MAMBO YALIYOJIFICHA NDANI YA WIMBO 'LEKA DUTIGITE'

Hakika wimbo wa Leka Dutigite, ulioimbwa na wasanii wa bongo fleva, mahiri kabisa nchini Tanzania, ni moja ya nyimbo chache ambazo ukiisikia kwa mara ya kwanza tuu unaupenda. Wimbo huo ni zao la ushirikiano wakali wa bongo fleva wenye asili ya mkoa wa Kigoma, mkoa ambao kiukweli umajaaliwa neema zote kubwa kubwa na ndogo ndogo.   
Kama haujaona basi chungulia fasta video hii hapa chini toka Youtube (hapo chini), utajionea jinsi wakali wa bongo fleva kama vile Diamond, Banana, Chege, wakiporomosha mashairi ambayo kwa hakika utakubali kuwa mzigo huo wa Leka Dutigite kweli umesimama.

Baadhi ya mambo yanayosemwa mitaani kuhusiana na wimbo huo, ambayo kwakweli mengine yana point sana ni kama yafuatayo:


Kabla sijakushushia udaku wa mtaani, kwanza nikudokeze tuu maana ya jina la  wimbo huo. Kwa maana ya mtaani –  jina Leka Dutigite laweza kuwa “ Acha Tule Bata”. Ukiacha  maana hiyo ya kitaa, jina la wimbo huo linaweza maanisha ‘Acha tucheze’, au ‘Acha Tujidai’ au ‘Acha Tujivunie’.


Turudi mtaani, huko mitaani wachambuzi wanasema hivi:


Mosi:

Wimbo umeweza kueleza kwanini Tanzania ni Masikini: Kuna wanaodai eti hata baadhi ya viongozi serikalini hawaelewi kwanini Tanzania ni Maskini,  hata hivyo wasaani wetu wa bongo fleva kupitia wimbo huo wameweza kutupa bonge la dokezo kuwa kwanini Tanzania ni Masikini. 
Wimbo mzima umejaa mashairi ya kuisifu Kigoma, ikionyesha rasilimali kibao zilizopo humo mkoani.  Pamoja na kuwepo na Mbuga, Ziwa refu kabisa kuliko yote Afrika, madini, na hata rasilimali watu ambao wame prove kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa –mfano Miss Tanzania, bingwa wa ngumi, wanamuziki mashuhuri, wachezaji mpira mashuhuri, na hata wanasiasa hodari kabisa, maendeleo ya mkoa huo hayaendani na utajiri uliopo. Hii ni taswira halisi ya nchi yetu Tanzania. 
Kinachosemwa mtaani ni kuwa kumbe tatizo lipo ni katika matumizi ya hizi rasilimali na sio rasilimali. Tumsitafute mchawi.  
Watu wangu wa Kitaa wangependa kusikia katika wimbo huo, au achilia mbali kusikia basi waone hata picha za matunda yanayoendana na hizo rasilimali zinazotajwa na kusherehekewa katika wimbo huo. 
Rasilimali watu ziwekeze kweli huko mkoani kwao, na hizo rasilimali asilia kama madini na ardhi yenye rutuba vitumike vya kutosha kuleta maendeleo.

Si wanasema upendo ni matendo, basi kwa wapenda Tanzania nchi yetu , kila mmoja wetu ajitahidi kufanya kwa vitendo jambo linalowezesha kweli kuboresha hali za maisha ya watu wa Tanzania.

Pili:

Chege kapiga dongo la wazi wazi kwa wanaojifanya si watanzania ili hali ni watanzania. Kuna aina nyingi za kuwa mzalendo, sio tuu kuwa mzalendo kwa nchi yako, pia unatakiwa kuwa mzalendo kwa mkoa wako. Hii iende mbali hata kwa kijiji chako, na familia yako. 
Chege ananukuu maneno ya mama yake kuwa mkataa kwao ni mtumwa. Hata kuenzi basi lugha ya kwenu nalo jambo jema si ndio maana wimbo huu una jina la kilugha – Leka Dutigite! 
Hii ni bonge la hongera kwa chege kugusa swala hili kwani kuna baadhi yetu kwa kuenda nje ya nchi kidogo tuu basi, wanajidai wao si wabongo tena. 

Tatu:

Pamoja na mambo mengi mazuri ya kujifunza kutoka katika wimbo huo, usichukulia kila jambo kwa undani na ukataka kuiga mfano pale Diamond anaposema migebuka na ugali wa muhogo ndio umemfanya yeye kuwa Diamond, usidhani na wewe ukila ugali wa muhogo na migebuka basi kipaji cha kuimba cha Diamond  utakuwa nacho. 
Hizo zilikuwa ni ‘porojo’ tuu za Diamond,  pengine ni kuunganisha vina kama Peter Msechu naye alivyoweka porojo kuwa ‘Kigoma haijagoma, Kigoma yasonga mbele’, usiwazie sana haya maneno mfano ukajiuliza Kigoma ingegomaje ?
Share:

0 comments:

Post a Comment