USIYOYAJUA KUHUSU FC BARCELONA

Timu ya kwanza (First eleven) ya FC Barcelona inaundwa na zaidi ya 70% ya wachezaji waliokuzwa katika shule ya soka ya timu hiyo maarufu kama La Masia. Hapa ukitaka waweza taja kwa majina – Messi, Fabregas, Xavi, Iniesta, Puyol, Busquets, Valdés, Piqué, Pedro.

Utegemezi huu wa wahitimu wa La Masia kwa ajili ya First Eleven ni msingi mkubwa katika Falsafa ya Barcelona. Mambo mengine katika falsafa ya FC Barca kama yanavyofafanuliwa na bwana Albert Capellas (Mtaribu Mkuu wa Mafunzo ya soka kwa vijana FC Barca) kama alivyonukuliwa na blogu ya RMC9598.

Uchaguzi bora wa vijana wa kukuza: Barca wanadai wanasaka vipaji vikiwa ‘vibichi’ kabisa toka nchi mbalimbali duniani. Kisha wanawagawa katika makundi ya umri husika halafu kazi ya kuwapika vema inaanzia hapo. Kwa mtindo huu ndipo waliweza kukusanya vipaji kama Messi.


Kujali wachezaji: Katika falsafa ya Barca, kujali wachezaji inamaanisha kuhakikisha wanapata viwanja vizuri vya mazoezi, huduma bora kabisa za matibabu, mawasiliano, na kuwajenga kisaikolojia kuwa Barca ni zaidi ya soka, bali ni sehemu ya wao kuuishi utu wao na kuonyesha thamani ya uhai na maisha kwa ujumla.
Jionee hapa video ya Messi akiwa Mdogo, mechi yake ya kwanza Barcelona.

Muundo wa kitaalamu na shule ya soka ya La Masia: Barca inasisitiza sana mambo ya msingi katika soka kama vile pasi na kumiliki mpira. Mambo mengine yanayosimamiwa ni uwezo wa mchezaji kushambulia, kufunga, na kulinda. Bila shaka ndio maana watu wengi husikika wakisema Barca haina ‘namba’ kwani wachezaji wote huweza kucheza namba zote.
Kwa kusisitiza mambo haya ya msingi kwa wachezaji wote, iwe timu za watoto, hadi timu kubwa Barca imejenga mfumo mmoja tuu wa uchezaji wake. Pasi fupi, wanasonga mbele, pasi wanasonga mbele. Baadhi ya wadau wasoka wameipa jina staili hii ya uchezaji kuwa ‘tik tak’

Staili hii ya ‘tik tak’ ni ya msingi sana kwa Barca na ndiyo staili pekee ambayo Barca nzima iwe ya watoto au ya wakubwa wanajifunza. Ni maamuzi makubwa ya kuamua kutumia staili moja ili kuweza kuboresha mchezo wao. Hata wawe wanaongoza magoli 8-0 au wamefungwa magoli 0-8 Barca wataendelea kutumia staili yao hiyo hiyo.

Falsafa ya Barca inaelezwa katika mambo makuu

Falsafa Namba 1: Timu
Timu nzima inahusishwa katika maamuzi

Falsafa Namba 2: Mafunzo
Kama ilivyoelezwa hapo awali timu zote za Barca zinafuata mfumo mmoja wa mafunzo.
Jionee hapa jinsi walivyo na mfumo mmoja wa uchezaji na ufungaji-  toka under 14.


Falsafa Namba 3: Bwana Mkubwa anajua yote
Kocha mkuu wa Barca ya wakubwa –kwa sasa ni Guadiola na wasaidizi wake wote wanafuatilia muundo na uendelezwaji wa La Masia.

Falsafa Namba 4: Soka Moja
Timu zote zinafuata mfumo mmoja wa uchezaji soka toka U7 hadi timu za wakubwa.

Falsafa Namba 5: Wasifu wa Mchezaji Kwanza
Kabla mchezaji hajachezea timu ya wakubwa ya Barca au kuingia katika shule ya soka ya La Masia ni lazima atambulike kuwa anaweza kufikia viwango vilivyowekwa vya mchezaji wa Barca kwa madaraja mbalimbali.

Falsafa Namba 6: Upokeaji wa wachezaji ulio murua
Kila mchezaji anayepokewa na Barca iwe anaingia timu kubwa moja kwa moja au anaingia kwanza La Masia, ni lazima ahakikishiwe mahitaji yake yote ya msingi kama vile shule, nyumba na mengine ya kifedha yametimizwa. Hii inahusu pia hata familia yake na ndugu zake wa karibu. Mfano mzuri ni kwa Messi, alipochukuliwa na Barca, timu hiyo iliingia gharama zote za matibabu ya gharama kubwa kwa ajili ya Messi, pia timu hiyo inalipia gharama za makazi za familia yake Messi ambapo familia hiyo imehamishiwa Hispania toka Argentina. FC Barcelona pia ilikubali kulipa matibabu ya ugonjwa wa kudumu wa Messi ambapo kila mwezi inagharimu $900 sawa na TZS 1,440,000/=. Messi aliingia FC Barca akiwa na umri wa miaka 11.

Falsafa Namba 7: Kupima wachezaji wadogo
Wachezaji wa timu za vijana/watoto wanapewa nafasi ya kucheza katika timu ya kubwa hata hivyo nafasi hii mwamuzi wa mwisho ni kocha mkuu wa timu ya wakubwa endapo anaona inafaa. Mfano mzuri wa wachezaji waliopewa nafasi hii ni Messi ambaye alipata nafasi ya kuchezea timu ya wakubwa akiwa na umri wa miaka 16 chini ya kocha Frank Rijkaard.

Maelezo Haya kwa Uchambuzi toka: 
www.fcbarcelona.com
www.wikipedia.com 
www.rmc9598.blogspot.com
Share:

0 comments:

Post a Comment