PASSIVE AGGRESSIVE: AINA YA TABIA INAYOWATESA WENGI

Inakera sana unapomuambia mtu afanye jambo fulani na ukitarajia alifanye kwa ufanisi wa kiwango fulani, ila matokeo yake ni kinyume kwakuwa mtu huyo pengine asifanye kabisa au akafanya jambo hilo kwa kiwango duni  tofauti na uwezo wake. Pia inakera inapokubidi urudie rudie kumueleza jambo mtu , na mtu huyo haonyeshi kukubali kubadilika ili kufanya unayomuelekeza. Hali hii huwwasababishwa na mambo mengi ikiwemo tabia ya passive aggressive.

Passive aggressive ni aina ya tabia ambapo mtu huonyesha ukaidi usio wa moja kwa moja, badala yake hutumia vitendo kuwasilisha ujumbe wake wa kukataa jambo fulani.
Mfano , mtu anapewa kazi afanye na anatakiwa kuikamilisha kwa muda fulani, ila mtu huyo anapinga kufanya kazi hiyo, lakini hataki kueleza kupinga kwake kwa mtu aliyempa kazi. Badala yake atakubali kazi, lakini hatoifanya kwa muda uliopangwa,au kwa ufanisi unaotakiwa.

Watu wenye tabia ya passive aggressive, huwa tunawaita wakaidi, hata hivyo wao wenyewe ukiwadadisi kuhusu wayafanyayo kama kweli wanafanya kwa makusudi  hawatokubali , watatoa sababu mbalimbali kama vile kusahau, kutokujua, kufikiria sivyo ndivyo, n.k.

Wataaalamu wa tabia wanasema tabia ya passive aggressive hutokana na udhaifu wa watu wenye tabia hiyo kutokuweza kujielezea, kuwa na hofu ya kujieleza, au kutaka kufanya ushindani . Hii inamaanisha kuwa watu hawa wana mapungufu katika uwezo wa kuwasiliana vema na watu watu wengine.

Wataalamu wa tabia, wanaongeza pia kuwa tabia hii ya passive aggressive huchangiwa na mambo mengi ikiwa pamoja na malezi ambapo mtoto hapewi nafasi ya kuelezea hisia zake.Pia uwezo wa kutotawala hasira na kutokuweza kuelezea hasira, mara nyingi huwa tunasema ‘kubaki na jambo moyoni’.

Mambo mengine yanayochangia tabia hii  ni kutokuwa na uwezo wa kuchambua tatizo husika ambalo mtu anakumbana nalo, hivyo kujikuta anabaki kulaumu wengine au kuona wengine ndio chanzo cha matatizo , uwezo mdogo wa kutambua na kukubali mapungufu binafsi na kuwajibika kutokana na hali ya maisha inayomkumba mtu.

Hitimisho:
Tumeona kuwa tabia ya passive aggressive inakera sana, na inarudisha nyuma maendeleo hususani kama unamtegemea mtu afanye jambo halafu yeye ndiye ana tabia ya passive aggressive , basi itakuwa ‘imekula kwako’. 
Kwa wale ambao wana tabia ya passive aggressive, wapo kwenye hatari ya kupoteza kazi kwani hakuna bosi anayetaka  kuwa na mtu anayepinga maamuzi . Tabia ya passive aggressive ni mbaya pia hata kwa mahusiano na watu wengine ikijumuisha mpenzi  wako, kwani inakera na mtu hawezi kuendelea kuvumilia tabia kama hiyo inayojirudia rudia.
Kama una tabia ya namna hii njia rahisi ya kujirekebisha ni kukubali kwanza kuwa tabia hii ni tatizo. Jifunze kujieleza kama unahisi huwezi kufanya jambo fulani. Pia heshimu mtazamo wa wengine  na usiweke mtazamo hasi kila unapoambiwa  jambo.
Share:

0 comments:

Post a Comment