DOWNLOADS 6 USIZOTAKA KUZIKOSA !

Leo ninakuletea makala hii fupi, kukupa LINKS, zitakazoweza kukupatia vitu muhimu maishani.Bofya sehemu unapoona pameandikwa BOFYA HAPA, ili kuenda kwenye website ambayo itakuwezesha kufanikisha kupata kitu husika muhimu kama vile Biblia kwa Kiswahili, Quran kwa Kiswahili, uweze ku download movies kali , uweze kudownload hata vitabu ambavyo kwa njia za kawaida usingeweza kudownload.

1. Kudownload QURAN tukufu, tafsiri ya Kiswahili  BOFYA HAPA

2. Kudownload BIBILIA takatifu, tafsiri ya Kiswahili  BOFYA HAPA

3. Kudownload VITABU VYA GOOGLE, yaani vitabu ambavyo vinapatikana Google kama vile,kitabu kiitwacho ENTREPRENUERSHIP: Theory, Process, Practice BOFYA HAPA :

4. Kudownload documents ambazo zimewekwa password kiasi kwamba huwezi kuziprint, kucopy wala kupaste, BOFYA HAPA

5. Kudownload program ya kompyuta inayokuwezesha kutengeneza VIKATUNI,  BOFYA HAPA

6. Download program hii ya kompyuta UTORRENT, ili uweze kudownload MOVIES, kutoka mtandaoni kupitia website hii BOFYA
Share:

MASWALI MAGUMU KUHUSU MAISHA

'Pressure' za watu zimekufanya :

Kuwa na mpenzi uliye naye sasa

Kuamua kuoa au kuolewa na huyo mume uliye naye sasa

Kusoma masomo uliyosomea

Kufanya aina ya kazi unayofanya sasa

Kuwa na aina ya mavazi uliyo nayo sasa

Kuwa na aina ya marafiki ulio nao sasa

Kuishi mahali unapoishi sasa

Kujiunga na mitandao ya kijamii

Hata status zako zinalenga kutaka 'kuwa wa aina fulani' mbele za watu

---------JE LINI UTAANZA KUISHI MAISHA YAKO ?---------------

---------LINI UTAANZA KUISHI VILE UTAKAVYO ?---------------

---------LINI  WEWE NDIYE UTAKAYEAMUA VILE UTAKAVYO ?-----

---------LINI UTAACHA KUOGOPA WATU, UTAACHA KUOGOPA KUKOSEA BILA SABABU ZA MSINGI ?-----
Share:

MAMBO HAYA 6 YANAYOATHIRI UFAHAMU WETU

Vitabu vya dini vinasisitiza tutafute elimu, na katika Biblia (Hosea 4:6) kuna andiko linasema kuwa watu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Hivyo basi ni wazi kuwa tukifanya bidii katika kuboresha ufahamu wetu, tutaweza kutatua changamoto nyingi, na  tutaweza kuishi maisha yenye furaha na maendeleo.
Lengo la makala hii sio kusisitiza umuhimu wa kupata maarifa, bali makala hii inalenga kukudokeza mambo ambayo yanaweza kuwa adui yako katika juhudi zako za kutafuta maarifa.
Ifuatayo ni orodha ya mambo 6 kama yanavyotajwa na mtaalamu wa elimu ya jamii Earl Babbie katika kitabu chake “The Practice of Social Research” (2010), 12th edition, ukurasa wa 4-8.
Nimeongeza maelezo ya ziada katika points hizi toka kwa Babbie, ili kuboresha ufafanuzi kwa ajili yako:-

1. Tamaduni zetu: Sote tumejikuta tukiamini aina fulani ya maarifa kutokana na jinsi tamaduni zetu zinavyotuambia , na kwakuwa hivyo ndivyo kila mtu anavyofahamu, basi hatuoni haja ya kuhoji usahihi wa mambo husika, hata kama pengine si sahihi. Ingawa ni kweli kufuata tamaduni ni jambo jema, kuna hasara ya kutufanya tuwe wavivu wa kutafakari zaidi na kutafuta maarifa zaidi, na jambo baya zaidi ni kuwa tamaduni zinaweza kutufanya tukawa waoga wa kutafuta maarifa tofauti, kwani kufanya hivyo tutaonekana kuwa ni ‘waasi’ wa tamaduni. Kumbuka lugha, na dini zote ni sehemu ya tamaduni tulizorithi.

2. Mamlaka: Ni mazoea pia kufuata maarifa ya watu ambao tunawaona ni ‘viongozi’ katika jamii zetu. Wawe ni watu maarufu, wanasiasa, viongozi wa dini, au ‘wasomi’ wa vyuo vikuu. Kwa mpango huu , ni rahisi kwetu kukataa maarifa ya watu ambao hawana ‘mamlaka’ yoyote. Tatizo katika hali hii ya kufuata mamlaka ni kuwa kuna nyakati tunaweza tusipate maarifa sahihi, au tukajikuta hatufuati kweli maarifa kwa sababu ni maarifa bora, bali ni kwa sababu tunaangalia zaidi nani katoa maarifa husika.  Ni rahisi kwa mfano, kumsikiliza na kumuamini kiongozi wa kidini akitoa ushauri wa biashara kuliko kumsikiliza mfanyabiashara mdogo ambaye anao uzoefu wa miaka zaidi ya 10 katika biashara. Pia ni rahisi kuamini na kufuata mambo unayosoma kwa blogu ya mtu maarufu, kuliko kusoma blogu kama hii ya MBUKE TIMES, kwakuwa si ya mtu maarufu.

3. Kutokufuatilia mambo kwa umakini: Mara nyingi huwa tunajikuta tunafuatilia mambo juu juu,hivyo kutokupata taarifa zote na taarifa zilizosahihi. Mbaya zaidi unaweza kukuta mtu akipinga au kushutumu jambo ambalo hajalifuatilia kwa umakini.  Mfano mzuri katika hili ni namna ambavyo tunasoma magazeti au taarifa za mitandaoni. Je, huwa unatumia muda kupata taarifa zote kwa usahihi, kuchunguza kama habari ni muendelezo wa habari nyingine, au itafuatiwa na habari nyingine. Je, unaelewa maneno ya msingi katika makala husika unayoisoma ?. Kutokufuatilia mambo kwa umakini hujitokeza pia hata katika kutazama kwetu, je tunajifunza nini kutokana na mazingira tunayoyaona, rangi, aina ya mavazi , n.k ya watu tunaokutana nao ? 

4. Kutoa maamuzi ya jumla isivyo sahihi: Mara nyingi tumejikuta tukifikia hatua ya kuamini ‘ukweli’ fulani kwa sababu ya  kujirudia rudia kwa jambo, hivyo tukiamini kwakuwa tuu jambo limejirudia rudia mara nyingi, au kwakuwa watu wengi wana mtazamo unaofanana, basi jambo husika ni sahihi kwa watu wote, hivyo maarifa yetu yanajengwa katika imani au mtazamo usio sahihi. Mfano kwakuwa mara nyingi ukiwa na haraka na ukafika kituoni usikute daladala, na kwakuwa jambo hili huwatokea watu wengi, inaweza kusemwa kuwa ‘aah, ukiwa na haraka sikuzote hautokuta daladala kituoni’.  Pia kuna nyakati kutokana na aina ya mazingira tuliyonayo, aina ya watu tunaoishi nao, tunajikuta tukijiaminisha kuwa watu wengine mahali kwingine ni lazima watakuwa na tabia kama hizo. Ubaya wa aina hii ya kujenga maarifa yetu ni kuwa, inatufanya nyakati nyingine kupata maarifa yasiyo sahihi, na inatufanya kuwa wagumu kubadili mtazamo wetu. Chukulia mfano, kuna watu wanaamini kuwa blogu za kibongo hazina habari za msingi zaidi ya siasa, na udaku, na kwamba nyingi habari zake ni copy & paste, na hazijafanyiwa uchunguzi. Kwa imani hiyo, watu hao hawawezi kukuelewa kuwa kuna blogu kama MBUKE TIMES ambayo haipo hivyo wanavyodhani.

5. Kuchagua mambo ya kuchunguza: Kuna nyakati tunajikuta tunafanya uchaguzi wa aina ya mambo ya kutafakari kutokana na misukumo kadhaa katika maisha yetu, iwe kwa sababu ya tamaduni zetu, hasira, furaha, kuzoeana na watu , au taarifa za awali ambazo tunazo kuhusu watu au jambo fulani. Hali hii huwa ni tatizo katika utafutaji wetu wa maarifa sahihi, kwani tayari tunajiwekea kikwazo cha kupata maarifa zaidi. Mfano, kwakuwa umejiaminisha kuwa siasa ni uongo, basi unajikuta hautaki kusikiliza mtazamo wa wanasiasa, hata kama pengine wapo sahihi. Au kwakuwa wewe ni wa chama fulani cha siasa, basi unajikuta hautaki kusikiliza wala kutafakari hoja na mitazamo kutoka upande wengine wa siasa au wale ambao hawafungamani na siasa.

6. Ku ‘reason’ kusiko sahihi: Mara nyingi tunajikuta katika hali ambazo tunashindwa kuzielezea kwa urahisi , hivyo kujikuta tukibuni sababu za kutokea au kuwepo kwa hali husika. Kuna  sababu nyingi za uwepo au kutokea kwa hali fulani fulani ambako kwa kweli sababu hizo si sahihi, endapo utatafakari kwa undani utaona kuna uwezekano mwingine mwingi ambao bado hatujauangalia katika ku ‘reason’ kwetu.
Mfano 1: Utasikia mtu akisema ‘Aaah sawa tuu, niache niwe masikini kwakuwa sote hatuwezi kuwa matajiri, lazima wawepo masikini na matajiri’.  Ku ‘reason’ huku si sahihi kwakuwa kwanza hakuna ufafanuzi wa kutosha kuwa tatizo gani litatokea kama wote tutakuwa matajiri ? . Je, kama watu wote kuwa matajiri ni jambo lenye tatizo, kwanini basi tunaamini katika swala la Ahera /mbinguni, kwakuwa huko, bila shaka masikini hawatokuwepo.
Mfano 2: Utasikia mtu akitetea kutupa takataka  ovyo mjini au tuseme barabarani, kwa kisingizio kuwa anasaidia kutengeneza ajira kwa watu wa jiji !. Hii nayo ni aina ya ‘reasoning’ isiyo sahihi, kwani si kweli kuwa kama jiji litakuwa safi, basi ajira zitapungua, na si kweli kuwa watu wanaopata ajira katika kusafisha jiji, hawawezi kupata aina nyingine ya ajira, kama vile kuzibua mitaro, kutunza bustani, kusaidia kazi nyingine za usafi wa majengo n.k. Zaidi sana, kuna ushahidi wa kutosha kuwa ipo miji ambayo ni misafi, na bado halmashauri za miji hiyo, zimeajiri watu kwa shughuli mbalimbali zikiwemo shughuli za usafi.
Share:

MAMBO 5 YANAWEZA SAIDIA KUTIMIZA NDOTO ZAKO

Ni muhimu kuwa na utamaduni wa kuheshimu  ndoto zetu hata kama tunadhani kuwa ni ndoto ndogo kama vile ndoto ya kutembelea mkoa fulani, ndoto ya kutembelea nchi fulani, ndoto ya kumiliki aina fulani ya mali, n.k. Hata hivyo, kuweza kuheshimu ndoto zetu na kuzitimiza, kunahitaji nidhamu ya ziada, ingawa wapo wanaozifikia ndoto zao kwa bahati.
Wengi husema wanataka kutimiza ndoto zao, hata hivyo ni wachache hufanikiwa kutimiza ndoto zao. Kwa kuwa binadamu tuna ndoto tofauti tofauti, ni ngumu kuwa na kanuni moja ya jinsi ya kufikia ndoto zetu, hata hivyo uzoefu unaonyesha mambo kadhaa ambayo watu wengi waliofikia ndoto zao wamefanya. Mambo haya ndio tunayojadili katika makala hii:-

1. Ota ndoto kwa usahihi: Kuota ndoto ya mabadiliko ya maisha yako, sio tuu kuwaza au kutamani kufikia hali fulani, bali kuota kwa usahihi ni kutengeneza picha kichwani ya hali unayotaka kufikia, au mambo unayotaka kuyapata. Na zaidi sana, itengeneze picha ya hali unayotaka kufikiaau mambo unayotaka kufikia katika mawazo yako kiasi kwamba ufikie hatua ‘unahisia za kuwa tayari umefikia hali unayotaka au umeyapata hayo unayoyaota. Ikiwezekana weka katika maandishi ndoto zako ili iwe rahisi kuzikumbuka mara kwa mara.  

2. Tafakari kwa umakini: Ukishaipata kwa uhakika ndoto yako au ndoto zako, endelea kutafakari ili kutambua kwa undani  ili kutambua mambo ya msingi kuhusu ndoto yako kama vile:-
  • Mambo gani utatakiwa kufanya (Mfano kiwango cha elimu, kujua lugha za kigeni, kupata uzoefu fulani, n.k)
  • Aina ya mazingira yanahitajika ili kufikia ndoto hiyo (Mfano: Kupata washauri, Kujenga mtandao wa aina fulani ya watu n.k)
  • Kiasi gani cha juhudi au bidii inabidi uwe nayo ili kufikikia ndoto huto zako. (Mfano: Mazoezi ya kila siku, kujaribu biashara mbalimbali, n.k)
  • Aina gani ya msaada unahitajika (Mfano: Kama unahitaji fedha, unahitaji mtu wa kufundisha mambo fulani)

3. Weka mkakati: Mikakati ni yale yote unayoweza kufanya ili kufikia ndoto zako. Kupitia tafakari uliyoifanya kama ilivyoelezwa hapo juu, utaweza kupanga mbinu na namna ya kuzitekeleza mbinu za kufikia ndoto yako.

4. Amini na uwe mvumilivu: Tambua kuwa baadhi ya ndoto huchukua muda kutimia. Na pia sio juhudi zote utakazofanya zinaweza kufanikiwa. Hivyo unahitaji kuwa na uvumilivu na imani kubwa katika ndoto zako.  Usichoke pia kuchunguza mara kwa mara mikakati yako ili kuiboresha.

5. Fanya unachotakiwa kufanya kwa bidii na maarifa: Kuwa na ndoto pekee hakufanyi ndoto hizo kutimia. Unahitaji mikakati. Na zaidi sana unahitaji kufanyia kazi mikakati yako. Kumbuka kuwa ingawaje kuna swala la watu kufikia ndoto zao kwa bahati, tambua kuwa bahati ikikufikia wakati ambapo hauna uwezo au mazingira uliyonayo hayakuruhusu kuitumia bahati husika, basi bahati hiyo haitokuwa na maana kwako. 

Hitimisho: Maelezo hapo juu yanahitaji tafakari ya umakini, na utilie mkazo kila hatua. Anza kwa kuandika mambo unayodhani ndio ndoto zako. Usisahau kutembelea mara kwa mara orodha yako ya ndoto, tafakari ni ndoto zipi umefikia , na zile usizofikia tafakari jinsi ya kuzifikia. Nakutakia kila la kheri katika kufikia ndoto zako, najua ni furaha sana kufikia ndoto, hata kaka ni ndoto ‘ndogo’.
Share:

MAMBO 4 YAFANYAYO KUTAKA KUONEKANA ‘UPO JUU’ KUWA NI UTUMWA

Dale Carnegie aliwahi kusema “Kinachokufanya uwe na furaha Sio kile ulicho nacho, au vile ulivyo, au wapi ulipo, au kipi unafanya, bali ni vile unavyofikiria kuhusu hayo yote”. Hata hivyo miongoni mwetu , tumejikuta tuna wakati mgumu wa kujisikia na furaha kwakuwa tumetilia mkazo kufanya mambo kwa ajili ya kuonekana mbele za wengine.
Haijalishi namna gani ‘unauza sura’-yaani unatafuta kuonekana kuwa upo ‘juu’ iwe kwa kujibadili jina, kujidai kwa mavazi, mali kama nyumba au gari, kwa cheo, au kwa watu unaowafahamu, hayo yanaweza kuashiria upo kwenye mkumbo wa hali hii mbaya ambayo ukiitafakari kwa undani utagundua kuwa ina chembe chembe za utumwa wa kifikra.
Kuuza sura au kujidai kama ninavyojadili katika makala hii ni ile hali ya mtu kutaka kuonekana yupo ‘wa hadhi ya juu’ mbele za wengine, kwa lengo kuu la kutaka tuu kuwa juu kama njia ya kukubalika mbele ya jamii au kama njia ya ‘kupata heshima’ toka kwa hao anao walenga.
Kuna matendo mengi ambayo mtu anaweza akawa anatenda akatafsirika kama ‘anauza sura’ ingawa si kweli anauza sura, kwakuwa hana lengo la kutafuta heshima kama heshima, bali kuna malengo mengine ya ziada kama vile malengo ya biashara – kutangaza bidhaa, au kujenga jina lake kwa kutafuta umaarufu n.k.
Kuuza sura tunakokuzungumzia hapa kunaleta mambo yafuatayo:-

1.Tunasahau nini hasa tunahitaji: Tunapotilia mkazo  kujionesha kuwa sisi ni bora zaidi ya wengine kwa sababu za ‘kujidai’ tunajikuta tunaweka mkazo zaidi katika namna vile wengine wanategemea sisi tuwe, au tuseme tunaweka mkazo kwenye mambo yanayoonekana au kukubalika na wengi kuwa ‘ni matawi ya juu’. Hali hii inaweza kutufanya tusiweke mkazo katika tafakari ya mambo ya msingi ambayo sie wenyewe binafsi haswa tunahitaji. Mfano, badala ya kutilia mkazo mahitaji ya familia yako ya sasa, na hapo baadae kama vile elimu, afya n.k unaweza ukawekeza sana kwenye vitu vya kifahari ili na wewe uonekane upo ‘juu’. Ndio maana si ajabu, kusikia msanii maarufu aliye ‘tesa’ , akiombewa msaada wa kugharimiwa gharama za matibabu! Au kijana aliyeonekana miezi michache iliyopita ‘akitesa’, sasa amekuwa ombaomba misaada kwa watu mbalimbali.

2.Tunajiweka katika hali ya kujikataa: Kwa kuwa tayari tumeshakubali kuwa utimilifu wa furaha yetu ni kuwa ‘juu’ zaidi ya wengine, au kupata hisia kuwa wengine wanatuona tupo juu, tunajikuta tunajikataa sie wenyewe pale tunapoona kuwa hatujafikia viwango. Ndio maana si ajabu kusikia mtu akisema anaishi Masaki, wakati kiukweli kwao ni Tandale. Kwa hali hiyo hiyo, ndio maana si ajabu kumkuta mtu akipiga picha kwa nguo za kuazima, au kwa namna ya ubora zaidi itakayo ng’arisha muonekano wake na kuiweka Facebook ili hali, katika muonekano halisi hayupo hivyo.

3.Akili inapumbazika: Mambo mengi yanayotumika na watu kutafuta kuonekana wapo juu,  huwa si mambo halisi, bali ni mambo ya mpito, ambayo pengine watu hufuata mkumbo na kuyatumia isivyopaswa. Mfano, kuna wakati watu walitumia Flash Disks, kama kitu cha kuonyesha ‘wapo juu’, wengi walikuwa wanazibeba bila matumizi, na wakati huo huo, lengo la Flash Disk halikuwa kuonyesha ‘status’ ya mtu.
Mfano mwingine ni simu za mkononi , kuna wakati ilikuwa kuwa na simu ya mkononi ni kuwa ‘upo juu’. Hali kadhalika, siku za hivi karibuni kuwa na gari kumeonekana kama ni jambo la kuuza sura. Cha ajabu zaidi hata kuweka status na kuwa na likes nako kumechukuliwa kama sehemu ya kutengeneza ‘heshima’.
Viwango vya elimu pia vimekuwa vikitumika katika kutafuta ‘status’ wakati ki uhalisia, elimu ina kazi nyingine tofauti na hiyo ya ‘kutia adabu’ watu wengine. Utakuta kwa mfano, mtu akitafuta digrii, au Masters au akifanya uchaguzi wa jina la chuo, sio kwa sababu kuu ya manufaa ya uchaguzi husika bali ni kwa kuangalia namna ambavyo  ‘status’ yake itatafsirika, kuwa na yeye ‘yupo juu’.
Wengine huko Facebook, wamefikia hatua ya kuwa na majina ya ‘ajabu’ kama sehemu pia ya kuleta heshima mbele za wengine- majina kama DE VOS SHIZO NIZO, na kuweka picha za wasanii mbalimbali ni sehemu pia ya kuuza sura !!

4.Tunasahau uwezo wetu mkubwa:Kwakuwa tunajikita kwenye   kutafuta ‘ujiko’ au ‘heshima’ za bandia, na kwakuwa tunajisahau kufuatilia mambo haswa ya msingi tunayohitaji katika maisha yetu, tunasababisha Uwezo wa kuleta mabadiliko tulionao katika dunia hii kuwa umebanwa na mazingira tuliyonayo. Badala ya kufikiria ‘nje ya boksi’ tunajikuta mtazamo wetu wa maisha unajikita tuu ndani ya ‘boksi’ tulilomo, yaani ndani ya mazingira tuliyonayo – kwa kuangalia wenzetu wana nini, wamefanya nini, wanafikiria nini kuhusu sisi, na wanatarajia nini kuhusu sisi.

Hitimisho:
Makala hii haina lengo la kumaanisha kuwa kuwa kufanya mambo makubwa na mazuri kwa ajili yako kama vile kununua nguo nzuri, gari , nyumba , kupiga picha nzuri, kusafiri au kuishi maeneo mazuri ni vibaya, badala yake inapongeza kufanya mambo kama hayo, kwa manufaa ya mtu binafsi, na sio kuvutwa na kutaka kuvutia watu wengine.
Mwanasayansi na mwanahistoria Paul Rosenberg wa Freemanperspective.comkatika makala yake ya The contentment Revolution anasema:kuwa bora kwako si lazima kuwe na maana wengine wapo chini yako. Rosenberg anaendelea kusema kuwa kama tutajitahidi kufanya mambo kwa sababu yanatupendeza sisi, tukawaza zaidi nini tunahitaji basi ni wazi tutajikuta tunapunguza machungu yasiyo ya lazima ( mfano, machungu ya kujisikia upo chini ya watu wengine), na hata kupunguza hasara ya fedha, muda na mambo mengine tunayopoteza ili tuu kuwafanya watu wengine watuone kuwa eti sie tupo juu!.
Nimalizie kwa nukuu hii:

“Usiharibu kile ulichonacho, kwa kutaka kile usicho nacho”. Epicurus
“Do not destroy what you have, by desiring what you don’t have”. Epicurus
Share:

MAANA 3 TOFAUTI ZA UPENDO KATIKA MAHUSIANO

Ni jambo la kawaida kujiuliza kama unampenda Fulani au kama Fulani anakupenda. Katika tafakari hii, wengi hujikuta wakipata tafakari tofauti. Uzoefu wangu unanifanya niamini kuna maana tofauti kuu 3 zinazojitokeza miongoni mwetu wakati wa kutafakari swala la upendo katika mapenzi.
Jiunge nami katika tafakari hii kwa kusoma jinsi watu wanavyotafsiri tofauti neno Upendo katika mahusiano:’-

1.Kujali: Kuna wanaoamini kuwa kujali tuu inatosha kuonyesha kuwa unampenda fulani, au fulani kuonyesha anakujali basi hiyo ndio maana halisi ya upendo. Wengi hujikuta wakitumia muda mwingi kutafuta zawadi na surprises za ‘nguvu’ kama sehemu kuu ya kuonyesha upendo wao. Aina hii ya upendo inahusika sana hasa kwa watu waliopo mashuleni na vyuoni. Wengi wanaoamini maana hii ya upendo, husisitiza sana kuogopwa/kunyenyekewa kama sehemu ya kuonyeshwa kuwa nao wanapendwa.

2. Kujitoa kafara: Katika maana hii, upendo ni swala la jinsi gani unavyojitoa kwa mwingine ili kuona anakuwa na furaha na ajihisi kuwa salama kutokana na uwepo wako. La msingi katika aina hii ya upendo ni kupenda kumfahamu vema mwenzi wako, kujua shida zake, na ndoto zake, na kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha anaona uwepesi katika shida zake, na kuwa anakuwa na matumaini ya kuwa ndoto zake zitatimia. Upendo wa namna hii huwa na subira, na huonekana zaidi kwa waliokomaa kifikra, na wenye kujiheshimu wao wenyewe.

3.Kuvutia: Kwa wengine upendo ni namna gani wanavyovutiwa kimapenzi na mtu husika, au vile wanavyojisikia kuwa salama mbele ya mtu fulani.  Utakuta mtu anasema anampenda kaka fulani kwakuwa tuu amevutiwa na uhodari wa kijana husika katika masomo, kujiheshimu kwa kijana husika, sifa au umaarufu alionao mhusika. Na kwa upande mwingine, mtu anaweza kuvutia kwa uzuri wa sura au umbile la mtu fulani. Kutokana na mvuto wa hisia kama hizo na wakati mwingine hisia hizi za mvuto huwa kali sana, basi mtu akadhani hiyo ndiyo maana halisi ya Upendo. Wenye tafakari hii ya upendo wengi wao hawana subira na ukichukua muda mrefu kutafakari hisia hizi, unaweza kukuta ni za muda mfupi tuu.

Hitimisho: Pamoja na ukweli kuwa mvuto wa kimapenzi kwa mtu unayejenga nae mahusiano ni muhimu. Na kwamba kujaliana na kunyenyekeana ni vigezo muhimu katika kujenga mahusiano yenye furaha, mambo hayo pekee hayatoshi kusema kuna upendo. Upendo ni jambo lisilo na ubinafsi, haliangii nafsi yako inataka kunufaika kiasi gani, bali unataka kuinufaisha nafsi ya mwingine kwa kiwango gani. Hivyo kwa upande wetu, maana ya upendo tunayoipendekeza ni Kujitoa Kafara, kama tulivyoielezea hapo juu.
Yote katika yote, inakupasa utambue kuwa upendo pekee hautoshi kujenga mahusiano yenye furaha na yenye kudumu. Katika makala SABABU 5 KWANINI UPENDO HAUTOSHI KUJENGA MAHUSIANO BORA nilieleza kwa kirefu kuhusu hili. Bofya hapo ujisomee zaidi.

Share:

SABABU 7 KWANINI UENDELEE KUAJIRIWA BADALA YA KUJIAJIRI

1.Hauna Wateja Makini: Unashidwa kueleza kwa ufasaha wateja unaolenga hasa ni akina nani-yaani ni kundi gani la watu, na kwanini watu hao watanunua bidhaa yako. Haitoshi tuu kusema kwa mfano, utaanzisha kampuni ya mambo ya IT, au Advertising, lakini hauna maelezo ya kina akina nani hasa watanunua bidhaa unazotaka kuuza. Haitoshi kusema kwa mfano, “wateja wangu ni watu wote na asasi zinazohitaji huduma za IT, au Advertising,  inabidi uwe na uchambuzi wa kina aina gani ya watu na asasi zinazoweza kweli kuhitaji bidhaa zako, na kwanini unadhani watakuja kununua bidhaa zako. Kumbuka sio lazima uwe na majina ya asasi au watu unaotazamia waje wanunue kwako, ila kuwa na mtazamo wa kina wa tabia na wasifu wa kipekee wa wateja wako watarajiwa ni jambo la msingi.

2.Hauna Bidhaa Ya Kipekee:  Ili kuhakikisha unapata kipato cha kuridhisha na kuwa na biashara endelevu, inakupasa uwe na bidhaa ya kipekee katika kujiajiri kwako. Kama hauwezi kueleza kwa kifupi walau kwa sentensi tano, upekee wa bidhaa na uendeshaji wa biashara yako, ni dalili kuwa kujiajiri kwako hakutokuwa na tija.

3.Una haraka ya mafanikio:Mtazamo wako mkuu ni kujenga biashara yenye kukua ‘chap chap’, na pengine kwakuwa una mtazamo huu, una amini kuwa namna pekee ya wewe kuanzisha biashara yako ni kuwa kwanza na mtaji mkubwa wa kifedha. Ingawaje ni kweli kuwa fedha nyingi ni muhimu katika kuanzisha na kuendeleza biashara, mtaji mkubwa si wa lazima kwa kila aina ya biashara, na kwanza njia bora ya kuanzisha biashara ni kuanza kidogo kidogo. Hata biashara kubwa kama kampuni ya Apple inayotengeneza simu za iPhone – ilianzia tuu kwenye kachumba kadogo ka gereji, kampuni ya kompyuta ya DELL-inayotengeneza kompyuta aina ya Dell, ilianza kwenye kachumba kadogo ka bweni la chuo, tena kwa mtaji wa $1000 tuu !.

4.Hauna Mtandao wenye tija:Ni wazi kuwa watu watakaotoa mchango mkubwa katika mafanikio ya biashara yako ni wale ambao unamfahamiana nao kwa karibu, kupitia mtandao wako. Haitoshi tuu kufahamiana na watu wengi, bali watu hao wengi wakufahamu pia haswa haswa wakufahamu kwa mazuri na uwezo wako katika mambo makubwa, ni rahisi hapo baadae kupata humo katika mtandao wako, washirika wa biashara, wateja na hata wasambaji wa bidhaa na huduma kwa biashara yako. Na kama inavyosemwa: “ Katika dunia tuliyopo sasa, sio tuu una nini na una jua nini, bali je unamfahamiana na akina nani ?”

5.Hauna mkakati maridhawa wa kifedha:Biashara utakayoianza itahitaji fedha na pia wewe binafsi na familia yako mtahitaji fedha. Kwa kuwa ni muhimu kuweka tofauti mambo ya biashara na mambo yako binafsi, ni unatakiwa uwe na mkakati wa maridhawa wa kifedha wa matumizi na mapato yako binafsi na  yale ya biashara.Hata kama unafikiria kuwa biashara itakuingizia fedha za kujikimu na kusukuma maisha, je mapato kuchukua kwako huko fedha toka kwa biashara kutaathiri vipi mwenendo wa biashara, ambayo ndiyo itakuwa chanzo kikuu cha ajira yako?

6.Hauna Ufahamu wa kutosha kuhusu biashara uitakayo:Ufahamu wa biashara utakayo kuianzisha ni muhimu kwani utakuwezesha kujua kama kweli inalipa au la, na pia kujua mbinu za kuiboresha na kuifanya endelevu kwa siku za usoni. Ufahamu wa kutosha wa biashara utakuwezesha kutafakari pia kwa undani wateja gani hasa unawalenga, washindani gani hasa utakabiliana nao, na pia changamoto na matatizo ya biashara husika kabla haujaingia kuianza.

7.Hauna mvuto wa kutosha kwa biashara uitakayo kuanzisha: Unahitaji kusikia kitu kama wito au mvuto wa kipekee wa kitu unachotaka kukifanya kama biashara ili kweli uweze kukifanya kwa uendelevu , kwani kutakuja nyakati ambapo biashara haitaingiza kipato cha kutosha, utapitia changamoto na matatizo mengi, na wakati huo, kitu kitakachokupa msukumo wa kipekee wa kuendelea na kuwaongoza hata washirika na wafanyakazi wako muendelee na biashara, ni kule kupenda (wito) wako na hiko unachotaka kukifanya kama biashara.
Share:

JINSI YA KUTUMIA FURSA 5 ZILIZOPO KATIKA AJIRA ( UKIACHA MSHAHARA)

Baada ya kumaliza masomo yako, ajira huchukua nafasi kubwa ya maisha yako. Pamoja na ukweli kuwa lengo kuu  la kuajiriwa ni kuingiza kipato, inakubidi utafute namna nyingine za ziada za kufurahia ajira yako zaidi ya kusubiri tuu kupata mshahara mwisho wa mwezi. Mazoea ya kusubiri kufanya kazi kwa ajili ya mshahara tuu, yanaweza kukufanya ukajihisi kuichoka haraka ajira yako, au kujikuta usiye na furaha kazini, ukitilia maanani kuna changamoto nyingi za kifamilia, na kijamii utakazokuwa ukikutana nazo.
Makala hii inachambua fursa 5 ukiacha kupata mshahara. Fursa hizi 5 zinahusu mambo mengine yatakayokufanya uone ajira yako ina maana zaidi ya mshahara unaoupata. Inawezekana ajira uliyonayo sasa isiwe na fursa zote ninazozitaja hapa chini, hata hivyo ni matumaini yangu kuwa ukitafakari kwa umakini unaweza kuambulia fursa walau moja katika hizi zinazoelezwa hapa chini:-

1.Kushiriki katika kumiliki asasi husika: Kuna baadhi ya asasi zina sera ya kuruhusu wafanyakazi kuwa wamiliki wa asasi husika. Pia waweza vutia wamiliki wa asasi uliyopo kukualika uwe mshirika katika umiliki wa asasi yao, kutoka na ufanisi wako wa kiwango cha juu na kujitoa kwako kwa asasi husika. Ili kufanikiwa katika hili, boresha ufanisi wako, jenga mahusiano mazuri na wamiliki, na ujitoe kwa dhati katika kufanikisha mafanikio endelevu ya asasi unayofanyia kazi.Kwako ajira iwe zaidi ya mshahara, bali ni namna unavyoijenga asasi utakayoimiliki hapo baadae.

2.Kujenga mtandao: Unapokuwa umeajiriwa unakutana na watu wa aina nyingi, ukianzia na wafanyakazi wenzako, wateja wa asasi uliyopo, mabosi wako, na wasambazaji wa huduma na bidhaa mbalimbali. Katika makundi yote haya ya watu utaweza kupata wateja wako  wa baadae utakapotaka kujiajiri, pia unapata kujuana na kujenga mtandao wa wasambazaji wa bidhaa na huduma kwako hapo baadae kama vile watu wa benki, wamiliiki au wafanyakazi wa vyombo vya habari, n.k. Pia katika kundi hili unaweza kupata washauri –mentors ambao watakujenga kitaaluma na kuongeza uwezo wako wa kumiliki mambo yako binafsi. Utaweza pia kupata watu ambao wanaweza kuwa wahisani wako wa baadae au watu utakaomiliki nao biashara hapo baadae.

3.Kuboresha ujuzi wako: Ajira yako inakupatia fursa ya kupata ufahamu kwa njia ambazo pengine zingekugharimu sana kama wewe mwenyewe ungekuwa unazilipia. Mfano unaweza kuwa unapata huduma za internet muda wote uwapo ofisini, unapata nafasi ya mafunzo mbalimbali kupitia semina, na hata kozi mbalimbali unazolipiwa ukasome. Tumia vema internet ya ofisi kuongeza pia ujuzi wa mambo mengi ya msingi kielimu na kifikra, na pia kozi au semina unazoenda ziboreshe ujuzi ambao utaboresha utendaji wako hapo ofisini ili upate fursa nyingine zaidi zinazokuja na ajira, lakini pia ujuzi huu utauhitaji utakapokua umejiajiri au umebadili sehemu ya ajira toka asasi ya sasa kwenda asasi nyingine.

4.Kufanya maandalizi ya kujiajiri: Kuwepo kwako katika ajira ni fursa tosha ya kujifunza kwa vitendo jinsi asasi zinavyoendeshwa ili utakapokuja kujiajiri utumie uzoefu na uelewa ulioupata kufanya asasi yako iwe ya mafanikio. Kuna mapungufu utakayoyaona toka katika asasi uliyopo, na mazuri utakayoweza kuiga. Mambo ni mengi unayoweza jifunza toka aina ya nyaraka zinazotakiwa katika kuendesha asasi, jinsi ya kuendesha mikutano mbalimbali ndani ya asasi yako, kanuni na sera zinazofaa katika kuendesha asasi, hadi katika namna ya kujenga mifumo ya ufuataliaji wa maendeleo ya asasi yako utakapojiajiri.

5.Kutengeneza jina kwa ajili ya watu wengine: Ufanisi wako kazini, mahusiano yako bora na bosi wako na wafanyakazi wako, na kwa kupitia mtandao wako utaweza kuja kusaidia watu wengine kupata kazi kwa kuwapendekeza kwa mtandao wako au kwa mabosi wako.  Na kwakuwa tayari umejijengea heshima na uaminifu mbele za watu wengine, ni rahisi kusikilizwa hivyo ukaweza kusaidia ndugu zako, jirani au jamaa mbalimbali kupata ajira kwa mgongo wako.

Hitimisho: Kuzitambua fursa hizi na kuweza kuzitumia vema kunategemea sana na jinsi wewe mwenyewe unavyodhibiti mwenendo wako kazini. Je, una mahusiano ya aina gani na wafanyakazi wenzako, bosi wako, na wateja wa asasi yako ? Je, unabidii kiasi gani ya kujifunza mambo mapya ukiwa kazini, je una ufanisi wa kiwango cha juu katika utendaji kazi ? Je, unakabiliana vipi na changamoto unazokumbana nazo? Je unaheshimu vipi taratibu na sera za asasi uliyopo? Je unajua kiwango gani cha ufanisi unatazamiwa kuwa nacho hapo kazini kwako ? Je, wajua majukumu yako na unayatekeleza kwa kiwango gani ? n.k
Share:

MAMBO 5 YANAYOUMIZA WENGI KATIKA MAHUSIANO

1. Kuna jambo huwezi ficha: Kuna jambo hata ukijaribu kulificha, ukweli wake utajulikana tuu hususani kama utakuwa na mahusiano ya muda mrefu na mtu husika. Jambo hilo ni ukweli  kama unampenda kwa dhati mwenza wako au la. Mpenzi wako akiwa makini atagundua ‘kufeki’ kwako , kutokana na matendo yako hususani vile unavyojali hisia zake, usikivu wako kwake, heshima yako kwake, na unavyojali umoja na kudumu kwa uhusiano wenu.

2. Fedha sikuzote itawasumbua: Hata kama mtajitahidi kupuuzia umuhimu wa fedha katika mahusiano yenu, fedha itabaki kuwa mhimili mkubwa wa mahusiano yenu. Hata kama nyote mna ingiza kipato kuna changamoto mtazipata kama vile kupanga kwa pamoja jinsi ya kutumia fedha zenu, au kujieleza kuhusu matumizi fulani ambayo mwenzi wako atahoji. 

3. Kazi ya ziada: Haijalishi una hisia na makusudio mazuri sana, bila matendo yanayomridhisha mpenzi wako, hautoweza kujenga furaha ya kweli katika mahusiano yenu. Ni muhimu pia kutambua kwamba pamoja na kuwa na makusudio na matendo mazuri, inakupasa kutilia mkazo kuwa matendo yako na makusudio yako yanaaminika kwa mpenzi wako.

4.Kuna mambo hautokaa ujue ukweli wake: Haipendezi ila ndio uhalisia kuwa pamoja na ukweli kwamba nyie mmeshibana katika mahusiano yenu, bado kutakuwepo na siri ambazo haitaambiana. Mbaya zaidi katika siri hizo, inaweza kuwepo siri ya hisia halisi kuhusu upendo wa mpenzi wako kwako, au upendo wako kwake. Mfano, wapo waliooana lakini mmoja wapo sio kwamba kweli anampenda mwenzake, ila alitaraji kujenga upendo akiwa kwenye ndoa, na kweli anapokuwa kwenye ndoa anajikuta amejenga kumjali mpenzi wake, hatimaye anajikuta ameweza kumpenda moja kwa moja. 

5.Makosa haya ni magumu sana kusahaulika: Kwa kawaida binadamu wengi hukumbuka mabaya kwa urahisi kuliko mazuri tunayowafanyia. Na katika mahusiano, makosa haya mawili ; kwanza ni ‘ku cheat’ na pili kutokuonyesha mvuto wa kimapenzi kwa mpenzi wako, yanaweza kuwa makosa ambayo si rahisi kusahaulika, ingawaje mtu atajitahidi kusamehe, na kujaribu kufanya mahusiano yaende kawaida.
Share:

NJIA HIZI 5 ZITAKUINGIZIA KIPATO UKIWA INTERNET

Bila shaka unapata manufaa kadha wa kadha kupitia internet. Je, unaingiza fedha kupitia mtandao, au wewe ni mtu wa kutumia tuu fedha kwa ajili ya internet lakini bado haujaanza kuingiza fedha kupitia mtandao? Makala hii inachambua namna ambavyo unaweza kutumia internet kuingiza kipato.

1.Kutafutia watu taarifa: Wapo watu  wengi wenye shida ya kupata taarifa fulani kwa uharaka na kwa usahihi, hata hivyo wanakumbwa na vikwazo vingi kama vile wapo ‘bize’ sana –hata kama wanayo kompyuta na internet connection masaa 24, au pengine ni kwakuwa hawana ujuzi wa kutosha wa kupata taarifa kwa ufanisi zaidi. Watu wa aina hii pengine ni wanafunzi wa elimu ya juu, wafanyabiashara au watafiti wa fani mbalimbali.  Uwezo wako wa kutafuta taarifa kwa ufanisi, na kuweza pia kutambua wateja walengwa wa huduma hii , kunaweza kukufanya kuingiza kipato.

2.Kuuza bidhaa kwa bei poa kabisa:  Kupitia internet utaweza kupata taarifa za bei za bidhaa mbalimbali. Umakini na juhudi zako za kutafuta bei nafuu zaidi kunaweza kukufanya ukajua bei poa kabisa za bidhaa fulani, kasha ukatafuta wateja wa kuwauzia bidhaa hizo. Jambo hili limerahisishwa sana siku hizi kwa kutumia mitandao ya kijamii kwani  wapo watu tayari ambao huingia kwa mitandao ya kijamii kama Facebook, wakitaja aina ya bidhaa wanazotafuta. Tembelea NIPENI DILI group la Facebook, utajiona fursa hii.

3.Kutangaza bidhaa za watu/makampuni:  Kupitia mtandao mkubwa utakaoweza kujenga kwa kutumia internet, utaweza kutangaza bidhaa za watu au asasi mbalimbali. Mfano waweza tangaza bidhaa za watu kupitia blogu yako(yenye wasomaji wengi), au kupitia ukurasa wako wa Facebook, au kupitia huduma maalum ya kutangaza kwa barua pepe, ambapo utawaomba watu wajiandikishe kupata updates mbalimbali ikiwemo matangazo ya ofa mbalimbali za  bidhaa. Waweza pia tangaza bidhaa kwa website/blogu yako kwa kupitia Affiliate programs, ambapo utalipwa kuendana na ‘clicks’ zitakazoingiza wateja kwa asasi fulani.

4.Kutangaza bidhaa zako:  Kuna njia nyingi za kutangaza bidhaa zako kupitia internet, kuanzia kutangaza bure au hata kulipia matangazo yako. Waweza kutumia akaunti  yako ya Facebook au GooglePlus kutangaza bidhaa zako. Waweza tengeneza blogu  na kupitia blogu hiyo ukaweka matangazo yako. Au ukaamua kulipia matangazo kwa blogu za watu wengine, ukatangaza kupitia Facebook, na website mbalimbali.

5.Kuandaa kipato kikubwa cha baadae: Ukiachilia kupata kipato cha haraka haraka kwa wakati huu, unaweza kutumia mtandao kuandaa mapato makubwa ya baadae. Unaweza kufanya hivi kwa kutumia internet kujenga mtandao utakaokusaidia hapo baadae-mfano kutumia Linkedin, Facebook au Twitter kujenga mahusiano na watu ambao baadae watakuwa wateja wa bidhaa zako, au washirika katika biashara, au hata waajiri wako wa baadae. Pia waweza kutumia internet kujenga ufahamu na ujuzi fulani ambao hapo baadae utaweza tumia ujuzi huo kuingiza kipato. Mfano kuna website nyingi zinazotoa mafunzo bure ya ujuzi adimu kama website design, programming, marketing, n.k.

Hitimisho
Ukitafakari maelezo hapo juu , utaona kuwa kuna mianya mingi ya jinsi ya kuingiza kipato kwa kupitia internet. La msingi ni matumizi yako ya busara ya internet, na kuendelea kujifunza siku hadi siku namna bora ya kuboresha matumizi yako ya internet. Hata kama kwa sasa unadhani unaingiza kipato cha kutosha, hautodhurika kwa kujifunza njia nyingine za kuongeza kipato chako.
Share:

MAMBO 5 YATAKAYOONDOA UVIVU AU KUAHIRISHA AHIRISHA MAMBO YA MSINGI

Baadhi ya watu wamekumbwa na tabia ya kuahirisha mambo ya msingi bila kuwa hata na sababu ya msingi ya kuahirisha huko. Wengine ni uvivu wa kuanza au kuendeleza jambo fulani. Zipo sababu nyingi kwa nini uvivu au kuahirisha huko hutokea. Wengine huwa ni kisingizio maarufu cha kuwa wapo ‘bize’ sana, wakati wengine ni kwa sababu ya kujiachia- yaani kuridhika na hali waliyo nayo sasa (tunasema watu wa aina hii wapo kwenye ‘comfort zone’).
Makala hii inachambua mambo matano (5) ambayo ukizingatia unaweza kushinda uvivu, kuridhika na kuahirisha hairisha mambo ya msingi bila sababu ya msingi:-

1. Weka picha ya maisha mapya: Fikiria vile maisha yako yatakavyobadilika kutokana na kufanikiwa katika jambo ambalo sasa unakuwa mvivu kulifanya au unalifanya kwa kusua sua.  Pengine maisha yako yatabadilika kwa kuongeza mtandao wa watu muhimu katika maisha yako, pengine kipato chako kitaongezeka, pengine jina lako litakua na sifa kwako zitaongezeka, pengine utajitengeneza uhuru wa fikra n.k

2. Tambua wajibu ulionao kwa watu wako wa karibu: Jambo la msingi unaloona uvivu kulifanya au kuliendeleza kiasi kwamba unajikuta unaahirisha mara kwa mara, linaweza kuwa watu walio karibu nawe wanakutarajia ulifanye. Mfano , pengine umetoa ahadi ya kufanya jambo husika, pengine ni jukumu la kikazi, pengine jukumu la kibiashara,  kifamilia, au hata jukumu la kimapenzi (kuwa kufanya kwako jambo husika kutatimiza matarajio ya mpenzi wako).

3.Tambua wajibu wako wa kiroho: Kumbuka pia una jukumu la kiroho la kutenda mambo ya msingi na kuwa mtu wa msaada kwa wanaokuzunguka na dunia kwa ujumla. Haijalishi wewe ni wa dini gani, sote tuna jukumu la kuwa wa msaada kwa wenzetu. Hivyo kama kuanza au kuendeleza jambo unalotakiwa kufanya – iwe kujiendeleza kwako kielimu, kuanzisha biashara,kubadili tabia fulani iwe bora zaidi,  n.k , tambua kufanya hivyo hakutakunufaisha wewe peke yako, bali kutanufaisha wengi.

4.Fikiria ‘maadui’ zako:  Kumbuka kuwa kuna watu ambao wangependa kukuona haufanikiwi, hawa ni ‘adui’ zako. Hivyo kwa kadri unavyoahirisha mambo yako ya msingi au kuwa mvivu katika kuanza na kukamilisha mambo hayo, tambua unatengeneza nafasi za ‘ushindi’ kwa adui zako.

5.Jiambie unaweza: Ukiwa na mashaka ya kuweza kuanza au kuendeleza jambo unalolitamani au kulitafakari itakuwa ngumu pia kuanza jambo husika. Hivyo kujikuta ukiahirisha au kuwa mvivu tuu wa kuanza na kuanza au kuendeleza jambo husika. Watu wengine wanaweza ‘kukupa moyo’ katika jambo fulani, hata hivyo wewe mwenyewe ni muhimu ujione –utengeneze picha ya akilini , kuwa umekamilisha jambo husika kwa mafanikio.
Share: