MABADILIKO SITA (6) DUNIANI USIYOPASWA KUPUUZIA

Pilika zetu za kupata fedha, vyeo, kujenga mahusiano na kukubalika katika jamii zinaathiriwa na mabadiliko yanayoendelea kutokea katika jamii yetu. Makala hii inadokeza mabadiliko 7 muhimu kuyafahamu na kuyatawala ili usije kujikuta unapoteza furaha ya kweli ya kuishi kwa kuwa mtumwa wa fedha, mapenzi, cheo, mahusiano au mtumwa wa ‘misifa’.

1. Uhuru wa mawasiliano: Uwepo wa mitandao ya kijamii, kushuka kwa bei za simu na kompyuta , teknolojia ya upigaji picha na uandishi kama vile kutumia blogs, ni baadhi ya mambo yanayochochea uhuru wa mawasiliano kukua. Uhuru huu unaweza athiri malezi ya watoto,  uhuru pia unaweza athiri usiri wa mambo yako, na bila shaka unaathiri ufanisi wako kibiashara na kikazi pia.
Ili kuweza kujitawala na kutawala mabadiliko haya ya uhuru wa mawasiliano, inakupasa ujifunze vema matumizi ya teknolojia husika, au upate mtu wa kukusaidia kusimamia mambo yako ili yasiathirike na uhuru huu wa mawasiliano.
Fahamu yapi unastahili kufanya ukiwa mtandaoni – kwa simu na kwa kompyuta, tambua pia nini watu wanafanya ambayo yanaweza  kukuathiri.  Mfano mzuri,  ni pale unapoweka picha ya mpenzi wako aliyependeza vizuri, ila picha hiyo ukaikuta imewekwa kwenye mitandao ya ngono.
Mfano mwingine, usipofuatilia mara kwa mara anachoandika mtoto wako mtandaoni unaweza kushtushwa siku ukawa tagged picha binti yako aliyepo ‘boarding school’ akila ‘bata’ kwenye club ya usiku. Au kukuta ameandika status – “ Jamani, siwezi soma huyu BF wangu kila nimfanyiacho haridhiki, nimempa hadi  pocket money zangu akae nazo, ila haridhiki”.

2. Machafuko katika jamii:   Hali ngumu ya kiuchumi, mabadiliko katika uwezo wa kifikra wa watu, na ukandamizaji uliokithiri katika jamii zetu ni moja ya sababu zinazochochea machafuko ya kila siku yanayoendelea. Hata yale ambayo ulidhani kuwa hayawezi kutokea nchini mwetu, bila shaka utaanza kuyaona yakitokea. Hali hii ni muendelezo wa mabadiliko makubwa katika maisha yetu. Serikali zinazidi ‘kuchangikiwa’  kwakuwa mabadiliko yanatokea kwa haraka sana na ni mabadiliko makubwa ambayo hayakutazamiwa. Hivyo  serikali kujibu mapigo haya, inabidi zije na mbinu nyingi kali zinazoweza kuonekana kama ni za kidikteta.

3. Uzalishaji mkubwa wa ushindani wa hali ya juu:  Kupanuka kwa fikra za watu wengi, maboresho katika teknolojia, urahisi wa upatikanaji wa taarifa, na mijumuiko ya watu toka mataifa tofauti katika nchi tofauti,ni mambo yanayoleta ushindani katika uzalishaji. Mbinu zilizosaidia biashara fulani kuwa kubwa miaka 10 iliyopita, zinaweza zisiisaidie biashara hiyo hiyo, au nyingine inayofanana nayo kukua.
Wajasiriamali sasa wanazalisha bidhaa mpya, ubora unaboresha, bei zinazidi kuenda chini, na mbinu za kufikisha bidhaa kwa mteja zinaboreshwa.  Mabadiliko haya, yanahitaji mjasiriamali sio tuu ajue vema kuzalisha bidhaa yake, ila aifahamu vema jamii anayotaka kuiuzia bidhaa, ajenge mtandao mkubwa na wateja wake, na zaidi sana aweze kukusanya na kusimamia taarifa za jinsi ya kuboresha ushindani wake katika soko.

4.Utitiri wa taarifa:  Maboresho katika teknolojia ya habari na mawasiliano, yamechangia sio tuu kuwepo kwa websites na mitandao ya kijamii (social networks) bali yamerahishisha matumizi na hata umiliki wa mitandao. Mfano kuna blog kibao Tanzania pekee, na kurasa maelfu za Facebook. Kuna video mamilioni kwenye Youtube.
Usipoweza kutawala vema hali hii ya utitiri huu wa taarifa unaweza kujikuta unakuwa mtu wa kupotoshwa, na mtu usiye mfanisi katika mambo yako ya kielimu, kikazi na hata kibiashara. Hakuna wakati unaohitaji ujuzi wa kipekee wa kutawala muda wako, na pia kuweza kuchambua taarifa unazozipata.

5. Maboresho makubwa katika teknolojia mbalimbali: Si tuu upande wa teknolojia ya habari, bali aina nyingi za teknolojia kama vile teknolojia za uzalishaji wa vyakula na teknolojia za utengenezaji wa mashine.  Mambo haya si tuu yanaleta bidhaa mpya na kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa mambo mengi, pia yanaleta athari nyingine ambazo inatupasa kuwa makini nazo kama vile, athari za kiafya , athari za malezi (kuporomoka kwa maadili), athari za kiuchumi (biashara nyingi kuporomoka kwa kushindwa kushindana).

6. Uharaka wa usambaaji wa mabadiliko:  Kwa jinsi dunia ilivyo ‘kijiji’ mabadiliko yanayoendelea makubwa ya kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa , na kijamii yanaathiri si tuu taifa moja ambapo badiliko fulani limetokea, bali mabadiliko hayo husambaa kwa haraka kwa nchi nyingine. Kama ilivyo kwenye usambazi wa bidhaa mbalimbali unavyosambaa kwa haraka – kumbuka matoleo kadhaa ya simu kama iphone, Samsung, n.k yanavyofikia Bongo, tutarajie mabadiliko mengine yanayotokea nchi za maghariba na barani Asia kufika kwa haraka hata Tanzania.

Hitimisho: Elimu ya darasani pekee haitoshi kukusaidia kupita na kutawala mabadiliko haya makubwa, unahitaji kupenda kusoma ziada.
Hakikisha unapata taarifa sahihi kwa kufuatalia kuaminika kwa chanzo cha taarifa. Pia tumia search engine kama Google, kutafuta vyanzo vingine vya habari vinasema nini kuhusu taarifa unayodhani ni sahihi.
Linda sana utashi wako kwa kuwa huo pekee ndio mali kubwa zaidi kwa maisha yako. Ukipoteza utashi wako kwa tamaa ya mali, kufuata mkumbo n.k utajikuta unapotea zaidi.
Kuwa tayari kubadilika kuendana na mazingira na hali halisi – elimu, aina ya biashara, aina ya kazi, mahali pa kuishi, mahusiano, malezi ya watoto.
Katika nyakati tulizopo,  ni muhimu sana kuufahamu na kuuishi msemo huu “ Don’t  Work Hard, Work Smarter”yaani “ Usifanye tuu kazi kwa nguvu zako zote, bali fanya kazi kwa akili zaidi”.
Share:

SABABU 5 KWANINI UPENDO HAUTOSHI KUJENGA MAHUSIANO BORA

Ukisoma kwa kutafakari makala hii utagundua kuwa kuweza kujifahamu sisi wenyewe vema, kuweza kujitawala sisi wenyewe, na pia kuweza ‘kuwasoma’ vema wenzi wetu , ni mambo ya msingi sana ili upendo tulionao uweze kudumisha mahusiano.  Msisitizo ni kwamba, pamoja na ukweli kuwa upendo ni kitu cha muhimu katika mahusiano, makala hii inaeleza kuwa kutegemea upendo pekee kama nguzo kuu ya mahusiano bora kunaweza kuwa jambo la hatari kwa mahusiano, kwa sababu zifuatazo:-

1. Binadamu ni kiumbe huru: Ni muhimu kukumbuka hili hasa kama unadhani kwakuwa unampenda fulani na umemuonyesha mapenzi yako yote basi hicho ni kama kifungo kwake kuwa hatoweza kutoka katika penzi lenu. Kwa asili binadamu ni huru, na anaweza kuamua kuutumia uhuru wake kufanya maamuzi mengine yoyote tofauti na unavyofikiri ni lazima afanye.  Kwa kuwa pia ni mbinafsi, basi kama upendo wako wote kwake hauendani na yale anayotazamia , unaweza kukuta ameshindwa kukaa katika penzi , ambalo kwa watu wengi wanaona kuwa ni penzi zito.

2. Binadamu ni mbinafsi kwa asili: Binadamu kwa asili huangalia maslahi yake kwanza kabla ya kuangalia ya mwingine. Mfano dhahiri wa ubinafsi huu ni pale inapotokea ajali , mara nyingi mtu huwaza kujiokoa mwenyewe kwanza kabla ya kufikiria wa karibu yake. Tumesikia habari za mama mzazi kuacha kitoto kichanga ndani wakati moto ukiendelea na yeye kutoka nje. Kuna habari pia za mama kumtumia mtoto wake kama ‘kifaa’ cha kuvunjia kioo cha gari , ili aweze kujiokoa, pale ambapo ajali ilitokea. Hivyo upendo tuu pekee hautoshi kumfanya mtu aendelee kukaa katika ndoa au mahusiano kabla ya ndoa (uchumba), ni muhimu yawepo mambo mengine yenye manufaa kwa mtu husika.

3. Binadamu ana mahitaji mengi  na yasiyo na kikomo:  Mwenza wako ana mahitaji mengi na yanaongezeka na kubadilika siku hadi siku kutegemeana na mabadiliko mbalimbali kama vile hali ya hewa, aina ya kazi,  watu anaokutana nao, mabadiliko ya teknolojia, mabadiliko ya kiuchumi n.k. Upendo wenu, hausimamishi mahitaji haya yasitokee, na kwamba upendo pekee hauwezi kuwa jibu la kutimiza mahitaji hayo. Inahitajika bidii katika kujituma kujiletea kipato, kuwa na mawasiliano bora kati yenu, kutambua mabadiliko na kuchukua hatua kabla mabadiliko hayajawabidilisha, na zaidi sana muweze kuwa na utamaduni wa kupanga mambo pamoja na kuwa waaminifu katika kutimiza yale mnayopanga. 
Chukulia mfano, wa wanandoa walioishi vema kwa miaka 5 ya ndoa, halafu ndoa ikaanza kulemaa kwa kuwa mmoja wao anaona hakuna uwajibikaji katika kumsaidia mwengine kujiendeleza kielimu, kibiashara, au kutimiza ndoto nyingine ambayo mwanandoa amekuwa nayo.

4. Binadamu wengi wanashindwa kujitawala:  Uwezo wa mtu kujitawala unaweza ukakinzana na upendo wake kwa mwenza wake, hivyo kuleta hali ya kutoridhika kwa mwenzi wake, kitu ambacho kinapunguza  au pengine hata kuondoa raha ya mahusiano. 
Mfano utakuta kwa kufuata makundi ya marafiki aliyonayo, mwanaume anakuwa mlevi wa kupindukia,  na kujikuta akiingia katika anasa na maamuzi mengine yasiyo mazuri kwa mpenzi wake na familia kwa ujumla. Hata hivyo mwanaume huyo huyo ukimuuliza kama anampenda mke wake au la, atakujibu anampenda sana. Tatizo nini ? Utajibiwa, ni pombe tuu ndio mmemtawala, na kwamba jamaa ana ‘kampani’ mbaya.

5. Maana isiyo sahihi ya upendo: Kuna wengi wanaodai wanao upendo lakini kiukweli walichonacho sio upendo bali ni tamaa au matakwa ya kuhitaji kutimiziwa mambo fulani. 
Maana halisi ya upendo sio vile unavyotaka fulani akufanyie mambo au jambo fulani, upendo sio vile unavyojisikia baada ya fulani kukutendea jambo uliloliona jema kwako, upendo sio vile fulani anavyokufanya ujisikie kwa sababu ya sura yake au umbo lake, BALI, upendo ni utayari wako wewe kufanya mambo yanayompendeza mwingine, kuwa tayari kuona mwingine ana furaha juu yako.  
 Kwa maana rahisi , upendo si jambo linalokuhusu wewe unajisikiaje, bali ni vile unavyotaka mwingine ajisikie.
Kwa maana nyingine, utatimiza vema upendo wako kwa kujitahidi kumfahamu mwenza wako, kutimiza yale anayohitaji (ili awe na furaha) sio kutimiza yale unayotaka wewe kwa makusudio yako binafsi. Upendo unahitaji kumheshimu mwenza wako, kumsikiliza, kumfanya akuamini, na aendelee kukuamini.
Pamoja na kuwa hisia za kimwili (chemistry) ni muhimu sana katika kujenga mahusiano yenu,  hisia za kimwili zisichanganywe na upendo. 
Kwakuwa fulani amekuvutia kimwili haina maana kuwa basi unampenda mtu huyo. 
Kufanya tendo la ndoa, sio lazima iwe ndio ishara ya uwepo wa upendo katika yenu, kwani wapo hata wanaofanya tendo la ndoa kama biashara.

Hitimisho
Mahusiano hususani mahusiano ya kimapenzi yanatutaka tuwe waajibikaji kwa wenzetu, na kwetu wenyewe. Kuwajibika kwa wenzetu ni pale tunapojifunza vya kutosha tabia,  na yale yanayompendeza na yasiyompendeza mwenza wetu. Wakati tunawajibika kwetu wenyewe kwa kujifunza kuhusu mapungufu yetu, na kujituma kujirekebisha. Mapenzi yanaleta majukumu, na bila kutambua na kutimiza majukumu husika, mara nyingi mapenzi yatageuka kuwa karaha, badala ya furaha.
Share:

GOOGLE ILIVYOAMUA ‘KU DEAL’ NA AKAUNTI ZA MAREHEMU

Sasa unaweza kuacha urithi wa vitu unavyomiliki mtandaoni kutoka Google. Mfano kama una blog ( kupitia Blogger), una picha (zilizopo kwa Picasa Web Albums), na documents mbalimbali zilizopo kwa Google Drive, unaweza kuigiza Google kuwa endapo utafariki, vitu vyako hivyo vikabidhiwe kwa mtu fulani.
Tunapozungumzia kufariki ni kuwa Google haitojua kuwa umefariki au la, ila kutokana na kutokutumia kwako kwa muda mrefu akaunti yako ya Gmail, na kwa maagizo utakayokuwa umeacha kuwa endapo itatokea haujaitumia kwa muda mrefu basi Google itume kazi zako kwa huyo utakayeamua atumiwe.

Huduma hii maalum iitwayo Inactive Account Manager, inaweza pia kunufaisha hata pale mtu anapokuwa amepelekwa jela kwa muda mrefu, au ameamua kuacha kutumia huduma za Gmail, hivyo kuamua kufunga akaunti yake na huduma nyinginezo toka Google.

Unachotakiwa kufanya ili kuagiza Google waigawe akaunti yako, na vitu vyako vingine, fuata hatua hizi:

1. Nenda kwa ukurasa wa huduma hii Bofya hapa (Inactive Account Manager)
2. Kisha jaza hatua kwa hatua mambo taarifa ambazo Google wanataka toka kwako. Taarifa hizo ni :-

Alert Me : Hapa utajaza namba ya simu na email address nyingine ambapo Google watafanya jitihada za kukutaarifu kuhusu kutaka kwao kufunga au kugawa akaunti yako.

Time out period:  Hapa utajaza muda ambao unataka Google wasubiri kama upo kimya kutumia akaunti yako. Muda huu ndio utakaowawezesha kujua kama kweli wewe ni mtumiaji hai au la. Na mara baada ya muda huu kupita, basi Google watajaribu kukuandikia email kwa anuani nyingine uliyojaza au kukutumia SMS kwa namba utakayokuwa umeijaza katika kipengele cha Alert Me.

Notify contact and Share Data: Hii ni sehemu muhimu ambapo Google itagawa taarifa zako kwa mtu au watu utakaoagiza. Pia watu waweza kuagiza watu hawa wapewe taarifa. Na kama upo hai au unaweza bado kutumia email yako, basi watu hao watakuuliza wewe kabla ya kukubali kupokea taarifa zako.
Mtu au watu utakaowaorodhesha katika kipengele hiki wanaweza kutumiwa ujumbe unaoweza kutafsirika kama hivi, baada ya muda uliotaja wa Google kusubiri:


Optionally delete account: Hiki ni kipengele ambapo unaagiza Google waifute akaunti yako baada ya muda ulioujaza katika kipengele cha Time Out Period, kupita.

3. Ukisha jaza vipengele vilivyotajwa hapo juu, unabofya Enable, ili uanze kuitumia huduma hiyo.

Share:

MSAADA BINAFSI (BURE KABISA) KWA WANAOTAFUTA AJIRA

Kwakuwa swala la ku apply nafasi za kazi ni  jambo gumu kwa wengi, tumeamua kusaidia wale ambao watajitokeza kutaka kupata maelekezo binafsi ya jinsi ya kuandika barua ya maombi ya kazi na pia kuandika Curriculum Vitae.
Msaada huu ni BURE KABISA.
Kama kweli upo na nia ya kupata maelekezo, jaza fomu hii kisha bofya SUBMIT:
Share:

WAAJIRI WANACHOTAKA KUKIONA KATIKA BARUA ZA MAOMBI YA KAZI

Mara nyingi waajiri hutaka waombaji wa kazi wawasilishe barua ya maombi ya nafasi ya kazi ili waweze kuchambua watu wenye vigezo, ambao wanaweza kuwaita kwa usaili.
Mambo kadhaa ya kukumbuka:

Barua inaeleza ujuzi wako wa mawasiliano (communication skills)
Barua ya maombi ya kazi ni aina ya mawasiliano tunayosema mawasiliano rasmi. Hivyo unategemewa kufuata mpangilio sahihi (format) wa uandishi wa barua –kama vile kuandika vyema anuani yako, anuani ya muajiri, kichwa cha habari cha barua, salamu, tarehe,  hitimisho sahihi la barua, na sahihi yako. Pia kwakuwa ni mawasiliano rasmi, unatakiwa utumie lugha rasmi, badala ya kutumia lugha za mtaani au vifupisho visivyo rasmi. Vifupisho kama  ….am applying for this post…, na mwisho wa barua ukaandika
 Yours for real,
 John.
( Inaonyesha uwezo wako wa kuwasiliana vema ni mdogo).
Ukiachilia kutumia lugha rasmi, unatakiwa pia uweze kuandika kwa kufuata kanuni za lugha (grammar) sahihi. Haijalishi kama umeandika lengo lako ni kusema una uwezo mzuri wa kufanya mawasiliano bora, muajiri ataweza kugundua ukweli kwa haraka kupitia barua yako, mfano ukiandika hivi:-
 “ I am excellent communication skills”

Barua inaeleza aina gani ya mfanyakazi ulivyo
Namna ya uandishi wako na yale utakayoyaandika katika barua , yanaweza kuonyesha nini muajiri wako ategemee kutoka kwako kama mfanyakazi. Mfano wa mambo yanayoweza kujieleza katika barua yako ni:-
  • Je wewe ni mbunifu au la: Hii itaonekana kupitia namna ambavyo umeamua kujitofautisha katika uandishi wa barua tofauti na wengi wanavyoandika. Mfano jinsi unavyojieleza kuhusu vile unavyo ‘fit’ nafasi husika unayoomba. Vile unavyojieleza mafanikio (achievements) ulizowahi kufikia katika kazi zako za awali- mambo gani ya msingi uliyoyafanya ambayo yalinufaisha asasi uliyokuwepo hapo awali ( hata kama ulikuwa mwanafunzi bila shaka kama wewe ni mbunifu ulipata kufanya mawili matatu ya manufaa kwa watu wengine na kwako pia).  
  • Je wewe ni mchapakazi au la: Hii itaonekana kupitia namna ambavyo umeandika kwa umakini barua yako – je umekuwa na bidii ya kutosha kufuata maagizo yote ya tangazo la kazi ? Je, umekuwa na bidii kufuata vigezo vya mawasiliano bora? Je, umefanya utafiti wa kutosha kuhusu kazi unayoomba na asasi husika inayotaka kukuajiri ili kwamba unapoandika  barua yako, uonyeshe una uelewa na  hamasa ya kupata ajira husika?
Barua inaeleza kwanini wewe uchaguliwe au usichaguliwe
Kwa kuzingatia ushindani uliopo katika soko la ajira, na hitaji la ‘bidhaa bora’ yaani mfanyakazi bora, barua yako inabidi ikidhi vigezo hivyo, ili iweze kuwashawishi waajiri wakuite kwa ajili ya usaili na hatimaye kukuajiri. Vigezo kama kuwa mbunifu, mchapakazi, ujuzi, uzoefu na uwezo  bora wa mawasiliano ni mambo ambayo yanaweza kuleta maana katika namna unavyoandika barua.
Share:

BORESHA MATUMIZI YAKO YA EMAIL KWA MAUJANJA HAYA

Makala hii inakupa maelekezo ya mambo adimu katika kusimamia barua pepe zako, ili kuboresha ufanisi na- kufurahia kuwa na akaunti ya email. Mfano wa ‘maujanja’ hayo ni uwezo wa kuwa na folders maalum kwa watu au asasi maalum zinazokutumia email mara kwa mara ili kwamba ukitaka kupitia email toka kwa mtu fulani, basi wewe unaenda tuu kwa folder lake, mfano unakuwa na folder la MBUKE TIMES, basi email zote toka MBUKE TIMES zinaingia humo, haziendi kwa Inbox. Mambo mengine tutakayoangalia ni jinsi ya kuboresha ulinzi wa akaunti yako ya email.

Matumizi ya BCC, na CC
Unapotaka kutuma email kwa mtu au asasi fulani , na wakati huo huo email hiyo iende kwa mtu au watu wengine basi una njia mbili za kufanya hivyo:-

  • Tumia CC (Carbon Copy) : Utakapotumia CC ni kwamba yule uliyemkusudia kwa mara ya kwanza email yako iende ataweza kuona kuwa umewatumia ‘copy’ watu wengine. Mfano kama umetuma email kwa JOHN, halafu CC ikawa kwa ISSA, na MARIA, basi JOHN ataona kuwa ISSA na MARIA wamepokea email husika. Na pia ISSA na MARIA wataona kuwa email hiyo imeenda kwa JOHN.
  • Tumia BCC (Blind Carbon Copy): Utakapotumia BCC, ni kwamba yule uliyemkusudia kwa mara ya kwanza email yako iende atapokea email yako, na wale wengine watapokea ‘copy’ ya email hiyo, hata hivyo kila mmoja hatojua kama mwingine amepokea email hiyo hiyo. Hii ni muhimu hasa pale ambapo si busara kutoa email address za watu bila ruhusa yao. Kwani umeona hapo juu ukitumia CC, watu wengine wanaona email address za waliotumia ‘copy’ ya email husika.

SPAM Folder
Kumbuka mara kwa mara kutembelea folder lenye kubeba SPAM emails. Wakati mwingine utakuta email zako muhimu zimetupwa humo, kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mtu aliyekutumia kusahau kuandika kichwa cha habari (subject) au kuandika kichwa cha habari ambacho teknolojia inayotambua SPAM inatambua kuwa aina ya maneno katika kichwa cha habari au email ni utambulisho kuwa email ni SPAM.

Kuboresha Ulinzi wa akaunti ya email
Huduma nyingi za email kama vile Google na Yahoo zinakupa nafasi ya kuwa na namna bora zaidi ya ku sign in. Badala ya ku sign in kwa kuandika ID na PASSWORD tuu, kuna hatua nyingine inaongezeka ambapo unatakiwa ujaze CODE maalum ambayo utakuwa umetumiwa kwa njia ya SMS kwa namba yako ya simu. Hii ina maana kuwa hata kama mtu anayo password yako, hatoweza kufungua mpaka ajaze CODE maalum ambayo inapatikana tuu kwa njia ya SMS kwa namba yako ya simu. (Labda aibe hadi simu yako).
Jinsi ya kujiandikisha na huduma hii, angalia maelezo katika picha hapa chini, Mfano huu ni kwa huduma za GMAIL.
Ili kuanza kuitumia huduma ya  2 step verification, bofya mwanzo kulia mwa email akaunti yako kisha chagua Account.

Ukishabofya Account , kama ilivyoelekezwa hapo juu, nenda sehemu ya Security, kisha chagua sehemu ya 2 Step Verification. Halafu bofya Settings. Halafu Fuata Maelekezo rahisi utakayoyaona ikiwa pamoja na kuandika namba yako ya simu.
Ukiwa umefanikiwa kujiunga na 2 step verification, utaona kuwa kila utakapotaka ku sign in, utatakiwa kuweka Code kama unavyoona mfano wa picha hii hapo juu.

Tengeneza Folders Maalum
Ili kurahisisha kumbukumbu na utafutaji wa email ulizowahi kupokea toka kwa mtu au asasi fulani, waweza kutengeneza Folders maalum ili kila mara zinapokuja email husika, zinaingia katika folders hizo. Mfano kama mara kwa mara unapokea email toka kwa JOHN, basi waweza tengeneza FOLDER la JOHN, hivyo badala ya email toka kwa JOHN kuingia INBOX, zinaingia kwa FOLDER la JOHN. Hii itakurahisishia ufuatiliaji wa mazungumzo yako na JOHN.
Fuata hatua zifuatazo katika picha, kwa mfano toka GMAIL.
Kuanza kutengeneza Folders zako, angalia kulia mwa email akaunti yako bofya hapo kama unavyoona pichani,  kisha chagua Settings.
Ukiwa sehemu ya Settings, chagua FILTERS kisha nenda chini kidogo utaona sehemu ya Create a new filter.
Andika anuani ya huyo unayetaka kuwa email kutoka kwake ziingie kwa folder maalum. Kisha bofya Create filter with this search , kama uonavyo pichani chini. Ukibofya hapo utapelekwa kwenye ukurasa mwingine kujaza mambo mengine ya msingi.
Baada ya kuwa umechagua ku create filter kwa kutumia address fulani, utakutana na ukurasa huu, ukurasa huu. Chagua Skip the inbox, ili email zisiwe zinaingia kwa email, kisha chagua Apply the label, ili uweze kuonyesha ziingie wapi. Chagua options nyingine kama utapenda.
Hiyo sehemu ya Apply the label, ukichagua sehemu ya choose label, utaweza kutengeneza label , yaani jina la huyo unayetaka kuwa unatunza email zake kwa folder maalum. Andika jina lake kisha bofya Create. Kisha fuata maelekezo mengine na bofya Create Filter kumaliza kutengeza folder husika.
Share:

ELIMU ILIVYO MZIGO KWA WENGI WETU

Pamoja na kuwa elimu ni kitu muhimu sana maishani, kwa watu wengi kitu elimu kimekuwa ni mzigo mkubwa kiasi kwamba badala ya kuboresha maisha, elimu imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo. Badala ya elimu kumsaidia mtu kuwa na furaha , inamletea huzuni. Pia, si ajabu kukuta mtu mwenye ‘elimu kubwa’ au tumuite ‘msomi’ akifanya mambo ambayo hakutarajiwa kufanya. Makala hii inachambua mambo ya msingi ya kuangalia ili elimu isiwe mzigo kwako:-

Inatuweka njia panda:  Imani kuwa kiwango fulani cha elimu ndio msingi wa ‘kutoka’ kwako kimaisha, yaweza kukufanya ukaacha mengi ya msingi ambayo ungeweza kufanya na kufanikiwa kimaisha, badala yake ukajikuta unataka KWANZA upate kiwango hicho cha elimu unachodhani ukikipata ndio utaanza ‘kuishi’.  
Ingawa ni kweli kuwa elimu ni muhimu, hasa viwango vya juu vya elimu ni muhimu katika kukurahisishia kuongeza fursa mbalimbali, haina maana kuwa mafanikio yanapatikana kwa njia pekee ya kuwa na elimu ya kiwango kikubwa. Hivyo basi unapojikuta upo katika njia panda ya kuchagua kufukuzia kwanza kiwango fulani kikubwa cha elimu, hakikisha unawaza  na kutafuta njia nyingine mbadala za kupanua fursa mbalimbali kwa kutumia kiwango ‘kidogo’ cha elimu ulicho nacho. 
Uwe na mtazamo wa kuwa mzalishaji, mtu mwenye furaha , na unayeishi kwa namna ile uwezayo kweli kweli, sio kwa kufuata matarajio ya watu wengine. Kwani baadhi yetu hujikuta tunajikita na elimu kwa kuwa tuu hivyo ndivyo ndugu zetu , marafiki zetu, au familia inavyotegemea tutafanya. Au kwa kuwa unataka kushindana na watu fulani. Usiwe mwoga wa kutokuendana na matarajio ya watu wengine. Weka matarajio yako, na jiamini kuwa utayatimiza.

Inagharimu uhuru wa watu:  Kwa baadhi ya watu, elimu badala ya kuwaweka huru, inawafanya watumwa wa kifikra kwa namna mbalimbali, kama vile kuamini tuu kila aliyesoma sana anachosema ni sahihi, kuamini kuwa fani yake ya elimu ndio suluhisho pekee la matatizo au changamoto fulani, mfano mchumi kuamini kuwa matatizo ya ajira yatasuluhishwa na mbinu za kitabuni za wachumi waliopita.  
Elimu pia inaweza kumfanya mtu ajishushe thamani au ajione hafai kuwa na mtazamo tofauti na yule anayemuona kuwa amemzidi ‘elimu’, hata kama ni kweli kwa mtazamo huru , huyo anayeonekana kuwa ‘msomi zaidi’ anakosea, ila kwa kuwa tuu ana elimu zaidi, basi wengine inabidi wajishushe na kukubaliana nae. Ni kama vile kusema “mkubwa siku zote hakosei”. 
Tumedokeza pia, hamasa kubwa ya kutaka kiwango fulani cha elimu inaweza kumnyima mtu ‘uhuru’ wa kuangalia fursa nyingine za kimaendeleo.

Inarudisha nyuma uwezo wa kufikiri:   Elimu inarudisha nyuma uwezo wa kufikiri kwa baadhi ya watu hasa pale inapoleta uwoga wa kuwa na mtazamo tofauti na ule ambao mtu tayari ambaye anatambulika kuwa ni ‘msomi’.  Hatari zaidi ni kuwa baadhi ya watu huogopa kuwa na mtazamo tofauti na ‘ukweli’ ambao amefanya kuusikia tuu.
Pia kwa wale waliogemea sana fani zao, hujikuta wakitafsiri kila kitu kupitia fani zao, na hata kama haviendani  na hali halisi, wao huona ni sawa.  Hii ni kwakuwa kwa baadhi ya watu, elimu inaleta kujiaminisha usahihi wa wayafanyayo au wa yale wafanyao wengine wenye elimu fulani.
Inafanya watu wajitenge : Kwa baadhi ya watu, kiwango fulani cha elimu ndio utambulisho wa thamani ya mtu, na pia ndio  tiketi ya kukubalika kwake au kuwakubali watu wengine. Si ajabu basi kukuta mtu mwenye wazo zuri la kimaendeleo, akipuuzwa kwakuwa tuu , kiwango chake che elimu hakidhihirishi asemacho ni sahihi, yaani “hafanani” na anachosema. Utasikia mtu akimwambia mwenzake bila haya “ mi siongei na wasio soma”.

Inakosesha fursa:  Kwa sababu elimu kwa baadhi ya watu ni chanzo cha kutokuwa na uhuru wa kufikiri, kwakuwa elimu inawapelekea watu hao wawe wazito katika kufikiri kwa ufasaha,  kwa kuwa pia inawafanya watu wajitenge kwa kuwa na dharau, upo uwezekano wa elimu kuwakosesha fursa baadhi ya watu.

Hitimisho
Lengo la makala hii haikuwa ‘kuponda’ elimu au ‘wasomi’, bali kusisitiza kuwa elimu inafaa ilete manufaa kwetu. Na hivyo pale unapohisi inaleta mambo tuliyotaja hapo juu, au yanayofanana na hayo basi ni wakati wako kubadilika, au kutafuta msaada wa jinsi ya kurekebisha hayo. La msingi sana ni kuhakikisha kuwa elimu, pamoja na uzuri wake, haichukui nafasi ya ubinadamu wako, utashi wako na nguvu yako kubwa ya kufanya maamuzi.
Elimu ikusaidie kuona uhalisi katika uhalisi wake, sio ikuonyeshe hali tofauti na kukuaminisha kuwa ndio hali halisi.
Unalo jukumu la kuitawala elimu, na sio elimu ikutawale wewe, hii inamaanisha kuwa sio kila kitu utakachosoma utalazimika kukiamini, na kwamba uwe tayari kukubali kuwa mambo fulani uliyoyasoma na ukayaamini wakati fulani yanaweza yasiwe sahihi wakati mwingine hivyo ikakubidi utafute uelewa mbadala.
Share:

KWA NINI MAWASILIANO NI 'INSHU' KUBWA KATIKA MAHUSIANO

Watafiti ( University of Colorado Boulder) wanasema asilimia kubwa  ya migongano na mifarakano inasababishwa na kutokuwasiliana kwa ufasaha kwa wahusika waliopo katika mifarakano au migongano husika. Na inasemwa pia (Examiner.com) kuwa dawa namba moja ya kuzuia na kusuluhisha migongano ni kuboresha mifumo ya mawasiliano na kuhakikisha wahusika wanakuwa na mawasiliano fasaha. Ukiachilia na ukweli huu wa kitafiti, wengi wetu tumejikuta hatutoi kipaumbele katika kujifunza na kuboresha uwezo wetu wa kuwasiliana kwa ufasaha. Ikumbukwe kuwa, kumudu kuwasiliana kwa ufasaha, ni zaidi ya kuweza kusoma na kuandika. Ni zaidi ya kujua misamiati mbalimbali ya darasani ihusuyo mawasiliano kama vile (receiver, sender, barriers to communication n.k.).  Katika makala hii tutaangalia mambo ya msingi tunayoweza kuyaboresha katika mawasiliano ili kuboresha mahusiano yetu, yawe ya kimapenzi, kibiashara au kiofisi.

Ni muhimu kujua maana pana ya Mawasiliano Fasaha
Maana pana ya mawasiliano fasaha inatutaka tuchukulia swala la mawasiliano kuwa ni jambo la kila siku, jambo la kila wakati, hivyo ni swala endelevu ambapo kulimudu vema, linahitaji maamuzi thabiti ya mtu binafsi kuwa ataishi kwa kufuata kanuni husika. Ingawa kanuni za mawasiliano fasaha zaweza kuonekana kama vile ni nadharia,  umaana wa mawasiliano sahihi upo katika kufanya kwa matendo yanayotakiwa kukamilisha mawasiliano fasaha.
Acha basi, tuangalie maana pana ya mawasiliano fasaha (kwa kiingereza effective communication):
Mawasiliano fasaha ni yale mawasiliano ambayo yanatimiza vigezo vyote vifuatavyo:

  • Kigezo namba 1: Mawasiliano ambayo mtoaji ujumbe anaeleweka kama alivyokusudia, na pia mpokeaji ujumbe (receiver) anapokea ujumbe na kuulewa kama ilivyokusudiwa. Ndio maana basi kuna haja ya kujifunza namna bora ya kutoa ujumbe, na namna bora ya kupokea ujumbe.
  • Kigezo namba 2: Mawasiliano fasaha yanawezesha lengo kuu la mawasiliano kufikiwa. Mfano kama lengo ni kuomba ruhusa, basi ruhusa inapatikana, isipokuwa pale tuu mazingira mengine nje ya mawasiliano yanalazimisha ruhusa kutokutolewa. Hapa ina maana kuwa sababu kuu ya kutopata ruhusa sio kwakuwa mhusika hakueleweka vema au hakufanya mawasiliano kiufasaha, bali kuna mambo mengine nje ya mawasiliano yanafanya upatikanaji wa ruhusa kusiwe jambo fasaha. Mfano, kuna hali ya hatari kutokana na vurugu.
  • Kigezo namba 3:  Mawasiliano fasaha yanawezesha hali ya kuelewana hata baada ya mawasiliano kukamilika. Kigezo hiki kinamaanisha kuwa lengo sio tuu kufanikiwa kupata unachohitaji lakini pia uchukulie maanani jinsi unayosema au kuandika yanavyoweza kuathiri uhusiano wako  wa sasa au wa baadae na huyo unayewasiliana naye.

Jinsi ya kufanya mawasiliano fasaha
Ili kufanya mawasiliano fasaha kuna mambo 10 muhimu ya kuzingatia. Mambo haya yanaelezwa hapa:

  1. 1.Tambua uhusiano wako na mpokeaji wa ujumbe:  Hii inamaanisha kuwa tambua unawasiliana na nani , na kwamba wewe ni nani kwa huyo mhusika, na huyo mhusika ni nani kwako. Mfano, utasikia wapenzi wengi wamejikuta wapo katika mzozo kwakuwa tuu mmoja amehisi kudharauliwa kwa vile mwenza wake alivyomjibu, au alivyomueleza jambo fulani. Utasikia “ kwanini uzungumze hivyo kama vile mie sio mkeo?” au “ Kwanini uzungumze hivyo kama vile hujui unazungumza na mumeo?”
  2. Tambua hali ya kiakili aliyonayo mpokeaji wa ujumbe:  Hii inamaanisha kuwa kabla ya kuwasiliana na mhusika fulani fanya kautafiti walau kadogo kujua kwa kiasi gani mhusika yupo tayari kiakili kupokea kile unachotaka kuwasiliana naye. Si ajabu kukuta mwanadada analalamika kuwa mpenzi wake hakutimiza alilohitaji au hakuonyesha kujali alipokuwa anazungumza naye, wakati kiukweli mwanaume alikuwa ‘bize’ anaangalia mpira. Akili yake yote ilizama huko.                   Mambo yanayoweza kufanya akili isiwe tayari au isiweze kupokea mawasiliano kwa ufasaha ni kama vile mtu akiwa na hasira, mtu akiwa amechoka, mtu akiwa na mawazo, mtu akiwa na hofu, au huzuni, n.k 
  3. Tambua utamaduni wako na utamaduni wa mhusika unayewasiliana naye: Hapa neno utamaduni linamaanisha namna ya kuishi ya mtu fulani, mfano vile mtu anavyoamini katika mambo fulani, vile mtu anavyopenda kuonekana mbele za watu, vile mtu anavyosalimiana na wengine n.k. Ni muhimu kutambua hivi na kujua namna ya kufanya mawasiliano kiasi kwamba utamaduni wa mtu hauathiri kuelewana kwenu, na mahusiano yenu baada ya kuwasiliana.                                       Mfano, waweza simama wakati unamsalimia mkwe, ila kwa utamaduni wa mkwe, ulitakiwa upige magoti, hivyo hata baada ya kuondoka kwako, utaacha gumzo kuwa hauna heshima. Tayari hii itapelekea kutokuelewana kati yako na upande wa ukweni. Hali kadhalika , kama unayewasiliana naye ni mteja, halafu ukafanya kinyume na matarajio yake ni kwamba utajikuta umepoteza mteja.  Zingatia mawasiliano yasiyotumia maneno:  Kumbuka kwamba mbele ya watu wengine tunajikuta tunatoa ujumbe fulani kwao hata kama hatuelezi kwa maneno ujumbe husika.                                                                                                                                     Mambo kama vile kuguna, kurembua macho, kuangalia pembeni, kuziba masikio,  n.k yote yanatoa ujumbe fulani kwa mtu mwingine. Tatizo la aina hii ya utoaji ujumbe ni kuwa , kwakuwa hakuna maneno, basi mpokeaji wa ishara husika anaweza kuwa na tafsiri tofauti na unachokusudia. Mfano, unaweza kukuta mtu analalamika “ Kwa nini unanikaripia?” wakati kiukweli haukudhamiria kumkaripia, bali jinsi ulivyokuza sauti yako, mwingine ameelewa kuwa umekasirika.                         Hii pia inaweza kuchangiwa na namna unavyoonekana, pengine unazungumza huku umekunja sura.       
  4. Dhibiti vizuizi vya mawasiliano  (barriers to communication):  Hakikisha wakati wote unapotaka kuwasiliana na mtu kuwa mtu huyo ametoa usikivu wa kutosha kwako  au yupo na utayari wa kuwasiliana nawe ili kwamba unachotaka kukiwasilisha kwake kieleweke vema.                               Si ajabu kukuta mtu akilalamika kuwa mwenza wake hakufanya jambo fulani, eti kaonyesha dharau kwa kutokufanya hivyo, wakati ukweli ni kuwa mwenza huyo, wala hakuupata ujumbe husika. Au wakati ujumbe unamfikia hakuwa katika hali ya kumuwezesha kutilia maanani ujumbe husika.  Mfano wa vizuizi vya mawasiliano ni kama vile, makele, lugha unayotumia kuwasiliana na mwenzako pengine asiielewe vema – mfano ,umetumia vifupi vya maneno mengi, au umechanganya sentensi kiasi kwamba ujumbe kamili haueleweki vema, n.k
Share:

JINSI YA KUTUNZA FILES NA FOLDERS ZAKO ONLINE BILA MALIPO

Kwa huduma kama Google Drive, Dropbox, unaweza kujikuta hauhitaji kuwa na flash disk.
Fikiria umeandika kazi yako vizuri iwe utafiti, kazi ya darasani, taarifa fulani ya kiofisi, report fulani muhimu za kibiashara, halafu ukaihifadhi kwenye kompyuta au kwenye Flash disk, ila baadae unakuja kukuta kazi yako hiyo imepotea, kompyuta imeharibika hivyo na kazi yako kupotelea humo, au ukaja kujikuta umeipoteza Flash Disk au CD uliyotumia kuhifadhi kazi yako imepotea.
Lengo basi la Makala hii ni kukupa dokezo la njia mbadala ya kutunza files na folders ambapo, files na folders zako zitakuwa zipo ‘hewani’- mtandaoni hivyo hautokuwa na hofu ya kupoteza kazi zako kwa njia tulizotaja hapo juu.

Ili kuhifadhi mtandaoni files na folders zako, unaweza tumia huduma mbalimbali kama vile:

Katika makala hii tunachambua kwa ufupi huduma za Google Drive, Box, na Dropbox. Sehemu yetu ya kwanza leo hii tunatazama Google Drive.

Kuanza kuitumia Google Drive
Ili kutumia huduma hii, inakupasa uwe na akaunti ya Gmail. Kisha ingia kwa website ya Google Drive, andikisha akaunti yako ya Google Drive. Google wanakupatia 5GB za bure ili uweze kuhifadhi mambo yako humo Google Drive. Ukitaka kuongeza ukubwa wa Drive, basi itakubidi ulipie kwa kufuata maelekezo ya jinsi ya kuongeza ukubwa wa Google Drive.

Jinsi ya kuhifadhi files na folders kwa Google Drive
Unapotaka kuhifadhi files au folders inabidi uingie kwenye website hiyo ya Google Drive, halafu nenda sehemu ya Upload. Angalia picha hapa chini. Hii inamaanisha kuwa unaweza kupata files na folders zako popote pale utakapokuwepo. Ni kama vile kuwa na flash disk, isipokuwa kwa Google Drive inabidi uwe umeunganishwa na mtandao (internet).

Pichani kulia sehemu ya upload ndipo unapoweza kutumia ku weka files na folders zako online. Sehemu ya CREATE, ni kama unataka kuandika documents kwa kutumia program zinazofanana na MS WORD, POWERPOINT, na EXCEL.

Kuinstall Google Drive kwa Kompyuta yako
Huduma ya Google Drive, inakuwezesha pia kudownload program ya Google Drive, hivyo ukiwa ume install hiyo program kwa kompyuta yeyote utaweza kuwa unatupia tuu files na folders zako kwa kompyuta, kisha utaweza kuziona popote pale utakapoenda mtandaoni.
Hata hivyo kumbuka, sio lazima ku install Google Drive kwa kompyuta. Unatakiwa kufanya installation endapo tuu unataka kuwa na uwezo wa ku dumbukiza mafaili yako kwa kutumia kompyuta. Na pia kama unataka kuwa unafungua faili lililopo katika Folder lako la Google Drive, na ku save humo, basi moja kwa moja mabadiliko uliyoyafanya katika faili hilo yanakuwa yamefanyika katika Google Drive iliyopo hewani (mtandaoni).
Picha hii inaonyesha Google Drive ambapo, inakuwa umekwisha install kwa kompyuta hivyo unafanya kudumbukiza tuu files na folders zako. Unapofanya marekebisho katika files zilizopo humu , basi moja kwa moja, mabadiliko yanahifadhiwa kwenye Google Drive ya online.

Itumie Google Drive kwa Kuandaa kazi mbalimbali
Unaweza pia ukatumia Google Drive kuandika kazi zako mbalimbali, kama vile ufanyavyo kwa kompyuta binafsi kwani Google Drive ina program ya WORD, POWEPOINT na EXCEL. Ukishaandika kazi zako unaweza ukazihifadhi humo humo Google Drive, au ukaamua kuzituma sehemu yeyote uitakayo.

Unaweza Kushare files na folders zako zilizopo ndani ya Google Drive
Matumizi mengine ya msingi ya Google Drive ni kukuwezesha kutuma files na folders ambazo ni kubwa sana kiasi haziwezi kutumwa kwa kutumia njia ya email. Unachotakiwa kufanya weka files au folder lako kwa Google Drive, kisha nenda sehemu ya Share kulia mwa Google Drive, halafu fuata maelekezo ya jinsi ya kushare file au folder husika.
Kwa sababu inakupa uwezo wa kushare files na folders na watu wengine, Google Drive inakupa nafasi ya kufanya kazi kwa kushirikiana na watu mbalimbali. Kwani waweza andika kazi, uka isave kwa Google Drive, mtu mwingine akaja aka edit, au kuongeza kitu, kisha nae akasevu humo.
Share:

MADHAIFU MATANO (5) YANAYODIDIMIZA MAHUSIANO NA NDOA

Makala hii ni tafakari huru kuhusu mambo ya msingi katika mahusiano.  Hapa utapata tafakari ya maana ya maneno na imani ambazo zinatutatiza wengi wetu.

1. Mchanganyiko mkubwa kuhusu maana ya mahusiano, mapenzi na ndoa:
Labda kipengele hiki tuanze kwa kueleza kuwa kunaweza kuwepo ndoa, lakini yasiwepo mahusiano wala mapenzi. Inaweza kuonekana kama inachanganya kidogo, lakini ndio ukweli wenyewe.  Ndoa ni namna tuu ambayo wawili walio kwenye mahusiano wanaamua kuwataarifu rasmi watu wengine kuwa wao wapo rasmi katika mahusiano. 
Ndoa ni kiapo mbele ya watu wengine , na ni namna ya kutaka kumuhakikishia mwenza wako kuwa endapo kiapo hicho kitatokea kuvunjika, basi unakubali rasmi kuwajibika kwa mujibu wa taratibu zilizopo za ndoa husika, ikiwemo kukubali kuitwa kwenye mabaraza ya usuluhishi, kugawana mali, n.k. Na kwa upande wa kiroho, inabeba maana zaidi kuwa unaweka kiapo kwa Mungu wako kuwa utalinda mahusiano yako na huyo unayemchagua.
 Hivyo basi, ndoa haijengi mahusiano wala mapenzi. Kiuhalisi inabidi kwanza yawepo mahusiano na mapenzi kisha ndio kiapo kifanyike, kwani kinyume cha hivyo ni kuwa unakula kiapo ‘feki’.
Ndio maana basi, ni muhimu kwa wapenzi kutambua kweli kama wanahitajiana, kuwa kwenye mahusiano na kutafakari kwa uhuru kama kweli wanataka kuweka kiapo rasmi cha kuwa pamoja.
Kutumia ndoa kama kinga ya kuhakikisha mahusiano yako yanadumu ni maamuzi magumu ambayo pengine yanaweza yasilete faida hapo baadae.

2.Mahusiano na ndoa nyingi huyumbishwa na Matarajio yasiyo halisi
Kabla hata ya kuingia katika mahusiano na hatimaye ndoa wengi wetu huwa na matarajio binafsi ya kimaisha. Matarajio haya yanajumuisha vile tunavyotaka sie wenyewe kuwa hapo baadae, pamoja na matarajio ya vile tunavyotaka wenza wetu wawe.
Hata hivyo katika hali halisi tunajikuta sisi wenyewe hatuwezi kujibadilisha au kujiweka kwa usahihi vile tunavyotamani kuwa (kwa sababu kwa kila tunachojaribu kufanya kuwa bora, tunajikuta bado tuna madhaifu mawili matatu). Pamoja na ukweli huu, tunajikuta tupo na matarajio ya kuwafanya wenza wetu wawe watu wa aina fulani. Kwakuwa kiasili binadamu ni kiumbe huru, tunajikuta wenza wetu nao wakiwa ‘busy’ kutimiza ndoto za vile wanavyotamani kuwa iwe kimavazi, aina ya marafiki, utafutaji wa kazi , kujiendeleza kimasomo, aina ya mali za kununua, hata kufikiria tofauti aina ya maisha wanayotaka muishi.
Matokeo yake ukinzani huu wa matarajio ni mkanganyiko wa mgongano wa mawazo kati ya wawili nyie, na mwanzo wa vita ya chini kwa chini ya nguvu ya maamuzi katika mahusiano yenu.

3. Kuweza kumbadili tabia mwenza wako
Mojawapo ya jambo ambalo hufanywa na wengi walio katika mahusiano ni kuwa na ‘tamaa’ ya kutaka kumbadili tabia fulani mwenza wake. Hata hivyo ‘tamaa’ hii ni sehemu ya yale tunayoyaita matarajio yasiyo halisi, kwani tabia ya mtu hujengwa na mambo mengi sana, ikijumuisha aina ya makuzi, aina ya mfumo wa imani mtu anaouamini, aina ya marafiki alio nao, uwezo wake wa kujiamini katika kubadili tabia kwani wengine wameshakata tamaa kuwa hawawezi kukata tamaa, na zaidi sana, mabadiliko ya tabia huhitaji mfumo endelevu na wenye kusoma vema asili ya tabia ili kuweza kuirekebisha.
Hata hivyo wengi wetu kwenye mahusiano, hutegemea ‘mapenzi’au vitisho tuu kama vile ‘nitakuacha mie ’,  kama sababu ya kumfanya mtu abadilike kitabia.Udhaifu wetu katika kutambua asili ya tabia ya mtu husika na mbinu za kisayansi za kubadili tabia hufanya zoezi la kubadilishana tabia kuwa gumu na pengine lisilowezakana.

4. Kuvumilia ndio kuonyesha upendo na ndio kudumisha mahusiano
Hii ni aina nyingine ya matarajio ambayo sio halisi kwani kiukweli kila mtu analo jukumu la kufanya bidii kuwa mtu mwema, hivyo hauhitaji kubeba ‘uzembe’ wa mwingine kwa kisingizio tuu cha kuwa unaonyesha upendo hususani pale ambapo ni kwa uzembe tuu au kutokujali kwake mwenza husika amefanya jambo fulani.
Kwa jinsi kasumba hii ilivyo enea sio ajabu kukuta mtu akifanya mambo mabaya kwa mwenza wake kwa makusudi ili tuu eti apime kama kweli mwenza wake ni mvumilivu.
Kumbuka hapa hatumaanishi kuwa kusamehe ni kosa. Hapana, kusameheana ni muhimu, lakini sio kwamba ni muhimu tuu katika mapenzi. Kusameheana ni jambo la asili, na tunapaswa kusameheana kwa mambo mengi nje hata ya mahusiano. 
Tunachosema ni kuwa kuna  kasumba ya baadhi yetu kuona kuwa wanayo ‘haki’ ya msingi ya kukosea eti tuu kwakuwa tuu mwenza wake analazimika kusamehe ili kuonyesha kweli anao upendo wa dhati.
Amini usiamini, kasumba hii ya kutarajia aina ya pekee ya kusamehewa na kuvumiliwa kwa kisingizio tuu cha kuwa upo kwenye mapenzi na mwenza wako, hurudisha nyuma maendeleo ya mahusiano yenu kwani mwenzi wako nae ni binadamu na kumbuka anayo matarajio mengine ya maisha, isitoshe na yeye anahitaji upendo na kujaliwa na wewe, hivyo kutarajia kwako kusamehewa na kuvumiliwa kuna mnyima haki mwenza wako. Hatimaye kutegema kwako kusamehewa kila wakati, kunamfanya mwenza wako atilie mashaka upendo wako kwake.

5. Uaminifu = Upendo= Kudumu kwa mahusiano
Pamoja na ukweli kuwa mwenza wako anatarajia utakuwa muanifu kwake, elewa kuwa kuwa mwaminifu pekee katika mahusiano yako sio tiketi ya kudumu kwa mahusiano yenu kwakuwa watu wanaingia kwenye mahusiano sio tuu kwa kuwa wanataka kuwa na mtu mmoja muaminifu bali wana mahitaji mengine wanayohitaji.
Zungumza na mwenza wako, fanya utafiti wako binafsi kuhusu mpenzi wako ujue mambo mengine anayohitaji toka kwako. 
Pia msikilize anapokutaka urekebishe mambo kadhaa au ufanye mambo fulani. Inapendeza pale unapomfanyia mtu mambo yanayompendezesha kwa kuwa hivyo ndivyo anavyotaka, sio kwakuwa tuu wewe unadhani kufanya hivyo kutampendezesha mhusika.
Share:

WATAKA KUPOTEZA MUDA NA KUINJOI ONLINE ? TEMBELEA WEBSITE HIZI

Wanasema kazi na dawa, hivyo kuna wakati mtu unaweza kujisikia kujipumzisha na kupitia mitandao mbalimbali ili 'kupoteza muda'. Basi kama una lengo hilo, tunakupa leo hii orodha ya website 10 ambazo tunaona kweli zinaweza kutimiza hitaji lako hilo.
Fuata link ya websites hizi:
1. http://grouchyrabbit.com (Vituko na mawazo ya kijinga jinga)

2. http://www.thesartorialist.com ( Mambo ya Fashion zaidi)

3.http://www.anthropologie.com ( Fanya ‘window shopping’ ya nguo, vitu na vitu vingine vikali vikali duniani. 

4.http://awkwardfamilyphotos.com ( Picha za matukio ya kustaajabisha ya kifamilia)


5.http://www.reddit.com ( Habari na Maoni ya watu mbalimbali. Waweza changia pia maoni yako !)


6.http://www.postsecret.com ( Soma siri za watu mbalimbali wakieleza mambo yao ya ndani waliyoamua kuweka wazi)


7.http://www.sporcle.com ( Hii ni maalum kwa ‘games’ – michezo mbalimbali ambayo pamoja na kupoteza muda, itakuacha pia ukijifunza mambo mbalimbali.


8.http://iwastesomuchtime.com ( Hapa unapata vituko, picha, na mambo mengine mengine yote ya kupoteza muda ambayo pengine haujawahi kufikiria.


9.http://www.buzzfeed.com ( Kwa habari mbalimbali zenye kujibu mambo kadhaa ambayo watu wengi wanadadisi. Utapata pia picha na vituko vingine.

10.http://www.quora.com ( Ni website ambapo maswali mbalimbali yanajibiwa, waweza pia uliza swali lako ukajibiwa). Mfano wa maswali yaliyowahi kujibu QUORA ni: What are some of the most mind-blowing facts?
Share: