UJUMBE "MKALI" WA VALENTINE DAY HUU HAPA

Kuna wakati utasikia mtu anasema "aah mie kwa kutafuta dili ni mshenzi kweli kweli".
Lakini wakati mwingine neno mshenzi linaweza kuchukuliwa kama ni tusi.
Au chukulia mfano wa neno GIFT kwa kiingereza linamaanisha zawadi ila kwa kijerumani (Nukuu toka BBC Language) linamaanisha SUMU.
Ninachotaka kusema ni kuwa kumbuka MANENO tunayotumia, ni sisi binadamu ndio tunaamua yamaanishe nini. Na kuna wakati tafsiri :-
1. Inaweza kutumika vibaya ili kujenga picha ya kitu unachodhani ni sawa kumbe neno limebeba maana nyingine. Mfano mzuri ni neno KUPENDA linapotumika katika mahusiano ya mwanamke na mwanaume. Wengi wamekuwa wakilitumia sivyo ndivyo. Kwani wengine wamekuwa wakisema NAKUPENDA wakati wakimaanisha NAKUTAMANI.
Mtu huyo ana "take advantage" ya maana halisi inayofahamika ili kumrubuni mwingine. Au pengine tuseme ni kama neno GIFT kwa kiingereza na kijerumani ni tofauti hivyo huyu jama inawezakana maana yake ya UPENDO ni tofauti na ile tunayoifahamu sote kuwa:- Upendo ni kuwa kwako tayari kufanya yaliyo mema na bora kwa ajili ya mwingine. Upendo katika maana hii hauna maana ya nini unataka kupokea kutoka kwa mtu mwingine bali ni nini unataka kutoa kwa mtu mwingine.
Hata hivyo unapopenda inakuwa ni kama deni kwa unayempenda kwa kuwa:-
Unajisikia kujitoa kwa mwingine, basi furaha yake ni ya muhimu zaidi kwako. Na kwa sababu unataka kujitoa kwake basi unaona HAJA ya kuwa karibu na mtu huyo. Sio kwa sababu tuu ya uzuri wake, mali zake n.k bali ni kwa sababu ya kuwa wewe unataka kujitoa kwake.
--Hata hivyo UPENDO sio lazima utokee mara tuu mnapokutana na mtu, yawezekana baada ya kufahamiana vya kutosha, au baada ya tukio fulani hisia ya upendo ikaja. Upendo Haulazimishwi wala Hauigizwi. Mwisho wa kuigiza upendo ni AIBU.
--Ni kweli kuwa kwa mwanamke na mwanaume kuna hisia za kimwili, na hisia hizo ni muhimu katika kujenga uhusiano. Hapa neno uhusiano sio sawa na UPENDO.Hata hivyo sio kila hisia ya mapenzi ni Upendo.
2. Umesikia mtu akisema HANA MUDA ? Kesho tutaangalia maana ya msemo huu na kwanini ni ya kupotosha. Usikose TAFAKARI YA KESHO.
Share:

INAKUAJE MTU ANAWEZA KUANGALIA MOVIE NA KUTOKWA NA MACHOZI INGAWA ANAJUA WAZI SI KWELI?

Umewahi kuona au imekutokea wewe kuangalia Movie na ukajikuta machozi yanakutoka ? Au unaingiwa na HOFU kana kwamba na wewe umo katika movie.
Hii inakukumbusha kuwa hisia huweza kukufanya uamini jambo na hata udhani ukweli ndio huo kumbe kilichopo ni msukumo tuu wa hisia zako kuhusu kitu husika.
Na kama wanavyojifunza watu wanaotengeneza movie namna bora ya kujenga kitu chenye kubeba HISIA, usisahau wapo wengine wanaotumia MBINU HIYO YA HISIA, kukuaminisha mambo ambayo pengine sio sawa, pengine kwa akili ya kawaida usingeyakubali.
Upo uwezekano wa HISIA zako kutumiwa na mtu mwingine ku "take advantage of you " - sijui tuseme vipi kwa kiswahili -pengine neno sahihi la "take advantage of you" ni mtu kukufanya ufanye jambo kwa kutumia upenyo wa wema wako au kwa sababu wewe umeingia katika mtego waliouweka.
--Ingawaje inaweza kuwa ngumu kutumia AKILI mahali ambapo unatumia HISIA, naamini wewe kufahamu hili la kuwa HISIA zako zinaweza kutumika vibaya na mtu mwingine, kunaweza kukufanya uwe makini na maamuzi yako unayoyafanya kwa hisia.
--Maeneo ambapo HISIA zako zinaweza kutumika vibaya ni kama kwenye mapenzi, urafiki, dini na siasa. Hata hapa FB nimewahi kuona posts zikisema kama kweli wewe unapenda ...fanya hivi...Hii inalenga hisia zako kwani si kweli kuwa KUTOKUFANYA hicho wanachosema kunabadilisha lolote kuhusu UPENDO wako, au MSIMAMO wako kuhusu jambo fulani. 
N:B Hadithi ya hisia na movie ni kwa hisani ya Andy Hunt katika kitabu chake PROGRAMATIC THINKING AND LEARNING.
Share:

FAHAMU TEKNOLOJIA HIZI ZA KIPEKEE ZA USAFIRI ( Video na Picha)

Picha na Pegasus.
Maendeleo makubwa katika nyanja ya usafiri yanatarajiwa hapo baadae na baadhi yamekwisha anza kuonekana. Mfano;
1. Kuna magari ambayo yanapaa hewani. Yaani waweza amua kuliendesha barabarani au ukiona vipi unalipaisha juu. Mfano mzuri ni mradi wa PEGASUS, uitwao THE PEGASUS ATLAS PROJECT. Cheki link hapo chini.
2. Magari yanayojiendesha yenyewe ; Yanaitwa self driving cars. Magari haya yanajiendesha kwa msaada wa kompyuta. Google wapo kwenye mradi huo. Makampuni mengine yanayotajwa kutengeneza magari yanayojiendesha yenyewe ni kampuni ya TESLA na FORD. Cheki link hapo chini uone video ya gari linalojiendesha lenyewe toka Google.
 
3. TRENI zenye spidi kubwa tayari zimeshaanza kutumika huko Japan. Zipo treni kama Harmony CRH 380A inayoenda mwendo kasi wa km380kwa saa. Na huko Japan wapo mbioni kutengeneza treni mabayo itakuwa na mwendo kasi wa 581km kwa saa.

Vyanzo vya habari:
SMH.COM
PEGASUSATLAS.COM

Share:

TAFAKARI MAKINI LEO: UMEISIKIA HII KITU KUHUSU "FUTURE" YAKO ?

Kama umewahi kuwa kiti cha mbele cha gari wakati wa usiku wewe kama dereva au abiria utakumbuka kuwa pamoja na taa za gari kuwashwa, mwanga wake haufiki mbali kumulika njia yote, bali humulika hatua chache hapo mbele.
Hata hivyo hali hiyo ya kutoona mbele haizuii kufika mwisho wa safari yenu.
 
Je, iweje leo wewe uache kujishughulisha na mambo ya yatakayoboresha maisha yako, kisa tuu ni kuwa eti hauoni kama kweli hapo mbele utafanikiwa ?
Kumbuka hauihitaji kuona wazi wazi mafanikio yako yatakavyokuwa hapo baadae, la msingi ni 


JE UNAFANYA LILILO SAHIHI ? JE, UNAJITUMA VYA KUTOSHA ? 

JE, UNAENDELEA KUJIFUNZA SIKU HADI SIKU ILI KUBORESHA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO?
 

Kama unahitaji kuanza shule anza, kama unahitaji kuanza biashara anza, kama unahitaji kuanza kuboresha chochote kile anza leo, usisite kwa kuwa eti mafanikio hayapo wazi.
Na kumbuka hata kama hautofanikiwa, bado utakuwa umejifunza kitu na utaweza kuboresha safari yako.
 

--Ndio maana MBUKE TIMES inaendelea ingawaje nina ndoto tuu ipo siku itakuwa kitu kikubwa, ila kiukweli kwa sasa sina "picha halisi" itakuaje hapo baadae !
 

Mfano huu wa taa za gari ni kwa nukuu toka kwa E.L. Doctorow aliyelinganisha taa za gari na uandishi wa vitabu vya hadithi.
Share:

MAMBO 4 AMBAYO HAUJUI KUHUSU INTERNET (1 ni website ya kukodisha Mume)

Mambo haya bila shaka haukujua kuhusu INTERNET
1. ROBO ya shughuli za utafutaji (search) katika mtandao ilikuwa inahusu NGONO ( Takwimu, toka webroot.com)
 
2. Kuna website ambayo kazi yake yenyewe ni kukusanya kumbukumbu za muonekano wa websites mbalimbali. Hivyo kwa mfano ukitaka kujua MBUKE TIMES blog ilikuwa ikionekana vipi mwaka jana Agost, unaingia kwa hiyo website ya ARCHIVE.ORG kisha unaweka anuani ya blog ya mbuke times na kubofya sehemu ya kutafuta kumbukumbu. Waweza fanya hivyo mfano kujua FB ya mwaka 2005 ilikuwaje? Au Google ya mwaka jana ilionekana vipi.
Mbuke Times ya Agost 2013,picha toka archive.org
3. Na huko nchini Marekani kupitia website ya SHAREYOURMEAL.NET mtu anaweza kununua chakula toka kwa majirani zake, sio lazima aende hotelini.
Ipo hivi, kama wewe umepika chakula kingi kuliko unachohitaji basi unaweka tangazo kwa website hiyo kuwa una msosi unaoweza kushare na watu. Au kama wewe una njaa na haujisikii kupika wala kwenda hotelini, basi unacheki majirani zako wenye chakula unachoweza kujisevia !
 
4. Na kali ya mwisho ni hii website toka UINGEREZA ambayo inakodisha MUME. Inaitwa HUSBANDTORENT.CO.UK, kama mwanamke yupo "single" basi anaweza kupata Mume wa kumsaidia kazi za nyumbani kama kufanya matengenezo madogo madogo, kumtoa out n.k. 
--Na hiyo ndio habari yetu ya leo kuhusu TEKNOHAMA. Endelea kufuatilia MBUKE TIMES uufahamu ulimwengu wa TEKNOHAMA. Tafadhali usiache KUSHARE.

Share:

HII NDIO TEKNOHAMA: KWANINI HAITOSHI TUU KUJUA KUPOST, KUCOMMENT NA KUCHAT FB ?

Wapo wengi wanaoendesha magari na hawajui hata jinsi gari linavyofanya kazi zaidi ya kujua jinsi tuu ya kuendesha gari. Lakini hata kama haujui nini kinafanyika mpaka gari liongeze mwendo au kufunga breki, bado unahitajika kujua namna bora ya kutumia vioo vya pembeni, kioo cha kuangalia nyuma, matumizi sahihi ya taa-kama ni "full" au dim, na zaidi unahitaji kujua jinsi ya kufunga breki,kuongeza mwendo na kurudi nyuma ("RIVASI"). --
Hali hii ni tofauti kwa hapa MTANDAONI sio tuu kwamba unatakiwa kujua namna ya kuitumia TEKNOHAMA bali ili kuwa salama na kuepuka wewe KUTUMIKA isivyopaswa na wenye kuijua TEKNOHAMA , unahitaji kujua namna TEKNOHAMA inavyofanya kazi. 
Mfano: Wengi wanachojua khs FB ni kuwa unaingia unasoma posts za watu, unapost picha na status zako basi. Lakini haujui namna ambavyo taarifa zako za hapa FB zinavyoweza kufika mikononi mwa watu usiotarajia. Je, wajua kwa mfano unaweza chagua nani aone POSTS zako na nani asione? Je, wajua kuchagua nani anaweza tuma maombi ya kuwa rafiki yako hapa FB ? Je, wajua namna ya kuzuia taarifa zako zisitumiwe na FB kwa matangazo ? Je, wajua kuwa FB inafuatila mwenendo wako mtandaoni ili kupata kufahamu zaidi kuhusu wewe, na je kama hautaki unazuia vipi? 

Kama unajua programming, basi ni rahisi kwako kuelewa kwanini ni rahisi kwa FB kufanya hivyo wanavyofanya. 

Na kama umesoma lugha kama JavaScript na PHP utajua mambo mengi ambayo wenye kuendesha websites wanafanya juu yetu bila sisi kujijua.

N:B Soma kwa umakini hiyo habari kwani kuna walioielewa tofauti kama huyu fan wa ukurasa wetu
FAN ANASEMA: Mie nafahamu vizuri. Ila kwa mambo ya security kwenye post zako,friend requests na hata advertisement nadhani FB wenyewe wanatoa hiyo huduma sidhani kama mpaka ujue programming ndo uelewe hizo huduma. Na sidhani kama normal end user ana ulazima sana wa kujua hivo vitu labda awe exceptional kama mie na wewe tunavyofahamu programming na web languages pamoja na security scripting mfano hiyo javascript. Ni mgawanyo tu wa knowledge mbalimbali.

JIBU LANGU NI: Post haijasema MPAKA UJUE PROGRAMMING ndio UELEWE. Post inasema Kama unajua programming basi ITAKUWA RAHISI, kuelewa KWANINI NI RAHISI kwa FB kufanya hivyo. Na wala Post haijahusisha UELEWA WA PROGRAMMING na KUJUA HUDUMA ZA FB.
Na elewa kuwa ninapozungumzia kufahamu teknohama sio lazima kuwa mtu wa fani husika yaani wote tuwe programmers, hata kuwa tuu na uelewa kuwa hizi websites zinaendeshwaje, nao ni ufahamu mzuri katika kumsaidia mtu Kuwa na MATUMIZI BORA, sio kwamba bila hizo ELIMU hatoweza. Mfano mie ni MHASIBU na kazi zangu nyingi ni za MARKETING na UHASIBU, hata hivyo ufahamu wa TEKNOHAMA unaniwezesha kufanya mengi katika zama hizi za digitali  
Share:

KUTOKA MTANDAONI: MTOTO HUYU WA KIRUSI KAFANYA MAKUBWA JANA !

Picha na RT.COM
Jana dunia imeshuhudia umahiri wa hali ya juu toka kwa mtoto wa maiaka 15 aitwae Yulia Lipnitskaya, Mrusi aliyeshinda medali ya dhahabu ktk mashindano ya kuteleza kwenye barafu.
 
Kuna wakati Yulia aliweza kunyanyua mguu wake mmoja na kutengeneza umbo la namba moja huku akiendelea kuteleza, na wakati mwingine alipinda kutengeneza umbo la herufi L, na akizunguka kwa kasi.
 
Kinachovutia kuhusu YULIA ni kuwa mama yake kwa kuamini kipaji cha binti yake, aliamua kuacha kila kitu katika mji waliokuwa wakiishi zamani na kuhamia Moscow wakati Julia akiwa na Miaka 10 ili tuu ampe "sapoti" binti huyo.
 
Na kweli sapoti ya mama imezaa matunda kwani Yulia amekuwa bingwa wa Urusi, bingwa wa Ulaya mwaka 2014, na amewahi kuwa bingwa wa dunia wa mashindano ya World Junior Championship mwaka 2012.
Na jana amekuwa ndio mtereza kwenye barafu mwenye umri mdogo zaidi kwa nchi ya Urusi kupata medali ya dhahabu ktk mashindano ya Olympic.
JE UNATAMBUA KIPAJI CHA MTOTO WAKO ? UPO TAYARI KUKIENDELEZA ? 
 
Maelezo haya ni kwa uchambuzi toka RT.COM, Wikipedia na Buzzfeed.com 
 
Share:

HIVI NDIVYO ELIMU YAKO ITAKAVYOKUSAIDIA KUPATA KAZI (TAFAKARI)

Kuna wakati unaweza kusikia mtu akilalamika kuwa amefuata MAELEKEZO yote aliyopewa ili kufikia lengo fulani lakini hakufanikiwa. 
Katika hali hii kutokufanikiwa kunaweza kutokana na:
1. Maelekezo yenyewe inawezekana hayakuwa sahihi.
2. Ulifuata maelekezo kwa usahihi kabisa ila uliyafuata kwa tafsiri yako isiyo sahihi.
3. Mazingira yamebadilika hivyo pamoja na kufuata kwa usahihi na kwamba maelekezo kweli yalikuwa sahihi, lakini mazingira/nyakati haikuwa sahihi.
4. Pengine unahitaji tu uvumilivu kidogo kwani matokeo yanaweza kuchelewa.
Unganisha post hii na maisha ya kila siku. Wengi wanamaliza vyuo kisha kubaki mtaani wakiwa hawana kazi, pengine walisoma kweli kwa umakini na kupata alama nzuri hivyo wanataraji kupata kazi haraka iwezekanavyo. Hata hivyo jiulize:-
**Je elimu uliyopata ni sahihi kufanikisha upate kazi kiurahisi -je unao ujuzi kweli, je unaweza kujieleza?
**Mazingira ya kupata kazi yamekuwa tofauti na yataendelea kubadilika siku hadi siku, je elimu yako imekuandaa kupambana katika mazingira tofauti au inakupa tuu cheti ?
**Pengine ulielewa vibaya kuhusu ELIMU, wakati ule unapiga CHABO, na kuibia ukijipa imani kuwa la msingi ni CHETI tuu, labda hapo ndipo ulipotafsiri vibaya kuhusu ELIMU, ila leo unalalamika iweje haupati kazi au michongo mingine ingawaje una ELIMU.
Share:

FAHAMU CHUKI NI TATIZO LA KIFIKRA ZAIDI NA DAWA YAKE HII HAPA..

Sisi binadamu namna yetu rahisi ya kuelewa na kukumbuka mambo ni kwa kuyaweka mambo katika makundi mfano tunawagawa watu katika makundi kama marafiki, ndugu, watoto, maadui, warefu, wafupi, n.k. Makundi haya yanatusaidia kujenga picha ya haraka hata kama wakati fulani hatuwezi kuelezea wazi wazi kundi husika ni nini haswa na pia kunaweza kuwa na tofauti kati ya watu au vitu katika kundi husika. 
Mtindo huu wa kutambua vitu au watu kwa makundi ndio unaopelekea pia kuwepo kitu tuiitacho kwa kiingereza PREJUDICE yaani CHUKI.
Kwakuwa umezoea kuwaweka watu katika makundi fulani, na kuwatambua watu kwa makundi kutokana tayari na aina ya picha ya kundi husika , basi waweza kujikuta ukiwaweka tuu watu katika makundi na kuwatafsiri hivyo, ingawaje sio sahihi kwani ingawaje wewe unafikiria na kutambua kwa njia ya MAKUNDI, kumbuka kuna utofauti mkubwa kati ya mtu aliyepo katika KUNDI na maana unayoipa KUNDI husika. 
Hivyo unaweza kumtafsiri mtu kuwa MVIVU/MWIZI/MWONGO kwa sababu tuu unamuona yupo katika kundi fulani ambalo wewe huwaita wavivu/Wezi/waongo, ila kiukweli huyo mtu mmoja sivyo unavyodhani.
Mara ngapi umesikia mtu akisema "Vijana wa siku hizi wavivu", na wengine wamekosa kazi kwa sababu tuu eti wamemaliza chuo fulani hivyo "hawana ujuzi".
CHUKI au PREJUDICE ni pale unapowatafsiri watu wengine VIBAYA kwa sababu kiakili yako wapo katika MAKUNDI ambayo ni mabaya. Unaamini kwa mfano kila anayefanya biashara ONLINE ni tapeli, kila mwenye NGO basi ni tapeli, kila MNIGERIA ni mwizi, n.k
Kumbuka ili kuzuia CHUKI ya namna hii jitahidi kufikiria na kuwaona watu kama mtu mmoja mmoja na sio sehemu ya kundi.
Kuwa makini na namna unavyotafsiri watu kwa kuangalia UMRI , JINSIA, UTAIFA, DINI, KABILA, AINA YA KAZI, MIJI WANAPOTOKA, MAHALI WANAPOISHI n.k
Pia jichukulie wewe ndio ungekuwa una tafsiriwa vibaya ungejisikiaje ?

Soma zaidi kwa kufuata link hii toka ABOUT.COM
Share:

IFAHAMU KANUNI HII ITUMIWAYO NA UBONGO WAKO

Ubongo wetu unatumia kanuni ya "KAMA KITU HAKITUMIKI BASI HAKINA UMUHIMU" hivyo huwa ngumu kwa ubongo kukupatia majibu kwa haraka kwa vitu ambavyo havijaonyeshwa umuhimu na wewe mwenyewe.
Kuelewa vizuri embu chukulia mfano rafiki zako mliosoma darasa moja shule ya msingi, pengine leo ukiulizwa uwataje hata 10 tuu kwa majina hukumbuki, ingawaje mlikuwa mkiitana majina kila siku wakati mlipokuwa shule na enzi hizo ulikumbuka bila shida.
--Ni kwa sababu haujaitumia mara kwa mara ndio maana ubongo haukuletei kumbukumbu.
--Hivyo kama unataka uwe na uwezo wa kufanya jambo fulani kwa ubora zaidi inakupasa uwe unafanya jambo husika mara kwa mara. 
Hivyo kama unataka kuwa mtu wa kufanya mambo ya busara, kutoa points unapozungumza basi fanyia kazi swala hilo.
Ndio maana hata leo ukiangalia mazoezi ya timu ya FC Barcelona bado wanafanya mazoezi ya kupiga pasi, na kumiliki mpira.
--Na kumbuka pia ubongo hauna uwezo wa kutambua lipi ni bora kwako, wenyewe unaangalia umuhimu wa kukumbuka kwa kadri unavyotumia kitu husika. Hivyo ndio maana wengine unakuta kati ya neno na neno wameweka TUSI, kwakuwa ndio wamekwisha zoea hivyo. Ukijizoesha kusoma udaku na kufikiri udaku basi hayo ndio ubongo wako utakumbuka.
Kwa mujibu wa Brainworldmagazine.com na Lifehack.com
Share:

MBINU RAHISI YA KUJIFUNZA KUJITAMBUA

Tafakari yetu leo inahusu WEWE NI SEHEMU YA MFUMO ?
Karibu kila kilichoumbwa duniani ni sehemu ya kingine , kwa hiyo tuseme hata sisi binadamu ni mfumo. Lakini kabla sijaingia kwa binadamu embu tuangalie mfano rahisi wa MLANGO.

Wewe unapoutazama mlango mara nyingi unaangalia mlango kama mlango pekee lakini, mlango huo hauna maana kama hakuna kuta mbili kushoto na kulia kwake. Huo mlango pia usingekuwepo kama kusingekuwepo ardhi au sakafu hapo chini. Mlango wenyewe tuu umeundwa na vitu vingi kama kitasa au komeo, pia kulihitajika misumali n.k. Hata hivyo wewe bado unapozungumzia mlango akili yako moja kwa moja huangalia tuu Hicho ambacho sote huwa tunasema mlango ila kiukweli MLANGO ni jumla ya vyote vinavyofanya nyumba au chumba chako kijihifadhi kwa kuzuia kuingia kwa urahisi.

Wewe pia tunapokuangalia haraka haraka tunakuona wewe tuu, lakini wewe ni jumla au matokeo ya walezi wako, mke/mume wako, elimu uliyoipata, unachokula na kunywa, marafiki n.k. Ndio maana kama ukiishi eneo tofauti, ukawa na marafiki tofauti, ukapata elimu tofauti , ukawa na mpenzi/mke/mume tofauti, pengine wewe wa leo sio yule utakayekuwa wa wakati ujao.

--Kwa nini nimeleta tafakari hii ? Ni kwa sababu kama ukijitambua kuwa wewe ni sehemu ya MFUMO basi utajitahidi kuangalia namna vingine vinavyounda mfumo vinavyosababisha wewe kuwa hivyo ulivyo. 
Pengine ni aina ya mambo unayojifunza, aina ya siasa unayofuata, yale unayosoma na kuamini, pengine ni aina ya marafiki ulio nao, pengine ni mazingira unayoishi, n.k. 
Je kwa kiwango gani upo makini na kuvitumia vitu vingine au watu wengine katika mfumo wako ili uwe mtu bora zaidi ? 
Tafakari , chukua hatua ya KUJITAMBUA ZAIDI.
Share:

HUU NDIO USHAHIDI WA UTOFAUTI WA UBONGO WA MWANAMKE NA MWANAUME

Kuna ushahidi wa kisayansi kuwa ubongo wa mwanamke na mwanamme umeumbwa tofauti ndio mana :-
1. Kuna aina fulani ya shughuli au matukio mwanamke anaweza kufanya kwa ubora zaidi kuliko mwanaume, na kuna nyingine mwanaume anaweza kuwa bora zaidi kuliko mwanamke. 
Mfano, shughuli zinazotumia nguvu/misuli mwanaume anaweza kufanya kwa ubora zaidi kuliko mwanamke, wakati shughuli zinazohitaji kumbukumbu na kujenga picha ya mbali -bila kuwa na taarifa (intuition) basi wanawake ni bora zaidi. 
Mfano mwanamke ni bora zaidi katika MALEZI YA MTOTO kwa sababu ya uwezo wake wa kugundua mambo hata kama hakuwepo, na uwezo wake wa "kutabiri" yajayo hata kama hana taarifa rasmi kuhusu hapo baadae. 
 
2. Wanawake wana uwezo wa kubeba mambo mengi vichwani mwao na kukumbuka vitu vingi kuliko mwanaume ambaye huwa na jambo moja au vitu vichache tuu anavyoweza kufanya kwa wakati mmoja. Wanawake ni wazuri katika "multi-tasking"-yaani kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja.

---Ushahidi wa kisayansi kuhusu utofauti wa ubongo wa mwanamke na mwanaume, unaelezwa na watafiti toka chuo kikuu cha Pennsylvania cha huko Marekani kama walivyonukuliwa na jarida la mtandaoni la MEDICALNEWSTODAY.COM.
Picha na Medicalnewstoday

--Utofauti wenyewe wa ubongo ni muundo wa jinsi "nyaya" za ubongo zilivyounganishwa. Wanawake wao nyaya zao zimeunganishwa toka upande mmoja (kushoto/kulia) kwenda upande mwingine, wakati wanaume wao ubongo "nyaya " zake zimeunganishwa toka mbele kwenda nyuma na kwamba "waya" mmoja hauwezi kuwa pande mbili za ubongo, yaani kama waya upo upande wa kushoto basi utapita toka mbele kwenda nyuma upande huo huo wa kushoto. Hivyo hakuna mawasiliano upande mwingine wa kulia.
Share:

IFAHAMU POMBE IITWAYO "CHICHA" TOKA AMERIKA YA KUSINI

Kama ilivyo ada yetu kila ijumaa tunapata picha moja ya jambo, kitu au tukio la kipekee.
 
Leo hii tuangalie kinywaji hiki chenye jina la kufurahisha. Kinywaji hicho ni cha asili huku Amerika ya Kusini, hususani katika nchi za ECUADOR, COLOMBIA, BOLIVIA na PERU.
 
Kinywaji hicho kinaitwa CHICHA.
Kuna namna tofauti za kutengenezwa lakini maarufu zaidi ni CHICHA "linalotengenezwa" kwa mahindi.
--Watu hunywa kama kinywaji cha kawaida-hutumika kama bia. Ila zipo aina nyingine za CHICHA ambazo si kilevi, bali watu hunywa na kushiba kama msosi.
 
Picha na: seriouseat.com
Share:

MAMBO 6 MUHIMU YA KUJIFUNZA KUHUSU MIAKA 10 YA FACEBOOK


Facebook imetimiza miaka 10 toka ianzishwe. Na katika kusherehekea siku hiyo mwanzilishi wake Mark Zuckerberg aliandika barua (BOFYA HAPA KUSOMA BARUA YOTE) kwa watumiaji wote wa FB akieleza mambo kadhaa. Makala hii inachambua mambo ya baadhi ya mambo yalivyoelezwa na Mark, na nini waweza jifunza kutoka kwake:

1. MARK: I remember getting pizza with my friends one night in college shortly after opening Facebook. I told them I was excited to help connect our school community, but one day someone needed to connect the whole world.
TAFSIRI: Nakumbuka nikiwa napata PIZZA (chakula cha kiitaliano) na marafiki zangu usiku mmoja chuoni mara baada ya kufungua Facebook. Nikawaambia nilikuwa ninasisimka kwa kuunganisha jamii yetu ya chuo chetu, ila ipo siku kuna mtu atahitajika kuiunganisha dunia.
TAFAKARI: Kwanza hapa tunaona jinsi ndoto kubwa inavyosaidia kukuza biashara. Mark pamoja na kufurahia kuwa alipata mafanikio ya kuunganisha jamii ya chuo chake, bado hakubweteka na mafanikio hayo. Alijua kuwa kuna haja ya kuwa na kitu kama FB na alijikita kutimiza ndoto yake, na katika kutimiza huko amejipatia utajiri pia.
Pili tunaona kuwa aliwadokeza marafiki zake kuhusu ndoto yake. Hata hivyo hakuna aliyekuja kwa mtindo ambao FB walikuja nao. Kumbuka kabla ya FB ilikuwepo mitandao mingine ya kijamii, na hata baada ya FB imeanzisha mitandao mingine mingi ya kijamii.  Hapa wabongo wenzangu tujifunze kutafuta UPEKEE wa miradi yetu sio tuu ku copy na ku paste.

2. MARK: I always thought this was important -- giving people the power to share and stay connected, empowering people to build their own communities themselves.
TAFSIRI:  Daima niliamini kuwa hii ni muhimu- kuwapa watu nguvu ya ku “share” na kuwa karibu na wengine, kuwasaidia watu kujenga jamii zao wao wenyewe.
TAFAKARI:  Biashara endelevu na imara mara nyingi hujengwa baada ya kutambua tatizo haswa katika jamii, na kuleta suluhusisho ya tatizo hilo. Yaani biashara endelevu bidhaa zake ni Suluhisho la tatizo au matatizo katika jamii na sio tuu ili mradi kuingiza hela.

3. MARK: That's why I'm even more excited about the next ten years than the last... Now we have the resources to help people across the world solve even bigger and more important problems.
TAFSIRI : Ndio maana nina msisimko zaidi kuhusu miaka kumi ijayo kuliko miaka kumi iliyopita. ..Sasa tuna rasilimali za kuweza kusaidia watu duniani kutatua hata matatizo makubwa zaidi  na yale matatizo muhimu zaidi.
TAFAKARI : Biashara endelevu inajengwa katika msingi wa kufanya ukipendacho ndio maana unaona hapa Mark akisema anao msisimko zaidi. Pili unaona anarudia tena kuwa bidhaa yao kubwa FB ni kutafuta suluhisho la matatizo.

4. MARK: It's been amazing to see how all of you have used our tools to build a real community. You've shared the happy moments and the painful ones. You've started new families, and kept spread out families connected. You've created new services and built small businesses. You've helped each other in so many ways.
TAFSIRI : Ni jambo la kufurahisha kuona jinsi nyote mlivyotumia vyombo vyetu kujenga jumuiya zenu. Mme “share” nyakati za furaha na nyakati za huzuni. Mmeanzisha familia mpya, na kuendelea kupanua familia mlizokwisha unganisha. Mmetengeneza huduma mpya na kujenga biashara ndogo ndogo. Mmesaidiana kwa njia mbalimbali.
TAFAKARI: Daima utakumbana na changamoto na watu watakaokupinga katika jambo zuri unalotaka kufanya. Isitoshe ni kweli utakuwa na mapungufu katika shughuli zako lakini usiweke kichwani mapungufu kiasi cha kukukatisha tamaa. Daima kumbuka mazuri unayotengeneza na fanya bidii kupunguza hayo mapungufu. (Kumbuka FB imekuwa ikilalamikiwa na wengi kuwa haifai na wapo wanaozungumza kana kwamba FB ni huduma ya kupotosha watu).

5. MARK:  I feel a deep responsibility to make the most of my time here and serve you the best I can.
TAFSIRI : Najisikia toka moyoni kuwa nina jukumu la kutumia muda wangu mwingi hapa kuwahudumia kwa ubora niwezavyo.
TAFAKARI:  Ni muhimu kujisikia unawajibika kwa wateja wako,  na kwamba kutatua matatizo yao ni jambo bora zaidi na unatakiwa kulifanya kwa nguvu na maarifa ya juu kwa kadri uwezavyo.

6. MARK: Today, social networks are mostly about sharing moments. In the next decade, they'll also help you answer questions and solve complex problems.
Today, we have only a few ways to share our experiences. In the next decade, technology will enable us to create many more ways to capture and communicate new kinds of experiences.
TAFSIRI:  Leo mitandao ya kijamii kwa kiwango kikubwa  inahusu ku “share” matukio ya nyakati mbalimbali. Miaka kumi ijayo, mitandao ya kijamii itasaidia pia kujibu maswali na kutatua matatizo magumu.
Leo, tuna njia chache za ku “share” uzoefu wote  (yale tunayokumbana nayo). Miaka kumi ijayo , teknolojia itatuwezesha kujenga njia zaidi za kuweka kumbukumbu na kuelezea njia mpya zaidi za yale tunayokumbana nayo.
TAFAKARI:  Hapa Mark anadokeza mabadiliko makubwa ya FB yatakayokuja ndani ya miaka kumi ijayo. Ni muhimu kama una biashara kujaribu kuiboresha kila wakati hata kama unadhani wewe umekwisha fanikiwa sana.
Share: