FUNDISHO AMBALO KILA MJASIRIAMALI ANAPASWA KULIJUA

Wengi wanaweza kuanzisha biashara , hata hivyo ni wachache wanaweza kuendeleza biashara na hata kuwa na biashara zenye kukua na zenye faida.
Kuna mambo ukiyafahamu yanaweza kukusaidia kuwa mjasiriamali endelevu. Mambo hayo yanafanana na kuushinda mchezo wa MAZE.
Mchezo huo kama unavyoona pichani hapa chini ni kuwa unapewa njia ya kuingilia , na unaonyeshwa pa kutokea , hata hivyo utafikaje fikaje toka ulipoingia hiyo ni kazi yako kujua.
Ndivyo ilivyo katika ujasiriamali. Unapokuwa na wazo la biashara na malengo ya kuyafika mafanikio ya aina fulani. Unajua kuwa unaweza kuanza biashara husika, hata hivyo kuna mengi utakayokutana nayo kabla haujaipata njia ya mafanikio.
Ni kama ulivyo mchezo huu kuna njia nyingine ni rahisi tuu kuzipita, ila kuna nyingine unakutana na kuta ambazo inabidi uzivunje ili utokee sehemu nyingine.

Ni kweli pia unaweza kutumia muda mwingi sana na ukafanikiwa kupata njia ya kutokea salama kabisa katika mchezo huu wa MAZE, na ndivyo ilivyo hata katika ulimwengu wa ujasiriamali. Kuna wanaochukua miaka na miaka kufikia mafanikio yao, na kuna ambao hata hawafiki mbali wanakumbana na vikwazo na hawaoni njia ya kutokea.

Unafanyaje kupita salama mpaka mafanikio katika ujasiriamali ?

1. Elewa wazi kuwa ujasiriamali ni safari, sio jambo la mara moja tuu ufanikiwe halafu basi, uanze 'kula bata'. Ujasiriamali ni maisha, ni changamoto za kila siku na hivyo kubali aina hiyo ya maisha. Usiweke mbele sana wazo la kupata faida kwa haraka, maana utakata tamaa pale unapokumbana na vizuizi, wakati kama ulivyo mchezo huu wa MAZE, vizuizi ni sehemu tuu ya mchezo, ila kuna njia ya kufika.

2. Kazi yako kubwa kama mjasiriamali basi ni kutambua kwa haraka, tena kwa mtazamo wa juu vizuizi au changamoto unazoweza kukutana nazo, panga mikakati ya kutatua changamoto hizo. Kuna vizuizi vingine ni rahisi sana kama vile kuamua tuu kubadili njia, na kuna vingine ni lazima tuu uvishinde ili utokee upande wa pili. Kuvishinda vizuizi hivyo wakati mwingine si wewe peke yako unaweza. Unahitaji maelekezo na huduma za wataalamu, unahitaji fedha n.k

3. Kwa ujasiriamali endelevu ni lazima ujizoeshe kujisomea sana, na uweze kuwa na uwezo wa kuwa na watu wenye ujuzi wa kutatua matatizo.
Share:

UNATAKA BUSINESS PLAN TEMPLATE AU SAMPLE? CHEKI HIZI

Kama unataka kuandika business plan (Mchanganuo wa biashara) na unahitaji kuona sample (muundo wa jinsi inavyoandikwa) basi makala hii fupi itakufungua mwanga.
Kabla sijakuwekea link ya sehemu unazoweza kupata templates na sample hizo , nikukumbushe mambo machache:-
Business plan ni nyaraka muhimu sana kwa biashara yako kwakuwa inakupa picha ya matarajio ya namna biashara itakavyokuwa. Ukifanya mchanganuo huo kwa ufasaha kama inavyoelekezwa utaweza kutambua kama kweli biashara unayotaka kuifanya itakulipa au la. Pia utaweza kutambua matatizo na changamoto kabla haujaanza biashara.

Business plan kwa kiwango kiwango inahitaji utafiti ili kuweza kuandika vema mambo yanayoendana na biashara yako. Mfano unahitaji kufanya utafiti wa soko ili kujua kwa biashara yako ni akina nani hasa watakuwa wateja wako, na kwanini watakuja kununua bidhaa kwako. Pia unahitaji kufanya utafiti wa gharama utakazotumia kuendesha biashara. Pia gharama za ununuzi wa samani kama computer n.k


Business plan inakuhitaji ujue picha kubwa ya mazingira ya biashara yako pindi utakapoianzisha. Mfano maswala ya kodi, maswala ya kisheria kama sheria ya ajira, vibali, uendeshaji wa biashara n.k. Hivi vyote vinaweza kuwa tofauti na vilivyoandikwa katika Sample busness plan. Hivyo ni wewe ndio wa kufanya utafiti.

Na mwisho kama unataka kuandika business plan ili ukaombe mkopo, basi fikiria kwa umakini namna ambavyo utakuja kuulipa mkopo husika. Umejipangaje katika usimamizi makini wa biashara yako. Business plan pekee sio dawa ya mafanikio, unaweza kuja kukutana na changamoto nyingine nyingi ambazo hukuziandika katika business plan yako.
Haya sasa, links hizi hapa bofya hapa chini:-
1. I PLAN. NET

2. GOV. UK

3. SCORE.ORG

4. MICROSOFT

5. ENTREPRENUER.COM
Share:

JINSI YA KUPATA DILI ZA KUBORESHA MAISHA YAKO

Angalia jinsi maisha yanavyozidi kuwa magumu katika jamii zetu. Gharama za vyakula, usafiri, na mambo mengine zinazidi kuongezeka, pia mabadiliko ya kiteknolojia na kijamii yanaleta changamoto nyingi. Tupo katika zama ambapo kusimama kiuchumi kunahitaji kujidhatiti kweli kweli. Makala hii inachambua mambo ya msingi ambayo yanaweza kukusaidia kujipanga kupata dili zinazoweza kuinua maisha yako.

1. Jitafakari: 
Ni vizuri kujizoesha kutafakari kuhusu wewe ni nani, mapungufu yako, mambo gani makubwa na mazuri uliyokwisha wahi kufanya, na vitu gani hasa unavipenda na usivyovipenda. Tafakari hii itakupa picha ya aina gani ya mtu wewe ulivyo, na kukusaidia kujipanga kuziba yale mapungufu, na wakati huo huo, utaweza kuangaza fursa zilizopo na unazoweza kuzitumia kutokana na 'ubora' ulionao.
Tafakari hii itakuwezesha pia kutambua kitu kiitwacho kwa kiingereza 'passion', yani mambo unayoyapendelea sana kufanya au kuwa hapo baadae. Umuhimu wa kutambua passion ni kwamba ukiweza kuwekeza muda katika passion yako inaweza kuwa sehemu nzuri ya kujijengea maisha yenye furaha. Kwani passion itakufanya ufanye jambo utalotaka kulifanya kwa ufanisi na pia hata ukikumbana na changamoto, hautokata tamaa kirahisi rahisi.

2. Mambo mazuri hayataki haraka
Kumbuka hao wote unaowaona wamefanikiwa kimaisha, mafanikio ambayo pengine unatamani uwe nayo, sio kwamba mafanikio hayo yalikuja kwa siku moja. Kuna maandalizi kadhaa waliyafanya, magumu waliyoyapitia mpaka kufika hapo walipofika.
Hii kwako ina maana kuwa ni lazima ujue kuna muda ni lazima uutumie kufanya maandalizi, inabidi utambue kuwa utakutana na magumu, ila hautakiwi kukata tamaa. Na zaidi sana ni lazima ujue bidii inahitajika. Hata hivyo bidii zako zitazaa matunda kwa haraka kama utatambua mapungufu yako mapema, na pia passion yako hasa ni ipi. Ukitambua mapungufu yako mfano una tatizo la lugha ya kiingereza, basi utafanyia kazi pungufu hilo ili uwe bora zaidi.

3.Utafiti ni muhimu sana
 Ni muhimu sana kuwa na taarifa sahihi kuhusu nini vinaweza kufanikisha  mipango yako na matarajio yako ya kimaisha. Mfano kama unatamani kufanya biashara, basi tafakari aina gani ya biashara, tafuta taarifa za kutosha kuhusu wateja wa biashara husika, kiasi cha mtaji , mbinu za kimasoko , n.k Vyote hivyo vitakuwezesha kujipanga kwa ufasaha ili kupunguza hasara na muda mrefu wa kufikia mafanikio.
Hii pia inahusika katika aina ya kazi unayotamani kufanya, je ni kwa kiwango gani utahitaji lugha ya kigeni, uwezo wa kutumia teknolojia mpya, kiwango cha elimu , n.k

4.Kubali kuwa tofauti
Wewe na yule mna historia tofauti za maisha, malezi tofauti, tabia tofauti, na hata uwezo wa kufikiri na hisia tofauti. Vyote hivi vinaweza kuchangia katika namna tofauti za kukabiliana na changamoto za kimaisha, na hata katika kupata fursa. Hivyo basi badala ya kuwaza kutaka kuwa kama fulani, tafakari nini wewe kama wewe unaweza kufanya, kiwango gani cha uvumilivu na juhudi kinahitajika ili kufikia malengo yako, na jitahidi kufanya unayotakiwa kufanya kwa juhudi.
Hakuna  'shortcuts' za mafanikio. Na mafanikio ya 'kulazimisha' hayawezi kukuletea furaha ya kweli maishani mwako.
Utakuja kugundua kuwa la msingi sana katika maisha ni kuwa na furaha na amani ya moyoni.

HITIMISHO
Kujitambua mapungufu yako na kuyarekebisha , halafu ukatambua pia mambo uliyo mzuri sana katika hayo, kisha ukazitumia fursa zinazoendana na hayo, kutakufanya ujiweke katika namna nzuri ya kupata dili za kuboresha maisha yako.
Hata hivyo kwakuwa mafanikio ni safari , unapaswa kujipanga kwa kuwa na taarifa sahihi, kuwa na bidii endelevu katika mambo ya msingi, na zaidi sana uweze kujitofautisha na wengine ili uweze kutambulika ubora wako, na hatimaye dili kali zije kwa ajili yako.
Share:

UNAWEZA KUJILETEA FURAHA MAISHANI KWA NJIA HIZI TATU

Unataka maisha yenye furaha na amani ? Unataka mafanikio ? Je unao mkakati wa kufikia hayo ? Jibu ni rahisi sana kama unavyoenda kusoma makala hii. Tena jibu la maswali hayo lipo karibu kuliko unavyoweza kudhani, hata hivyo lina gharama kubwa, sio ya kifedha bali ya kisaikiolojia. Pengine itakugharimu mambo mengi ambayo ulidhani ni ya msingi. Ni gharama ya mabadiliko.
Kwanza tafakari sahihi ya maisha:
Kwanza kabisa, je na wewe ni mmoja wa watu "wanaotafuta" maisha ? Ni kawaida kuwasikia watu wakisema wanatafuta maisha. Hii ni dhana inayopotosha kufanya watu wengi waamini kuwa maisha ni kama kitu fulani kinachowezekana kufikiwa, yaani maisha ni dhana tofauti na wewe. Hapana, hauhitaji kutafuta maisha. Tayari unayo maisha, wewe ni sehemu ya maisha, kucheka kwako, kula kwako, kufanya kazi, kuwaza kwao, yote hayo ni sehemu ya maisha. Ukiwa na mtazamo wa "kutafuta" maisha unaweza kujikuta mtu usiye na furaha siku zote, mtu usiye makini na ulichonacho, na pia utashindwa kutambua uwezo wako mkubwa ulionao. 
Hivyo basi anza sasa kutambua kuwa tayari unayo maisha. Tafakari na jikumbushe siku zote uwezo ulionao -akili, marafiki, jamaa, mafanikio yako kielimu, mahusiano, biashara, n.k yote hayo ni "maisha" yako.
Faida ya kutambua kuwa tayari unayo "maisha" ni kuwa utaweza kuunganisha nguvu zako katika kufikia mambo mengine ya msingi, pia utatumia 'utajiri' ulionao kuweza kutimiza malengo mengine.

Kuta ulizojiwekea katika maisha:
Pili unatakiwa uondoe "kuta" ulizojiwekea wewe mwenyewe katika kupiga hatua zaidi za kimaisha. Soma vizuri, nimesema katika kupiga HATUA zaidi za KIMAISHA. Sio katika KUTAFUTA maisha. Kuta hizo ni kama vile uwoga wa kushindwa, Uwega wa Maumivu, Uvivu na Kujitegemeza kwa wengine.
Ni kweli ni mara ngapi umeweza kufanikiwa katika jambo ambalo hapo awali ulidhani usingeliweza ? Na je, ni wapi uliona mafanikio yamekuja bila kuwepo na mapungufu katika njia ya kufikia mafanikio hayo? Utajiuliza, sasa ikiwa makosa nitajaribu na kushindwa nitakuwa nimepoteza vingi sana, itakuwaje ? Swali hilo bado linadhibitisha kuwa unao uwoga. Amini kuwa baada ya kushindwa, kutatokea njia mbadala au utakuwa umejifunza zaidi ili usikosee tena. Swala la kuogopa hasara linakupa shida, ila kumbuka nafasi za kushindwa ni chache pia, na hata utakaposhindwa  utakuwa umejikusanyia uzoefu wa kushindana na kushindwa. Hivyo wakati mwingine hautoogopa, na pengine utaweza kupambana vema na kushindwa.
Ukuta wa kuogopa maumivu, inaendana na ukuta wa kuogopa kushindwa. Chukulia maumivu kama sehemu ya mafunzo na matayarisho ya FURAHA.
Uvivu ni adui yako mkubwa, hata hivyo pengine umemkaribisha na amekuwa kama sehemu ya wewe. Unachotakiwa kutambua ni kuwa ili mambo yafanyike ni lazima YAFANYIKE, hakuna cha ziada, hivyo basi FANYA, usiwe mtu wakusema NITAFANYA. Ni vema kuanza kidogo kidogo kuliko kusubiri majuto, ya kujiambia "ningejua".
Jambo lingine ambalo unafanya pengine kila siku ni kujishusha bila kukusudia. Mara ngapi ungeweza kujisomea ili kupata ufahamu fulani hata hivyo ukajiambia 'aah ntamuuliza fulani', mara ngapi ungeweza kujiwekea akiba ili kutimiza kusudio lako la kununua kitu fulani hata hivyo ukajisemea "aah ntamuomba fulani". Yaani hata haupati shida ya kujiuliza kama kweli hayo unayodhani wengine wafanye kwa ajili yako wewe mwenyewe unaweza kufanya. Hali hii ni pacha wa kufikia wa UVIVU.

Miliki Maisha Yako
Tatu jiunge katika ulimwengu wa msemo huu maarufu, yaani ni msemo maarufu katika kusemwa na watu kuliko jinsi wanavyouishi. Msemo huo ni "Miliki Maisha Yako, Ishi Maisha Yako".
Pengine hata wewe umewahi kuutumia tena bila hata kutafakari maana yake hasa ni nini, kwani utaishije maisha yako, wakati upo bize unayatafuta hayo maisha ? Si wewe peke yako, wengi wamekumbwa na hali hii kwakuwa tumefundishwa na kuaminishwa katika jamii zetu kutokuishi maisha yetu. Angalia matangazo ya biashara yanavyokuhamasisha kununua bidhaa fulani fulani. Angalia mfumo wetu wa elimu unavyoandaa watu kuwa wa aina fulani bila kujali kuwa tupo wa aina tofauti tofauti, tuna mahitaji tofauti na hata  uwezo tofauti wa kiakili, n.k
Hivyo unajikuta na wewe umekuwa wa kuiga, umejifunza kujikataa, umejifunza kutokuangalia nini hasa unataka, bali nini haswa marafiki, ndugu na jamaa wanataka au wanategemea wewe uwe vipi. Halafu ukiitafakari hali unaona ni kama vurugu kwani hakuna anayeishi maisha yake. Wewe nawe una mtoto wako au utakuwa na mtoto, tayari unawaza vile unavyotaka mtoto wako awe. Hali hii inakufanya uogope kuwa tofauti. Umetoa kafara mipango yako mingi, umeacha kufanya mengi ambayo pengine una uwezo nayo au ungependa kujifunza.
Ni wakati wako sasa wa kuanza kushinda hofu, kuondoa uvivu, kutambua kuwa unayo maisha, na kuanza kuishi. 
Kumbuka: "Wewe kujibandika Manyoya, hata kama ni mwili mzima, hakukufanyi uwe kuku".

Anza sasa kuondoa manyoya uliyojiweka na kufanya kweli katika maisha yako. UNAWEZA. Mafanikio yanakungoja...


Share: