HII NI KWA WAJASIRIAMALI WA SASA NA WATARAJIWA part 1

Wengi wetu tuna ndoto za kujiajiri na kufanya biashara. Au pengine tumeshajaribu kufanya ujasiriamali lakini tunajikuta tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele kimafanikio. Je, ni nini hasa kinafanya  wengine wafanikiwe katika ujasiriamali na wengine wasote na hata kukimbia ujasiriamali ? Katika makala hii tunaangalia mambo muhimu 11 ambayo kama mjasiriamali atayazingatia ataweza kujikuta  anakabiliana na changamoto za ujasiriamali na hatimaye kuwa na mafanikio endelevu.

1. Malengo  na mikakati ya muda mrefu:
Ni kweli kuwa lengo kuu la ujasiriamali ni kuingiza ziada ya mapato ili biashara iweze kujiendesha, kupanuka, na kuwalipa ipasavyo waanzishaji au muanzishaji wa biashara.  Hata hivyo, haitoshi tuu kutamani  kuwa na biashara kubwa bila kuwa na mikakati ya kufikia huko.  Hivyo ni muhimu kuweka bayana , ikiwezekana katika maandishi malengo ya muda mrefu ya biashara yako , na ufafanue mambo utakayotakiwa kufanya kufikia huko, aina ya watu unaotakiwa kuwa nao ili kufikia huko, mfumo wa uendeshaji unaotakiwa kuwa nao ili kufikia huko unakotaka kufikia, na uhakikishe pia watendaji / wafanyakazi ulio nao wanalielewa hilo.

2. Malengo na mikakati ya muda mfupi mfupi:
Malengo na mikakati  ya muda mrefu haitoshi, inabidi uweke pia malengo ya muda mfupi mfupi. Mfano malengo ya muda mrefu yanaweza kuwa ni malengo ya miaka mitano ijayo, ila inabidi uweke malengo ya muda mfupi mfupi, mfano malengo na mikakati ya kila mwezi, malengo ya kila robo ya mwaka, malengo ya kila mwaka n.k .
Kumbuka pia kuwa , kwasababu kuna mabadiliko ya mara kwa mara katika jamii, teknolojia , mazingira ya biashara n.k inabidi uwe tayari ku ‘adjust’ malengo na mikakati yako ili iendane na mabadiliko hayo.

3. Sheria zinazoongoza biashara:  
Ni muhimu kwa mjasiriamali, kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu sheria za nchi na taratibu zinazosimamia shughuli husika kwani kutokutambua sheria vema, kama vile sheria za kodi, sheria za vibali vya biashara, sheria za uandikishaji wa biashara kunaweza kumfanya mjasiriamali kuingia gharama zisizotarajiwa na zisizo na sababu. Mfano kushindwa  kwa mjasiriamali asiyetunza vitabu vyake kwa mujibu wa maelekezo ya sheria za kodi anaweza kujikuta anapata faini au hata biashara yake kufungiwa. Kwa kampuni kutokupeleka kwa msajili wa makampuni taarifa za kila mwaka za maendeleo ya kampuni ( Annual Return) kunaweza kuwa na matokeo ya faini zisizo na sababu. Pia kwa mjasiriamali aliyeajiri wafanyakazi kadhaa inabidi afahamu vipengele muhimu vya sheria zinazosimamia mikataba ya kazi kwani  mfano mfanyakazi anapofukuzwa bila kupewa ‘notice’ ya muda unaotakiwa kisheria,  mfanyakazi huyo anaweza kudai fidia, na pia kuna aina nyingine ya malipo ambayo mfanyakazi anapaswa kulipwa wakati ameachishwa kazi. Hivyo kama mjasiriamali hakujiandaa ipasavyo kufanya malipo hayo, hali ya kifedha ya biashara inaweza kutetereka.

4. Mipango na mikakati ya fedha
Ni muhimu kwa mjasiriamali kutambua namna ya kusimamia vema maswala ya fedha , kwani bila lengo ni kupata mapato yanayoleta ziada, na ili kupata mapato ni lazima kuingia gharama kadhaa. Hivyo mjasiriamali lazima awe na mbinu sahihi za  kudhitibi matumizi ili kweli matumizi  hata kama ni madogo basi kweli yalete ziada ya kutosha kwa biashara. Mjasiriamali inabidi adhibiti matumizi kwa kuweka miongozo imara ya jinsi biashara yake itakavyolipia gharama fulani, aweke mikakati ya jinsi ambavyo atahakikisha kweli mapato yote yanajulikana, na yanawekwa kwenye maandishi, na aweke mikakati ya jinsi ya kutunza taarifa za fedha. Ziwepo mbinu za kuchochea mapato makubwa , na shughuli za kimasoko zinazoendana na hili zisimamiwe kwa ufanisi, mfano kutoa punguzo la bei, kutoa ofa mbalimbali kwa wateja,  kutoa zawadi n.k vyote hivyo vinaweza kutumika kuchochea mapato, hata hivyo ni muhimu kuwepo muongozo sahihi wa mambo hayo, ili kweli yalete ziada ya mapato.


5.Masoko
Ni muhimu mjasiriamali atambue maana halisi na mbinu bora za kufanya shughuli za kimasoko (marketing). Shughuli za masoko hazianzi pale tuu mjasiriamali anapokamilisha bidhaa yake, hivyo anaanza kutafuta wateja. La hasha, shughuli za kimasoko zinajumuisha utafiti wa nini wateja wanataka, wanataka kivipi, na wanaweza kulipia kivipi, na wapate wapi bidhaa husika.  Kuelewa wateja vema ni shughuli ya kwanza na ya muhimu kwa kila mjasiriamali. Kisha mjasiriamali anazalisha bidhaa inayoendana na matakwa ya wateja (mfano bidhaa iendane na ujazo unaohitajika na wateja, aina ya radha inayotakiwa na wateja, rangi na muonekano unaotakiwa na wateja n.k). Kisha baada ya kuwa na bidhaa sahihi , mjasiriamali anaweka bei inayoendana na soko , bei hiyo pia iendane na mikakati yake mingine ya kibiashara, halafu anafanya shughuli za kuwataarifu wateja bidhaa yake husika,  na sio tuu kuwataarifu, bali mjasiriamali ni lazima atutumie mbinu za kuwafanya kweli wateja waone wanahitaji bidhaa husika kutoka kwake yeye mjasiriamali.

Tutaendelea na points nyingine kesho....
Share:

0 comments:

Post a Comment