ATAKAYELETA MAENDELEO YA KWELI BONGO

Tanzania kama taifa, tuna matatizo mengi yanayosababisha kuwa na maendeleo duni, mojawapo ya matatizo hayo ni:
 
1. Kutokukubali kuwa yawezekana sie wenyewe mmoja mmoja ni sehemu ya tatizo, badala yake tupo na bidii ya kuwaonyesha wengine vidole badala ya kuchukua hatua ya kujirekebisha sie wenyewe kwa kiwango cha mapungufu yetu. 
Mfano, mtu analalamika hakuna fursa za kutosha za biashara, ila hafanyi utafiti wa kutosha wa biashara , kuboresha ufahamu wake, kutafuta wataalamu haswa wa fani husika, au hata kutafuta ushirika na wafanyabiashara wengine, badala yake anamaliza waganga wa kienyeji.

2.Wengi wetu tumesha 'surrender' kwa udhaifu wetu na udhaifu uliopo katika jamii yetu, tunajionea 'poa' tuu. Si ajabu kusikia mtu akisema  ''aaa, ndio bongo yetu hiyo, tumeshajizoeleaga utumbo huu".
Unaenda ofisi ya mtu, au hata baa, unapata huduma mbovu, haulalamiki, haukosoi, unaishia tuu kusema....aaa hii ndio bongo.

3.Tunajadili zaidi matatizo kuhusu suluhu ya matatizo. Na zaidi sana, wengi tunashindana katika namna tunavyolifahamu tatizo. Ikifika kuchukua maamuzi, na utekelezaji. Tunakuwa na visingizio kibao. 
Ni kama ile habari ya Panya kumkamata Paka, wakafanya mkutano wamkamate, ugumu ukaja namna ya kuanza kumshambulia paka. Nani aanze kumfuata.! Wakaishia kutegeana. 
Hata waliposema twendeni wote kwa pamoja, kila mmoja akawa anasita kuwa mwengine anaweza asiende halafu 'ikawa imekula kwake'.

4. Wengi wetu tunajali sana faida ya muda mfupi, kuliko faida ya muda mrefu. Hivyo hata katika kujiajiri binafsi, hatufanyi vema, hatuna biashara au asasi endelevu. Na kwakuwa tayari tuna mapungufu haya, tunaogopa hata kuwasaidia wenzetu kwani tunaishi kiushindani zaidi, na ushindani wenyewe ni wasasa zaidi sio wa muda mrefu. 
Kuwa na EGO, ni kuzuri, ila EGO, inayokuangamiza na kudidimiza mambo endelevu hata ya kwako binafsi kweli ni tatizo.
Hili swala la kujali faida ya muda mfupi lipo hata kwa wanafunzi, hususani wanafunzi wa asasi za elimu ya juu. Badala ya kutilia maanani kuelewa kwa undani mambo wanayojifunza, kutafuta ujuzi na kubobea katika mambo fani zao, wapo baadhi huwa wameshajiandaa kumaliza tuu, kupata cheti, au kwa lugha rahisi ya mtaani 'gamba'. Hivyo elimu anayoipata mtu, haimsaidii kujiajiri, hamsaidii kubuni mikakati ya kujikwamua kutoka katika hali aliyonayo.

5. Wengi wetu tunafikiria zaidi yale tusiyokuwa nayo, badala ya kufikiria tunatumiaje yale ambayo tayari tunayo. Kijana aliyemaliza elimu ya chuo kikuu, anawaza kuwa hawezi kupata kazi kwakuwa tuu hana 'refa', au hawezi kujiajiri kwa kuwa hana mtaji. Hata hivyo kijana huyo huyo, amesahau kuwa kama anao uelewa wa kutosha wa mambo aliyosomea, anaweza kuomba kujitolea kwa asasi kadhaa zilizopo, au kwakutumia marafiki zake ambao anachat nao kila siku kwa mtandao angeweza kufanya mambo ya msingi. Yeye mwenyewe pia angeweza kubuni jambo ambalo lingeonyesha kweli ana uwezo wa kipekee wa fani yake, hivyo 'kuforce' kukubalika katika soko la ajira. Kijana huyo anayelalamika hana ajira wala hawezi kuanza ujasiriamali, ameacha kutumia vema mikutano anayohudhuria iwe shughuli za kidini, za kiukoo, au hata sherehe za marafiki, kutafuta wadau wanaoweza 'kununua' ujuzi wa kipekee alionao kijana huyo. Hata huko kutafuta kazi, amekuwa akitafuta kazi kwa njia moja tuu, ya magazeti. Amesahau kuwa mitandao ya kijamii, kuenda moja kwa moja kwa waajiri, kutumia mawakala wa ajira, na hata kujitolea kwa asasi fulani kungeweza kumsaidia kufanya mabadiliko.

6. Wengi wetu tunasubiri mabadiliko ya pamoja. Kama mfano hapo juu wa paka na panya, wengi wetu tunafahamu matatizo tuliyonayo katika nchi yetu, tunafahamu hata sababu ya kuwepo kwa matatizo hayo, hata hivyo tuna kila sababu ya kujiona hatuwezi kuchukua hatua sisi kama sisi mmoja mmoja. Kwa mtazamo wa wengi , suluhu ya matatizo yetu itatokana na maamuzi ya wengi, itatokana na serikali, itatoka kwa chama fulani. 

Kwa tafakari hiyo hapo juu, MBUKE TIMES inaamini kuwa pamoja na kuwa wapo wadau wengi wa kuleta maendeleo katika nchi yetu, kuna mtu wa pekee wa kuleta maendeleo ya kweli, maendeleo endelevu katika nchi yetu ya Tanzania. Mtu huyo ni WEWE.
Jiulize unafanya nini kushinda mapungufu yako, unafanya nini kuzuia mambo yasiyo yasiyoleta maendeleo ,yanayoharibu jamii yetu ? Unalalamika kuhusu wanawake na kuporomoka kwa maadili nchini, ila wewe ndio unatoa kipaumbele kuweka picha za utupu za wanawake katika akaunti yako ya Facebook na kwa blog yako.
Share:

0 comments:

Post a Comment