Pilika
zetu za kupata fedha, vyeo, kujenga mahusiano na kukubalika katika jamii
zinaathiriwa na mabadiliko yanayoendelea kutokea katika jamii yetu. Makala hii
inadokeza mabadiliko 7 muhimu kuyafahamu na kuyatawala ili usije kujikuta
unapoteza furaha ya kweli ya kuishi kwa kuwa mtumwa wa fedha, mapenzi, cheo,
mahusiano au mtumwa wa ‘misifa’.
1. Uhuru wa mawasiliano: Uwepo wa mitandao
ya kijamii, kushuka kwa bei za simu na kompyuta , teknolojia ya upigaji picha
na uandishi kama vile kutumia blogs, ni baadhi ya mambo yanayochochea uhuru wa
mawasiliano kukua. Uhuru huu unaweza athiri malezi ya watoto, uhuru pia unaweza athiri usiri wa mambo yako,
na bila shaka unaathiri ufanisi wako kibiashara na kikazi pia.
Ili
kuweza kujitawala na kutawala mabadiliko haya ya uhuru wa mawasiliano,
inakupasa ujifunze vema matumizi ya teknolojia husika, au upate mtu wa
kukusaidia kusimamia mambo yako ili yasiathirike na uhuru huu wa mawasiliano.
Fahamu
yapi unastahili kufanya ukiwa mtandaoni – kwa simu na kwa kompyuta, tambua pia
nini watu wanafanya ambayo yanaweza kukuathiri. Mfano mzuri,
ni pale unapoweka picha ya mpenzi wako aliyependeza vizuri, ila picha
hiyo ukaikuta imewekwa kwenye mitandao ya ngono.
Mfano
mwingine, usipofuatilia mara kwa mara anachoandika mtoto wako mtandaoni unaweza
kushtushwa siku ukawa tagged picha binti yako aliyepo ‘boarding school’ akila ‘bata’
kwenye club ya usiku. Au kukuta ameandika status – “ Jamani, siwezi soma huyu
BF wangu kila nimfanyiacho haridhiki, nimempa hadi pocket money zangu akae nazo, ila haridhiki”.
2. Machafuko katika jamii: Hali ngumu ya kiuchumi, mabadiliko katika
uwezo wa kifikra wa watu, na ukandamizaji uliokithiri katika jamii zetu ni moja
ya sababu zinazochochea machafuko ya kila siku yanayoendelea. Hata yale ambayo
ulidhani kuwa hayawezi kutokea nchini mwetu, bila shaka utaanza kuyaona
yakitokea. Hali hii ni muendelezo wa mabadiliko makubwa katika maisha yetu.
Serikali zinazidi ‘kuchangikiwa’ kwakuwa
mabadiliko yanatokea kwa haraka sana na ni mabadiliko makubwa ambayo
hayakutazamiwa. Hivyo serikali kujibu
mapigo haya, inabidi zije na mbinu nyingi kali zinazoweza kuonekana kama ni za
kidikteta.
3. Uzalishaji
mkubwa wa ushindani wa hali ya juu: Kupanuka
kwa fikra za watu wengi, maboresho katika teknolojia, urahisi wa upatikanaji wa
taarifa, na mijumuiko ya watu toka mataifa tofauti katika nchi tofauti,ni mambo
yanayoleta ushindani katika uzalishaji. Mbinu zilizosaidia biashara fulani kuwa
kubwa miaka 10 iliyopita, zinaweza zisiisaidie biashara hiyo hiyo, au nyingine
inayofanana nayo kukua.
Wajasiriamali
sasa wanazalisha bidhaa mpya, ubora unaboresha, bei zinazidi kuenda chini, na
mbinu za kufikisha bidhaa kwa mteja zinaboreshwa. Mabadiliko haya, yanahitaji mjasiriamali sio
tuu ajue vema kuzalisha bidhaa yake, ila aifahamu vema jamii anayotaka kuiuzia
bidhaa, ajenge mtandao mkubwa na wateja wake, na zaidi sana aweze kukusanya na
kusimamia taarifa za jinsi ya kuboresha ushindani wake katika soko.
4.Utitiri wa taarifa: Maboresho katika teknolojia ya habari na
mawasiliano, yamechangia sio tuu kuwepo kwa websites na mitandao ya kijamii
(social networks) bali yamerahishisha matumizi na hata umiliki wa mitandao.
Mfano kuna blog kibao Tanzania pekee, na kurasa maelfu za Facebook. Kuna video
mamilioni kwenye Youtube.
Usipoweza
kutawala vema hali hii ya utitiri huu wa taarifa unaweza kujikuta unakuwa mtu
wa kupotoshwa, na mtu usiye mfanisi katika mambo yako ya kielimu, kikazi na
hata kibiashara. Hakuna wakati unaohitaji ujuzi wa kipekee wa kutawala muda
wako, na pia kuweza kuchambua taarifa unazozipata.
5. Maboresho makubwa katika teknolojia
mbalimbali: Si tuu upande wa teknolojia ya habari, bali aina nyingi za
teknolojia kama vile teknolojia za uzalishaji wa vyakula na teknolojia za utengenezaji
wa mashine. Mambo haya si tuu yanaleta
bidhaa mpya na kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa mambo mengi, pia yanaleta
athari nyingine ambazo inatupasa kuwa makini nazo kama vile, athari za kiafya ,
athari za malezi (kuporomoka kwa maadili), athari za kiuchumi (biashara nyingi
kuporomoka kwa kushindwa kushindana).
6. Uharaka wa usambaaji wa mabadiliko: Kwa jinsi dunia ilivyo ‘kijiji’ mabadiliko
yanayoendelea makubwa ya kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa , na kijamii
yanaathiri si tuu taifa moja ambapo badiliko fulani limetokea, bali mabadiliko
hayo husambaa kwa haraka kwa nchi nyingine. Kama ilivyo kwenye usambazi wa
bidhaa mbalimbali unavyosambaa kwa haraka – kumbuka matoleo kadhaa ya simu kama
iphone, Samsung, n.k yanavyofikia Bongo, tutarajie mabadiliko mengine
yanayotokea nchi za maghariba na barani Asia kufika kwa haraka hata Tanzania.
Hitimisho: Elimu ya darasani pekee
haitoshi kukusaidia kupita na kutawala mabadiliko haya makubwa, unahitaji
kupenda kusoma ziada.
Hakikisha
unapata taarifa sahihi kwa kufuatalia kuaminika kwa chanzo cha taarifa. Pia
tumia search engine kama Google, kutafuta vyanzo vingine vya habari vinasema
nini kuhusu taarifa unayodhani ni sahihi.
Linda
sana utashi wako kwa kuwa huo pekee ndio mali kubwa zaidi kwa maisha yako.
Ukipoteza utashi wako kwa tamaa ya mali, kufuata mkumbo n.k utajikuta unapotea
zaidi.
Kuwa
tayari kubadilika kuendana na mazingira na hali halisi – elimu, aina ya
biashara, aina ya kazi, mahali pa kuishi, mahusiano, malezi ya watoto.
Katika
nyakati tulizopo, ni muhimu sana
kuufahamu na kuuishi msemo huu “ Don’t Work
Hard, Work Smarter”yaani “ Usifanye tuu kazi kwa nguvu zako zote, bali fanya
kazi kwa akili zaidi”.
0 comments:
Post a Comment