Kuna sababu nyingi zinazotofautisha watu
waliofanikiwa na wasiofanikiwa, lakini zaidi sana sababu ya utofauti huo ipo
katika MUDA. Ndio, sababu ni MUDA, muda
toka mtu ameamua kutenda anayohitajika kutenda ili afanikiwe, muda ambao mtu
anaweza kuvumilia, muda ambao mtu ameamua kupoteza bila kuwa na mkakati maalum,
muda unaotumika kufanya jambo la msingi, Muda wa kusubiria wakati muafaka wa
kufanikiwa kwako utimie n.k. Makala hii inachambua namna unavyoweza kujiongoza
vema kutumia muda ili kuleta mabadiliko chanya katika maisha yako.
Jambo la msingi zaidi kwanza:
Hii
inaonekana ni rahisi kusema kuliko kutenda kwa sababu wengi wetu hukumbwa na
kigugumizi katika kutambua jinsi ya kupanga mambo yetu kwa ngazi za umuhimu ili
lile la muhimu zaidi au la msingi zaidi lianze. Matokeo yake ni kujikuta
tunatumia muda mwingi kufanya mambo machache yasiyo na uzito mkubwa kwetu, na kuyapa muda mdogo yale mambo yaliyo na
uzito hasa kwetu. Kanuni rahisi ya
kukuweza kupanga mambo kwa ngazi za umuhimu ni kupima mambo kwa vigezo
vifuatavyo:-
Uwezekano
wa kuhairisha jambo: Je ni lazima jambo husika lifanyike muda huu ? Je
inawezekana kuliahirisha na kufanya baadae ? Je athari za kuahirisha ni zipi ?
Linganisha
faida za sasa na za baadae : Je, jambo hili na lile lipi litakunufaisha zaidi
sasa ? Je lipi litakunufaisha baadae ? Pia linganisha faida ya sasa na faida ya
baadae, jambo lipi linakupa faida zaidi?
Linganisha
rasilimali zinazotakiwa kutumika : Jiulize jambo lipi linatumia zaidi
rasilimali kuliko nyingine, na je unaweza kufanikisha kwa ufanisi zaidi jambo
gani kwa kutumia rasilimali unazoweza kupata.
Hivyo
basi , kanuni hii ya kufanya jambo la msingi zaidi kwanza, inatuhitaji tusiwe
watu wa kukurupuka, badala yake tuwe wachambuzi wa maisha na yale tunayokumbana
nayo ili tujipange vema. Wengi wetu hujipa moyo kwa kusema, “aah lakini hili jambo nifanyalo ni la muhimu”.
Wakati kinachotakiwa ni kufanya ‘la muhimu ZAIDI’
Muda ulivyo tabibu:
Kuna msemo usema “
unaposhinda, mheshimu uliyemshinda, na
unaposhindwa pia mheshimu aliyekushinda”.
Msemo huu una maana kubwa sana kuwa muda ni dawa au tabibu wa mambo
mengi. Wapo wengi waliokuwa matajiri wameporomoka, na wapo wengi waliokuwa
masikini wamekuwa matajiri. Hivyo kwa wewe uliye katika hali duni , usijione
kuwa basi hapo ulipo ndio mwisho. Kumbuka muda ndio kila kitu, na kwakuwa muda
bado upo, wewe unao uwezo wa kubadilika na kuwa juu, ukiweka nia, na juhudi ya
dhati. Kwa wewe ambaye upo na maisha ya
kuridhisha, usiwadharau wengine, hata wewe ni muda tuu ndio unakufanya ujihisi
hivyo ulivyo. Huu ni muda wako, kwani hata wewe , au waliokufanya hapo ulipo
nao walikuwa na muda wa kusota.
Kila jambo ni tokeo la juhudi na muda
uliotumika: Kutana na bwana PM,
mwenye umri wa miaka38, kwa sasa anasoma masomo ya ngazi ya cheti katika chuo kimoja binafsi jijini Dar es
salaam. Bwana PM alipomaliza kidato cha nne, hakufaulu, na hakukuwa na uwezo
katika familia yake ya kumpeleka masomo ya ziada. Alikaa mtaani kwa miaka
kadhaa ,kisha baadae akapata kibarua na kufanya kazi kwa miaka kadhaa. Mara kwa
mara alijikumbusha azma yake ya kujiendeleza, lakini kila wakati akawa
akijiambia hayupo tayari. Miaka imepita na sasa ana familia ya watoto wawili,
kisha anafikiria kuwa inabidi aonyeshe mfano kwa watoto wake kwa kujiendeleza
kusoma. Alifanya mitihani ya ku resit na
akapa credit za kumfanya aendelee masomo ya cheti. Bwana PM amefikia hapo alipo
kwa juhudi zake mwenyewe na muda alioutumia. Kama angefanya maamuzi mapema ya
kuanza kujisomesha, hivi leo angejikuta yupo mbali, kwani yeye mwenyewe anasema
miaka 6 nyuma alikuwa anapata kipato cha kutosha kujiendeleza kusoma, ila
alidhani hakuwa tayari kusoma.
Picha kubwa ya maisha:
Fikiria
kwa muda mfupi, aina gani ya maisha ulikuwa ukipenda uishi, je ni hayo uliyo
nayo sasa. Je, unadhani hapo ulipo ndipo ambapo ulitamani kuwa miaka 5 au 10
iliyopita? Je, mke au mume , au mpenzi uliye naye, ndio wa aina ile uliyowahi
kuifikiria na kujiambia kuwa utakuja kuwa na mtu wa aina hiyo ? Majibu kwa
walio wengi wetu ni kuwa, vile tulivyo leo, vitu au watu tulionao karibu,
maeneo tunayoishi, kazi tunazofanya, n.k sio vile ambavyo tuliwaza kuwa navyo.
Hata hivyo, sio kwamba maisha yamefikia mwisho. Hata kama hatujafikia vile
tuliwaza au kutamani kuwa, ni wazi kuwa maisha yanaendelea, na tuna imani ya
kufanya makubwa zaidi. Hili ni somo kubwa sana kuwa hatuna haja ya kujiona ni
bora zaidi ya wengine, kuwadharau wengine, au kuwakatisha tamaa wengine hasa
pale tunapodhani ‘tumekwisha toka
kimaisha’ kwakuwa hata hivyo tulivyo leo sio kwamba tulifikia kwa mikakati au
formula ya aina moja. Pengine tunao waona wapo chini yetu, ni kwamba nao
wanapitia na kujaribu mikakati fulani fulani ambayo mingine itafanikiwa,
mengine haitofanikiwa. Wengine hawafanikiwi kwa sababu ya watu kama wewe
unayewaangalia walio chini yako kama
‘washindani ‘ wako kimaisha, wakati kiukweli kila mtu ana picha ya peke yake ya kutoka
kimaisha.
Imani na matendo:
Jambo
la msingi ni kuamini kuwa unaweza kutimiza hilo unalolitaka. Imani peke yake
haisaidii, fanya matendo hasa yanaendeana na imani yako. Huwezi kumkuta padri
anaswalisha msikitini wala shekhe anaswalisha kanisani, kwakuwa Imani na
Matendo havitokuwa sawa, hivyo basi usitegemee kama imani yako ni kufanikiwa,
lakini matendo yako – ikiwa pamoja na kule kusoma kwako, mikutano yako na aina
ya watu ulio nao karibu haviendani na yale unayotamani kuwa.
0 comments:
Post a Comment