MAMBO 9 YA KUZINGATIA ILI UWE NA BLOG KAMA BIASHARA

Ni jambo la busara kuwa na vyanzo tofauti vya mapato. Haijalishi aina gani ya kazi uliyo nayo au kiwango chako cha elimu,  blog  inaweza kuwa chanzo chako cha mapato endapo utaifanya kwa umakini na kwa kujipanga.
Ninasema kama utaifanya kwa umakini na kwa kujipanga kwakua sio kila mwenye blog basi inamuingizia fedha. Wengi haswa walioanzisha blog kwa kuiga , kutaka matokeo ya haraka haraka , na bila kuwa na mkakati mathubuti na wa muda mrefu hawajafanikiwa na pengine wengi wao wameishia njiani.
Kuandikisha blog na kuiremba kwa muonekano ni jambo la msingi, ila kufahamu na kuweza kuiendesha ili kweli ikuletee kipato ni jambo tofauti na gumu zaidi linalohitaji kujipanga kweli kweli.
Katika makala hii ninakuelezea mambo ya msingi ya kuzingatia ili kweli blog ikuletee faida ya kifedha kama biashara, na kwa kufanya hivyo bila shaka utapata faida nyingine za kukua wewe kama wewe, kiufahamu na kimaendeleo yako binafsi.

1. Kutambua haswa namna kuingiza hela:
Kuna namna tofauti ambapo blog inaweza kukuingizia hela. Mfano waweza ingiza hela kupitia matangazo kwa blog yako. Nyingine ni kuwa kupitia blog yako na makala zako ukatambulika wewe kama mjuzi wa aina fulani na hivyo ukaingiza hela kwa kupitia huduma zako utakazotoa, au bidhaa ambazo utauza kwakua tayari umeshafahamika na kuaminika wewe ni wa aina gani.
Mfano,mapato ya Mbuke Times si kama wengi wanavyotarajia kuwa kipato cha blog kitoke katika MATANGAZO.
Utaona kuwa Mbuke Times haina matangazo ya biashara. Badala yake mie nimejikita katika kuwahudumia watu kupitia makala zangu, na watu hunitafuta niwahudumie kwa kazi zao mfano za kutengeneza website, kufundisha English, au kujipatia vitabu ambavyo nimeandika. Pia kama mshauri wa mambo ya biashara, wengi hunitafuta kwakua wanasoma makala zangu za ujasiriamali hapa Mbuke Times.
Wakati mwingine vyombo vya habari hunitafuta ili wanilipe niwapatie makala. Kwahiyo aina yangu ya kuingiza kipato niliyoichagua zaidi ni kuwafikia watu moja kwa moja ambao watafaidika na kuhitaji ujuzi wangu, na sio watu wa matangazo, ingawaje ikitokea kupata matangazo nitapokea.
Sio lazima ufanye kama mie. Kuna njia nyingi za kuingiza hela kupitia blog kama vile matangazo ya biashara, adsense, na kuuza bidhaa za watu wengine kupitia blog yako.
Hii ni sehemu ya makala zangu nilizotoa kwa gazeti la Mwananchi
2. Kutambua walengwa haswa ni akina nani:
Point hii inaendana na point ya hapo juu ya kutambua namna gani unataka kuingiza hela kupitia blog. Ukishajua aina gani unataka kuingiza kipato kupitia blog, basi itakupasa uchambue kwa umakini ni akina nani haswa unawalenga kuwa ndio wawe wasomaji wa blog yako.
Kujua aina ya wasomaji wako kutakufanya ujipange vema kuhusu aina ya lugha utakayoitumia kuandika blog yako, aina ya makala za kuandika , namna ya kuandika  makala zako. Nikupe mfano, mie nilichagua siku nyingi aina za walengwa wa blog yangu ndio maana unaona makala zangu ni ndefu na zina aina fulani ya uandishi ambayo huwezi ikuta kwa kila aina ya blog.
Kama umesoma hii makala hadi hapa , basi wewe ni mmoja wa walengwa wangu, na ukijiuliza kwa umakini utaona unakidhi sifa zifuatazo: Unapenda maendeleo kwa sana, unatamani kuwa zaidi ya hapo ulipo, unaamini unahitaji kitu fulani cha zaidi -maarifa ili ukue zaidi, kikwazo chako kikubwa katika kupiga hatua ya juu kimaisha ni mbinu, fikra, namna ya kujipanga, ujuzi zaidi na unahitaji sana muongozo wa mtu anayejua jambo fulani kwa upana.
Ndio maana unaona makala zangu nyingi katika Mbuke Times, zinalenga kujibu hizo shida zako au kukusiliza na kukufikia kwa namna hiyo.

3. Itachukua muda :
Kumbuka kuwa itachukua muda mrefu kutambulika na kujijengea wafuasi ambao watapenda kusoma blog yako mara kwa mara. Siri kubwa ya kuwa na blog yenye kukuingizia kipato ni kupata watu watakaoamini unayoandika, watakaopenda kurudi kusoma mara kwa mara, na ambao watajisikia kuunganika nawe, na hata waweze kukutambulisha kwa watu wengine.
Hivyo basi uwe na mkakati wa kuendelea kutoa makala za mara kwa mara kwa muda mrefu ili kweli watu waifahamu na kuikumbuka blog yako.

4. Kuandika mara kwa mara:
Point hii inaendana na point hapo juu kuwa inakupasa uandike mara kwa mara makala nyingi, kama ukishinda kabisa basi walau mara tatu kwa wiki.
jinsi ya kuandika makala nzuri za blog
Kuandika makala nzuri huchukua muda na huhitaji umakini wa hali ya juu na utafiti

5. Hakikisha unajitangaza:
Kuwa na blog ya kupendeza na makala nyingi nzuri hakutoshi kama watu wengi hawaifahamu biashara yako.
Tumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, WhatsApp, Instagram, Google+ kujitangaza. Angalizo usiweke matangazo yako huko kwenye mitandao ya kijamii kiasi kwamba uwakere watu. Usiwawekee links za blog yako sehemu ambayo haihusiki. Kwanza utajishushia heshima na kuonekana mbabaishaji. Mfano kwenye group la mambo ya siasa, wewe unaweka makala ya blog yako ya ushauri wa mambo ya mapenzi.

6. Kuwa na utambulisho maalum (Brand):
Sio kwa sababu Michuzi anaandika habari  za matukio na anapata matangazo mengi basi na wewe ni lazima uingie kuandika habari za matukio.La msingi katika unasiriamali ni kutambua haswa haswa ni tatizo lipi haswa linawakabili watu, na wewe utaweza kulitatua kwa namna gani.
Jijengee kufahamika kwa kutengeneza muonekano wako binafsi na wa blog kiasi kwamba hao watakaosoma blog yako, posts zako katika mitandao ya kijamii kweli wakuamini na wakuone wewe ni wa aina ambayo kweli unaweza saidia, haubagui, unaheshimu wote, na kweli una maaanisha na kuendana na hicho unachoandika.
Angalizo epuka lugha za udhalilishaji, au ambazo zitatafsirika kuwa unadharau au kuwaangalia watu wa aina fulani kwa ubaya mfano, epuka posts ambazo zitatafsirika kama dharau kwa jinsia fulani, dini fulani, au aina fulani ya watu katika jamii kwani yawezekana kabisa hao unaowalenga katika blog yako wanatoka katika kundi husika unalolionyesha dharau.

7. Kuwasiliana na walengwa wako:
Unahitaji kuwa karibu na wasomaji wako kwani kuwa na blog ni kutoa huduma. Wasomaji wako watakuongelesha kupitia comments watakazoacha kwa blog yako, au kupitia akaunti zako za mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram au WhatsApp.
Wewe mwenyewe pia unaweza kuanzisha mazungumzo nao kupitia kuwaomba wajaza fomu maalum utakazowauliza maswali.
La msingi ni kukumbuka kuwa unaanzisha blog ili uguse watu kwa namna fulani kupitia makala yako. Unapoanza kufanya uchunguzi na kuandika makala kwa umakini, unajenga imani kwa watu na watu wanategemea kukusikiliza zaidi na kutatua yale yanayowasibu. Hivyo kuwa nao karibu kwa kuwasiliana nao ni jambo la msingi.

8. Kuchambua muelekeo wa blog yako:
Ni vema mara kwa mara kujua haswa haswa blog yako inaelekea vipi,  aina gani ya watu wanasoma blog yako, wanasoma wakitokea wapi, ni aina gani haswa za posts zinasomwa , aina gani za posts zinapata likes nyingi au kuwa shared au watu kucomment.

9. Ifanye blog yako ipatikane kupitia Google:
Ili upate watu wengi zaidi kufika kwa blog yako unahitaji kuandika na kuandaa blog yako kiasi kwamba mitandao ambayo husaidia watu kupata taarifa mtandaoni iweze kupata taarifa zako. Hapa nazungumzia kuwa iwe rahisi mtu akisearch kitu fulani kwa Google, basi Google imuonyeshe blog yako. Mbinu hii maalum ya kufanya blog yako iwafikie watu wanaosearch huitwa kwa kitaalamu SEARCH ENGINE OPTIMIZATION (SEO).
Mfano watu wengi waliokuja kwa blog yangu ya Mbuke Times na nikawahudumia, ni kwa sababu walikua wanasearch mambo fulani kwa Google mfano wengine wameniambia walikua wanasearch kuhusu kujifunza English , ndio wakaona Google imewaambia kuhusu Mbuke Times.
Mfano wa jinsi mtu anavyoweza kusearch akaiona blog yako hapo mtu anasearch jinsi ya kujifunza English na Mbuke Times inaonekana katika majibu. Unaweza kufikia hivi kwa kitu tunachoita SEO


Hitimisho na ANGALIZO
Yote hayo yanawezakana endapo utaanza vema na kuchambua aina gani ya posts au blog unataka kuwa nayo na akina nani haswa unawalenga. Makala hii ni kwa ajili tuu ya maelezo ya jumla si kama ushauri binafsi.

Kama unahitaji ushauri binafsi na msaada zaidi wa jinsi ya kuchambua wazo lako la blog, kusaidiwa jinsi ya kuandikisha na kutengeneza blog yako ipendeze, au kujua namna ya kuandika makala zitakazopendwa au kuchambua muelekeo wa blog yako, tafadhali wasiliana nami kwa WhatsApp +57 301 297 1724 au kwa email john.myungire@gmail.com
Nitafute pia ili nikusaidie jinsi ya kufanya SEO kwa blog yako na namna ya kutengeneza BRAND.
Share:

4 comments: