BORESHA MALENGO YAKO KUPITIA MUONGOZO HUU

MUHIMU KUJUA KUWA
Katika kuweka malengo au ndoto yako kimaisha kuna mambo haya usiyasahau:-

1. Kitu cha kipekee: Inalipa sana kama kile unachotaka kuwa, vile unavyojifikiria uwe , basi kiwe au uwe wa kipekee.  Haimaanishi kwamba ni lazima ugundue kitu kipya duniani, yaani hata kuweza kuboresha kilichopo, kuwa na mtindo bora zaidi wa kutoa huduma au bidhaa fulani, ni upekee pia. 
Fanya bidii ujitofautishe. Mfano nimekuwa nikijaribu sana kuitofautisha Mbuke Times na blog nyingine, ingawa kiukweli MBUKE TIMES ni blog tuu kama blog nyingine,inaandika mambo mengi kama ya blog nyingi ila waweza jua utafauti wake , au sio ?

2: Uwezo wako: Mara nyingi hakikisha unajitambua vema ni nini haswa unaweza na kwa namna gani utaweza kutumia uwezo wako huo kufanya kitu cha msingi. Usiwe na kasumba ya watu wengi ambapo wao mara nyingi hujiona hawawezi, huangalia zaidi mapungufu yao. 
Jiulize na tafuta muda wote kujua ni nini haswa unaweza. 
Mfano mie nikitafakari maisha yangu toka shule nilipenda kufundisha wenzangu, nina uwezo wa kusoma vitu vingi ndani ya muda mfupi,  kuelewa kwa haraka, na naelewa vema nikijifundisha mwenyewe kuliko kukaa darasani. Nimetumia kujitambua huku kuandika MBUKE TIMES kwani ninasoma vitu vingi na kuandika kwa tafakari ya kipekee.

3; Madhaifu yako: Ni muhimu kujua kuwa ni nini hauwezi. Hata hivyo kutokuweza huko kusikufanye ujione hautoweza kufanikiwa. Bali tumia kujua madhaifu yako kwa mambo mawili makuu. 
Kwanza: Kujipanga ili kuondoa madhaifu hayo. 
Mfano nilipoanza kuandika blog sikuwa najua kabisa mambo ya coding yaani JavaScript, HTML na CSS. Nilitamani kuwa na blog ya muonekano mzuri. Nilijaribu kuwaomba watu waniboreshee ila wengi walinipiga kalenda. Hii ilikuwa changamoto, nikajifunza mpaka leo nimeweza na ninasaidia wengine.
Pili: Ukijua madhaifu yako, utaweza jua yapi haswa uweke nguvu na wapi usiweke nguvu, hii itakusaidia uwe na ufanisi. Mfano mie najua wazi pamoja na kujua Adobe Photoshop, bado sio mtaalamu wa kutosha. Ntaendelea kujifunza ila kwa sasa ni bora nitumie zaidi PowerPoint kutengeneza picha nyingi ninazotumia kwa blog kuliko kukomaa na photoshop na kupoteza muda mwingi wakati muda huo naweza tumia kuandaa makala bora kabisa. Kuna wakati ninapohitaji haswa ubunifu mkubwa wa Photoshop huomba marafiki kama vile Francis Mtey wa TANZANIANEWS.COM.

4: Fursa zilizopo na zinazoweza kujitokeza: Ndio ni muhimu kuwa na ndoto fulani kubwa hata hivyo isikufanye ukaacha fursa mbalimbali zinajitokeza nje ya ndoto yako. Pia jaribu kuangalia mazingira unaweza kukuta mambo mapya yanakuja. Mfano sikuwahi kuwa na lengo la kuandika kitabu cha HTML na CSS. Ila jinsi mazingira yalivyo na umuhimu wa ufahamu huu nimeandika na kusaidia wengi walio nunua. Hata wewe waweza nunua ni Tshs. elfu 6 tuu. Unalipia kwa mtandao wa Tigo Pesa au Mpesa kisha Bwana Mushi atakutumia kitabu kwa email. Namba zake ni Mpesa: 0755872462, Tigopesa: 0713643703.

5: Uchanganuzi wa ndoto au lengo katika mafanikio madogo madogo:
Ni muhimu kuwa na lengo kubwa halafu ukaligawa lengo hilo kwa vilengo vidogo vidogo ili kufikia lengo kubwa. Wengi hufanya kosa la kuwa na lengo moja tuu kubwa , bila kuwa na vilengo vidogo vidogo vinavyoweza kujikusanya kufikia lengo kubwa. 
Mfano nina lengo la kuwa na biashara kubwa bongo, na pia kuendelea kuwa mshauri wa kimataifa wa mambo ya management. Siwezi kusubiri mpaka niwe na fedha nyingi eti ndio lengo langu litimie. 
Nimeligawa kwa visehemu vidogo vidogo, mfano hata kuwa na MBUKE TIMES ni kalengo kadogo cha kufikia lengo kubwa. Kwani kupitia MBUKE TIMES najifunza mengi na kukutana na wateja wangu watarajiwa na mtandao na watu mashuhuri kama vile William Malecela wa Dar es salaam - BLOGU YA WANANCHI, au dada Jestina George Meru wa Uingereza anayeendesha blog ya JESTINA GEORGE
Pia najenga Mbuke Times kama  chombo cha habari ambacho kitasaidia kutangaza bidhaa zangu nitakazoziuza nikiwa mfanyabiashara mkubwa.
Picha ya Jan 2013 nikiwa na William Malecela kushoto wa kwanza, na
rafiki yangu Twaha Bahrain kulia , afisa wa SIDO.
Sijawa bado mfanyabiashara au mshauri wa uongozi wa biashara wa kimataifa, ila malengo madogo madogo ya kufikia huko yanatimia siku hadi siku ikiwemo kuishi nje ya nchi (nimeishi Afrika Kusini na hapa Colombia) kupata ujuzi na uzoefu wa kimataifa ni sehemu tuu. Hii tunaita KUISHI NDOTO YAKO. Yaani hata ukiwa na ndoto kubwa na ukakuchukua muda kuifikia bado una vitu vinavyofanya maisha yako yawe ya thamani na ufurahie maisha.

6: Kuwa mvumilivu na kukumbuka picha kubwa ya kile unachotaka kukipata: 
Ukishakumbuka picha kubwa ya vile unavyotamani kuwa , hautopata shida ya kuvumilia changamoto za hapa na pale. Mambo yatakuwa magumu ila usikate tamaa, usipoteze mwelekeo. 
Inaweza kukubidi kubadili mbinu na mikakati hata hivyo haimaanishi kuwa umepoteza muelekeo wako. Mfano kwa takriban miezi minne nilisimamisha kupost kwa blog ya MBUKE TIMES kwa kuwa haikuwa inapata wasomaji wengi. Ilikuwa haizidi wasomaji 250 kwa siku. Ilinipasa kutafuta mbinu mpya. Ila sasa wasomaji kwa siku ni zaidi ya 700 baada ya kuibuni upya. 
Natumaini wataongezeka zaidi. Lengo sio kufikia wengi kama zile blog za UDAKU, kwani najua aina ya makala zangu si za wasomaji wengi. Ila lengo ni kuboresha ili watu wengi zaidi wasome.
--Kila la kheri katika ndoto yako.
Share:

0 comments:

Post a Comment