Chukulia wewe ni mwanafunzi wa sekondari, umesoma kwa nguvu zako zote ili kufaulu na kufikia kiwango kilichowekwa na shule tuseme wastani wa 55%, hata hivyo pamoja na juhudi zako zote umefikia wastani wa 53% hivyo haujaweza kupita kwenda ngazi ya juu. Unahitaji kurudia mwaka.
Bila shaka utajisikia vibaya. Hivi ndivyo hata maisha yetu yasiyo ya shule yanavyotuadhibu, na wakati mwingine ni wewe mwenyewe unajipa adhabu kwa kutojithamini pale unapokosea jambo.
Kama shule katika mfano hapo juu isivyojali uwezo wako halisi, isivyojali maendeleo yako mengine , au kama uliwahi fanya vizuri katika mitihani na mambo mengine ya shule, ndivyo wewe mwenyewe wakati fulani unajishusha kwa kujiona haufai, unajikatisha tamaa kwakuwa umekosea jambo fulani. Unaona kama vile dunia ndio imeshafika mwisho.
Leo hii nakutaka utafakari upya makosa yako. Makosa yako hata kama ni makubwa kiasi gani kama kupata hasara ya biashara, kupoteza ajira, kufeli shule, makosa hayo yote hayamaanishi kuwa wewe SI KITU. Hayamaanishi kuwa HUWEZI kufanya bora zaidi ya hapo. Kumbuka mazuri uliyokwisha wahi fanya,kumbuka uwezo wako mwingine, kumbuka watu wanaokupenda na kukutegemea, kumbuka ndoto zako za kimaisha, usitishwe na kosa moja ulilolifanya.
Usijiwekee WASTANI wa kufeli na kufaulu ili ukifeli ujirudishe nyuma. Badala yake kukosea kwako kuwe changamoto ya kufanya makubwa zaidi. Na kizuri zaidi ni kuwa UNAWEZA KUWA vyovyote ukiamua na kufanyia kazi uamuzi wako.
Usikubali pia kukatishwa tamaa na kuambiwa hauwezi. Hayo ni mawazo ya watu wengine, huo ni mtazamo wao pengine ni kwa sababu ya tabia zao, pengine wao walijaribu wakashindwa, pengine ndivyo tuu walivyoaminishwa siku zote bila kufikiria tofauti, ila wewe sio wao. Wewe waweza amua tofauti, wewe waweza fanya tofauti.
Nikuache na msemo huu wa Kevin Walker :
“You are not worthless. Even if you've been called that your entire life.”
"Wewe ni wa thamani , hata kama umekuwa ukiitwa usiye na thamani maisha yako yote "
0 comments:
Post a Comment