SOMO ZITO KUHUSU HATUA ZA KUWA MBUNIFU

Ubunifu na uthubutu wa kudadisi ni moja ya nguzo kuu za maendeleo na mafanikio ya mtu binafsi na hata mataifa. Rais Barack Obama ananukuliwa na website ya White House, akisema:
"The first step in winning the future is encouraging American innovation...... What we can do -- what America does better than anyone else -- is spark the creativity and imagination of our people. "
Ambapo twaweza tafsiri maneno hapo juu kama ifuatavyo:
"Hatua ya kwanza katika kuwa washindi hapo baadae ni kuhamasisha ubunifu wa Kimarekani....Kile tunachoweza kufanya --Kile ambacho Marekani inaweza kufanya kwa ubora zaidi zaidi ya wengine- yaani kuchochea ubunifu na udadisi wa watu wetu"
 Ubunifu unaleta faida kwa mtu binafsi kama vile:-
  • Kuweza kukabiliana na changamoto na ugumu wa kimaisha
  • Kuweza kuona nafasi za ziada za kuboresha maisha -"opportunities", kwani kiasili hatutengenezi "opportunities" bali tayari opportunities zipo, ila tunachofanya ni kuzitambua, na kuanza kuzitumia.
Kwa jamii kwa ujumla, Ubunifu husaidia:-
  • Kuweza kusaidia watu wengine
  • Kuweza kuongeza bidhaa na huduma kwa jamii
  • Kusaidia jamii kukabiliana na changamoto zilizopo
Makala hii inachambua kwa kifupi jinsi ya kuwa mbunifu. Haijalishi ubunifu ni wa namna gani - iwe kuandika kitabu, kuzalisha vyakula, kutoa huduma za ufundi n.k , yote hayo yanaweza kufanyika kwa ubunifu na kuleta manufaa.

Zingatia hatua zifuatazo:-

1. Jifunze kulikubali tatizo kama changamoto na fursa ya kuleta suluhisho: Wapo wengi ambao wanapoona ugumu katika jambo fulani, wanasita kuendelea au wanasubiri suluhisho toka kwa wengine. Ni kweli kuna mambo utawaachia wengine, lakini lile 'lililo karibu' na uwezo wako waweza litatua. Mfano ukaribu ninaozungumzia hapa inawezekana ni mazingira unayoishi, aina ya ujuzi wako, na uwezo wako

2. Tumia muda wa kutosha kujifunza: Ili kuwa mbunifu inakupasa uwe na taarifa za kutosha kuhusu tatizo unalotaka kutatua, ujue pia wengine wamefanya nini. Kujifunza ndio kunakopelekea uzoefu, na uzoefu au kubobea katika kitu ndiko kunakoleta ubunifu. Kumbuka kujifunza sio lazima uende darasani, waweza jifunza kwa kuona, kusikia, kujisomea, au kwa kufundishwa-darasani au sehemu nyingine yoyote ile.
Ndio maana STEVE JOBS aliwahi kusema :-
“Creativity is just connecting things. When you ask creative people how they did something, they feel a little guilty because they didn’t really do it, they just saw something. It seemed obvious to them after a while. That’s because they were able to connect experiences they’ve had and synthesize new things. And the reason they were able to do that was that they’ve had more experiences or they have thought more about their experiences than other people". 
Twaweza kutafsiri hivi:
"Ubunifu ni namna tuu ya kuunganisha vitu. Ukiwauliza watu wabunifu waliwezaje kufikia walivyofanya, wanajisikia hatia kwakuwa kiukweli hawakufanya lolote, bali waliona tuu kitu fulani. Ilionekana wazi kwao baada ya muda fulani. Hiyo ni kwa sababu waliweza kuunganisha uzoefu waliokuwa nao, na kuweka vitu kwa pamoja.Na sababu ya wao kuweza kufanya hivyo ni kuwa walikuwa na uzoefu, au walitumia muda mwingi zaidi kufikiria kuliko watu wengine, kuhusu uzoefu wao".
3. Thubutu Kuota: Baada ya kulitambua tatizo, ukawa tayari kulitatu, ukajawa na hamasa ya kujifunza, na ukajifunza vya kutosha kuhusu hali husika, kinachofuata ni wewe sasa kufikiria suluhu ya tatizo husika. Unachopasa sasa ni kupendekeza njia tofauti ya kufanya jambo, aina mpya ya bidhaa au huduma, na kujaribu hicho unachofikiria ili kilete mafanikio. Katika hali hii, Usiogope kukosea, na wala usiogope kuwa kitu chako kitakataliwa au kuonekana cha ajabu mbele ya watu wengine. Kwani kiuhalisi, ni kweli ni kitu tofauti hivyo jinsi watu wengine watakavyokipokea itakuwa tofauti.
Ndio maana Albert Eistein aliwahi kusema:-
"If at first, the idea is not absurd, then there is no hope for it".
Yaani: 
"Kama wazo, mwanzoni halionekani kuwa ni wazo la ajabu ajabu, basi hakuna matumaini juu yake".
Share:

TIBA YA MAMBO 5 YANAYOKWAMISHA BIASHARA BONGO

Wafanyabiashara wa Tanzania kama wale nchi nyingine,  hukumbwa na changamoto nyingi katika uendeshaji wa shughuli zao. Changamoto hizi ndizo zinaweza pia kuwa utofauti wa biashara zinazokua na zile zinazokufa.
Makala hii inachambua mambo matano ambayo huwa ni mzigo mzito kwa wajasiriamali , na pia makala inaonyesha baadhi ya njia za kukabiliana na changamoto hizo.

Kikwazo Namba 1 , Ubia:  Mara nyingi imekuwa ni ngumu kwa watu wengi kufanya biashara kwa kushirikiana na watu wengine, hususani katika hatua za mwanzo za uanzishwaji wa biashara. Vikwazo vinavyojitokeza katika kufanya ubia na watu wengine ni vingi kama vile : Kutokupata watu waaminifu, Kupata watu wasio na moyo wa kujitolea kufanya shughuli za biashara yenu, kupata watu wanaokuwa wagumu kujitolea mtaji wa kutosha kufanya biashara yenu, na zaidi sana, kupata watu wasio na muelekeo au mtazamo wa mbali wa kijasiriamali, yaani wao wanawaza faida ya haraka haraka, na kwamba kwao biashara ni sehemu ya kuingiza fedha ya ziada tuu ya leo au kesho.

Dawa yake:- Usiwe na haraka ya kufanya ubia na mtu, msome tabia yake vema. Jifunze pia kuhusu mtazamo wake wa maisha, na biashara, fahamu kuhusu familia yake na majukumu yake ya kijamii. Kisha pima uone kama majukumu yake, tabia yake, mtazamo wake , na imani yake vinaendana na biashara mnayotaka kuanzisha au malengo na mtazamo wako wa baadae wa biashara husika. Chunguza vyote kwa umakini, na usijidanganye, kumbuka dalili ya mvua ni mawingu, waweza jua mapema kama mtu atakuwa mshirika bora kwako mapema kabla hamjaanza kufanya biashara pamoja. 
Usichanganye urafiki, udugu au kujuana kwa namna nyingine na biashara yako. Anaweza kweli kuwa rafiki mzuri kwako, lakini biashara yenu inahitaji mtaji wa kutosha na kujituma kwa mhusika, kitu ambacho huyo rafiki yako hatoweza kufanya kutokana  na majukumu yake ya kifamilia.

Kikwazo Namba 2, Usimamizi wa wafanyakazi: Mambo magumu yanayojitokeza katika usimamizi wa wafanyakazi ni wafanyakazi kukosa uaminifu na kuwa na ufanisi wa chini ya kiwango. Usipoangalia utapata hasara, na hata kupoteza wateja kwani wateja kwa ujumla huja kufuata bidhaa na huduma zako ambazo zinatolewa na hao wafanyakazi.

Dawa yake:- Kuna namna kadhaa za kupambana na tatizo hili. Hatua ya kwanza ni wewe mwenyewe kujenga muundo mzuri wa biashara yako ikiwa pamoja na mpango bora wa kifedha ili uweze kulipa wafanyakazi kwa kiwango cha kuridhisha. 
Ukishakuwa na mpango mzuri wa kifedha maana yake utaweza pia kuajiri watu wanaokidhi kiwango cha kazi unachotaka wafanye, na sio basi tuu ili mradi watu. 
Kingine unachoweza kufanya ni kuweka muundo maalum wa utendaji katika biashara yako ili kila mfanyakazi afahamu majukumu yake, anaripoti kwa nani, anahitajika kufanya nini, na kwa kiwango gani. Fungua mianya ya mawasiliano ili kujua matatizo wanayokumbana nayo watendaji wako. 
Zaidi sana hakikisha watendaji wanao ujuzi na vifaa vinavyoendana na kazi wafanyayo na ufanisi unaotakikana. 
Tumia muda kujua tabia za watu unaotaka kuwaajiri, na endelea kuwa karibu nao na kujifunza kuhusu wao ili uweze kujua namna ya kuwachochea pia utendaji wao. Je, unafanya nini kuwachochea waonyeshe bidii na ubunifu. Je, unaruhusu ubunifu ? Je unawaheshimu na kuwathamini watendaji wako ?

Kikwazo Namba 3, Muundo wa biashara: Hili limekuwa ni tatizo kwa watu wengi hususani wafanyabiashara wadogo na wa kati. Ni tatizo zaidi kwakuwa wafanyabiashara wenyewe wengi hawaoni kama ni tatizo, wakitoa visingizio kuwa eti uendeshaji wao wa biashara ndio muundo bora zaidi  "kibongo bongo". 
Hapa nazungumzia kuwa na biashara ambayo haina mgawanyiko wa majukumu, haina mchanganuo wa biashara, haina utunzaji sahihi wa taarifa, na wala haifuati taratibu za kisheria kama usajili, kuwasilisha taarifa za fedha , kulipa kodi, kuwa na akaunti benki, n.k.
Hili ni tatizo kwa kuwa biashara hizo hazijaandaliwa kukua, na hata zinapofanikiwa kukua zinakumbana na ugumu wa kuwa endelevu. 
Hivyo kuleta ugumu wa kuongeza mtaji kupitia mikopo ya benki na asasi nyingine, ugumu wa kuendeshwa kitaalamu zaidi kwani madaraka yameshikiliwa na mtu mmoja, na ugumu wa kupanua fursa za kibishara kama vile kushirikiana na biashara kubwa zaidi , kushiriki katika kuomba Tenda, n.k. 
Na mbaya zaidi inapotokea mmiliki au mmoja wa wamiliki kufariki au kushindwa kuendelea kuendesha biashara, biashara huyumba na hatimaye kufa kwakuwa hakukuwa na muundo unaoeleweka wa uendeshaji wa biashara husika.

Dawa yake:-Kama haufahamu jinsi ya kuunnda muundo imara wa biashara yako,  mkodi mtu akufanyie kazi hiyo, au jifunze ili uweze kufahamu namna ya kuweka muundo vema. Heshimu taaluma za watu, na omba ushauri inapobidi. 
Fanya bidii uzungukwe na wafanyakazi unaowaamini na wenye uzoefu na ujuzi wa kile wanachokifanya. Jifunze mambo mengi zaidi kuhusu usimamizi wa biashara, na kuwa macho na changamoto unazokumbana nazo kwani hizo zinakupa mafundisho ya kuboresha biashara yako.

Kikwazo Namba  4, Mtaji: Kikwazo hiki hujitokeza katika mitazamo mitatu, kwanza wakati wa kutaka kuanzisha biashara, pili wakati biashara imeshaanza ila fedha hazitoshi kuendesha vema, na tatu pale mfanyabiashara anapokusudia kupanua biashara yake.

Dawa yake: Ili kukabiliana na kikwazo cha mtaji yafuatayo yanaweza kusaidia:
Kuanza biashara kidogo kidogo: Hii namaanisha kuwa kufikiria namna ambazo unaweza kuanzisha biashara kwa mtaji mdogo na wakati huo huo ukafanya kwa ufanisi. Hii inaweza kwa kuchunguza kwa umakini gharama zisizo za lazima, mambo ambayo unaweza fanya wewe mwenyewe au kusaidia na watu wengine bila kuajiri, pia chunguza aina ya bidhaa ambazo kweli ni za lazima kuanza nazo. 
Kutunza taarifa za biashara yako kwa ufasaha na kuwa na muundo bora wa uongozi, hii itakusaidia kuwa kutimiza masharti ya benki, na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha ambao wanaweza kukuongezea mtaji. 
Zingatia pia kuwa na mali zisizohamishika, na pia kuna na mahusiano mazuri na wadau mbalimbali kwani wao wanaweza kuwa vyanzo vya kukupatia mtaji. Mfano Badala ya kununua bidhaa kwa fedha taslimu, unaweza kukopa- mtaani tunaita "Mali Kauli".

Kikwazo Namba 5, Ushindani wa kibiashara: Kikwazo hiki kinajitokeza kwa namna nyingi ikiwa ni pamoja na uwezekano mkubwa wa kuigwa na watu wengine. Ni kawaida watu kutaka kuiga kama ufanyavyo hasa pale unapoonekana kufanikiwa. 
Kikwazo hiki hujitokeza pia katika namna ya bidhaa mpya zinazokuja kuwa mbadala wa bidhaa yako, na hata kuwa katika bei ya chini zaidi. 
Kumbuka siku hizi wateja wengi wana mianya mingi ya kupata taarifa za bidhaa mbalimbali na bei zake toka kwa wauzaji mbalimbali. Hivyo kufanya biashara kwa mazoea tuu kwakuwa una 'jina' kubwa haitoshi.

Dawa yake:- Jifunze kusoma alama za nyakati, kwa kufuatilia habari zaidi zinazohusiana na aina ya biashara unayofanya, wafahamu wapinzani wako vema, soma taarifa pia za mambo ya kijamii, kimataifa, siasa na hata burudani, vyote hivi vinaweza kukupa muelekeo wa mambo katika jamii hivyo kujituma zaidi na wewe kubadilika. 
Kujifunza kwako kuhusu wapinzani au wafanyabiashara wengine hakutokuwa na maana kama hautokuwa na muundo imara wa uendeshaji wa biashara yako, na pia ukaboresha ufanisi wako siku hadi siku.
Pia jitahidi kujenga uwezo wa kuitofautisha biashara yako na biashara nyingine , na kuwa na kitu cha kipekee ambacho wengi hawawezi kuiga, na hata kama wataiga, hawatoweza kufikia kiwango chako.

Hitimisho: Wewe msomaji kama mdau wa ujasiriamali , niambie hapa chini kwa ku comment, wadhani ni changamoto gani huwa vikwazo kwa wajasiriamali , na je tunazipatia tiba. 

Share:

MAMBO 4 YA MSINGI ILI KUPATA SCHOLARSHIP YA ELIMU

Haraka haraka unapoliona tangazo la Schorlaship,unajisikiaje? Je, umekata tamaa ya kupata schorlaships? Pengine bado unayo nafasi ya kupata scholarship, endapo utazingatia mambo ya msingi. Makala inadokeza mambo hayo ya msingi.  

1. Kupata nafasi ya chuo : Ni wazi kuwa unataka schorlaship (uhisani) ili kusoma katika chuo fulani, basi ni muhimu kwanza uwe umepata chuo. Unahitaji kupata chuo kwa sababu kuu zifuatazo:
  • Kwanza mhisani unayetegemea akufadhili ni muhimu kwake awe na uhakika kuwa unakidhi viwango vya kusoma kozi fulani, na kuthibitisha hivyo, ndio maana umeweza kukubaliwa kujiunga na chuo husika.
  • Pili, unapokuwa umekubaliwa katika chuo fulani maana yake utapokea maelekezo ya gharama zote za masomo yako chuoni hapo, na pia itakuwa rahisi kwa mhisani kuwa na uhakika wa gharama unazomtajia.
  • Tatu , wahisani wengi hutoa ufadhili moja kwa moja kupitia vyuo, hivyo unapokuwa umepata kukubaliwa na chuo fulani, basi ni rahisi kuomba ufadhili toka kwa wahisani wanaofadhili kupitia chuo husika ulichokubaliwa. Mfano: MASTER SCHORLASHIP IN SWEDEN
2. Maandalizi kabla ya kuaply:
  • Hakikisha una matokeo mazuri ya darasani: Wahisani wanataka kuwa na uhakika kuwa utaweza kuhitimu masomo watakayokufadhili, hivyo basi matokeo yako mazuri ya darasani kabla ya ufadhili wako, ni dalili nzuri kuwa unao uwezo wa kuenda kusoma na kufanikiwa kumaliza hivyo, fedha za wahisani hazitopotea bure. Baadhi ya wahisani huenda mbali zaidi kwa kutaka kufahamu kuwa elimu watakayokupatia itakuwa kweli ya manufaa kwako na kwa jamii hivyo hupenda kupata maelezo toka kwako namna ambavyo utaitumia elimu utakayopata. Ndio maana maombi yako ya ufadhili mara nyingi huambatana na barua ya. kujitambulisha na kujieleza malengo yako kuhusiana na fani unayoenda kuisomea.
  • Hakikisha lugha hususani kiingereza kinapanda vema: Nimetaja hapo juu, kuwa kuna kujieleza kuhusu fani unayoenda kusoma inavyoendana na malengo yako na manufaa kwa jamii kwa ujumla. Utaweza kujieleza vema kupitia lugha mara nyingi ni kiingereza.
  • Boresha uwezo wako wa mawasiliano: Utahitaji kuandika barua na wakati mwingine hata kuhudhuria usaili wa ana kwa ana na wahisani, hivyo uwezo wako wa kufanya mawasiliano fasaha ni muhimu. Jizoeshe kufuata kanuni za mawasiliano fasaha. Rudia tena kusoma Communication Skills.
3. Wakati wa kuapply
  • Soma maelekezo vema:  Amini usiamini, kila elekezo lililowekwa katika tangazo la schorlaship lina kusudio lake maalum, hivyo basi hakikisha unasoma maelekezo yote, na tena kwa ufasaha. Hii inajumuisha,  kusoma mambo kama vile lini mwisho wa kuapply, mambo gani unatakiwa kueleza katika barua ya maombi, nyaraka unazotakiwa kuambatanisha wakati wa kutuma maombi, jinsi ya kutuma maombi n.k.
  • Fuata Maelekezo kwa usahihi: Kusoma tuu maelekezo haitoshi, bali unatakiwa uyafuate vema.
4. Nini cha kutarajia kuhusu Schorlaships
  • Gharama zitakazolipiwa: Tambua pia inawezekana kabisa wahisani wasifadhili kila aina ya gharama za masomo yako. Hivyo unaweza kuendelea kutafuta wahisani wengine zaidi ili kupata ufadhili wa kutosha kulipia gharama zako. Msisitizo hapa ni kuwa usiwaze tuu kupata mfadhili mmoja , angalia uwezekano wa ufadhili mwingine, na pia wewe mwenyewe namna unavyoweza kujilipia.
  • Schorlaship za kusoma ndani ya bongo zipo: Ni kukumbusha tuu kuwa kuna schorlaship nyingine nyingi tuu za kusoma kwa vyuo mbalimbali ndani ya Tanzania. Tembelea mara kwa mara websites za vyuo kama UDSM.
 

Share:

JINSI FACEBOOK INAVYOINGIZA FEDHA KUPITIA KWAKO

Kwakuwa na akaunti ya Facebook, sio tuu unapata manufaa, bali pia unainufaisha kampuni ya Facebook
Facebook ambayo kwa sasa inapatikana katika lugha 70 ulimwenguni, ni mtandao wa jamii ambao unaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi zaidi duniani. Wewe na mie kama watumiaji wa Facebook tunainufaisha kampuni hiyo ya Facebook, kwani kupitia kuitumia kwetu kunaiwezesha Facebook kuingiza mapato kwa njia ya moja kwa moja au nyingine.
Makala hii inakuchambulia namna ambavyo Facebook inaingiza "vijisenti" vyake:-

1. Kupitia Matangazo: Kwakuwa inao watumiaji wa mtandao wengi, ni rahisi kwa Facebook kushawishi watu binafsi na makampuni kutangaza bidhaa zao kupitia aina mbalimbali za matangazo yanayorushwa hewani na Facebook. Mfano , kampuni inaweza kudhamini POST yake, ili ionekane kwa watu wengi zaidi na mara nyingi. Pia kuna matangazo ya biashara ambapo unaweza kutengeneza tangazo lako la biashara na kulirusha hewani kupitia Ukurasa wako wa Facebook (Facebook Page).  Ili kutengeneza tangazo Facebook, unaweza kuenda sehemu maalum ukiwa Facebook imeandika CREATE AN AD.
Unahitaji kuwa na Credit Card au Umejisajili na unayo akaunti ya Paypal ili kuweza kulipia huduma hii.
Mfano wa matangazo yanayoingizia Facebook 'vijisenti'
Namna nyingine kampuni ya Facebook inavyoingiza 'vijisenti'
2. Salio maalum la Facebook ( Facebook Credit)
Ni kama vile unavyonunua salio la simu yako ili utumie salio hilo kupiga simu, ila kwa Facebook, unaponunua Facebook Credit, ni kwa ajili ya kuweza kutumia credit hiyo kulipia kucheza Games, au hata kununua vitu katika baadhi ya maduka yanayouza bidhaa zao ndani ya Facebook.
Unahitaji kuwa na Credit Card au Umejisajili na unayo akaunti ya Paypal ili kuweza kununua Facebook Credit.
Sehemu ya Games ndani ya Facebook, baadhi ya Games inabidi ulipie, na unaweza tumia Facebook Credits kulipia.

3. Kupitia Kuudha bidhaa mbalimbali
Facebook inayo huduma ya kuuza bidhaa mbalimbali kwa mtindo wa "Gift" ambapo wewe mtumiaji unachagua nani unataka kumnunulia bidhaa , kisha unaenda kwa profile ya huyo unayetaka kumuuzia bidhaa. Utaona sehemu imeandikwa GIVE GIFT, ukibofya hapo utakutana na aina mbalimbali za zawadi na maelekezo. Hata hivyo huduma hii ya kutoa zawadi kwa watu haipataki kwa kila nchi. Inabidi ucheki Profile ya mtu husika unayetaka kumpa zawadi kuona kama GIVE GIFT ipo katika profile yake.

Share:

USHAURI WA P.DIDY NA LIL WAYNE KWA WATAFUTAJI KAMA WEWE

Mara nyingi tumejikuta tukitamani kujua ‘siri’ ya mafanikio, au kanuni maalum ya kufuata ili tufanikiwa. Na kuna nyakati tumejikuta tukitamani kuiga wale tunaowaona wamefanikiwa ingawaje kiukweli hatufahamu kwa undani nini wamefanya kufikia hapo walipofikia.
Katika video hapo chini, utajifunza kuwa mara nyingi tunapoona mafanikio ya watu tukatamani kuwa kama wao , na tukajikuta tunaiga mambo fulani fulani ili kujiweka kama hao watu, pengine kuna kitu tunakosea kwani mara tunasahau, kuna mambo mengi ya ziada nyuma ya pazia hatuyajui kuhusu watu tunaojaribu kuwaiga, au tunaotamani kuwa kama wao.
La msingi P.Diddy na Lil Wayne wanasema ni kujitahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kadri ya uwezo, usiige watu wengine, na jitahidi kuishi wewe kama wewe. Ina maana ni lazima kama unataka mafanikio endelevu, kwanza ujitambue, utambue nini unataka katika maisha yako, kisha utafute mbinu za kipekee na za uhakika za kufikia huko unakotaka kufikia. Zaidi sana usisahau bidii katika kujishughulisha ili kufanikiwa, hii inajumuisha kusoma sana ili kuongeza maarifa ya ujuzi wako, na kuwa mbunifu bila kuchoka.
Haya ni baadhi ya maneno katika video hii utakayoiona hapa chini:-

"Literally you just have to be really into what you are doing and what you are saying. You have to live it.... You don't have to try to be different, because when you try to be different, you all end up being the same because every body is trying to be different.
But you know what you got to do is be YOU, and if that doesn't work, then you know that is not what you should be doing”.

Share:

UMEKOSA AJIRA NA HAUNA MTAJI?: FANYA HAYA 7 UBADILI MAISHA YAKO

Makala hii inalenga kuibua tafakari ya namna bora ya kutafuta ajira na kuanzisha shughuli binafsi za kijasiriamali. Ingawa ni kweli kuwa kuhitimu ngazi fulani fulani za elimu ni jambo la msingi katika kupata ajira au kuwa na shughuli imara za kijasiriamali, wengi wamejikuta ngazi zao za elimu haziwasaidii kukabiliana na changamoto za ajira na ujasiriamali.

1. Boresha uwezo wako wa ufasaha wa lugha : Lugha ndio msingi mkuu wa mawasiliano. Jikite vema katika Kiswahili fasaha, na kiingereza kinachofuata kanuni sahihi katika kuongea na kuandika. Haijalishi una kiwango gani cha elimu, fanya bidii kuboresha uwezo wako wa kuandika vema na kuongea. Tumia hata internet kutafuta namna bora za kuboresha uwezo wako wa kuongea na kuandika kwani ‘broken’ english haitokufikisha popote, na Kiswahili kisichofuata kanuni hakitokufanya watu wakuchulie ‘serious’ katika maamuzi yao ya kufanya kazi nawe, iwe kibiashara au kiajira.

2. Jikite katika ujuzi fulani: Kama unataka kuitegemea elimu yako kuzalisha huduma au bidhaa fulani, ni lazima basi uwe kweli na ujuzi wa uhakika katika jambo fulani, na  sio tuu kuwa na cheti. Tafakari kwa umakini katika vyeti ulivyo navyo, ni mambo gani haswa unaweza kuyafanya kwa ufasaha, jikite katika hayo, ili kuwa na ujuzi imara utakaokupa heshima na kukubalika mbele ya wateja wako watarajiwa. Zaidi sana kumbuka, unaweza kujifunza ujuzi mpya usiokuwepo katika vyeti vyako.

3. Jitangaze : Kupitia mtandao wako, kupitia mikutano mbalimbali unayohudhuria iwe ya kifamilia, kidini, marafiki au vikundi vingine, hakikisha watu wanatambua uwepo wako , na kuwa wanajua kuwa unao ujuzi fulani. Zaidi sana sio tuu wajue unao ujuzi fulani, bali wajue pia kazi ulizokwisha fanya kupitia ujuzi fulani ulio nao. Watambue pia kuwa upo unapatikana kama utahitajika kwa ajira au kibiashara. Mitandao kama Facebook, inaweza pia kutumika kujieleza uwezo wako.

4. Jenga mtandao wa watu mbalimbali: Kuwa karibu na watu mbalimbali ili uweze kujifunza mengi toka kwao, na pia watu hao wanaweza kuwa wa msaada mkubwa kwako kama wateja wako, au wasambaji wa bidhaa fulani unazohitaji. Pia watu katika mtandao wako wanaweza kukusaidia kupata mtaji wa kuanzia ujasiriamali wako. Hata hivyo kumbuka, watu wamsingi katika kujenga nao mtandao wanahitaji kukutambua wewe kama mtu muhimu kwao pia, hivyo jiweke kama mtu muhimu kwa kuonyesha uadilifu, ujuzi wako, na heshima kwa wengine. Soma zaidi jinsi ya kujenga mtandao imara bofya hapa

5. Kuwa mbunifu: Tambua kuwa kinachowafanya watu kununua bidhaa fulani ni kwakuwa wanaamini bidhaa hiyo itakidhi hitaji lao. Hivyo basi tumia muda wako kuangalia matatizo au changamoto katika jamii na jinsi unavyoweza kuleta suluhu za changamoto hizo. Sio lazima uzalishe bidhaa mpya kabisa, hata kusaidia kuleta huduma adimu sehemu fulani, kusaidia kuboresha utendaji kazi wa watu kwa huduma za kiakili unazoweza kutoa kama ushauri, ni moja ya ubunifu unaoweza kufanya. Kumbuka ubunifu si jambo la haraka, unahitaji muda kusoma mazingira, fani na watu, kisha utafakari namna unavyoweza kutumia ufahamu wako wa mazingira, ujuzi mbalimnbali, na tabia za watu, ili kuleta huduma au bidhaa itakayohitajika na watu.

6. Fikra sahihi:  Kila mmoja wetu ana njia ya kipekee ya kufikia mafanikio yake maishani. Ingawaje ni kweli kuwa ajira na biashara zinatuingizia kipato cha kujikwamua kimaisha, hakuna kanuni moja ya namna gani utaingia katika ajira au biashara ili ufanikiwe kama fulani. Hivyo basi , usijilinganishe na watu wengine, kubali kuwa maisha yako ni ya kipekee, fikiria hali uliyo nayo kuwa ni ya kipekee na inahitaji suluhu ya kipekee. Hivyo tafuta njia yako ya kipekee ya kujiajiri kwa kuangalia hobbies zako, mtandao wako,  ujuzi wako n.k. Pengine hata kutokupata kwako kazi ni kwa sababu unawaza kupata ajira kama fulani na fulani walivyopata, au unawaza aina fulani ya kazi ndiyo ‘itakayokutoa’ kimaisha. Kumbuka kuna baadhi ya watu wana degree mbili na hawana kazi nzuri zaidi ya watu wenye degree moja, na kuna watu waliishia darasa la saba tuu, ila wana kipato kizuri na maisha bora.

7. Ota kwa usahihi na ujiamini: Hata kama unahisi hali yako kimaisha sio nzuri, bado unahitaji kuweka picha kubwa ya maisha yaliyo bora hapo baadae. Kuota sahihi ni kufikiria kwa umakini nini hasa unapenda kufanya, nini hasa unatamani yawe mafanikio yako, na zaidi sana kuota huku kunakuwezesha kujiona kabisa umefikia hali husika unayoitamani kwani unaamini na kujiamini kuwa zipo njia za kufikia huko. Kuota na kujiamini ni muhimu kwani ndiko sikuzote kutakako kusukuma kuendelea na unachofanya hata kama unapitia magumu, ndio wahenga walisema “palipo na nia, pana njia”.  Ukiota vema na ukajiamini, hautokaa tuu bure bure, ukilalamika ajira ngumu, au hauna mtaji, badala yake utatafuta mbinu za ziada, na kuwa mbunifu kwakuwa unakitu kinachokusuma kukifikia katika maisha yako, na hasa ndoto hiyo ikiwa inajumuisha kuleta mabadiliko katika maisha sio tuu, mabadiliko kwa maisha yako peke yako, bali kwa jamii pia.
Share:

TWITTER: NINI NA NAMNA UNAVYOWEZA KUITUMIA

Kama unataka kuwa “up to date” na taarifa mbalimbali ziwe ni makala toka website mbalimbali au habari za matukio mbalimbali, basi twitter, ndio njia maarufu sana katika kukufanikisha katika hilo. Makala hii inakupa maelezo ya jinsi ya kuanza kuitumia twitter, na pia kama umeanza kutumia basi inakupa mwanga zaidi wa mambo ya msingi kufahamu ili kuboresha matumizi ya twitter.

Twitter ni nini

Twitter ni mtandao unaokuwezesha kuandika ujumbe mfupi wa maneno usiozidi maneno 140 na ku ‘share’ . Ujumbe huo wa maneno 140, ndio huitwa ‘tweet’,  na kitendo cha kuandika na kurusha hewani ‘tweet’ yako ndio huitwa “ku tweet”.
Unaweza pia ‘kushare’ tweets za watu wengine, kitendo cha kushare tweets za watu wengine huitwa “ku retweet”.
Unaweza pia kutuma ujumbe kwa mtu binafsi aliyejiunga na tweeter, endapo umejiunga nae katika mawasiliano yenu ya tweeter.

Je unajiunga vipi na twitter
Ili kujiunga na twitter, kwanza inakupasa uwe na anuani ya barua pepe (email address), kisha ingia www.twitter.com  na utaona sehemu ya kujisajili (sign up). Katika kujisajili kwanza utatakiwa kuandika Jina lako, na pia utatakiwa kuandika barua pepe yako, na uandike password utakayokuwa ukiitumia kufungua hiyo akaunti yako ya twitter. Ukishamaliza kufanya hivyo, bofya Sign Up for twitter, na utakutana na ukurusa mwingine ambapo utakuwezesha kuchagua aina la jina utakalotumia katika Twitter. Angalia sehemu imeandikwa “Choose your user name”.
Jina lako la twitter huitwa “handle”, hivyo mtu anaweza kuambia “Niambie twitter handle yako”

Je unapata vipi watu wa kuwasiliana nao kwa twitter
Marafiki waliokualika au kukujumisha wewe kama rafiki yao  katika twitter wanaitwa “followers”, na wale unaowajumuisha wewe wanaitwa “following”. Mara kwa mara utapokea kutoka twitter wenyewe mapendekezo ya akina nani uwajumuishe kama “following” wako, hata hivyo, wewe mwenyewe pia unaweza kutafuta kwa sehemu ya search katika twitter majina ya watu au habari unazotaka kufuatilia, kisha ukawajumuisha watu kama “following” wako kwa kubofya sehemu ya “follow”

Je unapost vipi ‘status’:
Kushoto mwa ukurasa wako wa twitter kuna sehemu imeandikwa “ Compose new tweet”. Hapo ndipo unapoandika status yako na kisha kubofya “ TWEET”. Utaona pia alama ya picha, basi bofya hapo kama unataka kupost picha.

Matumizi ya alama ya #
Kwa usahihi, alama ya # hutumika kuifanya status iingie katika kundi maalum la aina ya status. Mfano kama utaweka #Majanga, basi unailazimisha status yako iingizwe katika kundi la status zinazotumia hiyo alama ya Majanga. Hii ina maana kuwa kama kuna watu wengine wametumia hiyo alama ya #Majanga, basi nyote status zenu zitaorodheshwa huko.

Picha ya Profile yako
Kama ilivyo katika Facebook, unaweza pia kuweka picha mbili kwa profile yako, ili kufanya hivyo nenda sehemu ya kuedit profile yako, ( Kulia juu mwa akaunti yako kisha bofya edit profile). Utakuta sehemu ya kuweka Photo, na sehemu ya kuweka picha ya Header.

Kuunganisha akaunti yako ya twitter na Facebook
Ndio, unaweza kuamuru twitter iwe inaonyesha tweets zako kwenye akaunti yako ya Facebook. Ili kufanikiwa katika hilo, unatakiwa kuingia sehemu ya Edit Profile, kisha angalia sehemu imeandikwa Connect to Facebook. Bofya hapo kisha ufuate maelekezo utakayoambiwa.

Twitter katika simu yako
Ndio unaweza kuitumia twitter kwa urahisi ukiwa ume download na ku install program maalum kwa simu za mkononi. Ukiwa kwa simu yako, nenda google.com, kisha waweza andika Download twitter for (android) kama simu yako inatumia system za android. Kama ni Nokia, basi andika Download twitter for Nokia. Kisha chagua chaguo la kwanza linalokupeleka kwenye ukurasa wa kudownload hiyo program, ukiisha install, utaweza tumia vema twitter katika simu yako.
Hata hivyo, hata kama hauna program ya twitter, unaweza tumia twitter, kwa kuandika anuani ya twitter kwenye sehemu ya kuandika anuani za website yaani www.twitter.com, kisha fuata maelekezo kama unataka ku sign in, au ku sign up.
Share:

BLOG 10 ZA KITANZANIA ZINAZOINGIZA HELA ZAIDI NI ZIPI ?

Kwa bahati mbaya Google haitoi majibu ya swali hapo juu- yaani ni blog zipi za kibongo ambazo zinaingiza fedha zaidi, au ni bloggers gani wa kibongo wanaingiza fedha zaidi. Hata ukiuliza hilo swali hapo juu kwa kiingereza bado hautopata jibu.
Sina uhakika kama kuna mtu mwenye takwimu au taarifa za 'ranking' za namna hii kwa nchi yetu ya Tanzania. Kama kuna mwenye taarifa hizi anaweza kutupia maelezo au link hapo chini sehemu ya kutoa maoni.
Picha ya makala hii hapo chini inaonyesha bloggers 10 wenye kuingiza fedha zaidi huko India. Link, hii hapa inaonyesha blogs 50 zinazoingiza fedha zaidi huko nje ya Tanzania.
Hata hivyo, lengo la makala hii sio kutafuta majina ya akina nani hasa wanaingiza fedha nyingi bali kupitia makala hii nataka kuibua tafakari ya jinsi wenzetu wa nchi mbalimbali wanavyoweza kuingiza fedha nyingi kupitia blogs.
Yafuatayo ni mambo ya msingi unayoweza kuona kutoka nchi za wenzetu:
  • Karibu blogu zote zinazoongoza kwa kuingiza fedha zinaandika mambo ya kimaendeleo hususani teknolojia
  • Karibu blogu zote zinazoongoza kwa kingiza fedha zinaongozwa kitaalamu, na kwamba hata wamiliki wake wana upeo mkubwa wa mambo wanayoyaandika na pia uwezo mkubwa wa kusimamia blogu zao hata ikibidi kuandika 'codes'
  • Hakuna blogu zilizoshika nafasi katika kumi bora kwa kuandika habari za udaku, na kuweka picha za ngono.
  • Karibu blogu zote zinazoongoza kwa kuingiza fedha zimejikita kwa habari zenye kulenga aina fulani maalum ya wasomaji.
  • Karibu blogu zote zinazoongoza kwa kuingiza fedha zina mwonekano mzuri sana , na kwamba matangazo hayachukui nafasi ya kwanza katika kuonekana. Msisitizo umewekwa kwenye kuonyesha kwa haraka makala za blogu husika.
  • Karibu blogu zote zinazoongoza kwa kuingiza fedha zimejikita katika kuhakikisha 'search engine' zinazitambua kwa haraka na  hivyo unapotafuta taarifa fulani mfano katika Google, majibu yako yatajumuisha makala toka blogu hizo, endapo unachotafuta kimeandikwa pia katika blogu husika. Hii inaitwa SEO ( Search Engine Optimization)
  • Karibu blogu zote zinaoongoza kwa kuingiza fedha, zimejikita katika kuleta upekee, iwe kwa aina ya makala wanazoandika, au hata muonekano wa nje ya blogu husika.
Jionee hapa chini 'wakali' wa India, kama walivyoandikwa katika BLOGGINGTIPS.COM
Share: