JINSI ULIVYO KATIKA HATARI NA VIRUSI VYA KOMPYUTA

Virusi vya kompyuta au tuite Computer Virus, ni program ambazo zimetengenezwa kwa madhumuni ambayo wewe mtumiaji wa kompyuta hauyahitaji ndio maana hata jinsi vinavyoingia kwa kompyuta ni kwa kuvizia kutokufahamu kwako kuwa program hizo zinafanya nini na kwamba zinaingia humo kwa kompyuta. Virusi huingia kwa kompyuta fulani kwa njia mbalimbali mfano kwa kusambazwa kwa email, kwa kusambazwa kwa kutumia flash disk, CD,DVD, au kwa kubofya ‘link’ yenye kubeba kirusi husika kwa kompyuta iliyounganishwa na internet.

Kwanini virusi vipo?
Kuna sababu kadhaa kwanini watu watengeneze Virusi;

Sababu za kibiashara: Baadhi hutengeneza virusi ili waweze kuuza dawa za virusi hivyo (Anti virus), na wengine hutengeneza virusi ili waweze kuua biashara za washindani wao.

Wizi: Baadhi ya watu hutengeneza virusi ili waweze kuiba taarifa fulani fulani za wengine, ikiwemo  password, taarifa za mbinu za kibiashara, taarifa nyingine za kiutendaji na kimaendeleo n.k

Burudani: Wapo baadhi ya watu ambao hutengeneza virusi kama njia ya kujiburudisha , pale wanapoona kuwa ujuzi wao unaweza kutengeneza kitu fulani halisi na kikasumbua watu wengine basi hujisikia raha, na kujiaminisha kuwa wamefanya jambo kubwa.

Uadui:  Baadhi ya virusi hutengenezwa kama njia ya kumuadhibu mtu fulani , hata hivyo kwakuwa virusi husambaa, unaweza kukutwa hata wasio husika na ugomvi au kutokuelewana nao wanajikuta wavipata virusi hivyo. Mfano mie nimekasirishana na ndugu X, nikamtumia email yenye kirusi ndani yake, yeye bila kujua , akaituma kwa rafiki zake, basi rafiki zake wataiona.

Na sasa tambua aina mbalimbali za virusi vya Kompyuta:-

Virus: Jina hili (Virus)  hutumika kueleza aina zote za program zinazosambaa kutoka kompyuta moja kwenda kompyuta nyingine na kuacha madhara toka kompyuta hadi kompyuta. Hata hivyo , virus havisambai peke yake, vinategemea binadamu kuvisadia kusambaa kwa  kupitia njia kama vile kutuma email, kusave files kwa flash disk , au CD na kuenda kutumia kuhamishia mafaili hayo kompyuta nyingine.

Worm:  Hii ni aina ya kipekee ya virusi ambavyo hujizalisha vyenyewe hivyo kuongeza idadi na madhara yake kwa kompyuta.  Kingine kinachoitambulisha Worm ni uwezo wake wwa kusambaa bila msaada wa binadamu. Uwepo wa files au taarifa fulani unatosha kabisa kufanikisha virusi hivi kusambaa. Kwakuwa worm hujizalisha yenyewe hufanya kazi ya kujaza kompyuta , na pia inaweza kuathiri hata usambazi wa taarifa kwa network fulani.

Trojans:  Hii ni aina maalum ya virusi ambayo tofauti na worm, vyenyewe havizaliani, ila huingia kwa kompyuta kwa njia ya kumlaghai mtumiaji wa kompyuta kwa kumfanya adhani kuwa anakubaliana na program nzuri kumbe ndani ya program hiyo kuna hicho kirusi ambacho kinakuja kuleta madhara kwa kompyuta. Hivyo unaweza kujikuta umeingiza program moja nzuri tuu unayoifahamu ila ndani yake kuna hicho kirusi ambacho kinasubiri tuu ubofye sehemu ambayo itakiruhusu kianze kazi zake.

Je, Madhara ya Virusi vya Kompyuta ni yapi ?

Madhara ya virusi vya kompyuta yanategemea na aina ya kirusi husika, yaani madhumuni ya kuundwa kwa hiyo program tunayoiita virus. Mfano:

  • Virusi huiba taarifa fulani fulani na kupatia watu wengine
  • Virusi husababisha usumbufu kwa mtumiaji wa kompyuta kwa kuifanya kompyuta iwe slow,
  • Virusi husababisha files na folders kufichwa au kupotea hivyo kuleta usumbufu kwa mtumiaji
  • Virusi husababisha kompyuta kujaa hivyo kuathiri ufanisi wa kompyuta
  • Virusi husababisha kompyuta kutokufanya kazi kwa sababu zipo program (virus) ambazo huondoa uwezo wa operating system kufanya kazi kwa kufuta mafaili muhimu ya utendaji wa system.
Share:

0 comments:

Post a Comment