HII NI KWA WANAOGOPA KUUMIZWA KATIKA MAPENZI

Ni jambo lisilofichika kuwa wapo watu wengi wanaogopa kuumizwa katika mapenzi. Kuumizwa huku kunaweza kuwa kwa namna kadhaa kama vile kumpenda mtu halafu mtu husika asionyeshe kukujali, au kuwa katika mahusiano na mtu halafu mtu huyo baada ya muda fulani akakuacha na kuenda zake na mpenzi mwingine.
Kwa mtazamo huu watu wanaogopa kuumizwa katika mapenzi wapo wa aina mbili; wale ambao wanaogopa hata kuwa na mpenzi kwa sababu ya kuogopa kuumizwa, na wale ambao wapo katika mapenzi lakini hawaamini kama wapo salama, maisha yao ni ya wasiwasi kuwa muda wowote mpenzi anaweza kumuacha ‘solemba’.
Makala hii inachambua namna ya ‘kudeal’ na hofu ya kuumizwa katika mapenzi.

Sababu za kuogopa:
Mambo kadhaa yanaweza changia mtu kuogopa kuumizwa katika mapenzi. Zifuatazo ni baadhi:
  • Mtu alishawahi kuachwa ‘solemba’ na mpenzi hapo kabla
  • Mtu ameshuhudia rafiki, ndugu au jirani akiachwa ‘solemba’
  • Wivu uliopitiliza kwa mpenzi husika bila kuwa na sababu za msingi za wivu.
  • Kuishi kwa kufuata matarajio ya watu wengine:Yaani mtu yupo katika mapenzi lakini ni kama vile anaripoti mambo yake ya mapenzi kwa watu wengine. Hivyo anaogopa ‘jina’ lake litachafuliwa endapo itaonekana mpenzi kamuacha.  Kwani kwa wengine kuachwa katika mapenzi kunamaanisha udhaifu wa kutokufanikiwa katika maisha.
  • Kumtegemea sana mpenzi , hususani kumtegemea kifedha:  Hii hutokea pale mtu anapoamini na kuishi kuendana na imani yake kuwa mpenzi wake ndiye ‘kila kitu’ katika maisha. Wapo wanaotegemea wapenzi wao kwa kila kitu kuhusiana na elimu yao (msaada wa materials, kuandika reports, n.k), wapo wanategemea wapenzi wao kwa kila kitu kuhusiana na matumizi yao –chakula , mavazi, n.k

Mambo ya msingi ya kuzingatia kushinda hofu ya kuumizwa

1.Uoga hausuluhishi tatizo:  Kuogopa kuwa utaachwa au hautapendwa vile unavyotarajia kupendwa hakuleti suluhu ya hofu yako. Tumia muda kutambua chanzo cha hofu yako ni nini haswa. Jipe muda kumfahamu mpenzi unayetaka kujenga nae mahusiano, au yule ambaye tayari upo nae. Jishushe vya kutosha ukiamini kuwa wewe ni sehemu ya suluhisho ya tatizo. Hivyo tambua namna tabia yako, matarajio yako, na uelewa wako kuhusu mahusiano kunavyoweza kuchangia kuboresha mahusiano ili usiumizwe.

2.Binadamu kwa kawaida ni mbinafsi:  Kwa asili binadamu huangalia maslahi yake , na kuwa angependa kunufaika zaidi na zaidi. Hivyo angalia namna unavyoendesha mahusiano kama kweli unampatia sababu mpenzi wako kuona ananufaika zaidi na zaidi. Je, kuna mambo anayoyalalamikia kwako na ungeweza kuyarekebisha? Je, unaboresha mawasiliano kati yenu ili kujua hisia kati yenu?Je unazungumzia mambo unayohofia na yale usiyoyapenda?

3.Chunguza matarajio yako kuhusiana na mahusiano : Tusipokuwa makini kuhusu yale tunayoyatarajia katika mahusiano  tunaweza kujikuta tunawapoteza wapenzi wetu, kwani pengine matarajio yetu ni zaidi ya uwezo wa wapenzi wetu au pengine yanapingana kwa kiwango kikubwa na matarajio ya wapenzi wetu.  Mfano uharaka wa kutaka mpenzi wako ajenge, alipe mahali,  akununulie mali kadhaa n.k vinaweza kumpoteza. Chukua muda kujifunza hali halisi ya mpenzi wako, na kanuni za kimaisha anazoziamini.

4.Ishi wewe kama wewe:  Usiige maisha ya watu na wala usitake kujionyesha mbele za watu kuwa wewe ni bora kutokana na aina ya mpenzi uliye naye, au kwa vile ‘unavyo enjoy’ maisha. Mapenzi yako ni kwa ajili yako. Unapoanza kuingiza mitazamo ya watu wengine au kutaka ‘kuwauzia sura’ watu wengine mapenzi yako, unatengeneza deni ambalo matokeo yake ni kujikuta unaishi kwa hofu ya kuachwa na uliye naye, kwani kuachwa kwako kutakuumiza zaidi kwa kuwa kutakuaibisha mbele ya watu wengine.
Share:

‘IDEAS’ 7 ZA JINSI YA KUANZISHA BLOGU ZENYE MVUTO

Ukifuatilia sana fani ya blogging nchini kwetu Tanzania, utagundua changamoto kubwa iliyopo ni katika ubunifu na uandishi wa taarifa za kuweka katika blogu. Tatizo la ubunifu linajionyesha wazi kwa utitiri wa blogu zenye mwelekeo mmoja kwamba nyingi ni blogu za habari za matukio ya kila siku, na kwamba habari zenyewe nyingi ni ‘copy & paste’.
Imefikia hatua sasa, watu wengi kuchukulia kuwa blogging ni jambo la kama vile mzaha mzaha tuu,na kwamba mtu yoyote yule ili mradi anajua kutumia computer ,ataweza kufungua blogu yake na kuwa ana copy na ku paste habari toka vyanzo mbalimbali na kuweka kwa blogu yake.
Hata hivyo, bado kuna uwezekano mkubwa wa watu wanaotaka kuanzisha blogs wakatumia ubunifu kidogo kuboresha blogs zao kwa kuleta upekee wa taarifa wanazoweka, na la msingi sana tutazame thamani ya taarifa tunazoweka kwa wasomaji wetu.
Tanzania ni yetu sote, na kwamba blogs zina mchango mkubwa kama chombo cha habari kuelimisha na kuelekeza jamii kwenye muelekeo sahihi. Ni kweli kuwa picha za utupu, na habari za udaku ‘zinauza sana’ lakini tukumbuke  kuna mambo mengine mengi tuu ambayo tungeweza kuandika kama bloggers na kutoa mchango kwa jamii yetu.
Kuna msemo unaosema “ Be change you want to see” Yaani wewe mwenyewe uanze kwanza kufanya mabadiliko kabla ya kudai mabadiliko  yatokee tuu.
Zifuatazo ni baadhi ya ‘ideas’ ambazo zinaweza kutengeneza blogs zenye ‘kuuza’ (kuleta wasomaji wengi) na pia zikaleta mchango chanya katika jamii.  UPO HURU KUTUMIA ‘IDEAS’ HIZI KUTENGENEZA BLOGU YAKO


1.Fursa kwa wajasiriamali :  Waweza anzisha blogu mahsusi kwa fursa motomoto kwa wajasiriamali wa sasa na wale wanaotaka kuwa wajasiriamali. Blogu hii haitojihusisha na makala kuhusu ujasiriamali (maana wapo wengi wanaandika kuhusu hilo) badala yake itajikita katika kuweka taarifa motomoto za upatikanaji wa mafunzo ya ujasiriamali, mikutano, semina, mikopo, na asasi mbalimbali zinazosaidia wajasiriamali. Waweza pia weka links za blogs zinazohusiana na ujasiriamali ili kufanya blogu hii iwe nyumbani kwa wajasiriamali.

2. Shule za Kata: Habari nyingi zinaandikwa kuhusu shule za kata. Ili kuleta upekee blogu yako hii itajikita kueleza mafanikio , changamoto na jinsi shule za kata zinavyojitahidi kujikwamua. Takwimu na picha ni muhimu sana kwa blogu hii. Pia unaweza onyesha program mbalimbali za maendeleo zinazosaidia shule za kata. Kuhoji wanafunzi wa shule husika, na kuonyesha maisha ya shule za kata. Lengo ni kusaidia wazazi na walezi kutambua mazingira na maendeleo ya shule wanazopeleka watoto wao, au wanazotarajia kupeleka watoto wao. Maana wapo wengi mtoto toka Form 1 hadi Form 4, hawajakanyaga shule anaposoma mtoto.

3.Picha Uwanjani: Kuna blogu nyingi zenye habari na michezo na burudani.  Ili kuleta upekee, blogu yako hii itakuwa ni ya picha tuu. Tena picha kali zaidi , ikisindikizwa na Facebook page, yenye kusheheni picha za matukio mbalimbali ya burudani na michezo. Si unajua kuwa picha inatoa maneno maelezo zaidi ya Maneno ? Ndio hivyo, hakikisha picha unazoweka zinabeba ujumbe au taarifa fulani, ambayo hautoelezea kwa maneno ila mtazamaji atajionea mwenyewe. Kumbuka kutaja vyanzo vya picha ambazo haukupiga wewe mwenyewe.

4.Nukuu zetu: Unakumbuka nukuu kama vile “…ukitaka kula ukubali kuliwa”?. Basi waweza tengeneza blogu maalum ya  nukuu toka Tanzania. Waweza zigawa katika makundi ya Siasa, Jamii, Teknolojia, Uchumi, Michezo, Elimu, n.k. Usisahau ile nukuu ya Tanzania ni muungano wa visiwa vya Zimbabwe, Pemba na Tanganyika. Kumbuka kupata nukuu sahihi, na ikiwezekana utaje kabisa nani alitoa maneno hayo. Blogu hiyo ya nukuu zetu, itaburudisha na kuelimisha pia, na kutukumbusha wapi tunatoka, na wapi wapi tutarajie kuenda.

5.Skonga:  Blogu hii itakuwa maalum kwa wanafunzi na wazazi. Ni kama vile shule, ila shule ya mtandaoni, ambapo Matokeo mbalimbali ya Form 4, 2, QT, FORM4, yatawekwa. Msaada kwa wanafunzi kwa njia ya ‘materials’ ya kujisomea yataweka, na makala zenye kujaa mbinu za kusoma, changamoto za maisha ya kishule, habari motomoto zihusuzo elimu zitawekwa humu. Mambo mengine ya maisha ya kishule kama vile majina ya walimu, ambayo wanafunzi huwatunga yatawekwa humu. 

6.Wakali wa Bongo: Badala ya kuandika habari za watu maarufu na mashuhuri kama udaku, blogu hii ya wakali wa Bongo, itajitofautisha kwa kuangalia maisha ya watu hawa katika muonekano chanya. Blogu itachambua changamoto wanazokumbana nazo, nini wamejifunza kuhusu mafanikio, na wanafanya nini kuendelea kubaki kuwa na mafanikio. Pia blogu itaangalia wakali wengine waliopo katika jamii lakini hawajapata kuwa mashuhuri kama vile wanafunzi waliofaulu kwa viwango vya juu kabisa katika masomo yao. Itaangalia pia biashara zinazotamba Tanzania, Shule zinazotamba na zilizowahi kutamba kama vile TAMBAZA, wanasiasa, na asasi zisizo za kiraia. Blogu hii itanogeshwa na mahojiano na wahusika, picha, na historia mbalimbali. Unataka kuanza blogu hii ? Embu fuatilia na kuandika ukali wa shule ya TAMBAZA.  Enzi hizo TAMBAZA ilivyosifika kwa fujo lakini pia kwa ubora wa wanafunzi.

7.Mkali wa Facebook:  Blogu hii ni mahsusi kwa mambo yanayovutia kuhusiana na Facebook. Mambo kama vile picha zilizopata ‘likes’ nyingi (zisiwe picha za mtu binafsi), status kali, au comments zenye mvuto zaweza kuwekwa humo. Mambo mengine ni taarifa za kiufundi kuhusu applications mbalimbali zinazopatikana Facebook kama vile BranchOut, na mambo mapya ya matumizi ya Facebook yanayoletwa na kampuni ya Facebook kama vile Timeline.
Share:

SABABU 4 KWANINI RAFIKI ZAKO NI HATARI ZAIDI KULIKO ADUI ZAKO

Pamoja na ukweli kwamba rafiki ni muhimu katika maisha, makala hii inachambua namna nne (4) ambapo rafiki wanaweza kuwa hatari zaidi ya adui zako. Kinachoelezwa katika makala hii ni kuwa uhatari wa rafiki upo katika namna urafiki unavyoendeshwa. Jisomee mwenyewe:-

1. Kioo: Mara nyingi tunajikuta kuwa tunaamini zaidi mtazamo wa rafiki zetu kuhusu sie, kuliko vile utashi wetu unavyotuambia. Tunafanya mambo mengi kwa imani na ufahamu tuliojijengea kichwani kuwa kufanya hivyo ndio kunakotarajiwa na rafiki zetu. Kwa kifupi, yale yanayoonekana kuwa yanafaa machoni mwa rafiki zetu –iwe mavazi, lugha, matumizi ya fedha, hata aina ya mwenza wa maisha, ndio hayo tunayojitahidi kuyafanya. Hivyo kama rafiki zetu wana mtazamo usio chanya, basi tunajikuta tunaelekea pabaya pia.

2. Tunajiweka watupu mbele zao: Kwakuwa tumewapa ‘kitambulisho’ cha kuwa wao ni rafiki zetu, tunajihisi tupo salama kuelezea mambo yetu ya msingi kimaisha kama vile habari za familia, biashara, masomo, na hata mapenzi. Tena kuna nyakati tunadiri hata kuwaambia siri zetu. Hali hii ya ‘kujiweka mtupu’ mbele yao ni hatari kwani taarifa tunazo ‘share’ nao zinaweza kutumika kutuangamiza, si umewahi kusikia “Information is Power” ? Kwa sababu hii ni rahisi kwa marafiki kutudhuru kama mwanamuziki Shaa alivyoimba katika wimbo Shoga.


3. Ushindani: Kwakuwa rafiki ndio watu wa karibu zaidi kwetu, na kama tulivyoeleza hapo juu mara nyingi wao ndio kioo chetu, tunajikuta tukijiingiza kwenye ushindani nao kwa kusudia au bila kutarajia, kwakutaka kuwa kama wao au  zaidi yao. Na wao pia kwa kukusudia au bila kukusudia kwakuwa wanatufahamu vizuri nao wanajikuta wakianzisha ushindani ili kuwa kama sisi au zaidi yetu. Hali hii ya kutaka ushindani kati yetu, ukizingatia kuwa tumekwishajiweka  ‘watupu’ mbele za rafiki zetu, inafanya rafiki hao kuwa ni hatari zaidi ya hata adui zetu wa sasa.
Wakati mwingine ushindani wa marafiki zetu hujidhirisha waziwazi kama mwanamuziki Nyota Ndogo alipokeza kwenye wimbo Watu na Viatu.
 
4. Dhambi ya kutenga watu: Tunaposisitiza kutazama binadamu wenzetu katika makundi mawili ya adui na rafiki, twaweza kujikuta tukiwapa umuhimu na thamani kubwa rafiki, na kuwatenga maadui. Kutenga huku kutaendelea kwani ndani ya hao unaoona rafiki, unaweza chambua zaidi na zaidi na kuona kumbe baadhi sio rafiki, ni maadui. Kutenga huku mara nyingi hufanyika wazi wazi, hivyo kumfanya rafiki kujihisi wa kipekee, nap engine kutumia nafasi hii kukuumiza, bila wewe kutambua kwa haraka, kwani ni unajua huyo ni mmoja wa watu wako.

HITIMISHO:
Ni jambo zuri sana kuwa na rafiki, na rafiki ni muhimu sana. Hata hivyo, ni jukumu lako kusimamia vema urafiki wako na watu wengine. Haitoshi tuu kuwa na rafiki wema, bali unapaswa kujua namna ya kuishi na hao rafiki wema. Endelea kuwa na maamuzi binafsi, tafuta uhuru wa fikra na usiogope kuwa na mtazamo tofauti na rafiki zako.
Nimalizie makala hii kwa nukuu hizi:

“ Tunaweza kuwamudu adui zetu, Mungu tulinde dhidi ya Rafiki Zetu” – Martin Luther
“ Nilimuomba Mungu aniondolee maadui, nikaanza kuona rafiki wakipungua”- Meek Mill.
Share:

MBINU 6 ZA KUSHINDA HALI NGUMU YA AJIRA NA MAISHA


Wataalamu wa uchumi na historia wanasema, dunia tuliyonayo sasa sio tuu kwamba inakumbwa na machafuko mengi, ila ni dhahiri kuwa machafuko haya yataendelea kwa muda mrefu. Hivyo basi ni muhimu tujifunze njia za kujiimarisha ili tuweze kupita salama katika machafuko haya:- 

1. Uhuru wa fikra:  Kama kuna nyakati ambapo unahitaji uwezo wa kuiona dunia kama ilivyo na sio kama unavyotaka iwe, basi ni sasa. Ni muhimu kuboresha ufahamu wako wa mambo mengi ya kimsingi ya kimaisha kama vile mapenzi, biashara, tabia, teknolojia , mbinu za kutatua matatizo, lugha, na zaidi sana  maswala ya kiroho.
Uhuru wa kifikra utakuwezesha uweze kujitawala vema, kwani kimsingi wewe ndiye mtu wa kwanza kabisa unayeweza kuleta mabadiliko makubwa na maendeleo kwa maisha yako, kwakuwa unayo nguvu ya utashi,  kufanya maamuzi au kuacha watu waamue mambo kwa ajili yako.

2. Kuwa mzalishaji: Katika machafuko haya, bidhaa na huduma mbalimbali zitakuwa  adimu, na kwa wazalishaji wachache watakaoweza kuzalisha kwa ufanisi wataweza kujikuta wakiendesha maisha vizuri.  Hivyo pamoja na kuwa mtumiaji wa fedha zako kwa mambo ya burudani, unahitaji kuhifadhi fedha zako kwa namna ambayo fedha zako hazitopoteza thamani zake, na wakati huo huo, ukifanya utafiti wa aina ya bidhaa au huduma ambazo utakuwa ukizalisha, ili nawe unufaike na mazingira tuliyonayo.  Kuendelea kuwa muingizaji wa kipato (kwa njia ya ajira pekee) na kuwa mtumiaji zaidi ya mwekaji akiba, si jambo la busara, hasa katika hali ngumu ya kiuchumi na kijamii tuliyonayo.

3. Kuboresha mtandao:  Kwakuwa unahitaji kutambua fursa nyingi kwa kadri inavyowezekana na kwakuwa wewe ni mzalishaji, unahitaji sana kujenga mtandao mkubwa na mtandao wenye manufaa ili kuweza kutambua fursa mbalimbali kupitia mtandao wako, na pia kuweza kuuza bidhaa zako kupitia mtandao huo. Soma zaidi kuhusu jinsi ya kujenga mtandao wa watu ‘wazito’ katika makala yetu hii (bofya) JINSI YA KUJENGA MTANDAO WA VIGOGO

4. Kaa tayari kwa kusafiri:  Fursa zinaweza kutokea popote pale, hivyo kuwa tayari kusafiri nje ya mkoa uliopo sasa, na zaidi sana nje ya nchi. Hakikisha una passport halali na isiyoisha muda wake, na tambua taratibu za kusafiri nje ya nchi, kama vile mambo ya visa,  na gharama za maisha kwa nchi tofauti. Bofya makala kuhusu SAFARI YA BONGO -AFRIKA KUSINI, upate picha ya mambo ya msingi katika kusafiri nje ya Tanzania. 

5. Mipango ya muda mrefu: Tambua kuwa hali hii ngumu ya maisha ni swala ambalo litaendelea kwa muda mrefu, hivyo ni muhimu kujipanga wewe na familia yako. Kama una watoto au una mpango wa kuwa na watoto, basi ni wakati wa kufikiria pia namna ya kuja kuwawezesha watoto wako wawe na ujuzi wa uhakika, na kuwa wawe wazalishaji.  Hakikisha unajitengenezea ujuzi na uzoefu uliokomaa katika jambo fulani au mambo kadhaa tofauti, ili uweze kuja kuuza ujuzi na uzoefu wako huo katika soko gumu la huduma tunalokumbana nalo.

6. Kuwa mwepesi wa kubadilika: Mambo mengi yanabadilika kwa haraka sana, ufahamu uliokuwa nao jana , mbinu ulizotumia siku za nyuma  hata kama zilifanikiwa, inawezekana kabisa zisifanikiwe kwa sasa, na kwa kadri mambo yanavyozidi kubadilika. Ushindi wa kipekee unakuja pale unapoweza kuwa mwepesi wa kubadilika, kwa kubuni njia mpya na bora za kukabiliana na mazingira unayokumbana nayo.

Share:

FANYA HAYA 6 KUZUIA WATU WASIINGILIE MAPENZI YENU

Sio mbaya kwa marafiki wa karibu au ndugu na jamaa kufahamu kushirikiana nanyi katika mapenzi yenu kama vile wakati wa sherehe au msiba. Pia sio mbaya kujuliana hali na kutambulisha mambo ya msingi yanayoendelea katika mahusiano yako wewe na mpenzi wako. Hata hivyo kuna wakati watu wengine wa pembeni, wawe majirani, ndugu, wazazi au marafiki wanaweza kuwa ‘sumu’ ya mahusiano yako, hasa pale unapowategemea sana kutoa msaada, maoni au maelekezo katika maisha yako ya mapenzi.  Makala hii inaeleza mambo ya msingi unayoweza kufanya ili kupunguza uwezekano wa rafiki, ndugu, jamaa, au wazazi kuwa ‘sumu’ ya mapenzi yako.

1. Udhibiti wa taarifa kwa wengine:  Kadri unavyoelezea mahusiano yako kwa watu wengine ndivyo unavyowapa nafasi watu kutoa maoni, na hata kudhani kuwa wana dhamana ya kukuelekeza unavyotakiwa kuishi na mwenza wako. Hivyo basi, chukua muda wa kutosha kutafakari na kufanya uchunguzi kuhusu maswala yako ya mahusiano kabla haujaanza kutafuta maoni, ushauri kwa watu wengine. Ni bora ukasoma vitabu, na makala mbalimbali, hususani zihusuzo tabia na maisha ya mahusiano, zitafakari vema ili kuona zinahusiana vipi na unayokumbana nayo katika mahusianao yako.

2. Upekee wa mambo:  Tambua kuwa tabia ya mpenzi wako inaweza kuwa ni ya kipekee, mazingira pia ya tukio linalokufanya utake ushauri au maoni kwa wengine yanaweza kuwa ni ya kipekee, hivyo ushauri au maoni utakayopokea yanaweza yasikusaidie moja kwa moja katika suluhisho lako. Ukitambua hili, utafanya bidii ya kujenga uwezo binafsi wa kuchambua tatizo unalokumbana nalo katika mahusiano na kutafuta suluhisho kabla ya kutegemea watu wengine.

3. Mwenye maamuzi ni wewe: Ni kweli kuwa kuna nyakati ni muhimu kupata ushauri kutoka kwa watu wengine, na zaidi sana watu wenye uelewa sahihi na unaowaamini, hakikisha kuwa unatambua kuwa wewe mwenyewe ndio mwenye kubeba lawama ya maamuzi utakayochukua. 

4. Kuwa na subira: Usichukue maamuziya haraka katika mahusiano hususani uamuzi wa kuamua kuwashirikisha watu wengine habari ya mambo yahusuyo uhusiano wako. Unapofanya uamuzi wa kuwashirikisha wengine kwa haraka  unajinyima nafasi ya kulichunguza jambo kwa ufasaha hususani madhara yanayoweza kutokea kwa kuwaeleza wengine, au kama ni tatizo, basi kufikiria njia sahihi ambazo ungeweza  kuzitumia kupata suluhu ya tatizo. 

5. Fungua njia za mawasiliano kati yenu: Pengine chanzo cha wewe kutaka kuzungumza mambo ya ndani yanayohusu mahusiano yenu kwa watu wengine ni kwakuwa umekosa  nafasi ya kuzungumza kwa ufasaha na mwenzi wako. Tafuteni nafasi za kutosha, jengeni mazingira ya kuzungumzia mambo yenu kabla ya kutaka kuwashirikisha watu wengine. 

6. Kuweni peke yenu:
Hata kama hautaki kueleza watu kuhusu mambo yanayoendana na maisha yenu, mazingira unamoishi yanaweza kuchangia watu kutaka kuingilia mahusiano yenu –kwa kutoa maelekezo, ushauri au maoni  kuhusu muishivyo wewe na mpenzi wako. Inapobidi hakikisha hamuishi karibu na wazazi wenu, ndugu au rafiki wa karibu. Au haufanyi kazi na mwenzi wako sehemu moja, kwani hiyo itakuwa njia rahisi sana ya watu kuona mnavyoishi.  Inapobidi kuwa karibu na watu wengine , hakikisha mnakubaliana wewe na mwenza wako namna bora ya kuendesha mawasiliano kati yenu mbele za watu, ili msiwape nafasi ya wao  kumi‘soma’ na kisha kuanza waje waanze kutoa ‘maelekezo’ ya vile wanavyoona mnapaswa kuishi.

7. Nenda ‘darasani’ :  Kumbuka mahusiano yanahitaji sana uelewa mkubwa wa jinsi ya kufanya mawasiliano fasaha, kuelewa hisia za mwenzi wako, kutambua mbinu za kusuluhisha migogoro, na zaidi sana kufanya mipango ya muda mrefu ya uhusiano wenu. Jizoeshe kusoma makala na vitabu mbalimbali vyenye kuboresha ufahamu wa mambo ya msingi kama hayo tuliyoeleza hapo juu. Mfano wa makala unazoweza kusoma ni kama vile: MADHAIFU MATANO KATIKA MAPENZI
Share:

JINSI YA KUWA MBUNIFU KATIKA UJASIRIAMALI

Ni jambo lililo wazi kuwa sote tunakumbana na matatizo , ingawaje aina ya matatizo na kiwango ambacho yanatusumbua vinaweza kuwa tofauti.
Hata hivyo, sote tunaweza kutafuta mbinu za kutatua matatizo husika, ingawaje ni kweli mbinu zetu za kutafuta suluhu zinaweza kuwa tofauti.
Katika makala hii kutana na wabunifu Ed na Ross kutoka UK, wanaoendesha biashara yao iitwayo BUY MY FACE.

Ed na Ross  kutoka UK
Vijana hawa walianzisha biashara ya kuuza nafasi za matangazo kwa kutumia sura zao. Wanachofanya ni kuandika tangazo kwa uso zao, kisha huzunguka maeneo tofauti tofauti ya mji ili watu waweze kuona tangazo husika.
Na wameshafanya matangazo ya makampuni makubwa kama vile Ernest & Young.
Jionee picha zao hapa
Mambo kadhaa yanayoweza kukufanya kuwa mbunifu:-

1. Ondoa uwoga: Usiogope kuwa wazo lako litakuja kushindwa. Chukulia kuwa hata kama litakuja kushindwa, utakuwa tayari umeshapata uzoefu wa kutengeneza wazo lingine bora zaidi.

2. Usijilinganishe na watu wengine:  Usiangalie wengine unao dhani wamekuzidi uzoefu au ujuzi wamefanya nini , kiasi kwamba ukajishusha kuwa eti wewe hauwezi kufikia kuwa na kitu kizuri cha ubunifu.

3. Zingatia Upekee: Kama unataka kufanya UBUNIFU , lakini mawazoni mwako unapata ukinzani wa kutaka kufanya kama fulani, basi ujue hapo kuna tatizo. Sisitiza kuwa na upekee, na upekee tuu ndio utakaoleta maana haswa katika ubunifu wako, hata mbele za wateja. Hata hivyo hii haimaanishi kuwa hautakiwi kuangalia wengine wamefanya nini, hapana, angalia wengine kwa lengo la kujifunza, na kutambua mapungufu.

4. Zingatia kukidhi mahitaji ya binadamu:  Ubunifu wako hautokuwa na maana kama haukidhi mahitaji ya watu. Hivyo njia rahisi ya kuanza ubunifu ni kuisoma jamii, kuangalia matatizo yanayoikumba jamii. Sio lazima uangalie mbali sana, waweza hata kutafakari matatizo ambayo yamekuwa yakikutatiza wewe mwenyewe, kisha ukaamua kubuni kitu cha kuleta suluhisho. Fanya uchunguzi kujua wengine wamekumbana na matatizo kama yako.
Mfano mzuri,Drew Houston mwanzilishi wa huduma ya kuhifadhi documents online,  DROPBOX anasema alianzisha huduma hiyo baada ya yeye mwenyewe kuwa mpotezaji wa flashdisk wakati akiwa chuoni MIT.

Share:

MAMBO 6 YA KUFANYA UPATE AJIRA KWA URAHISI

Pamoja na ukiritimba uliopo katika  soko la ajira, kutokana na rushwa na mambo ya kujuana, bado kuna nafasi kubwa ya wewe kupata kazi unayoipenda na kazi inayolipa. Kabla ya kuanza kulalamika kuwa watu wanapeana ajira kwa kujuana, tafakari kwanza ni kwakiwango gani wewe kama wewe unakidhi matakwa ya waajiri. Wakati wengine wanalalamika kupata kazi Tanzania ni tabu, wapo watu ambao wanabadilisha waajiri wanavyotaka wao, iwe ndani ya Tanzania au hata mipaka ya Tanzania.
La msingi kukumbuka ni kuwa utaajiriwa ili ufanye kazi, tena sio tuu ufanye kazi ili mradi, unatakiwa ufanye kazi kwa ufanisi. Katika makala hii, tunaonyesha mambo 6 ya kuzingatia ili kurahisisha utafutaji wa nafasi ya ajira.
1. Mtandao wako : Kila mmoja wetu anahitaji msaada toka kwa watu fulani. Hivyo hata katika ajira ni muhimu kuwa na mtandao utakaokusaidia kufikia malengo yako ya ajira. Mtandao utakusaidia kwa njia nyingi kama vile kukupa taarifa ya nafasi za kazi , kukusaidia katika kujiandaa na usaili. Pia mtandao wako unaweza kukusaidia katika kukutambulisha kwa waajiri ili kuongeza imani ya waajiri kuhusu wewe. 

2. Uwezo wa lugha ya kiingereza: Kiingereza ni lugha kuu ya mawasiliano katika ajira. Hakikisha una uwezo mzuri wa kuongea na kuandika kwa ufasaha. Hapa tunazungumzia ujue vema kanuni za lugha hiyo kama vile matumizi ya nyakati mbalimbali, viunganishi , n.k , sio tuu kujua kuunganisha maneno mawili matatu. Jizoeze kuandika kwa ufasaha pia. Lugha ya kiingereza itakusaidia kukupa maksi wakati wa usaili (interview). Hali kadhalika uwezo wa kusoma na kuandika kwa ufasaha wa kiingereza utakusaidia katika kufanya kazi kwa uhakika, na hata kuwa mbunifu kwa kujifunza mambo mapya na kuyaelezea.

3. Ujuzi wa uhakika: Kumbuka kuwa sababu kubwa waajiri makini wanakuhitaji ufanye kazi kwao ni kwamba utaweza kuwa mfanisi kwa kile ambacho utatakiwa kukifanya. Hili litawezekana tuu endapo wewe kweli una ujuzi ambao unadai unao, wakati wa kuomba kazi. Kumbuka unaweza kufoji vyeti, ila ujuzi na uzoefu wa kazi, hauwezi kufoji.

4. Uwezo wa kufanya mawasiliano fasaha: Jitahidi sana kufuata kanuni zote za mawasiliano fasaha, ikiwemo kusikiliza kwa umakini  kabla ya kutoa maelezo yako, aina ya mavazi, na muonekano wako. Salamu na ufuatiliaji wa mambo madogo madogo kama kusema ahsante, kufuata maelekezo yote ya matangazo ya kazi kwa ufasaha.

5. Unajitangaza vipi: Katika kutafuta ajira, ni muhimu kuwataarifu waajiri na pia watu wengine kuhusu hitaji lako la kuajiriwa. Hivyo basi jipange vema kuwataarifu ndugu, jamaa na marafiki. Kingine unachoweza kufanya ni kuandaa kazi binafsi zinazotumia ujuzi wako ili watu wakiona kazi zako zilivyo nzuri unaweza kujikuta umepata ajira. Ni muhimu sana kutembelea ofisi za waajiri watarajiwa, ukaomba nafasi ya kuongea na mtu mwenye majukumu ya kuajiri, ili uweze kujieleza au kuacha maombi ya kufanya kazi huko.

6. Taswira uitoayo kwa jamii: Waajiri wako watarajiwa wapo katika jamii unayoishi, na hata wale ambao wanaweza kukufanyia ‘mpango’ ukapata ajira wapo pia katika jamii, hivyo basi ili wakuamini, na wategemee utendaji bora toka kwako ni muhimu uonyeshe kujiheshimu, na kwamba ni mtu unayeweza kuaminika  na kutumainiwa kufanya kazi kwa ufasaha, na kuwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi wengine. Angalia aina ya status na picha unazoweka Facebook, Google Plus, au Twitter. Pia kama kuna ka ujasiriamali unafanya sasa, hakikisha biashara yako haiharibu uaminifu na taswira njema kwa jamii.
Share:

MALENGO HAYA MANNE (4) YANATOA PICHA YA MJASIRIAMALI WA ‘UKWELI’

Ninaamini kuwa lengo la mwanzilishi wa biashara lina nafasi kubwa sana katika ku ‘shape’ biashara husika itakavyokuwa, kwakuwa  lengo hili ndio huweka picha ya akilini vile mtu alivyo tayari kujitoa kwa ajili ya biashara yake : wateja wake, wafanyakazi na uzalishaji wa bidhaa.
Makala hii inachambua aina kuu nne (4) za malengo ambayo watu huwa nayo wanapoanzisha biashara:- 

1. Kuongeza kipato cha ziada:  Wenye lengo hili pekee hujikita kwenye kuanzisha biashara hususani biashara za msimu, ili mradi kipato kipatikane. 
Mara nyingi huwa hawana mchanganuo wa kina wa biashara husika, na hawajali mambo ya msingi katika usimamizi wa biashara kama vile kuboresha huduma, kuboresha teknolojia wanazotumia katika biashara husika, kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha. 
Kwa wenye lengo kuu la kuongeza kipato cha ziada tuu, biashara zao ni jambo la ziada kwao kwani hujikuta wakitegemea mambo mengine kama vile ajira, kipato cha familia, au biashara nyingine.

2. Biashara kama Ajira mbadala: Wenye lengo hili huchukua muda mrefu kupanga jinsi ya kuanzisha biashara husika, na huweka msisitizo kwenye kipato. Ni wachaguzi sana wa aina ya biashara watakayoanzisha, mara nyingi biashara zao sio za msimu. 
Wajasiriamali wa lengo hili, hutazama zaidi kujenga mtandao kama sehemu muhimu katika kufanikisha biashara zao. Kwa watu wenye lengo hili, la msingi kwao ni kuendelea kuwepo katika biashara hata ikibidi kupata faida ndogo au kupoteza wateja wa aina fulani. 
Wana matazamio ya kukuza biashara zao, hata hivyo hukumbwa na tatizo la mtaji na ukosefu wa uzoefu katika biashara husika. 
Ni wagumu kuamini watu wengine (hususani wafanyakazi wa biashara zao), hivyo hujikuta wanahodhi madaraka yote. Hii inaweza kuchelewesha ukuaji wa biashara zao. Hata hivyo wanapofanikiwa kuongeza mtaji wa biashara zao, ni rahisi kwao kuboresha biashara na kupunguza kuhodhi madaraka. 

3. Kuonyesha ufahari wa kumiliki biashara:  Wenye lengo hili mara nyingi hufuata mkumbo  wa muelekeo wa biashara zinazoonekana kuwa ‘mahiri’ ili waweze ‘kuuza sura’. 
Hawafanyi uchambuzi wa kutosha wa biashara wanazotaka kufanya, na si  wabahiri katika kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha ili mradi tuu biashara itajenga na kulinda heshima wanayotaka kuwa nayo. 
Wajasiriamali wa namna hii si watendaji wa kila siku wa shughuli za biashara, hata hivyo hupenda kupata taarifa za mara kwa mara za biashara husika ili nao waweze jidai kwa kundi ambalo wapo. 
Hujali zaidi muonekano wa nje wa biashara kama vile mazingira ya ofisi, vifaa vya kazi, magari n.k, kuliko ubora wa wafanyakazi na kuwaendeleza wafanyakazi. 
Pamoja na kuwa si wabahiri katika kuwekeza katika vitu vinavyoboresha muonekano wa biashara zao, watu hawa wengi wao huwa wabahiri katika kulipa mishahara mizuri kwa wafanyakazi wao, na hawapendi kuona wafanyakazi wakibadilika kimaendeleo.

4. Biashara kama urithi wa baadae: Kwa wengine  lengo la kuanzisha na kufanya biashara ni mchanganyiko wa mambo mawili makuu ambayo ni kutoa mchango kwa jamii na kuboresha hifadhi yao ya mali na fedha. Kwa watu hawa malengo ya muda mrefu ni jambo la msingi sana. 
Pia wapo tayari kujifunza na kujaribu mambo mapya. Wanathamini wafanyakazi wao kuwa ni washirika katika kufikia lengo wanalotaka la kujenga kitu kikubwa katika jamii. 
Biashara kwao sio tuu kuuza bidhaa ili waingize fedha, bali ni kuuza bidhaa zenye kuleta kukidhi mahitaji ya mteja. 
Watu wenye lengo hili kwa kutambua kuwa wateja ndio washirika wao wa kuduma, hujitahidi sana kuwekeza katika mahusiano bora na wateja wao. Hii inajumuisha kujifunza maisha ya wateja, mabadiliko katika maisha ya wateja, kusikiliza malalamiko na mapendekezo ya wateja.
Watu wenye lengo la namna hii, hukakikisha biashara zao zinakuwa na kitu kimoja au (hata zaidi) ambacho kweli ni cha kipekee ambacho siku zote watajivunia nacho na kitadumu vizazi na vizazi, iwe aina yao ya utendaji kazi, bidhaa zenye upekee, mfumo wa uendeshaji wa biashara, au mahusiano na wafanyakazi.
Zaidi sana, watu wenye lengo hili, huwa ni wepesi kutilia maanani mambo madogo madogo ya kitaalamu katika biashara zao, kama vile utambulisho wa biashara zao (rangi za biashara, nembo), mifumo ya mawasiliano ya uhakika, n.k
Mjasiriamali wa namna hii, hana papara wala haraka ya kukuza mauzo yake, bali ana mtazamo wa kuwa na mauzo endelevu na kuona biashara inapanuka siku hadi siku.

HITIMISHO:
Je wewe upo katika kundi lipi ? Inawezekana kabisa mtu kutoka kundi moja kuingia katika kundi lingine.
Share:

PATA THAMANI YA FEDHA YAKO KWA KUTEMBELEA WEBSITES HIZI

Je, wewe ni mmoja wa watumiaji wa mtandao lakini haujaona bado mchango chanya wa mtandao katika kubadilisha na kuboresha maisha yako? Je, kwako internet ni sehemu ya ‘kupoteza muda’ tuu au ‘kuuza sura’?. Je, kwako mtandao ni sehemu ya kuingia kujua fulani kafanya nini, au usalimie tuu rafiki zako? Je, mtandao kwako ni sehemu ya kufanya tuu kazi ulizotumwa na bosi au assignments za chuoni ?.
Umefika wakati wewe mwenyewe uchukue utawala wa maisha yako, kwa kuhakikisha una ufahamu wa kutosha wa mambo kadha wa kadha yanayokuzunguka, bila kungoja kusikia kwa watu wengine au kufuata maoni tuu ya walio soma au kusikia mambo fulani huko mtaani. Mafanikio binafsi katika karne hii ya 21 yanategemea sana aina gani ya taarifa au ufahamu unao, na namna unavyotumia ufahamu husika.
Na kwakuwa imekuwa rahisi sana kutengeneza habari/taarifa mbalimbali, ni muhimu kwako kujua vyanzo vingi tofauti vya taarifa ili uwe na uhakika wa taarifa, isitoshe inabidi ufanye maamuzi sahihi ya vyanzo gani vya taarifa utavitumia katika kujifunza mambo mbalimbali.
Katika makala hii tunaonyesha vyanzo  saba ambavyo unaweza kutumia kupata ufahamu wa kuboresha maisha yako ya kishule, kijasiriamali, kikazi, na hata kimapenzi.

1. Videos:

Tumia videos mbalimbali zinazopatikana mtandaoni kupitia YouTube, TED, na, Vimeo, kujifunza mambo ya msingi. Waweza fanya hivi kwa kutembelea tuu website hizo au ukiwa kwa website hizo uka search kwa kuandika topic husika. Waweza pia tembelea WISE GEEK, huko unaweza pata majibu ya maswali mengi pamoja na Video za mada husika.

2. Kozi za bure:

Waweza jiandikisha online kwa kozi mbalimbali zitolewazo bure kabisa. Baadhi ya website unazoweza kutumia ni kama COURSERA, ALISON, STANFORD ONLINE, MIT OPEN COURSEWARE, na CLASSCENTRAL.
Kutoka katika website hizi utapata kujiandikisha katika vyuo vikubwa duniani kama Stanford, Duke, MIT, na kuhudhuria kozi mbalimbali ziwe za Saikolojia, Computer Science, Ujasiriamali, au hata Hesabu. Kama unapenda kupata vyeti, basi hakikisha unahitimu kozi husika, na utatumiwa cheti toka kwa chuo husika ulichojiandikisha.

3.Websites maalum : 

Kuna websites na blog kadhaa zenye makala maalum zenye uzito wa kimantiki katika kukusaidia kukua kifikra, kijasiriamali na kielimu. Website kama vile Big Think, Early To Rise, MattMorris, Mashable, Freeman Perspective, Casey Daily Dispatch, ni baadhi ya websites ambazo zinaibua mitazamo mipya ya kiteknolojia, kifikra, na kijasiriamali.

4.Google na Yahoo Alerts:

Tumia huduma hizi kupata habari zenye uzito wa kipekee kwako. Unachofanya ni kuenda kwenye website husika mfano Google Alerts, kisha unaorodhesha aina ya taarifa unazozitaka kupata. Kisha kupitia email uliyoiweka katika huduma husika, utakuwa ukitumia updates.

5.Subscribe:  

Tembelea mitandao mbalimbali yenye habari za kujenga, jisajili kupata taarifa toka kwao au kupata vitabu vya bure kutoka kwao. Mfano mzuri, kama unataka taarifa za marketing basi tembelea Hub spot na unaweza kujisajili kupata taarifa kibao, pamoja na vitabu vizuri sana vya mambo ya content marketing.

6.Mitandao ya kijamii:

Mitandao ya kijamii hususani Facebook inaweza kutumika pia kupata taarifa za kujenga.  Unachotakiwa kufanya ni ku LIKE kurasa zenye kusambaza taarifa za kukujenga, kisha utakuwa ukipata updates toka kurasa husika.  Ku LIKE pekee haitoshi, pia tembelea mara kwa mara kurasa husika ili kuona mambo mapya yaliyopostiwa huko. Kwani jinsi mitandao ya kijamii inavyooendeshwa, inawezakana isiwe rahisi kuona kila updates toka kwa kurasa ulizo LIKE. Ukiwa kwenye mitandao ya kijamii waweza jifunza lunga mfano Spanish kupitia ukurasa wa SpanishDict .

7. Hifadhi za nyaraka mbalimbali:

Tembelea websites kama vile Slide share, Prezi, Edocr na Scribd ambazo zinahifadhi makala mbalimbali ambazo watu wameandaa na kuziweka humo. Baadhi ya makala hizo unaweza ku download bure mtandaoni.
Share:

ZITAMBUE CHANGAMOTO SITA (6) KWA KILA UCHUMBA/NDOA

Ukweli ni kuwa watu wawili wanapoamua kwa dhati kuwa katika mahusiano ni kwamba wanakuwa tayari katika akili zao wamejenga matarajio au matumaini ya kunufaika na uhusiano husika, hata kama hawawezi ambiana moja kwa moja kuwa “ aisee, mie kuwa na wewe nataraji moja , mbili, tatu….”.
Kunapokuwepo na upendo, basi pia kunaleta majukumu, ambapo bila ya kutimizwa kwa majukumu yanayotarajiwa kutimizwa, maana halisi ya mahusiano bora inapotea.
Hii si tuu kwa mahusiano ya kimapenzi, bali hata dini zinatufundisha kuwa Mungu anatupenda, na katika hilo, tunajukumu la kutii amri zake, na kwamba tusipotii amri zake, tunakuwa tumeharibu maana nzima ya upendo wake, kwani tutajikuta tumeingia motoni/jehanamu (Kinyume cha upendo).
Hata katika familia, tumesikia mzazi pamoja na upendo alioonyesha kwa mtoto wake toka yupo tumboni mpaka mtoto ameweza kujitegemea, endapo mtoto husika akashindwa kumjali ( hili ndio jukumu linalokuja na upendo wa mzazi), basi unaweza sikia mzazi huyo akitoa ‘laana’ au ‘akamwachia radhi’ mtoto wake mwenyewe wa kumzaa.
Ni wazi kuwa mara nyingi majukumu yanayoletwa na upendo huwa hayaelezwi wazi wazi, hata hivyo katika mahusiano, mambo yafuatayo yanaweza kuwa sehemu ya matarajio ambayo  wapenzi wanaweza kuwa makini ili waweze kuwapendeza wenzao. Kwa maana nyingine ni kuwa yafuatayo, ndio maeneo ambayo mtu aliye kwenye mahusiano ni muhimu ‘acheze’ vema ili kulinda mahusiano/penzi:-

Fedha:  Katika swala la fedha, jambo kubwa linalojitokeza ni namna ya kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya fedha.  Ni muhimu kuweka mikakati ya pamoja kwa mambo ya msingi kimaisha , na kila mmoja kutilia maanani mipango hiyo, kabla ya kuamua kutumia kipato chake kwa mambo ambayo pengine hayapo nje ya mipango ya kifedha ya wawili nyie kama wapenzi.  Bila shaka, kuendana na aina yenu ya kipato, aina yenu ya maisha, kama wapenzi mtakuwa na kiwango fulani cha fedha ambacho si busara mmoja wenu kuamua kutumia bila kumtaarifu mwenzake , hata kama matumizi husika ni muhimu sana, na haijalishi nani kazitafuta fedha husika.

Imani: Katika swala la imani, ni muhimu kufahamiana vema mwenendo wa kiimani wa mwenza wako, na kuheshimu kuwa swala hili ni nyeti, na mabadiliko ya kweli hayawezi kulazimishwa. Imani inaweza athiri namna mnavyoweza kuwasiliana kama wapenzi – kwani mwingine mwenye msimamo mkali wa kidini, anaweza kukataa jambo fulani hapo baadae, jambo ambalo pengine mwenza wake anaona ni jambo la kawaida tuu. Imani inaathiri malezi ya watoto, na inaweza athiri shughuli za kiuchumi za wawili nyie, mfano pale mmoja wenu anapoamua kujikita katika  ‘huduma’ zaidi, kuliko familia na shughuli za kuingiza kipato.

Mahali pa kuishi:  Mtaa gani , wilaya gani, mkoani gani, nchi gani au bara gani kila mmoja wenu anatazamia muishi ni jambo la msingi kuliweka wazi kati yenu. Jambo hili linaweza kuendana na mambo mengine mengi ambayo yanachochea mabadiliko ya muda mfupi na hata muda mrefu katika maisha yenu, kama vile , aina ya kazi mnazotarajia kila mmoja wenu kufanya, na aina ya kazi unazotamani au kufikiri ni vema mwenza wako afanye.

Watoto: Hili ni jambo zito haswa katika vipengele vya lini watoto wapatikane (ujauzito), idadi ya watoto, aina ya malezi kwa watoto watakaopatikana, na zaidi sana majukumu ya kifedha katika malezi ya watoto (mfano, nani atalipa ada ya shule, n.k). Pamoja na kutafakari hayo, watu wawili mlio katika mahusiano, ni muhimu mkatengeneza picha ya maisha ya watoto wenu endapo mmoja wenu atatangulia mbele za haki (atafariki), na hata ikiwezekana  mwaweza fikiria na kupanga aina ya maisha mnayotaka watoto wenu waishi pale nyote wawili hamtokuwepo  duniani. Inapotokea mambo kama hayo yaliyotajwa hapo juu hayajawekwa wazi mbele yenu, ni rahisi mmoja wenu kufanya mambo yasiyompendeza mwengine –mfano wakati mwingine anafikiria akiba ya baadae ya watoto ili wakasome international school, mwingine anafikiria namna ya kutanua ili ‘kuuza sura’.

Falsafa ya maisha:  Swala hili linahusu wa kipekee na tafakari huru ya kila mmoja wenu kuhusu mambo kadhaa ya kimaisha kama vile mtazamo wa kila mmoja wenu kuhusu biashara (mwingine biashara ni kitu cha kuweka heshima kwa jamii, wakati mwingine biashara ni kielelezo cha huduma kwa jamii na hivyo kinahitaji muendelezo).
Falsafa pia inahusu namna kila mmoja wenu anavyochukulia mambo kama vile kusaidia watu wengine,  kuwa na mahusiano na watu wa jinsia tofauti (wapo wasiotaka hata classmet ampigie simu mpenzi wake). Falsafa pia inahusika na namna kila mmoja anavyotafsiri mafanikio katika maisha, na alivyo tayari kufanya yanayopaswa kufanywa kufikia mafanikio (Mfano, wengine mafanikio ni mali na umaarufu, wakati kwa wengine mafanikio ni namna anavyoweza kuwa na furaha na uhuru , pamoja na kusaidia wengine).
Katika juhudi za kufikia mafanikio unawea kukuta wapenzi mnatofautiana kwani mmoja anaweza amini rushwa ndio suluhisho pekee la kufikia anakotaka, wakati mwingine anaamini tofauti na hivyo.  

Hisia za kimapenzi: Ni jambo la msingi kutokupuuzia hisia za kimapenzi za kila mmoja wenu. Tambua vile mwenzako angependa akuone unamvutia na vile ambavyo unamjali hisia zake. Ni kweli kuwa katika mahusiano, hisia za kimapenzi zinaweza zisichukue nafasi kubwa kati yenu kwani kuna mambo mengi ya kufanya pamoja kama wapenzi, hata hivyo pamoja na udogo wake wa muda, jambo hili nyeti lisipopewa kipaumbele, linaweza sababisha mengine yote kuharibika. Zaidi sana, kumbuka wewe na mpenzi wako, ni watu wa jinsia mbili tofauti, kinachowafanya muungane kiasili ni hizo hisia za mapenzi kati yenu.

Hitimisho: Sio lazima kama watu wawili mlio katika mahusiano muwe na mtazamo sawa katika hayo yote yaliyoelezwa hapo juu, hata hivyo, ni muhimu sana kwenu nyote kuwa na picha kichwani ya mtazamo wa mwenza wako kuhusu mambo hayo niliyotaja hapo juu.
Pale mnapokubaliana kutofautiana katika mambo yaliyotajwa hapo juu (mf.mambo ya fedha, na imani), hakikisheni mnakubaliana bila kutofautiana kuhusu athari za kutofautiana kwenu, na jukumu la kukubali athari hizo kwa mahusiano yenu.
Share: