WAAJIRI WANACHOTAKA KUKIONA KATIKA BARUA ZA MAOMBI YA KAZI

Mara nyingi waajiri hutaka waombaji wa kazi wawasilishe barua ya maombi ya nafasi ya kazi ili waweze kuchambua watu wenye vigezo, ambao wanaweza kuwaita kwa usaili.
Mambo kadhaa ya kukumbuka:

Barua inaeleza ujuzi wako wa mawasiliano (communication skills)
Barua ya maombi ya kazi ni aina ya mawasiliano tunayosema mawasiliano rasmi. Hivyo unategemewa kufuata mpangilio sahihi (format) wa uandishi wa barua –kama vile kuandika vyema anuani yako, anuani ya muajiri, kichwa cha habari cha barua, salamu, tarehe,  hitimisho sahihi la barua, na sahihi yako. Pia kwakuwa ni mawasiliano rasmi, unatakiwa utumie lugha rasmi, badala ya kutumia lugha za mtaani au vifupisho visivyo rasmi. Vifupisho kama  ….am applying for this post…, na mwisho wa barua ukaandika
 Yours for real,
 John.
( Inaonyesha uwezo wako wa kuwasiliana vema ni mdogo).
Ukiachilia kutumia lugha rasmi, unatakiwa pia uweze kuandika kwa kufuata kanuni za lugha (grammar) sahihi. Haijalishi kama umeandika lengo lako ni kusema una uwezo mzuri wa kufanya mawasiliano bora, muajiri ataweza kugundua ukweli kwa haraka kupitia barua yako, mfano ukiandika hivi:-
 “ I am excellent communication skills”

Barua inaeleza aina gani ya mfanyakazi ulivyo
Namna ya uandishi wako na yale utakayoyaandika katika barua , yanaweza kuonyesha nini muajiri wako ategemee kutoka kwako kama mfanyakazi. Mfano wa mambo yanayoweza kujieleza katika barua yako ni:-
  • Je wewe ni mbunifu au la: Hii itaonekana kupitia namna ambavyo umeamua kujitofautisha katika uandishi wa barua tofauti na wengi wanavyoandika. Mfano jinsi unavyojieleza kuhusu vile unavyo ‘fit’ nafasi husika unayoomba. Vile unavyojieleza mafanikio (achievements) ulizowahi kufikia katika kazi zako za awali- mambo gani ya msingi uliyoyafanya ambayo yalinufaisha asasi uliyokuwepo hapo awali ( hata kama ulikuwa mwanafunzi bila shaka kama wewe ni mbunifu ulipata kufanya mawili matatu ya manufaa kwa watu wengine na kwako pia).  
  • Je wewe ni mchapakazi au la: Hii itaonekana kupitia namna ambavyo umeandika kwa umakini barua yako – je umekuwa na bidii ya kutosha kufuata maagizo yote ya tangazo la kazi ? Je, umekuwa na bidii kufuata vigezo vya mawasiliano bora? Je, umefanya utafiti wa kutosha kuhusu kazi unayoomba na asasi husika inayotaka kukuajiri ili kwamba unapoandika  barua yako, uonyeshe una uelewa na  hamasa ya kupata ajira husika?
Barua inaeleza kwanini wewe uchaguliwe au usichaguliwe
Kwa kuzingatia ushindani uliopo katika soko la ajira, na hitaji la ‘bidhaa bora’ yaani mfanyakazi bora, barua yako inabidi ikidhi vigezo hivyo, ili iweze kuwashawishi waajiri wakuite kwa ajili ya usaili na hatimaye kukuajiri. Vigezo kama kuwa mbunifu, mchapakazi, ujuzi, uzoefu na uwezo  bora wa mawasiliano ni mambo ambayo yanaweza kuleta maana katika namna unavyoandika barua.
Share:

0 comments:

Post a Comment