VIDEO: USIMAMIZI WA ‘PUBLIC RELATIONS’ UMEKUWA ‘INSHU KUBWA’

Si ajabu umeshasikia vyeo vifuatavyo afisa mahusiano, msemaji wa timu, afisa mawasiliano, n.k. Hivyo ni baadhi ya vyeo vinavyoelenga katika kusimamia mahusiano ya asasi na jamii yake. Hata hivyo fani ya usimamizi wa mahusiano na jamii (Public Relations Management) haijapata umaarufu sana ukilinganisha na fani nyingine kama vile udaktari, uhasibu, masoko, na uhandisi, ingawaje kwa kiwango kikubwa usimamizi wa mahusiano na jamii ndio mhimili wa uhai wa asasi husika. Katika makala hii tunaangalia maana ya mahusiano na jamii na manufaa ya kuzingatia usimamizi ulio bora wa hayo mahusiano.


Share:

HII NI KWA WAJASIRIAMALI WA SASA NA WATARAJIWA. Part 2

Leo tunaendelea na makala yetu ya mambo ya msingi kwa kila mjasiriamali kuyatilia maanani ili kuweza kuwa na mafanikio endelevu. Elewa tunaposema mafanikio endelevu tunamaanisha kuwa ni zaidi tuu ya kupata wateja leo, na kesho, bali uwezo wa kuendeleza biashara kwa miaka mingi kwakuwa mjasiriamali anaweza kumudu changamoto na matatizo yanayojitokeza katika fani hii ya ujasiriamali. Tuangalie sasa points zilizobaki , yaani 6-11:-

6. Kujenga Mtandao sahihi na kuutumia
Tunasema kujenga mtandao sahihi na kuutumia, na sio tuu kuwa na mtandao wa watu wasio na tija kwako kwakuwa pengine hawana cha kukupatia, au wewe mwenyewe hauna maono ya jinsi ya kuutumia mtandao wako. Chunguza vizuri mtandao wako unaweza kukuta wapo wateja wako watarajiwa, wapo watu wanaoweza kukuuzia bidhaa, wapo watu wanaoweza kukupa ushauri bora wa kiundeshaji, wapo watu wanaoweza kukusaidia kifedha au hata watu wanaoweza kukuunganisha na watu wengine ambao watakuwa na tija kwako. Ni kweli kuwa hakuna mtu ‘asiye wa umuhimu’, unatakiwa kuwaheshimu watu wote, lakini pia ujue jinsi ya kutenda kazi zako na watu ili hata wale wanaoonekana kuwa ‘sio wa muhimu’ waonekane wa muhimu. Hata hivyo waepuke wale wanaokurudisha nyuma au wanaoweza kukurudisha nyuma.

7. Mahusiano na wateja
Biashara yako ni sehemu ya maisha yako, basi hata wateja nao ni sehemu ya maisha yako na ya biashara yako, hivyo ni muhimu kuweka mahusiano yenye tija na wateja husika.  Mahusiano ya wateja yanaanza kabla hata hajanunua bidhaa toka kwako, iwe kupitia utafiti wako wa soko – kutambua kwa undani mambo ya msingi yanayoweza kukufanya uuze bidhaa yako. Mahusiano yanaendelea pale mteja anapokuja kununua bidhaa kwako, na hayaishi  tuu hapo anaponunua bidhaa bali yanaendelea kwani ukiboresha mahusiano yako na mteja , anaweza kurudi tena kununua bidhaa toka kwako atakapohitaji, au anaweza kuwaambia watu wengine. Lakini pia mahusiano mazuri na wateja yanakuwezesha kujua namna unavyotakiwa kuboresha shughuli zako pamoja na bidhaa zako. Hivyo jifunze kusikiliza kwa ufasaha malalamiko ya wateja na kuyafanyia kazi, jitahidi kufuatilia taarifa zinazokuwezesha kujua hisia zao kuhusu biashara yako. Katika kujenga mahusiano bora na wateja, ni muhimu basi kuwa na mfumo mzuri wa kukusanya na kutumia taarifa zinazohusu mwenendo wa wateja wako. Kuna program maalum za kompyuta zinazokuwezesha kukusanya taarifa za wateja, hata hivyo waweza fuatilia mitandao ya kijamii kama Facebook ili kutambua tabia, mabadiliko na mitazamo ya wateja wako. Weka wazi mifumo ya kuwasiliana na wateja wako, mfano wateja waweze wasiliana nawe kwa barua pepe, simu, kuonana ana kwa ana, au hata kwa kuweka maoni yao katika kisanduku cha maoni.

8. Mahusiano na wanaokuuzia bidhaa/huduma
Unajenga mahusiano bora na wanaokuuzia bidhaa au huduma ili  kupata manufaa ya punguzo la bei, kuweza kukopeshwa bidhaa baadae,  na pia kuweza kutambua mabadiliko au maboresho kwa upande wa wanaokuuzia bidhaa /huduma  ambapo mabadiliko au maboresho hayo yanaweza kuathiri uendeshaji wa shughuli za biashara yako. Mfano, chukulia kampuni X unayoitegemea kwa ajili ya kupatia bidhaa fulani ambazo wewe huwa unauza , mara ghafla unapata taarifa kuwa imesitisha utengenezaji wa bidhaa zake, hivyo kujikuta wewe una athirika kwani ulikuwa unatarajia kupata bidhaa hizo toka kwake, na haukuwa umejipanga kifedha kununua kwa kampuni nyingne ambayo kwa kawaida huuza bidhaa kwa bei ya juu zaidi.  Laiti kama ungekuwa unafuatilia taarifa za kampuni husika unayoitegemea , ungekuwa tayari umejipanga iwe kununua kwa muuzaji mwingine kwa bei ya juu, au hata kufanya utafiti wa kutosha wa sehemu nyingine ya kununua bidhaa husika kwa bei nafuu.

9. Makubaliano /mikataba
Kuna mikataba au makubaliano kadhaa ambayo mjasiriamali utakutana nayo kama vile makubaliano na watu unaotaka kushirikiana nao kuanzisha biashara, makubaliano na wateja wako, makubaliano na wafanyakazi, makubaliano na wanaokuuzia bidhaa/huduma n.k.  La msingi hapa ukumbuke kulinda maslahi yako, na uhakikishe unaelewa vema vipengele vyote vya makubaliano, na ikibidi makubaliano hayo yawe katika maandishi na yashuhudiwe na mwanasheria. Hakikisha mfano wewe na washirika wako wa biashara mnakubaliana kuhusu mgawanyo wa majukumu yenu, jinsi mtakavyogawana faida, jinsi mtakavyo suluhisha migongano mbalimbali, jinsi mtakavyochangia mtaji wa biashara na namna ya mfumo wa uongozi wa biashara yenu.  Wengi huacha kuweka mikataba kwa kuwa tuu eti wanaaminiana. Kama wewe ni mmoja wao unaofikiria hivyo, tambua kuwa mkataba sio kwa sababu ya kutoaminiana, bali ni namna ya kuweka msisitizo wa kuelewana kwenu, na pia mnataka mambo yenu yaende vema, na inapotokea kutokuenda sawa, basi muwe na pa kuanzia katika kutafakari  jinsi ya kuboresha mambo yenu.

10. Utafiti
Kabla ya kufanya maamuzi ya msingi katika biashara yako kama vile kuajiri wafanyakazi wapya, kununua mashine mpya, kuzalisha bidhaa au huduma mpya, ni muhimu  sana kuwa na uchambuzi usio na mashaka unaotetea maamuzi yako ya kufanya hivyo unavyotaka kufanya.  Uchambuzi huo ndio tunaouita utafiti. Fanya utafiti kuhusu mfanyakazi unayetaka kumuajiri – mfano kupitia interview, kuwasiliana na waajiri wake wa awali, kutafuta historia ya maisha ya mfanyakazi mtarajiwa n.k. Hii itakuwezesha kujua kweli mfanyakazi au wafanyakazi unaoajiri kweli wataweza kutimiza yale unayokusudia wafanye. Hali kadhalika, unapotaka kufanya shughuli za kimasoko, inabidi ufanye utafiti ili kutambua kama kweli shughuli hizo zitaendana na hali ya soko, na kama kweli zitaleta tija kwako. Kumbuka rasilimali ulizonazo ni chache , hivyo ni muhimu uwe na nidhamu katika kuzitumia, na njia mojawapo ya kuwa na nidhamu ni kufanya utafiti kama kweli matumizi yako ya rasilimali yataleta tija. Utafiti sio lazima uwe wa gharama kubwa, waweza fanya utafiti kwa kusoma tuu makala na habari mbalimbali toka vyanzo tofauti, au kwa kuongea na wateja/wafanyakazi.

11. Usimamizi wa taarifa
Wataalamu wanasema katika ulimwengu wa teknolojia tulio nao sasa, mafanikio ya biashara yanachangiwa  na aina bora ya taarifa ambazo wamiliki/watendaji wa biashara wanazo, na ambazo wanaweza kuzitumia. Taarifa hizi ni kama vile mwenendo wa wateja, mwenendo wa wafanyakazi, mwenendo wa washindani wa biashara, mwenendo wa mabadiliko ya teknolojia, mabadiliko ya kijamii, na kisiasa n.k. Mjasiriamali inabidi uwe na uwezo wa kuendana na wakati kwa kupata na kutumia taarifa sahihi ili usiachwe nyuma na washindani wako, au wateja wasikukumbie kwakuwa haukidhi mabadiliko wanayoyahitaji.
Share:

HII NI KWA WAJASIRIAMALI WA SASA NA WATARAJIWA part 1

Wengi wetu tuna ndoto za kujiajiri na kufanya biashara. Au pengine tumeshajaribu kufanya ujasiriamali lakini tunajikuta tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele kimafanikio. Je, ni nini hasa kinafanya  wengine wafanikiwe katika ujasiriamali na wengine wasote na hata kukimbia ujasiriamali ? Katika makala hii tunaangalia mambo muhimu 11 ambayo kama mjasiriamali atayazingatia ataweza kujikuta  anakabiliana na changamoto za ujasiriamali na hatimaye kuwa na mafanikio endelevu.

1. Malengo  na mikakati ya muda mrefu:
Ni kweli kuwa lengo kuu la ujasiriamali ni kuingiza ziada ya mapato ili biashara iweze kujiendesha, kupanuka, na kuwalipa ipasavyo waanzishaji au muanzishaji wa biashara.  Hata hivyo, haitoshi tuu kutamani  kuwa na biashara kubwa bila kuwa na mikakati ya kufikia huko.  Hivyo ni muhimu kuweka bayana , ikiwezekana katika maandishi malengo ya muda mrefu ya biashara yako , na ufafanue mambo utakayotakiwa kufanya kufikia huko, aina ya watu unaotakiwa kuwa nao ili kufikia huko, mfumo wa uendeshaji unaotakiwa kuwa nao ili kufikia huko unakotaka kufikia, na uhakikishe pia watendaji / wafanyakazi ulio nao wanalielewa hilo.

2. Malengo na mikakati ya muda mfupi mfupi:
Malengo na mikakati  ya muda mrefu haitoshi, inabidi uweke pia malengo ya muda mfupi mfupi. Mfano malengo ya muda mrefu yanaweza kuwa ni malengo ya miaka mitano ijayo, ila inabidi uweke malengo ya muda mfupi mfupi, mfano malengo na mikakati ya kila mwezi, malengo ya kila robo ya mwaka, malengo ya kila mwaka n.k .
Kumbuka pia kuwa , kwasababu kuna mabadiliko ya mara kwa mara katika jamii, teknolojia , mazingira ya biashara n.k inabidi uwe tayari ku ‘adjust’ malengo na mikakati yako ili iendane na mabadiliko hayo.

3. Sheria zinazoongoza biashara:  
Ni muhimu kwa mjasiriamali, kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu sheria za nchi na taratibu zinazosimamia shughuli husika kwani kutokutambua sheria vema, kama vile sheria za kodi, sheria za vibali vya biashara, sheria za uandikishaji wa biashara kunaweza kumfanya mjasiriamali kuingia gharama zisizotarajiwa na zisizo na sababu. Mfano kushindwa  kwa mjasiriamali asiyetunza vitabu vyake kwa mujibu wa maelekezo ya sheria za kodi anaweza kujikuta anapata faini au hata biashara yake kufungiwa. Kwa kampuni kutokupeleka kwa msajili wa makampuni taarifa za kila mwaka za maendeleo ya kampuni ( Annual Return) kunaweza kuwa na matokeo ya faini zisizo na sababu. Pia kwa mjasiriamali aliyeajiri wafanyakazi kadhaa inabidi afahamu vipengele muhimu vya sheria zinazosimamia mikataba ya kazi kwani  mfano mfanyakazi anapofukuzwa bila kupewa ‘notice’ ya muda unaotakiwa kisheria,  mfanyakazi huyo anaweza kudai fidia, na pia kuna aina nyingine ya malipo ambayo mfanyakazi anapaswa kulipwa wakati ameachishwa kazi. Hivyo kama mjasiriamali hakujiandaa ipasavyo kufanya malipo hayo, hali ya kifedha ya biashara inaweza kutetereka.

4. Mipango na mikakati ya fedha
Ni muhimu kwa mjasiriamali kutambua namna ya kusimamia vema maswala ya fedha , kwani bila lengo ni kupata mapato yanayoleta ziada, na ili kupata mapato ni lazima kuingia gharama kadhaa. Hivyo mjasiriamali lazima awe na mbinu sahihi za  kudhitibi matumizi ili kweli matumizi  hata kama ni madogo basi kweli yalete ziada ya kutosha kwa biashara. Mjasiriamali inabidi adhibiti matumizi kwa kuweka miongozo imara ya jinsi biashara yake itakavyolipia gharama fulani, aweke mikakati ya jinsi ambavyo atahakikisha kweli mapato yote yanajulikana, na yanawekwa kwenye maandishi, na aweke mikakati ya jinsi ya kutunza taarifa za fedha. Ziwepo mbinu za kuchochea mapato makubwa , na shughuli za kimasoko zinazoendana na hili zisimamiwe kwa ufanisi, mfano kutoa punguzo la bei, kutoa ofa mbalimbali kwa wateja,  kutoa zawadi n.k vyote hivyo vinaweza kutumika kuchochea mapato, hata hivyo ni muhimu kuwepo muongozo sahihi wa mambo hayo, ili kweli yalete ziada ya mapato.


5.Masoko
Ni muhimu mjasiriamali atambue maana halisi na mbinu bora za kufanya shughuli za kimasoko (marketing). Shughuli za masoko hazianzi pale tuu mjasiriamali anapokamilisha bidhaa yake, hivyo anaanza kutafuta wateja. La hasha, shughuli za kimasoko zinajumuisha utafiti wa nini wateja wanataka, wanataka kivipi, na wanaweza kulipia kivipi, na wapate wapi bidhaa husika.  Kuelewa wateja vema ni shughuli ya kwanza na ya muhimu kwa kila mjasiriamali. Kisha mjasiriamali anazalisha bidhaa inayoendana na matakwa ya wateja (mfano bidhaa iendane na ujazo unaohitajika na wateja, aina ya radha inayotakiwa na wateja, rangi na muonekano unaotakiwa na wateja n.k). Kisha baada ya kuwa na bidhaa sahihi , mjasiriamali anaweka bei inayoendana na soko , bei hiyo pia iendane na mikakati yake mingine ya kibiashara, halafu anafanya shughuli za kuwataarifu wateja bidhaa yake husika,  na sio tuu kuwataarifu, bali mjasiriamali ni lazima atutumie mbinu za kuwafanya kweli wateja waone wanahitaji bidhaa husika kutoka kwake yeye mjasiriamali.

Tutaendelea na points nyingine kesho....
Share:

PASSIVE AGGRESSIVE: AINA YA TABIA INAYOWATESA WENGI

Inakera sana unapomuambia mtu afanye jambo fulani na ukitarajia alifanye kwa ufanisi wa kiwango fulani, ila matokeo yake ni kinyume kwakuwa mtu huyo pengine asifanye kabisa au akafanya jambo hilo kwa kiwango duni  tofauti na uwezo wake. Pia inakera inapokubidi urudie rudie kumueleza jambo mtu , na mtu huyo haonyeshi kukubali kubadilika ili kufanya unayomuelekeza. Hali hii huwwasababishwa na mambo mengi ikiwemo tabia ya passive aggressive.

Passive aggressive ni aina ya tabia ambapo mtu huonyesha ukaidi usio wa moja kwa moja, badala yake hutumia vitendo kuwasilisha ujumbe wake wa kukataa jambo fulani.
Mfano , mtu anapewa kazi afanye na anatakiwa kuikamilisha kwa muda fulani, ila mtu huyo anapinga kufanya kazi hiyo, lakini hataki kueleza kupinga kwake kwa mtu aliyempa kazi. Badala yake atakubali kazi, lakini hatoifanya kwa muda uliopangwa,au kwa ufanisi unaotakiwa.

Watu wenye tabia ya passive aggressive, huwa tunawaita wakaidi, hata hivyo wao wenyewe ukiwadadisi kuhusu wayafanyayo kama kweli wanafanya kwa makusudi  hawatokubali , watatoa sababu mbalimbali kama vile kusahau, kutokujua, kufikiria sivyo ndivyo, n.k.

Wataaalamu wa tabia wanasema tabia ya passive aggressive hutokana na udhaifu wa watu wenye tabia hiyo kutokuweza kujielezea, kuwa na hofu ya kujieleza, au kutaka kufanya ushindani . Hii inamaanisha kuwa watu hawa wana mapungufu katika uwezo wa kuwasiliana vema na watu watu wengine.

Wataalamu wa tabia, wanaongeza pia kuwa tabia hii ya passive aggressive huchangiwa na mambo mengi ikiwa pamoja na malezi ambapo mtoto hapewi nafasi ya kuelezea hisia zake.Pia uwezo wa kutotawala hasira na kutokuweza kuelezea hasira, mara nyingi huwa tunasema ‘kubaki na jambo moyoni’.

Mambo mengine yanayochangia tabia hii  ni kutokuwa na uwezo wa kuchambua tatizo husika ambalo mtu anakumbana nalo, hivyo kujikuta anabaki kulaumu wengine au kuona wengine ndio chanzo cha matatizo , uwezo mdogo wa kutambua na kukubali mapungufu binafsi na kuwajibika kutokana na hali ya maisha inayomkumba mtu.

Hitimisho:
Tumeona kuwa tabia ya passive aggressive inakera sana, na inarudisha nyuma maendeleo hususani kama unamtegemea mtu afanye jambo halafu yeye ndiye ana tabia ya passive aggressive , basi itakuwa ‘imekula kwako’. 
Kwa wale ambao wana tabia ya passive aggressive, wapo kwenye hatari ya kupoteza kazi kwani hakuna bosi anayetaka  kuwa na mtu anayepinga maamuzi . Tabia ya passive aggressive ni mbaya pia hata kwa mahusiano na watu wengine ikijumuisha mpenzi  wako, kwani inakera na mtu hawezi kuendelea kuvumilia tabia kama hiyo inayojirudia rudia.
Kama una tabia ya namna hii njia rahisi ya kujirekebisha ni kukubali kwanza kuwa tabia hii ni tatizo. Jifunze kujieleza kama unahisi huwezi kufanya jambo fulani. Pia heshimu mtazamo wa wengine  na usiweke mtazamo hasi kila unapoambiwa  jambo.
Share:

BUSARA HII KATIKA MATUMIZI YA MUDA INA MANUFAA MAKUBWA

Kuna  sababu nyingi zinazotofautisha watu waliofanikiwa na wasiofanikiwa, lakini zaidi sana sababu ya utofauti huo ipo katika MUDA. Ndio, sababu ni MUDA,  muda toka mtu ameamua kutenda anayohitajika kutenda ili afanikiwe, muda ambao mtu anaweza kuvumilia, muda ambao mtu ameamua kupoteza bila kuwa na mkakati maalum, muda unaotumika kufanya jambo la msingi, Muda wa kusubiria wakati muafaka wa kufanikiwa kwako utimie n.k. Makala hii inachambua namna unavyoweza kujiongoza vema kutumia muda ili kuleta mabadiliko chanya katika maisha yako.

Jambo la msingi zaidi kwanza: 
Hii inaonekana ni rahisi kusema kuliko kutenda kwa sababu wengi wetu hukumbwa na kigugumizi katika kutambua jinsi ya kupanga mambo yetu kwa ngazi za umuhimu ili lile la muhimu zaidi au la msingi zaidi lianze. Matokeo yake ni kujikuta tunatumia muda mwingi kufanya mambo machache yasiyo na uzito mkubwa kwetu,  na kuyapa muda mdogo yale mambo yaliyo na uzito hasa kwetu. Kanuni rahisi ya kukuweza kupanga mambo kwa ngazi za umuhimu ni kupima mambo kwa vigezo vifuatavyo:-

Uwezekano wa kuhairisha jambo: Je ni lazima jambo husika lifanyike muda huu ? Je inawezekana kuliahirisha na kufanya baadae ? Je athari za kuahirisha ni zipi ?
Linganisha faida za sasa na za baadae : Je, jambo hili na lile lipi litakunufaisha zaidi sasa ? Je lipi litakunufaisha baadae ? Pia linganisha faida ya sasa na faida ya baadae, jambo lipi linakupa faida zaidi?
Linganisha rasilimali zinazotakiwa kutumika : Jiulize jambo lipi linatumia zaidi rasilimali kuliko nyingine, na je unaweza kufanikisha kwa ufanisi zaidi jambo gani kwa kutumia rasilimali unazoweza kupata.
Hivyo basi , kanuni hii ya kufanya jambo la msingi zaidi kwanza, inatuhitaji tusiwe watu wa kukurupuka, badala yake tuwe wachambuzi wa maisha na yale tunayokumbana nayo ili tujipange vema. Wengi wetu hujipa moyo kwa kusema, “aah lakini hili jambo nifanyalo ni la muhimu”. Wakati kinachotakiwa ni kufanya ‘la muhimu ZAIDI’

Muda ulivyo tabibu: 
Kuna msemo usema “ unaposhinda, mheshimu uliyemshinda,  na unaposhindwa pia mheshimu aliyekushinda”.  Msemo huu una maana kubwa sana kuwa muda ni dawa au tabibu wa mambo mengi. Wapo wengi waliokuwa matajiri wameporomoka, na wapo wengi waliokuwa masikini wamekuwa matajiri. Hivyo kwa wewe uliye katika hali duni , usijione kuwa basi hapo ulipo ndio mwisho. Kumbuka muda ndio kila kitu, na kwakuwa muda bado upo, wewe unao uwezo wa kubadilika na kuwa juu, ukiweka nia, na juhudi ya dhati.  Kwa wewe ambaye upo na maisha ya kuridhisha, usiwadharau wengine, hata wewe ni muda tuu ndio unakufanya ujihisi hivyo ulivyo. Huu ni muda wako, kwani hata wewe , au waliokufanya hapo ulipo nao walikuwa na muda wa kusota.

Kila jambo ni tokeo la juhudi na muda uliotumika:  Kutana na bwana PM, mwenye umri wa miaka38, kwa sasa anasoma masomo ya ngazi ya cheti  katika chuo kimoja binafsi jijini Dar es salaam. Bwana PM alipomaliza kidato cha nne, hakufaulu, na hakukuwa na uwezo katika familia yake ya kumpeleka masomo ya ziada. Alikaa mtaani kwa miaka kadhaa ,kisha baadae akapata kibarua na kufanya kazi kwa miaka kadhaa. Mara kwa mara alijikumbusha azma yake ya kujiendeleza, lakini kila wakati akawa akijiambia hayupo tayari. Miaka imepita na sasa ana familia ya watoto wawili, kisha anafikiria kuwa inabidi aonyeshe mfano kwa watoto wake kwa kujiendeleza kusoma.  Alifanya mitihani ya ku resit na akapa credit za kumfanya aendelee masomo ya cheti. Bwana PM amefikia hapo alipo kwa juhudi zake mwenyewe na muda alioutumia. Kama angefanya maamuzi mapema ya kuanza kujisomesha, hivi leo angejikuta yupo mbali, kwani yeye mwenyewe anasema miaka 6 nyuma alikuwa anapata kipato cha kutosha kujiendeleza kusoma, ila alidhani hakuwa tayari kusoma.

Picha kubwa ya maisha:
Fikiria kwa muda mfupi, aina gani ya maisha ulikuwa ukipenda uishi, je ni hayo uliyo nayo sasa. Je, unadhani hapo ulipo ndipo ambapo ulitamani kuwa miaka 5 au 10 iliyopita? Je, mke au mume , au mpenzi uliye naye, ndio wa aina ile uliyowahi kuifikiria na kujiambia kuwa utakuja kuwa na mtu wa aina hiyo ? Majibu kwa walio wengi wetu ni kuwa, vile tulivyo leo, vitu au watu tulionao karibu, maeneo tunayoishi, kazi tunazofanya, n.k sio vile ambavyo tuliwaza kuwa navyo. 
Hata hivyo, sio kwamba maisha yamefikia mwisho. Hata kama hatujafikia vile tuliwaza au kutamani kuwa, ni wazi kuwa maisha yanaendelea, na tuna imani ya kufanya makubwa zaidi. Hili ni somo kubwa sana kuwa hatuna haja ya kujiona ni bora zaidi ya wengine, kuwadharau wengine, au kuwakatisha tamaa wengine hasa pale tunapodhani   ‘tumekwisha toka kimaisha’ kwakuwa hata hivyo tulivyo leo sio kwamba tulifikia kwa mikakati au formula ya aina moja. Pengine tunao waona wapo chini yetu, ni kwamba nao wanapitia na kujaribu mikakati fulani fulani ambayo mingine itafanikiwa, mengine haitofanikiwa. Wengine hawafanikiwi kwa sababu ya watu kama wewe unayewaangalia walio chini yako kama  ‘washindani ‘ wako kimaisha, wakati kiukweli  kila mtu ana picha ya peke yake ya kutoka kimaisha.

Imani na matendo:
Jambo la msingi ni kuamini kuwa unaweza kutimiza hilo unalolitaka. Imani peke yake haisaidii, fanya matendo hasa yanaendeana na imani yako. Huwezi kumkuta padri anaswalisha msikitini wala shekhe anaswalisha kanisani, kwakuwa Imani na Matendo havitokuwa sawa, hivyo basi usitegemee kama imani yako ni kufanikiwa, lakini matendo yako – ikiwa pamoja na kule kusoma kwako, mikutano yako na aina ya watu ulio nao karibu haviendani na yale unayotamani kuwa.
Share:

USIPITWE NA MABADILIKO HAYA YA TEKNOHAMA

Maendeleo katika teknolojia ya mawasiliano hususani kwa vifaa vya matumizi ya mkononi kama vile simu yanazidi kuongezeka. Tunapoelekea ni kuwa watabaki watu wachache sana watakaotumia kompyuta za mezani (desktop computer), na hata laptop zinaelekea kupungua watumiaji, badala yake, watu wanaingia zaidi katika matumizi ya kompyuta ndogo na zinazohamishika toka sehemu moja kwenda nyingine. Katika makala yetu ya leo tunaangalia maendeleo makubwa tunayoyatarajia katika teknolojia ya mawasiliano:
Spidi kubwa ya mawasiliano:  Katika kurahisisha mawasiliano, wataalamu wamegundua teknolojia ya  LTE ( Long Term Evolution) ambayo pia huitwa 4G (4th Generation) ambayo ndio inayoelezwa kuwa tegemeo la kuifanya dunia iwe na mawasiliano ya kasi kubwa zaidi na kutokana na uwezo huo, basi vifaa vingi vitaweza kuunganishwa kupitia internet, na zaidi sana kuwezesha simu kufanya matumizi mengi ambayo yanafanyika sasa kupitia kompyuta kama vile kuangalia movie, kudownload movies hata za ukubwa wa 2GB, au hata kuangalia Youtube, n.k. Soma zaidi kuhusu teknolojia ya LTE katika makala yetu kwa kubofya hapa.

Kuchaji simu bila kutumia waya:
Makampuni kadhaa kama vile ZTE, Google , AT & T, Starbucks na Nokia yamewekeza katika utafiti wa kuwa  na teknolojia itakayowezesha watumiaji wa simu kuchaji simu zao bila ya kuzichomeka ukutani . Kwa taarifa zilizopo kwenye mtandao wa Youtube, tayari Nokia wameshatoa simu zinazoweza kuchajiwa bila waya (wireless charging). Simu hizo za Nokia ni Nokia Lumia 920 na Nokia Lumia 820. Kampuni ya LG pia imetoa simu zake za LG Nexus 4 zinazotumia teknolojia ya wireless charging.

Website maalum za kuonekana kwenye simu:
Katika mabadiliko haya tunayoendana nayo ambapo watu wengi zaidi watatumia simu kuliko kompyuta, kuna haja basi ya kuwezesha websites ziwe na muonekano kama wa kwenye kompyuta za kawaida kwa watazamaji watakaotumia simu. Website hizo huitwa Mobile website. Kumbuka , kwa website kuwa Mobile website sio kwamba tuu eti inaweza kuonekana kwenye simu, hapana bali inakuwa imetengenezwa maalum kuwa na muonekano bora kwenye simu.
Pia tazama muonekano wa MBUKE TIMES blog kwa mobile version yake, hapo chini.
Kushoto ni mobile version, na kulia ni Mbuke Times ya 'kawaida' yaani haijatengenezwa bado maalum kwa kuonekana kwenye simu
Hitimisho
Mabadiliko yote haya yanamaanisha kuwa maisha yetu yanaenda kubadilika sana. Kuna ajira mpya na kuna watakaopoteza ajira au wateja. Mfano program mpya zinaendelea kubuniwa ili kurahisisha  matumizi ya simu ikiwa ni pamoja na kuwezesha simu kutype documents, kusave, kuprint, kama ambavyo watu wanafanya kwa kutumia desktop computer au laptops. Kwa wabunifu na watengenezaji wa website, wanatakiwa wajiboreshe katika kujua mabadiliko haya makubwa kwani tayari kuna muongozo wa jinsi ya kuprogram website ziendane na teknolojia za simu.
Wamiliki wa website na blogs wataanza kwa wingi kubadilika kuelekea kutumia teknolojia itakayofanya websites na blogs zao zionekane vema kupitia simu.

Waweza jisomea zaidi:
ZTE commits to wireless mobile charging

Nokia Wireless Charging

Five Mobile Technology Trends to watch in 2013

8 Tools to create mobile version of your website

Standards for web applications on mobile from WC3.
Share:

KWANINI INASEMWA PAPA MPYA ANAMILIKI TIMU YA SOKA?

Jina la timu ni San Lorenzo de Almagro, maskani yake ni Buenos Aires, huko Argentina. Timu hiyo inapatikana kwa website ifuatayo www.sanlorenzo.com.ar . Kisa cha watu kusema timu hii inamilikiwa na papa mpya, Papa Francis, ambaye jina lake halisi ni  Jorge Mario Bergoglio, ni kutokana na ukweli kuwa Papa Francis, ni mmoja wa wajumbe wa umoja unaomiliki timu hiyo, na yeye mwenyewe ana kadi ya uanachama wa timu hiyo.

Zaidi sana, hivi karibuni baada ya Papa huyo mpya kutangazwa, timu hiyo kongwe iliyoanzishwa rasmi kama klabu mwaka 1908, ilianza kutumia jezi maalum zenye picha za Papa huyo.
San Lorenzo de Almagro, pamoja na kushinda mataji 10 makubwa katika ligi daraja la kwanza huko  Argentina, haijawahi kushinda mashindano makubwa ya kimataifa,achilia mbali mashindano ya bara la America ya kusini. Ndio maana Lucas Roldan, mshabiki wa timu pinzani ya Boca Juniors amenukuliwa na nesn.com akiibeza San Lorenzo kuwa , kuchaguliwa kwa Papa huyo , ndio ushindi wa kipekee wa kimataifa wa timu ya San Lorenzo.

Timu ya San Lorenzo de Almargo, inahusishwa na kanisa katoliki kwakuwa hapo mwanzo vijana walikuwa wakicheza mitaani, lakini padri Lorenzo Massa, aliwaonea huruma vijana wa mitaani hivyo akawaita wacheze kwenye uwanja wa kanisa, na inasemwa kuwa yeye mwenyewe padri Lorenzo, ambaye baadae alikuja kutangazwa kuwa Mtakatifu, aliwahi kununua magoli ya uwanja huo, na alikuwa akiwafundisha dini wachezaji hao.

Habari hii ni kwa uchambuzi  toka:
www.nesn.com
Share:

ZITAMBUE NAFASI ZA KAZI 'FEKI' ZA ONLINE

Umekua ukitamani kupata nafasi ya kufanya kazi, na kwa bahati nzuri siku isiyo na jina unapofungua inbox ya email account yako  unakutana na habari ya nafasi ya kazi , ambayo kiukweli inavutia kama barua pepe hii hapa:

“MARRIOTT HOTEL CANADA HAS EMPLOYMENT OPPORTUNITIES FOR AN EXOTIC
CANDIDATES IN DIFFERENT SKILLS,SEND YOUR CURRENT CV/RESUME AND APPLICATION
LETTER IN MICRO SOFT. (marriothotel_cn@hotmail.com)”

Bila shaka jambo la kwanza utakalofanya ni kutafuta wapi CV yako ipo, kisha fasta unatuma hiyo CV, ukisubiria wakujibu kwa kukueleza pengine aina ya kazi unayoweza kuapply.
Jambo la msingi unapopata email kama hiyo sio kuharakisha kuijibu. Email zozote zenye kueleza ‘ofa’ fulani ni vizuri kufanya uhakiki kabla ya kuzijibu. Kuna nafasi za kazi feki kama hizo hapo, na zaidi sana kuna matapeli wengine wa kwenye mtandao humu wanaoweza kukuingiza mjini kwa jinsi mbalimbali iwe kwa dili la kupata schorlaship, vyuo, misaada ya fedha n.k.
Email nyingine za nafasi za kazi feki zinaweza kuwa na maneno kama:

"After registering your Direct Deposit confirmation, please respond back to this email with your ideal interview date/time. Remember, you need your Direct Deposit account info prior to your interview, as we will be processing your payment information at that time."

Mbaya zaidi ni kuwa, kuna wakati unaweza kweli kutuma CV, yako ukajibiwa ujaze fomu ambayo inapatikana katika website fulani. Hapo kuna mawili, moja ukajikuta ukiwa kwenye hiyo website yako ya kujaza fomu, ukahamishwa na kupeleka kwenye website nyingine itakayokuwa feki. 

Au pili ukafanikiwa kweli kujaza fomu na hata ukapata kazi, ambayo ni kazi ya kufanya kwa mtandao. Baada ya wiki moja au mbili au hata mwezi kampuni hiyo unayofanya kazi ikakuambia imekutumia hundi. Na kweli ukapata details zote za hiyo hundi. Ila baada ya muda wakasema wamefanya makosa, katika kiasi fulani, hivyo inabidi urudishe kwa kumtumia mtu mwingine ambaye walikuwa wamemlenga. 

Hata hivyo ukweli ni kuwa hizo hundi walizokutumia ni feki, na kwamba utakapotuma fedha zako binafsi, ukiwa unasubiri kwa hamu kupokea mshiko wako, utajikuta unaambiwa na benki yako cheki ni feki.
Jihadhari, kumbuka msemo wa kiingereza usemao “ If a deal is too good to be true, think twice”. Usione haya kushurikisha wengine, ukiona email kama hizo. Uchoyo wa kuwaambia watu vitu unavyohisi ‘dili’ unaweza kukuponza.

Utazitambua nafasi za kazi feki kwa mambo kadhaa kama yafuatavyo:

  • Zinahitaji wewe kutanguliza malipo fulani

  • Zinahitaji maelezo yako binafsi ya kifedha- mfano namba ya akaunti yako ya benki

  • Ukitafuta kwa kutumia Google mfano, hauoni website ya kampuni husika inayotoa ajira

Share:

ATAKAYELETA MAENDELEO YA KWELI BONGO

Tanzania kama taifa, tuna matatizo mengi yanayosababisha kuwa na maendeleo duni, mojawapo ya matatizo hayo ni:
 
1. Kutokukubali kuwa yawezekana sie wenyewe mmoja mmoja ni sehemu ya tatizo, badala yake tupo na bidii ya kuwaonyesha wengine vidole badala ya kuchukua hatua ya kujirekebisha sie wenyewe kwa kiwango cha mapungufu yetu. 
Mfano, mtu analalamika hakuna fursa za kutosha za biashara, ila hafanyi utafiti wa kutosha wa biashara , kuboresha ufahamu wake, kutafuta wataalamu haswa wa fani husika, au hata kutafuta ushirika na wafanyabiashara wengine, badala yake anamaliza waganga wa kienyeji.

2.Wengi wetu tumesha 'surrender' kwa udhaifu wetu na udhaifu uliopo katika jamii yetu, tunajionea 'poa' tuu. Si ajabu kusikia mtu akisema  ''aaa, ndio bongo yetu hiyo, tumeshajizoeleaga utumbo huu".
Unaenda ofisi ya mtu, au hata baa, unapata huduma mbovu, haulalamiki, haukosoi, unaishia tuu kusema....aaa hii ndio bongo.

3.Tunajadili zaidi matatizo kuhusu suluhu ya matatizo. Na zaidi sana, wengi tunashindana katika namna tunavyolifahamu tatizo. Ikifika kuchukua maamuzi, na utekelezaji. Tunakuwa na visingizio kibao. 
Ni kama ile habari ya Panya kumkamata Paka, wakafanya mkutano wamkamate, ugumu ukaja namna ya kuanza kumshambulia paka. Nani aanze kumfuata.! Wakaishia kutegeana. 
Hata waliposema twendeni wote kwa pamoja, kila mmoja akawa anasita kuwa mwengine anaweza asiende halafu 'ikawa imekula kwake'.

4. Wengi wetu tunajali sana faida ya muda mfupi, kuliko faida ya muda mrefu. Hivyo hata katika kujiajiri binafsi, hatufanyi vema, hatuna biashara au asasi endelevu. Na kwakuwa tayari tuna mapungufu haya, tunaogopa hata kuwasaidia wenzetu kwani tunaishi kiushindani zaidi, na ushindani wenyewe ni wasasa zaidi sio wa muda mrefu. 
Kuwa na EGO, ni kuzuri, ila EGO, inayokuangamiza na kudidimiza mambo endelevu hata ya kwako binafsi kweli ni tatizo.
Hili swala la kujali faida ya muda mfupi lipo hata kwa wanafunzi, hususani wanafunzi wa asasi za elimu ya juu. Badala ya kutilia maanani kuelewa kwa undani mambo wanayojifunza, kutafuta ujuzi na kubobea katika mambo fani zao, wapo baadhi huwa wameshajiandaa kumaliza tuu, kupata cheti, au kwa lugha rahisi ya mtaani 'gamba'. Hivyo elimu anayoipata mtu, haimsaidii kujiajiri, hamsaidii kubuni mikakati ya kujikwamua kutoka katika hali aliyonayo.

5. Wengi wetu tunafikiria zaidi yale tusiyokuwa nayo, badala ya kufikiria tunatumiaje yale ambayo tayari tunayo. Kijana aliyemaliza elimu ya chuo kikuu, anawaza kuwa hawezi kupata kazi kwakuwa tuu hana 'refa', au hawezi kujiajiri kwa kuwa hana mtaji. Hata hivyo kijana huyo huyo, amesahau kuwa kama anao uelewa wa kutosha wa mambo aliyosomea, anaweza kuomba kujitolea kwa asasi kadhaa zilizopo, au kwakutumia marafiki zake ambao anachat nao kila siku kwa mtandao angeweza kufanya mambo ya msingi. Yeye mwenyewe pia angeweza kubuni jambo ambalo lingeonyesha kweli ana uwezo wa kipekee wa fani yake, hivyo 'kuforce' kukubalika katika soko la ajira. Kijana huyo anayelalamika hana ajira wala hawezi kuanza ujasiriamali, ameacha kutumia vema mikutano anayohudhuria iwe shughuli za kidini, za kiukoo, au hata sherehe za marafiki, kutafuta wadau wanaoweza 'kununua' ujuzi wa kipekee alionao kijana huyo. Hata huko kutafuta kazi, amekuwa akitafuta kazi kwa njia moja tuu, ya magazeti. Amesahau kuwa mitandao ya kijamii, kuenda moja kwa moja kwa waajiri, kutumia mawakala wa ajira, na hata kujitolea kwa asasi fulani kungeweza kumsaidia kufanya mabadiliko.

6. Wengi wetu tunasubiri mabadiliko ya pamoja. Kama mfano hapo juu wa paka na panya, wengi wetu tunafahamu matatizo tuliyonayo katika nchi yetu, tunafahamu hata sababu ya kuwepo kwa matatizo hayo, hata hivyo tuna kila sababu ya kujiona hatuwezi kuchukua hatua sisi kama sisi mmoja mmoja. Kwa mtazamo wa wengi , suluhu ya matatizo yetu itatokana na maamuzi ya wengi, itatokana na serikali, itatoka kwa chama fulani. 

Kwa tafakari hiyo hapo juu, MBUKE TIMES inaamini kuwa pamoja na kuwa wapo wadau wengi wa kuleta maendeleo katika nchi yetu, kuna mtu wa pekee wa kuleta maendeleo ya kweli, maendeleo endelevu katika nchi yetu ya Tanzania. Mtu huyo ni WEWE.
Jiulize unafanya nini kushinda mapungufu yako, unafanya nini kuzuia mambo yasiyo yasiyoleta maendeleo ,yanayoharibu jamii yetu ? Unalalamika kuhusu wanawake na kuporomoka kwa maadili nchini, ila wewe ndio unatoa kipaumbele kuweka picha za utupu za wanawake katika akaunti yako ya Facebook na kwa blog yako.
Share:

JINSI YA KUWA NA JINA NA NEMBO (LOGO) KALI

Unapofikiria kuanzisha biashara au asasi ya aina yoyote, kuna mambo mawili makubwa ni lazima uyaamue kwa usahihi ili kukuza umaarufu wa shughuli yako, na pia kuleta hamasa kwa wafanyakazi wako. Mambo hayo mawili tunayoyazungumzia katika makala hii ni JINA na NEMBO (LOGO).
Wataalamu wa masoko na mahusiano ya kijamii, wanataja mambo yafuatayo kuwa ya msingi katika kuamua nini hasa jina au nembo ya biashara au asasi yako viwe:-

Taswira unayotaka kuijenga kwa jamii: 
Jina na nembo huwakilisha vile ambavyo watu wanatakiwa wafikirie kuhusu asasi yako. Mfano jina kama Studio Mastered Sound (SMS) la kampuni ya kutengeneza headphones la 50CENT inalenga kuipa jamii taswira kuwa bidhaa za kampuni hiyo zina ubora wa juu wa sauti katika kutumia hizo headphones za kampuni ya SMS Audio.
Pia ukiangalia nembo ya shirika la usambaji wa vifurushi la FedEx, utaona katika ya E na X kuna alama ya mshare, hivyo kuashiria uhakika, umakini na uharaka wa wasafirishaji hao wa vifurushi.
Au pia angalia nembo ya duka kubwa la mtandaoni la bidhaa mbalimbali liitwalo AMAZON. Angalia kamshare kahiyo nembo inaonyesha toka A mpaka Z, hivyo kutaka jamii iamini kuwa kuna website hiyo ina kila aina ya bidhaa unazotaka kununua ukiwa mtandaoni.
Waweza pia jifunza kutoka katika nembo ya Volkswagen, yenye herufi V na W. Herufi V inawakilisha Voks – Watu, na neno  Wagen maana yake gari. Hivyo nembo inamaanisha Gari la Watu. Lengo hapa ni kuiambia jamii kuwa kampuni hii inalenga katika kutengeneza magari yenye kutimiza haswa mahitaji ya watu.

Mambo ya msingi ya kiutendaji unayotaka watendaji wajue:
Majina na logo pia hutumika kueleza mkakati wa muda mrefu wa asasi husika na kutoa maelekezo kwa wafanyakazi au watendaji kuhusu mambo ya msingi ya kufuata ili kufikia malengo ya kampuni. Mara nyingi hii huendana na muono wa waanzishaji wa asasi au biashara husika.
Mfano, kwa mujibu wa vyanzo vya habari vilivyonukuliwa na wikipedia, jina Toyota lilichaguliwa na waanzishaji wa kampuni maarufu ya kutengeneza magari ya Toyota Motor Corporation ya Japan, kama kielelezo cha jinsi walivyotaka kutofautisha biashara yao na mambo yao binafsi – kwani jina la familia ya wamiliki waanzishaji wa Toyota Motors Corporation ni TOYODA na hapo kabla magari yao yaliitwa Toyoda, ila kwakuwa Toyoda inamaanisha kilimo cha mpunga, wakaamua kuitofautisha kwa kuita TOYOTA, neno ambalo pia linamaanisha bahati, hivyo kuonyesha . Hivyo badala ya kuita TOYODA wakaamua kuita Toyota. Hali hii inamaanisha kuwa watendaji walitakiwa wawe na uelewa wa kuwa TOYOTA inaenda kuwa kampuni kubwa zaidi na inaenda kufanya mabadiliko makubwa ya kiteknolojia, na kwamba ni jambo kubwa kufanya kazi katika kampuni hiyo (bahati).
Nembo ya TOYOTA inayoonyesha vijiduara vitatu, vinavyowakilisha mteja, bidhaa na teknolojia na fursa zisiyo na kikomo. Hivyo watendaji wanatakiwa kuzingatia mambo haya katika kuleta mafanikio ya mteja.

Urahisi wa jina au logo kukumbukwa:
Ni muhimu kwa jina kuwa rahisi kukumbukika vichwani mwa watu, ndio maana kuna majina kama Google, Yahoo,  Adobe, Microsoft, Apple, Toyota, Sony, Nokia, VODACOM, MTN, n.k. Mbinu rahisi ya kufanya jina likumbukike ni kuhakikisha unakuwa na jina fupi. Ndio maana jina kama ADOBE, jina tuu la mto unaopita nyuma ya nyumba ya Mwanzilishi wa kampuni hiyo John Warnock ya ADOBE. Aliamua kuiita hivyo ili kurahisisha kutamkika na kukumbukwa. Au chukulia mfano jina ADIDAS, linatokana na jina la mmiliki wa kampuni hiyo Adolf (Adi) Dassler.

Upekee na Mvuto: Ili kuvutia watu kuangalia na kujua zaidi kuhusu asasi yako, ni vema kuwa na jina na nembo ya kipekee na yenye mvuto.

Hitimisho la makala hii ni kuwa, inabidi tutambue kuwa nembo na majina yanabeba mambo mengi ya msingi katika uendeshaji na mafanikio ya asasi husika. Hivyo wamiliki wa biashara au asasi nyingine zisizo za kibiashara ni muhimu wachukue maamuzi sahihi katika kuchagua nembo na majina. Rangi na mambo mengine kama vile michoro ya nembo inawakilisha mambo kadhaa ya msingi. Hata kama unampa mtu kazi ya kubuni jina au nembo ya asasi yako, ni vizuri kuwa na ufahamu huu kuwa nembo na jina utakalolipata kweli lisadifu malengo makuu, uendeshaji wa asasi yako , na iwe rahisi kukumbukwa. Hii inajumuisha pia majina ya blog, websites, na hata barua pepe.
Share:

MAUJANJA YA MSINGI KATIKA MICROSOFT WORD 2010

Inawezekana unaandika taarifa ndefu yenye kuhitaji uweke  namba za kurasa tofauti ili kuleta mvuto na uelewa fasaha wa taarifa husika. Mfano ungependa kurasa zinazoonyesha Yaliyomo (Table of contents) , Shukrani (Acknowledgement), Orodha ya vifupisho ( List of abbreviations) , na Ufupisho wa taarifa (Abstract), n.k  ziwe na namba za kirumi (I, ii, iii,n.k), halafu sura (chapters) za taaarifa yako ziwe katika namba za kiarabu/namba za kawaida yaani 1, 2, 3, …nk.

Makala hii inaangalia jinsi ya kuweka page numbers za kirumi na pia za kawaida, mfano ukurasa wa kwanza mpaka wa tano ziwe (i) –(v), halafu kurasa zinafuata namba zianzie 1, 2, 3,……n.k.

Tuchukulie mfano unataka kuwa na page numbers za kirumi kwa ukurasa wa kwanza mpaka wa tano, unachotakiwa kufanya nenda hadi ukurasa wako wa tano,  chini ya huo ukurasa wa tano, weka cursor mwisho kabisa wa maneno yote, kisha ingia PAGE  LAYOUT, halafu chagua, Breaks, halafu bofya sehemu ya  Section Breaks iliyoandikwa Next Page.

Baada ya kubofya hiyo section break ya Next Page ,  nenda moja kwa moja kwenye Insert, kisha Page Numbers, na kuchagua chaguo la Bottom ili namba zako zikae chini ya kurasa. Kisha bofya style unayotaka number iwe, bila shaka unataka namba ikae katikati.

Ukishapata page number iliyokaa kati, sasa unahitaji kufanya mabadiliko kidogo ya hiyo namba ili iwe ya kirumi. Kufanya mabadiliko  nenda  sehemu ya Format Page numbers kama unavyoona katika picha. 

Unaweza kuipata sehemu ya  Format Page numbers kwa kubofya pia INSERT kisha PAGE NUMBERS, halafu angalia katika menu zinazotelemka, utaiona hiyo Format Page Numbers.
Ukiwa katika Format Page Numbers ,  angalia menu  Number format, kisha chagua namba za kirumi, na kubofya OK.

Hapo tayari umeweka namba zako za kirumi toka ukurasa wa kwanza mpaka wa tano. Ili kuendelea na mtindo mwingine wa namba yaani 1, 2, 3, ….. kwa ukurasa unaofuata yaani ukurasa wa SITA, na kuendelea, nenda ukurasa wa sita, au wowote ule baada ya huo wa tano, kisha bofya INSERT, halafu PAGE NUMBERS, kisha fanya uchaguzi kadri utakavyo kama namba hizo zikae juu au chini, na kama zikae pembeni kulia, au katikati. Ukishafanya uchaguzi, bofya OK, na hapo tayari kazi yako imeisha.
Share:

KUTOKA KUAJIRIWA MPAKA KUJIAJIRI: MAMBO 8 MUHIMU YA KUZINGATIA

Kuna sababu mbalimbali kwanini mtu atake kuajiri, badala ya kuajiriwa, mfano kipato kidogo anachopata katika kazi husika, hitaji la kutaka uhuru zaidi binafsi wa kufanya kazi, hitaji la kuweza kutoa ajira kwa wengine na zaidi sana kuweza kutumia vema kipaji na uwezo wa kuzalisha ambao katika kazi ya sasa mtu hapati nafasi ya kufanya hivyo.  
Kujiajiri ni jambo linalohitaji maandalizi ya muda mrefu na kuna mambo ya msingi kuyafahamu, haiwezekani tuu , ukaacha kazi na kusema ok, acha nijiajiri.
Makala hii inachambua mambo ya msingi ya kujiandaa na kuyafahamu kabla mtu hajaamua kuacha kuajiriwa.
 
Mkakati ni muhimu: Wazo au ndoto isiyo na mkakati wa kuitimiza ni upuuzi yaani ndoto hiyo au wazo hilo halina maana, hivyo basi ndoto yako ya kujiajiri siku moja, ni lazima iwekewe mkakati wa kuifanikisha ikiwa ni pamoja na muda hasa wa lini utaitimiza hiyo ndoto. 
Katika kuweka mkakati huu wa kutimiza ndoto yako, fanya utafiti wa kina kuhusu mipango yako binafsi ya maisha, mtazamo wako kuhusu maisha, mpenzi/mke wako, familia yako, na hali ya jamii kwa ujumla inavyoenda kama vile mabadiliko ya hali ya kisiasa, teknolojia, na uchumi. 
Tengeneza malengo ya aina ya shughuli unayotaka kuifanya ukiacha kuajiriwa, na pima uwezekano wa shughuli hiyo kufanyika kweli na kama itakulipa. Utambue pia aina ya watu na rasilimali nyingine utakazozihitaji, na jinsi utakavyozipata.

Unahitaji fedha: Ndio, unahitaji kiasi cha fedha za kutosha kununua vifaa na malighafi za kutengenezea bidhaa yako. Pia unahitaji fedha za kuwalipa wafanyakazi wako, na zaidi sana , unahitaji fedha za kuendesha maisha yako na familia yako , kwa kipindi fulani kabla ya biashara kuanza kukulipa mshahara. Hivyo kabla haujaacha kibarua chako, hakikisha umetengeneza bajeti ya kutosha na una akiba ya kutimiza mahitaji ya bajeti yako. Usingependa uache kazi halafu uanze kuwa omba omba kwa rafiki na jamaa, au uanze kujuta.

Network ni muhimu: Kumbuka katika kujiajiri kwako, utahitaji wateja, washirika, wafanyakazi na hata washauri mbalimbali ili mambo yako yaende vizuri. Hivyo, wakati ukiwa umeajiriwa ndio wakati wako muafaka wa kutengeneza na kupanua wigo wako wa watu unaowafahamu na waliokaribu nawe.
Kumbuka kuendeleza mawasiliano kwani watu hawapendi kuona wewe unataka kuwatumia tuu kisha unawatupa. Endeleza mawasiliano walau hata kwa salamu tuu. Zaidi sana, heshimu watu wote, hata usiowafahamu au wale unaodhani 'sio watu muhimu'. 
Jenga taswira nzuri kwa jamii kwa lugha fasaha, picha na matukio mengine, usifanye watu wakufikirie vibaya.

Usipitwe na wakati: Hakikisha kuwa unafuatilia taarifa za matukio, dili na watu wanaohusiana na aina ya shughuli unayopanga kuifanya wakati utakapojiajiri. Hii itakusaidia kupata uzoefu na kusoma alama za nyakati, na pengine kutambua fursa nyingine zaidi. 
Endelea kujifunza zaidi kuhusu kazi yako, watu na jamii kwa ujumla kwani kujiajiri kunahitaji uzoefu zaidi, na zaidi sana uwezo wa kupambana na changamoto nyingi ambazo nyingine haujawahi kukutana nazo kabisa, ila taarifa za awali na kujua jinsi mambo yanavyoenda kwa ujumla katika jamii vitakufanya ushinde changamoto.

Maana halisi ya biashara: Baada ya kuacha kuajiriwa, hautarajii kuwa mtu wa ‘kuganga njaa’ yaani kufanya biashara ili mradi tuu hela iingie, lakini haujui mwelekeo wa biashara yako upoje, na wala hakuna mkakati wa kuikuza na kuimarisha biashara husika. 
Biashara inahusu kutimiza mahitaji ya watu, kwahiyo ili mradi utakuwa na uwezo mkubwa wa kutimiza mahitaji ya watu, na kuendelea kuhamasisha watu zaidi kuja kwako uweze kutimiza mahitaji yao , basi biashara itakua, na itaendelea kuwa endelevu. 
Kinyume cha hapo, ushindani utakutoa katika biashara kwani wateja watakambilia kwa wengine. Biashara sio tuu kupata wateja, ni vile kuweza kuendelea kupata wateja na kuendelea kupanua biashara. 
Inabidi uipende shughuli husika unayoifanya, na uweze kutimiza mahitaji ya wateja kupitia biashara husika. 
Muda wako mwingi utautumia katika shughuli yako mpya utakayojiajiri hivyo, kama ambavyo kazi uliyonayo pengine ‘inakuboa’, hakikisha ajira yako binafsi ‘haikuboi’.

Umuhimu wa wafanyakazi: Watendaji wa shughuli husika za biashara yako utakayoianzisha ni muhimu wawe wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha wa kufanya shughuli husika, na uweke mikakati ya kuwapatia nyenzo zote muhimu za kufanyia kazi ikiwemo teknolojia na mazingira mazuri ya kazi. Hivyo basi wakati unajiandaa kujiajiri tilia maanani hili katika bajeti yako ya kuajiri. Usingependa wafanyakazi wao wajisikie vibaya kama vile wewe ulivyojisikia vibaya katika ajira yako fulani (pengine ajira yako ya sasa). Muda huu ambao umeajiriwa, ndio muda pia muafaka wa kusaka 'vipaji'- yaani watu ambao utafanya nao kazi utakapojiajiri.

Inakuhusu wewe : Mafanikio yako katika kujiajiri yanategemea mambo mengi ila zaidi sana yanakutegemea wewe. Je, nini hasa sababu yako ya kutaka kujiajiri? 
Ni kweli una bidhaa au huduma haswa ya kupeleka sokoni itakayokufanya iendeshe maisha yako na kuiendeleza biashara husika au ni hasira tuu za jinsi bosi wako anavyokuchulia hapo ofisini kwako, au kwakuwa mshahara uliopo sasa haukutoshi. Je, mipango yako mingine ya maisha ipoje? 
Ndoto zako za kusoma, au kuishi sehemu tofauti tofauti, pengine mkoa mwingine tofauti na uliopo sasa, au pengine hata nchi husika. Je, yote hayo yanaathiri vipi mipango na mikakati yako ya kujiajiri, bila kusahau msukumo toka kwa familia yako.

Ndoto sahihi: Ni kweli kuwa upo sahihi kufikiria au kuota kufanya biashara kubwa na yenye mafanikio sana, lakini kumbuka mafanikio hayaji kwa usiku mmoja, na hata kama yatakuja kwa usiku mmoja, inahitajika kazi ya muda mrefu kuyafanya yawe endelevu. 
Hivyo basi, usingoje wakati ‘muafaka’ wa wewe kuwa na kiasi kikubwa cha fedha au kwamba ‘umeyaset’ vema mambo yote. 
Anza kidogo kidogo, kubali kufanya makosa, na tambua kuwa hata kama utafanya uchambuzi na uchunguzi wa kutosha kuhusu soko, jamii na teknolojia, hali halisi unayoenda kukumbana nayo inaweza kuwa tofauti na ile uliyojifunza wakati wa uchambuzi au uchunguzi wako kwakuwa hicho unachoenda kufanya ni kipya hakikufanyiwa uchambuzi, bali unakifanya kutokana na uchambuzi uliofanya hapo awali. 
Kuna mtu mwingine atakuja kutumia makosa au mafanikio yako kupanga mambo yake.
Share:

ILIVYO KUSAFIRI KWA BARABARA DAR- JOBERG (AFRIKA KUSINI)

Hakuna shaka kuwa Afrika Kusini ndio nchi iliyoendelea zaidi katika bara la Afrika. Pengine ungependa kuitembelea ili kujionea ilivyo hasa mji maarufu wa Johannesburg. Makala hii inachambua mambo kadhaa unayoweza kukumbana nayo kama utasafiri kwa njia ya barabara hususani kwa njia ya kupanda mabasi kutoka Dar es salaam hadi Johannesburg aka Joberg aka Egoli. Mojawapo wa sababu za kusafiri kwa basi  ni kujionea kwa macho nchi nyingine kama vile Zambia, Msumbiji, au Zimbabwe. Wengine hufikiria swala la kupunguza gharama ya nauli kwa kupanda  basi badala ya kupanda ndege ambayo ni gharama zaidi. Makala hii inaangalia safari ya Dar-Joberg kupitia Harare, Zimbabwe.

Siku za kusafiri:  Safari nzima kutoka Dar es salaam mpaka Joberg ni ya siku nne(4). Siku nne hizo ni kama ifuatavyo, kutoka Dar- Harare, Zimbabwe siku tatu, na kutoka Zimbabwe mpaka Joberg ni siku moja. Kumbuka kuwa sio kwamba siku zote hizo basi litakuwa likitembea. Kuna muda wa mapumziko ya msosi, kuchimba dawa, na masaa kadhaa ya kusubiri abiria wagonge mihuri ya viza kwani basi likifika mpakani husimama na kuwataka abiria wote washuke ili waweze kukaguliwa. 
Wakati mwingine abiria hutakiwa kushusha mizigo yao yote, hata iliyopo kwenye buti ili ikaguliwe. Hivyo muda mwingi hupotea wakati basi halitembei.

Nauli: Kwakuwa hakuna basi la moja kwa moja kutoka Dar es salaam mpaka Joberg, tarajia kulipa nauli ya Dar es salaam – Harare, Zimbabwe, halafu kutoka Zimbabwe unapanda basi lingine la moja kwa moja hadi Joberg. Hata hivyo unaweza amua kupanda Dar  - mpaka Lusaka, halafu kutoka Lusaka ukaamua kupitia nchi nyingine mfano ukaingia kwa Afrika Kusini kwa boda ya Msumbiji. Makala hii inajadili njia ya kupitia Harare Zimbabwe.
Kutoka Dar – Harare, Zimbabwe waweza lipa kwa fedha za kitanzania au kwa dola, kuendana na makubaliano yako na watu wa mabasi pale Ubungo Bus Terminal. Nauli ya Dar – Harare ni kati ya Dola za Kimarekani 80 -100. Wakati nauli ya Harare, Zimbabwe mpaka Joberg, Afrika Kusini ni kati ya Dola za Kimarekani 50-100 kutegemeana na msimu wa mwaka, kwani wakati wa sikukuu bei hupanda sana. Hivyo kwa hesabu za haraka haraka kwa makadirio ya juu, nauli kutoka Dar-Joberg ni jumla ya Dola za Kimarekani 200 ila inaweza kuwa hadi Dola za Kimarekani 150. Kumbuka hii ni nauli ya kwenda tuu.

Fedha za kigeni: Nchi tofauti zina sarafu tofauti hivyo jiandae kutumia sarafu tofauti kufanya manunuzi ya mahitaji yako ukiwa nchi husika. Mfano kwa nchini Zambia utatumia KWACHA, ukiwa Zimbabwe, sarafu kuu ya kutumia ni Dola ya Kimarekani, wakati utakapoingia nchini Afrika Kusini sarafu kuu ni RAND.
Unaweza kusafiri na kiasi chako cha kutosha cha fedha za kigeni za nchi tofauti kama tulivyotaja hapo juu, au ukaamua kuenda kununua kiasi cha fedha za kigeni unachohitaji utakapofika katika nchi husika. Mfano ukiwa Lusaka Zambia, utaweza kununua KWACHA kwa wauzaji wa fedha za kigeni hata pale pale kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Lusaka. Sio tuu KWACHA, waweza nunua pia hata Dola za Kimarekani. Waweza pia fanya manunuzi ya fedha za kigeni ukiwa Harare, Zimbabwe au hata Joberg katika maduka ya mabadilishano ya fedha za kigeni.

Vyakula na Gharama zake:  Katika nchi zote utakazotembelea tarajia kukuta vyakula unavyovifahamu kama vile ugali, wali, chipsi, kuku na nyama , hivyo usiogope sana kwamba hautopata misosi unayoipenda (Hata hivyo radha na mapishi vinaweza kuwa tofauti na vya bongo). Vinywaji pia vipo vya kawaida, kama soda na bia, hata hivyo pamoja na ukweli kuwa safari ni ndefu,  hauruhusiwi  kunywa bia ukiwa kwenye basi. Nchini Zimbabwe unaweza kupata msosi mzuri kwa kuanza Dola za Kimarekani 8-15, pia waweza lipa kwa RAND ukiwa Zimbabwe. Nchini Zambia unahitaji walau KWACHA 35000. Ukiwa Afrika Kusini , msosi wa kawaida unaweza kupata kwa RAND30 na kuendelea. Kumbuka msosi hapa unajumuisha na kinywaji pia.
Menu katika mojawapo ya mgahawa nchini Zambia

Mambo ya Uhamiaji:Kati ya mambo yanayochosha katika safari ya Dar- Joberg ni kuvuka mipaka ya nchi ambapo utatakiwa kuonyesha hati ya kusafiria (passport) ili igongwe muhuri wa viza. Kwanza kuna mpaka wa Tanzania na Zambia, halafu  kuna mpaka wa Zambia na Zimbabwe, na hatimaye kuna mpaka wa Zimbabwe na Afrika Kusini. Ni lazima uwe na passport halali ya nchi yako ili uweze kuionyesha  igongwe muhuri wa VIZA, na zaidi sana inabidi uwe na kadi ya chanjo ya homa ya manjano.  Pia tambua kuwa ukifika mipakani  kuna muda mrefu wa kusubiri mpaka passport yako ipate kugongwa muhuri. Unaweza kujikuta umesimama kwenye foleni ya mpakani kwa muda hata wa Masaa Matatu! Pia tarajia vurugu au hali ya kutokuwa na subira ya wasafiri wengine wakati wa kusubiri. Kwa bahati nzuri hakuna malipo kwa mtanzania kuingia au kutoka nchini Afrika Kusini, isipokuwa usizidishe siku 90 za kukaa kwako nchini humo.

Mambo ya Lugha: Lugha inayotumika sana na abiria wengi kutoka Dar es salaam mpaka Zambia ni Kiswahili kwani wengi wao ni Watanzania au watu kutoka Zambia ambao wanajua jua kwa kiwango walau kidogo jinsi ya kuzungumza kiswahili. Unapoingia Zimbabwe hali inaanza kubadilika kwani wengi hapo huzungumza Kiingereza kama lugha kuu ya Mawasiliano. Hata hivyo ukiwa stendi kuu ya mabasi utaweza kuona waTanzania wengine waishio Zambia au wafanyao kazi kwenye mabasi kutoka Tanzania kama vile Tawqa na Falcon. Kutoka Zimbabwe mpaka Joberg , lugha kuu ni kiingereza, hata hivyo si ajabu kusikia abiria wengi wakizungumza lugha nyingine zaidi ya kiingereza, mfano Kishona au Kindebele kwani tarajia abiria wengi kuwa ni Wazimbabwe wanaoenda Afrika Kusini. Mambo ya lugha yanaanza kubadilika zaidi utakapoingia Afrika Kusini, kwani yapo makabila mengi, na kuna lugha 11 maalum kwa mawasiliano, kiingereza ni mojawapo tuu ya hizo lugha rasmi.
Wenyeji wengi hutumia lugha zao asili ambazo pia ni lugha rasmi kama vile ki Xhosa, ki Zulu, ki Tswana, ki Afrikans, kiSutu, n.k.

Ukiingia Afrika Kusini: Ni mwendo wa masaa karibu nane hadi kumi kutoka ‘BODA’ ( mpaka) wa Afrika Kusina na Zimbabwe mpaka kufika Mji Mkuu wa Afrika Kusini Pretoria. Kutoka Pretoria, unatumia kati ya nusu saa hadi dakika 45 kufika Joberg.  
 Ukiwa Joberg unaweza bado kutembelea miji mingine mingi maarufu nchini Afrika Kusini kwa kutumia basi, mfano kutoka Joberg- Durban ni masaa Sita hadi Saba. Kutoka Joberg – Cape Town, ni zaidi ya Masaa 24. Kutoka Joberg kwenda Port Elizabeth ni  wastani wa masaa 20. Huduma ya malazi katika nyumba za wageni ni kati ya RAND 250 hadi R400 kutegemeana na eneo.  
Na nyumba za wageni nyingine unaweza kuhitajika kushare room na wageni wengine, yaani unaweza kulipa R250 na kuwekwa katika chumba ambacho mpo wageni wawili au watatu jumla. Kuna hoteli pia ambazo bei zake ni juu zaidi, pengine kuanzia R400 kwenda juu. 
Share:

HISIA KALI ZA MAFANIKIO YA CRISTIANO RONALDO

Story ya mafanikio ya Cristiano Ronaldo iliyosambazwa katika mitandao mbalimbali imekuwa gumzo kwa jinsi ambavyo inagusa hisia za watu wengi. Baada ya kusoma makala hii, jiulize jee unaamini kama kweli Ronaldo mwenyewe alisema maneno haya, na kama alisema nini unajifunza. Ifuatayo ni tafsiri ya maneno yanayodaiwa kuwa Ronaldo ametaja kuwa ni siri kubwa ya mafanikio yake ya kujulikana katika soka:
“Inabidi nimshukuru rafiki yangu wa zamani, Albert Fantrau kwa mafanikio yangu. Tulicheza pamoja katika timu moja katika mashindano ya U-18. Wakati kocha wa Sporting Lisbon alipokuja kuitembelea timu yetu alisema “ Yoyote anayefunga magoli mengi katika mechi atapata nafasi ya kuingia katika academy yetu”
"Katika mechi tuliyocheza, timu yetu ilifunga magoli 3 -0. Mie nilianza kufunga goli la kwanza, Albert akaja kufunga goli la pili, na goli la tatu lilikuwa muhimu sana kwetu.
Albert alikuwa ameshawatoka mabeki na golikipa, nami nilikuwa nyuma yake. Alichotakiwa kufanya yeye ni kufunga tuu, ila alinipatia pasi mie, nikafunga, nikapata nafasi ya kuenda Sporting Lisbon Academy.
Baada ya mechi nikamuuliza kwanini alifanya vile, na akanijibu kuwa “ Wewe ni mchezaji bora zaidi kuliko mie”

Na hata waandishi wa habari walipomhoji Albert nyumbani kwake, Albert alikubali kuwa CR7 alisema kweli. Na Albert akaongeza kuwa siku hiyo aliyomuachia CR7 afunge goli, ndio siku aliyoiacha fani ya soka na akabaki hana ajira mpaka leo.

Waandishi wakataka kujua imekuaje sasa anamiliki nyumba ya kifahari na gari bomba tuu. Na anaonekana kuwa mtu tajiri. Mali zote anapata toka wapi ?. Albert akajibu “Vyote hivi vinatoka kwa Ronaldo”.


N:B
Habari hiyo hapo juu haina uthibitisho wa moja kwa moja toka Cristiano Ronaldo mwenyewe. Website nyingi zinazoandika maelezo hayo, hazielezi wazi Ronaldo alisema lini maneno hayo, ingawaje ni kweli kuwa Ronaldo ana rafiki ambaye kwa sasa hana ajira naitwa Albert Fantrau.
Share: