Pamoja
na ukiritimba uliopo katika soko la
ajira, kutokana na rushwa na mambo ya kujuana, bado kuna nafasi kubwa ya wewe
kupata kazi unayoipenda na kazi inayolipa. Kabla ya kuanza kulalamika kuwa watu
wanapeana ajira kwa kujuana, tafakari kwanza ni kwakiwango gani wewe kama wewe
unakidhi matakwa ya waajiri. Wakati wengine wanalalamika kupata kazi Tanzania
ni tabu, wapo watu ambao wanabadilisha waajiri wanavyotaka wao, iwe ndani ya
Tanzania au hata mipaka ya Tanzania.
La
msingi kukumbuka ni kuwa utaajiriwa ili ufanye kazi, tena sio tuu ufanye kazi
ili mradi, unatakiwa ufanye kazi kwa ufanisi. Katika makala hii, tunaonyesha
mambo 6 ya kuzingatia ili kurahisisha utafutaji wa nafasi ya ajira.
1. Mtandao
wako : Kila mmoja wetu anahitaji msaada toka kwa watu fulani. Hivyo hata
katika ajira ni muhimu kuwa na mtandao utakaokusaidia kufikia malengo yako ya
ajira. Mtandao utakusaidia kwa njia nyingi kama vile kukupa taarifa ya nafasi
za kazi , kukusaidia katika kujiandaa na usaili. Pia mtandao wako unaweza
kukusaidia katika kukutambulisha kwa waajiri ili kuongeza imani ya waajiri
kuhusu wewe.
2. Uwezo
wa lugha ya kiingereza: Kiingereza ni lugha kuu ya mawasiliano katika
ajira. Hakikisha una uwezo mzuri wa kuongea na kuandika kwa ufasaha. Hapa
tunazungumzia ujue vema kanuni za lugha hiyo kama vile matumizi ya nyakati
mbalimbali, viunganishi , n.k , sio tuu kujua kuunganisha maneno mawili matatu.
Jizoeze kuandika kwa ufasaha pia. Lugha ya kiingereza itakusaidia kukupa maksi
wakati wa usaili (interview). Hali kadhalika uwezo wa kusoma na kuandika kwa
ufasaha wa kiingereza utakusaidia katika kufanya kazi kwa uhakika, na hata kuwa
mbunifu kwa kujifunza mambo mapya na kuyaelezea.
3. Ujuzi
wa uhakika: Kumbuka kuwa sababu kubwa waajiri makini wanakuhitaji ufanye
kazi kwao ni kwamba utaweza kuwa mfanisi kwa kile ambacho utatakiwa kukifanya.
Hili litawezekana tuu endapo wewe kweli una ujuzi ambao unadai unao, wakati wa
kuomba kazi. Kumbuka unaweza kufoji vyeti, ila ujuzi na uzoefu wa kazi, hauwezi
kufoji.
4. Uwezo
wa kufanya mawasiliano fasaha: Jitahidi sana kufuata kanuni zote za
mawasiliano fasaha, ikiwemo kusikiliza kwa umakini kabla ya kutoa maelezo yako, aina ya mavazi,
na muonekano wako. Salamu na ufuatiliaji wa mambo madogo madogo kama kusema
ahsante, kufuata maelekezo yote ya matangazo ya kazi kwa ufasaha.
5. Unajitangaza
vipi: Katika kutafuta ajira, ni muhimu kuwataarifu waajiri na pia watu
wengine kuhusu hitaji lako la kuajiriwa. Hivyo basi jipange vema kuwataarifu
ndugu, jamaa na marafiki. Kingine unachoweza kufanya ni kuandaa kazi binafsi
zinazotumia ujuzi wako ili watu wakiona kazi zako zilivyo nzuri unaweza
kujikuta umepata ajira. Ni muhimu sana kutembelea ofisi za waajiri watarajiwa,
ukaomba nafasi ya kuongea na mtu mwenye majukumu ya kuajiri, ili uweze
kujieleza au kuacha maombi ya kufanya kazi huko.
6. Taswira
uitoayo kwa jamii: Waajiri wako watarajiwa wapo katika jamii unayoishi, na
hata wale ambao wanaweza kukufanyia ‘mpango’ ukapata ajira wapo pia katika
jamii, hivyo basi ili wakuamini, na wategemee utendaji bora toka kwako ni
muhimu uonyeshe kujiheshimu, na kwamba ni mtu unayeweza kuaminika na kutumainiwa kufanya kazi kwa ufasaha, na
kuwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi wengine. Angalia aina ya status na
picha unazoweka Facebook, Google Plus, au Twitter. Pia kama kuna ka
ujasiriamali unafanya sasa, hakikisha biashara yako haiharibu uaminifu na
taswira njema kwa jamii.
Good
ReplyDelete