Matokeo ya kidato cha nne (form 4) kwa wanafunzi waliofanya
mitihani hiyo mwaka 2012 yameishtua jamii ya watanzania waliopo nchini na
waliopo nje ya nchi kwa jinsi ambavyo idadi kubwa ya wanafunzi kufeli ambapo
zaidi ya 60% ya watahiniwa walipata divisheni sifuli.
Makala hii inachambua nini kifanyike ili kumsaidia kijana
mmoja mmoja aliyefeli :
Tulirahisishe tatizo:
Katika maisha yetu kama binadamu tunapitia magumu mengi na
mazuri pia. Magumu kama vile kufeli ni sehemu ya maisha , ingawaje huwa
yanatuumiza na wakati mwingine tunakata tamaa. Waswahili wanasema maji
yakishamwagika hayazoleki, hivyo basi kwasasa
usiumie kichwa kwa kuwa umefeli badala
yake chukulia hiyo ni changamoto ya kutambua udhaifu wako uliokufanya ufeli, au
mapungufu mengine ya kifamilia na kijamii. Kumbuka pia maisha ni zaidi ya kufaulu au
kufeli mitihani ingawaje kufaulu kunaweza kukaharakisha kufanya mambo fulani,
lakini hakumaanishi wala hakukupi uhakika wa furaha na mafanikio ya maisha.
Jambo la msingi ni kwa mtu binafsi kutambua kuwa kushindwa jambo fulani
hakumaanisha kuwa jambo hilo haliwezekani . Kijana aliyeshindwa kufaulu
mitihani ya mwaka jana, haimaanishi kuwa amefeli maisha. Anayo nafasi ya
kujijenga sasa, akafanyia marekebisho yale mapungufu aliyo nayo kwani bado umri
unadai, maisha hayajaisha bado, anayo miaka zaidi 20 ijayo kuishi hivyo
ajipange na kuandaa maisha yake kwa msaada wa familia, jamaa na marafiki.
Nini cha kufanya
sasa:
Kuwa mkweli :
Ni muhimu kwa kijana mwenyewe binafsi
kutambua mapungufu yaliyosababisha kutokufaulu mitihani husika. Pengine
ni
kweli kuna magumu ya kijamii kama vile uhaba wa walimu, au magumu ya
kifamilia
kama vile hali ngumu ya kifedha, ila hizi ni changamoto tuu ambazo
zinaweza
kutatuliwa ili kuleta utulivu kwa mwanafunzi. Madhaifu kama vile
kutokuwa na bidii ya kusoma, kutafuta misaada zaidi, na kujituma hata
pale masomo yanapokuwa magumu.
Kujiboresha katika
English: Somo la English ni kati ya
masomo ambayo ni LAZIMA mwanafunzi alimudu vyema sio tuu kwa sababu inabidi alifaulu ila
English ndio msingi wa kuelewa masomo mengine, kwani mwanafunzi ataweza
kujisomea vitabu mwenyewe, na pia kuwa na uwezo wa kuandika majibu kwa ufasaha.
Kujiboresha katika Hesabu:
Kujiboresha katika hesabu ni muhimu , sio tuu kwa sababu hesabu ni somo
bali kujiboresha katika hesabu kunamfanya mwanafunzi kuwa hodari katika
kufikiria, na kuchanganua mambo. Uwezo wa kufikiria na kuchanganua mambo ni
muhimu katika kumuwezesha mwanafunzi kuelewa masomo mengine na hata katika
kujieleza.
Kujiboresha katika uwezo wa kutafakari (reasoning): Hii inawezekana kwa mwanafunzi kujihimiza kusoma
kwa umakini na kuelewa, kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kutambua mbinu za
ziada za maswali na jinsi ya ujibuji.
Kuamua kusoma kwa ufahamu: Mwanafunzi anatakiwa aamue kwanza kusoma na
kwamba adhamirie kuelewa anachokisoma.Maamuzi haya yanasaidia kumfanya awe na
usikivu na kujituma hata pale masomo yanapoonekana kuwa magumu. Waswahili husema: “huwezi kumlazimisha ng’ombe
kunywa maji”.
Hitimisho
ni kuwa pamoja na kuwa wengi tunaliangalia tatizo la kufeli kwa
wanafunzi kama tatizo la kijamii, makala hii inapendekeza kuwa pamoja na
juhudi za jumla za kutatua tatizo hili, kuna haja ya kutafuta njia za
kumsaidia mwanafunzi mmoja mmoja. Wazazi na walezi ni muhimu wakae na
wanafunzi na kutambua changamoto walizonazo, kuwasaidia mara kwa mara,
kwani kufaulu au kufeli mitihani ni matokeo ya maandalizi ya muda mrefu,
na kwamba familia, ndugu na jamaa wana mchango mkubwa katika kufanya
maandalizi ya mwanafunzi yawe bora.
0 comments:
Post a Comment