazi
wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha.
Kwa wenye lengo kuu la kuongeza kipato cha
ziada tuu, biashara zao ni jambo la ziada kwao kwani hujikuta wakitegemea mambo
mengine kama vile ajira, kipato cha familia, au biashara nyingine.
2. Biashara kama Ajira mbadala: Wenye
lengo hili huchukua muda mrefu kupanga jinsi ya kuanzisha biashara husika, na
huweka msisitizo kwenye kipato. Ni wachaguzi sana wa aina ya biashara watakayoanzisha,
mara nyingi biashara zao sio za msimu.
Wajasiriamali wa lengo hili, hutazama
zaidi kujenga mtandao kama sehemu muhimu katika kufanikisha biashara zao. Kwa
watu wenye lengo hili, la msingi kwao ni kuendelea kuwepo katika biashara hata
ikibidi kupata faida ndogo au kupoteza wateja wa aina fulani.
Wana matazamio ya
kukuza biashara zao, hata hivyo hukumbwa na tatizo la mtaji na ukosefu wa uzoefu
katika biashara husika.
Ni wagumu kuamini watu wengine (hususani wafanyakazi wa
biashara zao), hivyo hujikuta wanahodhi madaraka yote. Hii inaweza kuchelewesha
ukuaji wa biashara zao. Hata hivyo wanapofanikiwa kuongeza mtaji wa biashara
zao, ni rahisi kwao kuboresha biashara na kupunguza kuhodhi madaraka.
3. Kuonyesha ufahari wa kumiliki biashara:
Wenye lengo hili mara nyingi hufuata
mkumbo wa muelekeo wa biashara
zinazoonekana kuwa ‘mahiri’ ili waweze ‘kuuza sura’.
Hawafanyi uchambuzi wa
kutosha wa biashara wanazotaka kufanya, na si wabahiri katika kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha
ili mradi tuu biashara itajenga na kulinda heshima wanayotaka kuwa nayo.
Wajasiriamali wa namna hii si watendaji wa kila siku wa shughuli za biashara,
hata hivyo hupenda kupata taarifa za mara kwa mara za biashara husika ili nao
waweze jidai kwa kundi ambalo wapo.
Hujali zaidi muonekano wa nje wa biashara
kama vile mazingira ya ofisi, vifaa vya kazi, magari n.k, kuliko ubora wa
wafanyakazi na kuwaendeleza wafanyakazi.
Pamoja na kuwa si wabahiri katika
kuwekeza katika vitu vinavyoboresha muonekano wa biashara zao, watu hawa wengi
wao huwa wabahiri katika kulipa mishahara mizuri kwa wafanyakazi wao, na
hawapendi kuona wafanyakazi wakibadilika kimaendeleo.
4. Biashara kama urithi wa baadae: Kwa
wengine lengo la kuanzisha na kufanya
biashara ni mchanganyiko wa mambo mawili makuu ambayo ni kutoa mchango kwa
jamii na kuboresha hifadhi yao ya mali na fedha. Kwa watu hawa malengo ya muda
mrefu ni jambo la msingi sana.
Pia wapo tayari kujifunza na kujaribu mambo mapya.
Wanathamini wafanyakazi wao kuwa ni washirika katika kufikia lengo wanalotaka la
kujenga kitu kikubwa katika jamii.
Biashara kwao sio tuu kuuza bidhaa ili
waingize fedha, bali ni kuuza bidhaa zenye kuleta kukidhi mahitaji ya mteja.
Watu wenye lengo hili kwa kutambua kuwa wateja ndio washirika wao wa kuduma,
hujitahidi sana kuwekeza katika mahusiano bora na wateja wao. Hii inajumuisha
kujifunza maisha ya wateja, mabadiliko katika maisha ya wateja, kusikiliza
malalamiko na mapendekezo ya wateja.
Watu
wenye lengo la namna hii, hukakikisha biashara zao zinakuwa na kitu kimoja au (hata
zaidi) ambacho kweli ni cha kipekee ambacho siku zote watajivunia nacho na
kitadumu vizazi na vizazi, iwe aina yao ya utendaji kazi, bidhaa zenye upekee,
mfumo wa uendeshaji wa biashara, au mahusiano na wafanyakazi.
Zaidi
sana, watu wenye lengo hili, huwa ni wepesi kutilia maanani mambo madogo madogo
ya kitaalamu katika biashara zao, kama vile utambulisho wa biashara zao (rangi
za biashara, nembo), mifumo ya mawasiliano ya uhakika, n.k
Mjasiriamali
wa namna hii, hana papara wala haraka ya kukuza mauzo yake, bali ana
mtazamo wa kuwa na mauzo endelevu na kuona biashara inapanuka siku hadi
siku.
HITIMISHO:
Je
wewe upo katika kundi lipi ? Inawezekana kabisa mtu kutoka kundi moja kuingia
katika kundi lingine.
0 comments:
Post a Comment