TAFAKARI NZITO YA WIMBO WA MRISHO MPOTO : WAITE

Mrisho Mpoto. Picha na Wikipedia
Fans TAFAKARI yetu leo inahusu wimbo wa WAITE wa MRISHO MPOTO. Angalia   wimbo huu  YOUTUBE bofya HAPA
Kwa ujumla wimbo huu unazungumza NINI CHA KUFANYA UKIWA UMEKOSEA pia nafasi ya MARAFIKI ZAKO au WATU WA KARIBU katika KUANGUKA KWAKO.
--Nini cha Kufanya ukiwa UMEANGUKA?: Mrisho anasema kama umekosea basi kuendelea kukosea hakusaidii kutatua jambo. Ndio maana anasema " Mjomba Chutama, Muungwana akivuliwa nguo huchutama" -yaani ili ajisitiri). Huu ni ujumbe muhimu sana kwani wapo wengi wanapokosea badala ya kutafuta namna ya KUJISITIRI wao ndio wanazidi kuharibu kwa kufanya mabaya. Mojawapo ya njia ya "kuchutama" ni kuomba msamaha, ni kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wale uliowakosea. Ni kutafuta namna ya kutorudia tena kosa ulilofanya.
--Na Mrisho anasisitiza hilo anapomtaka mjomba awaite hata wale ambao wanaonekana kumkimbia. Anataka mjomba ajieleze kuwa kosa lilikuwa lake, na kwamba la msingi ni kukubali kosa, mambo yataenda. Ndio maana anasema " Usikubali kutenganishwa na MTO wakati kuna NGARAWA. Yaani usikubali tuu kubaki kuwa mwenye makosa bila kusuruhisha na kusitiri taswira yako mbele za hao uliowakosea. Na inabidi kweli ukubali na kuamua toka moyoni sio tuu juu juu ndio maana anasema "Muungwana hanuni kwa mashavu hununa moyoni."
--KUHUSU MARAFIKI NA WATU WA KARIBU: Tunaweza jikuta tunafanya mambo mengi yasiyo na msingi mbele ya rafiki zetu na wala wasitustue kuwa tunakosea kwa kuwa mbele yao sisi ndio tumejifanya kuwa WENYE NGUVU kuliko wao. Hivyo wao wanajiona dhaifu kutukosoa. Tena wengine wanaweza kutoa sifa zisizo na msingi kama anavyosema Mrisho khs waandishi wa habari " Msiba ulifana kweli , hakuna aliyelia nje ya key".
Hii ina maana kuwa pamoja na kupokea sifa toka kwa watu, sio kila sifa ni nzuri kweli wengine wanakupa sifa ili mradi tuu.
Ila jukumu la KUONGOZA MAISHA yako ni lako mwenyewe, mtu wa kwanza wa kumjadili unapogundua umekosea ni wewe mwenyewe -na kuna wakati utabaki wewe mwenyewe kuhangaika na matokeo ya uzembe, ujinga au bahati mbaya yako. Ndio maana anasema " Mwiba wa Kujichoma Hauna Pole"

Share:

0 comments:

Post a Comment