Utaona pichani hapo chini kuna maeneo tofauti nchini Afrika Kusini watu wanaishi kwenye nyumba za udongo ( picha no3) –na sio kijijini, ni mjini kabisa, pembezoni tuu mwa mji. Kuna wanaohangaika barabarani kutafuta riziki zao ( picha no1).
Lakini pia kuna sehemu ni nzuri na maendeleo makubwa, na wapo kweli wanaoishi kwa raha sana. Kama uonavyo picha ya barabara za juu mjini Port Elizabeth ( picha no2), na mojawapo ya mtaa ndani ya jiji la Cape Town ( picha no4).
1. Ajira: Ukifuatilia habari za mataifa mengi, ni kuwa ukosefu wa
ajira ni tatizo sugu duniani. Hata hivyo kuna aina za ajira ambazo bado zina
idadi ndogo ya watu wenye ujuzi husika. Mfano wa ajira hizo ni aina nyingi za
uhandisi – iwe wa uhandisi wa umeme, ujenzi , madini, n.k. Hivyo basi zingatia
yafuatayo kuhusu kupata ajira nje ya nchi:
Hata huko nje ya Tanzania, kuna
wazawa wa nchi husika ambao wanahangaika kutafuta ajira , na pia wana viwango
vya elimu kama digrii, diploma, n.k Hivyo jiulize wewe una ujuzi na uzoefu wa
kipekee wa namna gani utakaokuwezesha kupata ajira huko nje ya nchi ? Na je
unavyo vibali sahihi vinavyohitajika kukuruhusu kufanya kazi kwa uhalali katika
nchi husika. Usipokuwa na kibali husika, maisha yako yatakuwa ya wasiwasi na
magumu kwa kuwa hautopata kazi ya maana , na pia utakosa huduma nyingi muhimu
kama vile huduma za kibenki.
2. Malazi: Kupata chumba au nyumba ya kuishi ni jambo gumu na la
gharama karibu katika kila maeneo yaliyoendelea, na kama wewe unatamani kuishi
nje ya Tanzania, bila shaka unahitaji kuishi eneo bora na la usalama. Haileti
maana kama sehemu utakayoishi nje ya Tanzania itakuwa mbaya , na duni
ukilinganisha na unayoiacha Tanzania. Pengine unapoishi Tanzania ni bora kuliko
eneo na nyumba utakayopata huko nje ya Tanzania.
Usisahau, sehemu nzuri ya kuishi
ni jambo la muhimu hata kwa wazawa wa nchi unayofikiria kuenda kuishi, hivyo
jipange vya kutosha, usitemee urahisi rahisi.
3. Burudani: Burudani na starehe za kila namna zipo kama zilizopo
bongo, kwa maana ya kwamba starehe ni gharama pia. Kwakuwa lengo lako la kuenda
nje ya Tanzania sio kufanya starehe, utajiheshimu na kuwa na kiasi katika hilo, kwani usipoangalia
unaweza kujisahau kwa kujiona upo huru kufanya yoyote unayoona yanakufaa
kwakuwa huko nje ya Tanzania hakuna atakayekuhoji. Wengi wamekumbwa na hili na
kupoteza muda na pesa nyingi nje ya Tanzania kwa starehe, kwa kushindana au
kufuata mkumbo wa kustarehe kusiko na mpango.
4. Msaada bongo: Kumbuka kuwa ni watu wachache au pengine hakuna
kabisa ambao wanaweza kukataa msaada, na kuwa wengi wanatarajia kuwa unapoenda
kuishi nje ya nchi maana yake umeona maisha huko ni bora zaidi ya Tanzania,
hivyo upo kwenye nafasi ya kuwasaidia hata wao waliobaki Tanzania. Hata hivyo,
ukweli wa hali ya kifedha utakayokuwa nayo huko nje ya nchi, ni wewe mwenyewe
ndio unaujua. Hauwezi kuwapendeza watu wote, na pia wewe ndio mwenye kujua
mkakati wako wa kimaisha na bajeti yako ya kifedha ipoje.
5. Inakuhusu wewe: Wewe ndie mmiliki wa maisha yako, na unalitambua
hili hata katika kutafakari kwako kwanini uende ukaishi nje ya Tanzania. Kwa
maana hii basi tumia muda wa kutosha kuchunguza usahihi wa kuishi nchi husika,
na hata utakapoamua kuenda kuishi nchi fulani, ni wewe ndio unayeishi huko na
usisahau picha kubwa ya nini unataka kufikia katika maisha yako. Usiishe huko
nje ya nchi kwa kuwapendeza watu , na wala usiogope inapobidi kurudi Tanzania
kwani ni maisha yako, na wewe ndio uliyeamua kwa mara ya kwanza kuenda nje, na
wewe haukuishi kwa mashindano au kwa kutaka ‘kuwauzia sura’ watu wengine.
6. Faida za msingi: Katika kufanya kwako maamuzi ya kuenda kuishi nje,
ni busara kupima faida na hasara za kuishi nje ya nchi. Faida za msingi za
kuishi nje ya nchi ni kupanua ufahamu wako kuhusu changamoto na fursa za
kimaisha, utaweza pia kupanua mtandao wako, na zaidi sana ukiwa na kipato cha
kutosha na kuwa na nidhamu ya kimaisha utaweza kujiwekea akiba ya fedha
itakayokusaidia maishani mwako.
0 comments:
Post a Comment