Pamoja
na kuwa elimu ni kitu muhimu sana maishani, kwa watu wengi kitu elimu kimekuwa
ni mzigo mkubwa kiasi kwamba badala ya kuboresha maisha, elimu imekuwa ikirudisha
nyuma maendeleo. Badala ya elimu kumsaidia mtu kuwa na furaha , inamletea
huzuni. Pia, si ajabu kukuta mtu mwenye ‘elimu kubwa’ au tumuite ‘msomi’
akifanya mambo ambayo hakutarajiwa kufanya. Makala hii inachambua mambo ya
msingi ya kuangalia ili elimu isiwe mzigo kwako:-
Inatuweka njia panda: Imani kuwa kiwango fulani cha elimu ndio
msingi wa ‘kutoka’ kwako kimaisha, yaweza kukufanya ukaacha mengi ya msingi
ambayo ungeweza kufanya na kufanikiwa kimaisha, badala yake ukajikuta unataka
KWANZA upate kiwango hicho cha elimu unachodhani ukikipata ndio utaanza ‘kuishi’.
Ingawa
ni kweli kuwa elimu ni muhimu, hasa viwango vya juu vya elimu ni muhimu katika
kukurahisishia kuongeza fursa mbalimbali, haina maana kuwa mafanikio
yanapatikana kwa njia pekee ya kuwa na elimu ya kiwango kikubwa. Hivyo basi
unapojikuta upo katika njia panda ya kuchagua kufukuzia kwanza kiwango fulani
kikubwa cha elimu, hakikisha unawaza na
kutafuta njia nyingine mbadala za kupanua fursa mbalimbali kwa kutumia kiwango ‘kidogo’
cha elimu ulicho nacho.
Uwe
na mtazamo wa kuwa mzalishaji, mtu mwenye furaha , na unayeishi kwa namna ile
uwezayo kweli kweli, sio kwa kufuata matarajio ya watu wengine. Kwani baadhi
yetu hujikuta tunajikita na elimu kwa kuwa tuu hivyo ndivyo ndugu zetu ,
marafiki zetu, au familia inavyotegemea tutafanya. Au kwa kuwa unataka
kushindana na watu fulani. Usiwe mwoga wa kutokuendana na matarajio ya watu
wengine. Weka matarajio yako, na jiamini kuwa utayatimiza.
Inagharimu uhuru wa watu: Kwa baadhi ya watu, elimu badala ya
kuwaweka huru, inawafanya watumwa wa kifikra kwa namna mbalimbali, kama vile
kuamini tuu kila aliyesoma sana anachosema ni sahihi, kuamini kuwa fani yake ya
elimu ndio suluhisho pekee la matatizo au changamoto fulani, mfano mchumi
kuamini kuwa matatizo ya ajira yatasuluhishwa na mbinu za kitabuni za wachumi
waliopita.
Elimu
pia inaweza kumfanya mtu ajishushe thamani au ajione hafai kuwa na mtazamo
tofauti na yule anayemuona kuwa amemzidi ‘elimu’, hata kama ni kweli kwa
mtazamo huru , huyo anayeonekana kuwa ‘msomi zaidi’ anakosea, ila kwa kuwa tuu
ana elimu zaidi, basi wengine inabidi wajishushe na kukubaliana nae. Ni kama
vile kusema “mkubwa siku zote hakosei”.
Tumedokeza
pia, hamasa kubwa ya kutaka kiwango fulani cha elimu inaweza kumnyima mtu ‘uhuru’
wa kuangalia fursa nyingine za kimaendeleo.
Inarudisha nyuma uwezo wa kufikiri: Elimu inarudisha nyuma uwezo wa kufikiri kwa
baadhi ya watu hasa pale inapoleta uwoga wa kuwa na mtazamo tofauti na ule ambao
mtu tayari ambaye anatambulika kuwa ni ‘msomi’.
Hatari zaidi ni kuwa baadhi ya watu huogopa kuwa na mtazamo tofauti na ‘ukweli’
ambao amefanya kuusikia tuu.
Pia
kwa wale waliogemea sana fani zao, hujikuta wakitafsiri kila kitu kupitia fani
zao, na hata kama haviendani na hali
halisi, wao huona ni sawa. Hii ni
kwakuwa kwa baadhi ya watu, elimu inaleta kujiaminisha usahihi wa wayafanyayo
au wa yale wafanyao wengine wenye elimu fulani.
Inafanya watu wajitenge : Kwa baadhi ya
watu, kiwango fulani cha elimu ndio utambulisho wa thamani ya mtu, na pia
ndio tiketi ya kukubalika kwake au
kuwakubali watu wengine. Si ajabu basi kukuta mtu mwenye wazo zuri la
kimaendeleo, akipuuzwa kwakuwa tuu , kiwango chake che elimu hakidhihirishi
asemacho ni sahihi, yaani “hafanani” na anachosema. Utasikia mtu akimwambia
mwenzake bila haya “ mi siongei na wasio soma”.
Inakosesha fursa: Kwa sababu elimu kwa baadhi ya watu ni chanzo
cha kutokuwa na uhuru wa kufikiri, kwakuwa elimu inawapelekea watu hao wawe
wazito katika kufikiri kwa ufasaha, kwa
kuwa pia inawafanya watu wajitenge kwa kuwa na dharau, upo uwezekano wa elimu
kuwakosesha fursa baadhi ya watu.
Hitimisho
Lengo
la makala hii haikuwa ‘kuponda’ elimu au ‘wasomi’, bali kusisitiza kuwa elimu
inafaa ilete manufaa kwetu. Na hivyo pale unapohisi inaleta mambo tuliyotaja
hapo juu, au yanayofanana na hayo basi ni wakati wako kubadilika, au kutafuta
msaada wa jinsi ya kurekebisha hayo. La msingi sana ni kuhakikisha kuwa elimu,
pamoja na uzuri wake, haichukui nafasi ya ubinadamu wako, utashi wako na nguvu
yako kubwa ya kufanya maamuzi.
Elimu
ikusaidie kuona uhalisi katika uhalisi wake, sio ikuonyeshe hali tofauti na
kukuaminisha kuwa ndio hali halisi.
Unalo
jukumu la kuitawala elimu, na sio elimu ikutawale wewe, hii inamaanisha kuwa sio
kila kitu utakachosoma utalazimika kukiamini, na kwamba uwe tayari kukubali
kuwa mambo fulani uliyoyasoma na ukayaamini wakati fulani yanaweza yasiwe
sahihi wakati mwingine hivyo ikakubidi utafute uelewa mbadala.
0 comments:
Post a Comment