Vitabu vya dini vinasisitiza tutafute elimu, na
katika Biblia (Hosea 4:6) kuna andiko linasema kuwa watu wanaangamia kwa kukosa
maarifa. Hivyo basi ni wazi kuwa tukifanya bidii katika kuboresha ufahamu wetu,
tutaweza kutatua changamoto nyingi, na tutaweza kuishi maisha yenye furaha na
maendeleo.
Lengo la makala hii sio kusisitiza umuhimu wa
kupata maarifa, bali makala hii inalenga kukudokeza mambo ambayo yanaweza kuwa
adui yako katika juhudi zako za kutafuta maarifa.
Ifuatayo ni orodha ya mambo 6 kama yanavyotajwa
na mtaalamu wa elimu ya jamii Earl Babbie katika kitabu chake “The Practice of
Social Research” (2010), 12th edition, ukurasa wa 4-8.
Nimeongeza maelezo ya ziada katika points hizi
toka kwa Babbie, ili kuboresha ufafanuzi kwa ajili yako:-
1. Tamaduni zetu: Sote tumejikuta tukiamini aina fulani ya
maarifa kutokana na jinsi tamaduni zetu zinavyotuambia , na kwakuwa hivyo
ndivyo kila mtu anavyofahamu, basi hatuoni haja ya kuhoji usahihi wa mambo
husika, hata kama pengine si sahihi. Ingawa ni kweli kufuata tamaduni ni jambo
jema, kuna hasara ya kutufanya tuwe wavivu wa kutafakari zaidi na kutafuta
maarifa zaidi, na jambo baya zaidi ni kuwa tamaduni zinaweza kutufanya tukawa waoga
wa kutafuta maarifa tofauti, kwani kufanya hivyo tutaonekana kuwa ni ‘waasi’ wa
tamaduni. Kumbuka lugha, na dini zote ni sehemu ya tamaduni tulizorithi.
2. Mamlaka: Ni mazoea pia kufuata maarifa ya watu ambao tunawaona ni ‘viongozi’
katika jamii zetu. Wawe ni watu maarufu, wanasiasa, viongozi wa dini, au
‘wasomi’ wa vyuo vikuu. Kwa mpango huu , ni rahisi kwetu kukataa maarifa ya
watu ambao hawana ‘mamlaka’ yoyote. Tatizo katika hali hii ya kufuata mamlaka
ni kuwa kuna nyakati tunaweza tusipate maarifa sahihi, au tukajikuta hatufuati
kweli maarifa kwa sababu ni maarifa bora, bali ni kwa sababu tunaangalia zaidi
nani katoa maarifa husika. Ni rahisi kwa
mfano, kumsikiliza na kumuamini kiongozi wa kidini akitoa ushauri wa biashara
kuliko kumsikiliza mfanyabiashara mdogo ambaye anao uzoefu wa miaka zaidi ya 10
katika biashara. Pia ni rahisi kuamini na kufuata mambo unayosoma kwa blogu ya
mtu maarufu, kuliko kusoma blogu kama hii ya MBUKE TIMES, kwakuwa si ya mtu
maarufu.
3. Kutokufuatilia mambo kwa umakini: Mara nyingi huwa tunajikuta tunafuatilia mambo
juu juu,hivyo kutokupata taarifa zote na taarifa zilizosahihi. Mbaya zaidi
unaweza kukuta mtu akipinga au kushutumu jambo ambalo hajalifuatilia kwa
umakini. Mfano mzuri katika hili ni
namna ambavyo tunasoma magazeti au taarifa za mitandaoni. Je, huwa unatumia
muda kupata taarifa zote kwa usahihi, kuchunguza kama habari ni muendelezo wa
habari nyingine, au itafuatiwa na habari nyingine. Je, unaelewa maneno ya
msingi katika makala husika unayoisoma ?. Kutokufuatilia mambo kwa umakini
hujitokeza pia hata katika kutazama kwetu, je tunajifunza nini kutokana na
mazingira tunayoyaona, rangi, aina ya mavazi , n.k ya watu tunaokutana nao ?
4. Kutoa maamuzi ya jumla isivyo sahihi: Mara nyingi tumejikuta tukifikia hatua ya
kuamini ‘ukweli’ fulani kwa sababu ya
kujirudia rudia kwa jambo, hivyo tukiamini kwakuwa tuu jambo limejirudia
rudia mara nyingi, au kwakuwa watu wengi wana mtazamo unaofanana, basi jambo
husika ni sahihi kwa watu wote, hivyo maarifa yetu yanajengwa katika imani au
mtazamo usio sahihi. Mfano kwakuwa mara nyingi ukiwa na haraka na ukafika
kituoni usikute daladala, na kwakuwa jambo hili huwatokea watu wengi, inaweza
kusemwa kuwa ‘aah, ukiwa na haraka sikuzote hautokuta daladala kituoni’. Pia kuna nyakati kutokana na aina ya
mazingira tuliyonayo, aina ya watu tunaoishi nao, tunajikuta tukijiaminisha
kuwa watu wengine mahali kwingine ni lazima watakuwa na tabia kama hizo. Ubaya
wa aina hii ya kujenga maarifa yetu ni kuwa, inatufanya nyakati nyingine kupata
maarifa yasiyo sahihi, na inatufanya kuwa wagumu kubadili mtazamo wetu. Chukulia
mfano, kuna watu wanaamini kuwa blogu za kibongo hazina habari za msingi zaidi
ya siasa, na udaku, na kwamba nyingi habari zake ni copy & paste, na
hazijafanyiwa uchunguzi. Kwa imani hiyo, watu hao hawawezi kukuelewa kuwa kuna
blogu kama MBUKE TIMES ambayo haipo hivyo wanavyodhani.
5. Kuchagua
mambo ya kuchunguza: Kuna nyakati
tunajikuta tunafanya uchaguzi wa aina ya mambo ya kutafakari kutokana na
misukumo kadhaa katika maisha yetu, iwe kwa sababu ya tamaduni zetu, hasira,
furaha, kuzoeana na watu , au taarifa za awali ambazo tunazo kuhusu watu au
jambo fulani. Hali hii huwa ni tatizo katika utafutaji wetu wa maarifa sahihi,
kwani tayari tunajiwekea kikwazo cha kupata maarifa zaidi. Mfano, kwakuwa
umejiaminisha kuwa siasa ni uongo, basi unajikuta hautaki kusikiliza mtazamo wa
wanasiasa, hata kama pengine wapo sahihi. Au kwakuwa wewe ni wa chama fulani
cha siasa, basi unajikuta hautaki kusikiliza wala kutafakari hoja na mitazamo
kutoka upande wengine wa siasa au wale ambao hawafungamani na siasa.
6. Ku
‘reason’ kusiko sahihi: Mara
nyingi tunajikuta katika hali ambazo tunashindwa kuzielezea kwa urahisi , hivyo
kujikuta tukibuni sababu za kutokea au kuwepo kwa hali husika. Kuna sababu nyingi za uwepo au kutokea kwa hali
fulani fulani ambako kwa kweli sababu hizo si sahihi, endapo utatafakari kwa
undani utaona kuna uwezekano mwingine mwingi ambao bado hatujauangalia katika
ku ‘reason’ kwetu.
Mfano 1: Utasikia mtu akisema ‘Aaah sawa tuu,
niache niwe masikini kwakuwa sote hatuwezi kuwa matajiri, lazima wawepo
masikini na matajiri’. Ku ‘reason’ huku
si sahihi kwakuwa kwanza hakuna ufafanuzi wa kutosha kuwa tatizo gani litatokea
kama wote tutakuwa matajiri ? . Je, kama watu wote kuwa matajiri ni jambo lenye
tatizo, kwanini basi tunaamini katika swala la Ahera /mbinguni, kwakuwa huko,
bila shaka masikini hawatokuwepo.
Mfano 2: Utasikia mtu akitetea kutupa
takataka ovyo mjini au tuseme
barabarani, kwa kisingizio kuwa anasaidia kutengeneza ajira kwa watu wa jiji !.
Hii nayo ni aina ya ‘reasoning’ isiyo sahihi, kwani si kweli kuwa kama jiji
litakuwa safi, basi ajira zitapungua, na si kweli kuwa watu wanaopata ajira
katika kusafisha jiji, hawawezi kupata aina nyingine ya ajira, kama vile
kuzibua mitaro, kutunza bustani, kusaidia kazi nyingine za usafi wa majengo
n.k. Zaidi sana, kuna ushahidi wa kutosha kuwa ipo miji ambayo ni misafi, na
bado halmashauri za miji hiyo, zimeajiri watu kwa shughuli mbalimbali zikiwemo
shughuli za usafi.
0 comments:
Post a Comment