Safari ya kujfunza English ni ndefu na kwa bahati mbaya watu wengi hupita katika safari hii kwa mateso makubwa kwakua hawajiamini katika kuongea na kuandika English. Makala hii ni sehemu ya jibu nilimpatia mwanafunzi wangu Abdi Mkizu, ambaye alitaka kwanini kwa zaidi ya miaka kumi sasa amekua akijifunza English hata hivyo bado anashindwa kuongea kwa kujiamini wakati baadhi ya marafiki zake wanaweza kuongea vizuri. Anauliza, je ni kwa sababu amekosa kujiamini katika English, na je afanyeje ili apate kujiamini.
Jichukulie wewe ni mwanafunzi wa daima
Kupoteza kujiamini kunawezekana kuwepo kwakua tayari haujichukulii kama mwanafunzi. Unadhani kuwa umeshajifunza vyote vya kujifunza hivyo sasa ni wakati wa kuongea English kwa ufasaha. Ila ukweli ni kuwa sote ni wanafunzi wa lugha wa maisha kwani hata Kiswahili chetu tuu hubadilika badilika mara kwa mara na pia hatukijui vizuri.
Ukijihesabia wewe kama mwanafunzi wa English wa milele, hautoogopa kukosea, maana kukosa kujiamini huja kwa sababu ya hofu ya kuogopa kukosea.
Kama kuna watu fulani wanakukera au kukukatisha tamaa katika kujaribu kwako English, hao watu waepuke kwa kuanzia. Fanya mazungumzo ya English na watu waelewa au na watu ambao kweli unaweza jifunza kutoka kwao, na wanaweza kukurekebisha. Weka mazingira katika kuwasiliana kwa English yanayoonyesha kuwa kweli upo katika kujifunza na upo tayari kukosolewa na kusaidiwa.
Shinda hali ya kujisikia iliyo ndani yako
Wakati mwingine mtu unaweza kushindwa English ni kwa sababu unajisikia kuwa wewe ni bora sana, au ni wa hadhi fulani, iwe kielimu, kimadaraka, kifedha au kiumri uwa huwezi kuonekana unakosea mbele ya wengine. Unataka utengeneze picha kuwa wewe unajua English, kwakua unajiamini kuwa watu wanakutegemea wewe kuwa na kiwango fulani cha English.
Kumbuka lugha yeyote haina kazi zaidi ya kufanya watu wawasiliane. Sasa kama wewe utaendelea kujisikia kuwa kwa umri wako, elimu yako au nyadhifa yako kuwa eti huwezi kuonekana unakosea, jiulize je kwako English itakua na kazi gani zaidi ? Chukulia kujua English ni kama kujua kupika. Kuna maana gani ujue kupika kama haupiki chakula chochote ? Hata kama hakitotoka chakula kizuri kama unavyodhani watu wanategemea, la msingi jua wewe upo katika safari ya kuweza kupika msosi mzuri zaidi siku moja. Usikubali kuishi kwa kuogopa maneno ya watu au kutaka kuwapendeza watu.
Kumbuka haushindani na mtu yeyote:
Wakati mwingine kule kutokuajimini kunakuja kwasababu unadhani kiwango chako cha English inabidi kiwe kama cha fulani, au kwanini fulani anajua zaidi English kuliko wewe. Binadamu tupo tofauti, hivyo tuna uwezo tofauti katika kujifunza lugha. Jiambie tuu kuwa la msingi katika kujifunza lugha ni kuweza kuwasiliana. Kama unaweza kuelewa na wewe kueleza vitu vikaeleweka basi upo katika nafasi nzuri katika English. Na kwamba taratibu hatua kwa hatua ukiendelea kuitumia English utakuja kuweza vizuri.
Usijilanganishe na jinsi mwingine anavyotamka kwa ubora zaidi kuliko wewe, au mwingine anavyoandika status bomba kuliko wewe. English unayotaka kuijua ni kwa matumizi yako wewe na sio kama anavyohitaji mtu mwingine. Pia hujui mazingira aliyojifunza huyo mwingine, inawezekana alijifunza kwa urahisi zaidi yako au amepata fursa nyingi zaidi za kuitumia English kuliko wewe. Ni wakati wako sasa na wewe kuitumia kila fursa uipatayo kuzungumza au kuandika kwa English.
Haitoshi kujiona unajua endelea kujifunza English:
Kutokujiamini huja kama tayari umeshajihakikishia kisaikolojia kuwa kwa muda uliotumia kujifunza English, kwa “materials” uliyo nayo, ni lazima tuu uwe unajua au umefikia kiwango fulani cha English. Hivyo basi inapotokea ukashindwa kutamka sentensi fulani, au kuelewa mazungumzo fulani, wewe mwenyewe utajiangalia kwa mtazamo mbovu, kuwa kumbe wewe ni bure kabisa, au kujiambia maneno kama vile basi kumbe hautoweza English.
Hata hivyo nakusihi uamini kuwa lugha haina mwisho katika kujifunza. Inawezekana kabisa ni kweli ulijifunza kwa umakini hivyo ambavyo ulijifunza, hata hivyo kuna vitu vingine muhimu na mbinu kadhaa bado haukujifunza. Hivyo unapokosea au kushindwa kutunga sentensi au kuelewa sentensi fulani, badala ya kupoteza imani, unatakiwa hapo ndipo upate hamasa ya wapi haswa unaweza kurekebisha.
Tambua madhaifu yako katika English yapo wapi:
Jiulize katika kutojiamini kwako kuandika na kuongea English ni mambo gani haswa unadhani huyafahamu vizuri au utayakosea endapo utaongea au kuandika. Kuwa mkweli kwako wewe mwenyewe kwani inawezekana huko kujiona haujiamini ni kiashirio kuwa kuna mambo kadhaa inabidi ujifunze, ila wewe badala ya kutilia mkazo hayo mambo unayotakiwa kujifunza ili ujiboreshe, wewe unakataa bila kujua kwakua kukiri kuwa kuna mambo ambayo kweli bado inabidi ujifunze ni kujirudisha nyuma katika fikra zako za kwamba wewe tayari unajua English. Bila kujijua unapenda “idea” kuwa wewe upo fiti katika English, wakati ukweli ni kuwa bado kuna mambo mengi inabidi ujifunze.
Hitimisho
Mara baada ya kujifunza hayo yote niliyoeleza hapo juu ya namna ya kujiamini katika kuongea na kuandika English , unatakiwa mara moja uanze kuyafanyia kazi. Tafuta nafasi ambapo unaweza kweli ukatumia hiyo lugha. Ndio maana nilitengeneza group la WhatsApp la JifunzeEnglish ili kwamba wewe na wengine wote wenye kutaka kufanya mazoezi ya kuongea na kuandika English muweze kupata hiyo nafasi ya kutumia English , pia kujifunza kutokana na makosa ya wengine. Ni matumaini yangu kuwa katika group hili utajisikia huru kuongea na kukosea, lakini zaidi sana utajifunza kuwa haupo peke yako katika kukosea kwani mimi kama mwalimu, nipo kurekebisha wote wanaokosea.
Kama haujajiunga na group letu la WhatsApp la kujifunza English, nitumie maombi yako ya kujiunga kwa namba +57 301 297 1724. Na kama unataka darasa lako binafsi la English pia wasiliana nami, uanze kuweza kweli kujifunza English.
Kama haujajiunga na group letu la WhatsApp la kujifunza English, nitumie maombi yako ya kujiunga kwa namba +57 301 297 1724. Na kama unataka darasa lako binafsi la English pia wasiliana nami, uanze kuweza kweli kujifunza English.
God bless teacher for you opinion
ReplyDelete