Ukisoma kwa kutafakari makala
hii utagundua kuwa kuweza kujifahamu sisi wenyewe vema, kuweza kujitawala sisi
wenyewe, na pia kuweza ‘kuwasoma’ vema wenzi wetu , ni mambo ya msingi sana ili
upendo tulionao uweze kudumisha mahusiano.
Msisitizo ni kwamba, pamoja na ukweli kuwa upendo ni kitu cha
muhimu katika mahusiano, makala hii inaeleza kuwa kutegemea upendo pekee kama nguzo kuu ya mahusiano bora
kunaweza kuwa jambo la hatari kwa mahusiano, kwa sababu zifuatazo:-
1. Binadamu ni kiumbe huru: Ni muhimu kukumbuka hili hasa kama
unadhani kwakuwa unampenda fulani na umemuonyesha mapenzi yako yote basi hicho
ni kama kifungo kwake kuwa hatoweza kutoka katika penzi lenu. Kwa asili
binadamu ni huru, na anaweza kuamua kuutumia uhuru wake kufanya maamuzi mengine
yoyote tofauti na unavyofikiri ni lazima afanye. Kwa kuwa pia ni mbinafsi, basi kama upendo
wako wote kwake hauendani na yale anayotazamia , unaweza kukuta ameshindwa
kukaa katika penzi , ambalo kwa watu wengi wanaona kuwa ni penzi zito.
2. Binadamu ni mbinafsi kwa asili: Binadamu kwa asili huangalia maslahi yake
kwanza kabla ya kuangalia ya mwingine. Mfano dhahiri wa ubinafsi huu ni pale
inapotokea ajali , mara nyingi mtu huwaza kujiokoa mwenyewe kwanza kabla ya
kufikiria wa karibu yake. Tumesikia habari za mama mzazi kuacha kitoto kichanga
ndani wakati moto ukiendelea na yeye kutoka nje. Kuna habari pia za mama
kumtumia mtoto wake kama ‘kifaa’ cha kuvunjia kioo cha gari , ili aweze
kujiokoa, pale ambapo ajali ilitokea. Hivyo upendo tuu pekee hautoshi kumfanya
mtu aendelee kukaa katika ndoa au mahusiano kabla ya ndoa (uchumba), ni muhimu
yawepo mambo mengine yenye manufaa kwa mtu husika.
3. Binadamu ana mahitaji mengi na yasiyo na kikomo: Mwenza
wako ana mahitaji mengi na yanaongezeka na kubadilika siku hadi siku
kutegemeana na mabadiliko mbalimbali kama vile hali ya hewa, aina ya kazi, watu anaokutana nao, mabadiliko ya
teknolojia, mabadiliko ya kiuchumi n.k. Upendo wenu, hausimamishi mahitaji haya
yasitokee, na kwamba upendo pekee hauwezi kuwa jibu la kutimiza mahitaji hayo. Inahitajika
bidii katika kujituma kujiletea kipato, kuwa na mawasiliano bora kati yenu, kutambua
mabadiliko na kuchukua hatua kabla mabadiliko hayajawabidilisha, na zaidi sana
muweze kuwa na utamaduni wa kupanga mambo pamoja na kuwa waaminifu katika
kutimiza yale mnayopanga.
Chukulia mfano, wa wanandoa walioishi vema kwa miaka
5 ya ndoa, halafu ndoa ikaanza kulemaa kwa kuwa mmoja wao anaona hakuna
uwajibikaji katika kumsaidia mwengine kujiendeleza kielimu, kibiashara, au
kutimiza ndoto nyingine ambayo mwanandoa amekuwa nayo.
4. Binadamu wengi wanashindwa kujitawala: Uwezo wa mtu kujitawala unaweza ukakinzana na
upendo wake kwa mwenza wake, hivyo kuleta hali ya kutoridhika kwa mwenzi wake,
kitu ambacho kinapunguza au pengine hata
kuondoa raha ya mahusiano.
Mfano utakuta kwa kufuata makundi ya marafiki
aliyonayo, mwanaume anakuwa mlevi wa kupindukia, na kujikuta akiingia katika anasa na maamuzi
mengine yasiyo mazuri kwa mpenzi wake na familia kwa ujumla. Hata hivyo
mwanaume huyo huyo ukimuuliza kama anampenda mke wake au la, atakujibu
anampenda sana. Tatizo nini ? Utajibiwa, ni pombe tuu ndio mmemtawala, na
kwamba jamaa ana ‘kampani’ mbaya.
5. Maana isiyo sahihi ya upendo: Kuna wengi wanaodai wanao upendo lakini
kiukweli walichonacho sio upendo bali ni tamaa au matakwa ya kuhitaji
kutimiziwa mambo fulani.
Maana halisi ya upendo sio vile unavyotaka fulani
akufanyie mambo au jambo fulani, upendo sio vile unavyojisikia baada ya fulani
kukutendea jambo uliloliona jema kwako, upendo sio vile fulani anavyokufanya
ujisikie kwa sababu ya sura yake au umbo lake, BALI, upendo ni utayari wako
wewe kufanya mambo yanayompendeza mwingine, kuwa tayari kuona mwingine ana
furaha juu yako.
Kwa maana rahisi ,
upendo si jambo linalokuhusu wewe unajisikiaje, bali ni vile unavyotaka
mwingine ajisikie.
Kwa maana nyingine,
utatimiza vema upendo wako kwa kujitahidi kumfahamu mwenza wako, kutimiza yale
anayohitaji (ili awe na furaha) sio kutimiza yale unayotaka wewe kwa makusudio
yako binafsi. Upendo unahitaji kumheshimu mwenza wako, kumsikiliza, kumfanya
akuamini, na aendelee kukuamini.
Pamoja na kuwa
hisia za kimwili (chemistry) ni muhimu sana katika kujenga mahusiano yenu, hisia za kimwili zisichanganywe na upendo.
Kwakuwa
fulani amekuvutia kimwili haina maana kuwa basi unampenda mtu huyo.
Kufanya
tendo la ndoa, sio lazima iwe ndio ishara ya uwepo wa upendo katika yenu, kwani wapo hata wanaofanya
tendo la ndoa kama biashara.
Hitimisho
Mahusiano hususani mahusiano ya kimapenzi yanatutaka tuwe waajibikaji
kwa wenzetu, na kwetu wenyewe. Kuwajibika kwa wenzetu ni pale tunapojifunza vya
kutosha tabia, na yale yanayompendeza na
yasiyompendeza mwenza wetu. Wakati tunawajibika kwetu wenyewe kwa kujifunza
kuhusu mapungufu yetu, na kujituma kujirekebisha. Mapenzi yanaleta majukumu, na
bila kutambua na kutimiza majukumu husika, mara nyingi mapenzi yatageuka kuwa
karaha, badala ya furaha.
0 comments:
Post a Comment