Baadhi ya watu wamekumbwa na tabia ya kuahirisha mambo ya msingi
bila kuwa hata na sababu ya msingi ya kuahirisha huko. Wengine ni uvivu wa
kuanza au kuendeleza jambo fulani. Zipo sababu nyingi kwa nini uvivu au
kuahirisha huko hutokea. Wengine huwa ni kisingizio maarufu cha kuwa wapo
‘bize’ sana, wakati wengine ni kwa sababu ya kujiachia- yaani kuridhika na hali
waliyo nayo sasa (tunasema watu wa aina hii wapo kwenye ‘comfort zone’).
Makala hii inachambua mambo matano (5) ambayo ukizingatia unaweza
kushinda uvivu, kuridhika na kuahirisha hairisha mambo ya msingi bila sababu ya
msingi:-
1. Weka picha ya maisha mapya: Fikiria vile maisha yako yatakavyobadilika kutokana na kufanikiwa
katika jambo ambalo sasa unakuwa mvivu kulifanya au unalifanya kwa kusua
sua. Pengine maisha yako yatabadilika
kwa kuongeza mtandao wa watu muhimu katika maisha yako, pengine kipato chako kitaongezeka,
pengine jina lako litakua na sifa kwako zitaongezeka, pengine utajitengeneza
uhuru wa fikra n.k
2. Tambua wajibu ulionao kwa
watu wako wa karibu: Jambo la msingi unaloona uvivu
kulifanya au kuliendeleza kiasi kwamba unajikuta unaahirisha mara kwa mara,
linaweza kuwa watu walio karibu nawe wanakutarajia ulifanye. Mfano , pengine
umetoa ahadi ya kufanya jambo husika, pengine ni jukumu la kikazi, pengine
jukumu la kibiashara, kifamilia, au hata
jukumu la kimapenzi (kuwa kufanya kwako jambo husika kutatimiza matarajio ya
mpenzi wako).
3.Tambua wajibu wako wa
kiroho: Kumbuka pia una jukumu la kiroho la kutenda
mambo ya msingi na kuwa mtu wa msaada kwa wanaokuzunguka na dunia kwa ujumla.
Haijalishi wewe ni wa dini gani, sote tuna jukumu la kuwa wa msaada kwa
wenzetu. Hivyo kama kuanza au kuendeleza jambo unalotakiwa kufanya – iwe
kujiendeleza kwako kielimu, kuanzisha biashara,kubadili tabia fulani iwe bora
zaidi, n.k , tambua kufanya hivyo
hakutakunufaisha wewe peke yako, bali kutanufaisha wengi.
4.Fikiria ‘maadui’ zako: Kumbuka kuwa kuna watu ambao
wangependa kukuona haufanikiwi, hawa ni ‘adui’ zako. Hivyo kwa kadri
unavyoahirisha mambo yako ya msingi au kuwa mvivu katika kuanza na kukamilisha
mambo hayo, tambua unatengeneza nafasi za ‘ushindi’ kwa adui zako.
5.Jiambie unaweza: Ukiwa na mashaka ya kuweza kuanza au kuendeleza jambo unalolitamani
au kulitafakari itakuwa ngumu pia kuanza jambo husika. Hivyo kujikuta
ukiahirisha au kuwa mvivu tuu wa kuanza na kuanza au kuendeleza jambo husika.
Watu wengine wanaweza ‘kukupa moyo’ katika jambo fulani, hata hivyo wewe
mwenyewe ni muhimu ujione –utengeneze picha ya akilini , kuwa umekamilisha
jambo husika kwa mafanikio.
Asantee maudhui MAZURI mnayochapisha. www.tenachew.com
ReplyDelete