MOVIE: STARRING BILL GATES, MARK ZUCKERBERG

“Kila mmoja anaweza kufanya ‘Coding’ yaani kuwa na uwezo wa kuandika maelekezo yanayofanya program ya kompyuta ifanye kazi “. Huo ndio ujumbe uliopo katika movie fupi ya dakika 5 na sekunde 44 ambapo mastaringi wake ni Bill Gates, Mark Zuckerberg, will.i.am, Chris Bosh, Jack Dorsey, Tony Hsieh, Drew Houston, Gabe Newell, Ruchi Sanghvi, Elena Silenok, Vanessa Hurst, na Hadi Partovi. Movie imeongozwa na Lesley Chilcott. Itazame video hiyo hapa chini.

Katika ulimwengu tuliopo sasa, fani ya utengenezaji wa program za kompyuta ni muhimu sana kwani ufumbuzi wa suluhu wa mambo mengi ni kupitia kwa kompyuta, ambapo program na website mbalimbali zinaundwa kurahisha mambo.  
Cha kufurahisha zaidi ni kuwa kujifunza ‘coding’ kumekuwa rahisi sana kwani zipo websites nyingi zinazotoa mafunzo hayo bure kabisa. Pia zipo video nyingi kwenye mitandao mbalimbali kama vile YouTube. Website yenye kampeni kubwa ya kufanikisha hii inaongozwa na shirika lisilo la kiserikali la Marekani – CODE.ORG. Bofya hapa kuitembelea website ya shirika hilo.
Masomo yanayotolewa na CODE.ORG yanapatikana katika website iitwayo CODECADEMY.COM
Lengo la Makala hii sio kukufundisha jinsi ya coding, bali kukuhamasisha kuchukua hatua ili nawe uanze kujifunza kufanya coding. Hauhitaji ujuzi mwingine wowote wa ziada, zaidi ya kuweza kiingereza na kuwa na ufahamu wa awali wa mambo yanayohusiana na matumizi ya kompyuta.

Program hutengenezwa kwa kuunganisha maelezo kadhaa ambayo huandikwa kwa kufuata kanuni maalum (syntax) ambapo kanuni hizo maalum hutofautiana kuendana na aina ya ‘lugha’ unayotumia kuandika program husika.

Kuna lugha mbalimbali zinazotumika kufanya ‘coding’ mfano HTML, CSS, Java, Visual Basic, n.k.
Tembelea CODECADEMY.ORG,kwa kubofya hapa ujionee maelekezo ya jinsi ya kuandika codes kwa lugha kama vile HTML, CSS, au JAVA.   
Manufaa ya kuweza coding ni kuweza kupata ajira, au kuweza kuweza kuboresha shughuli zako mfano kama unablog, utaweza kuiboresha na kuiremba zaidi kwa kufanya marekebisho kwa codes mbalimbali. Mfano picha hapa chini inaonyesha jinsi nilivyo ‘cheza’ na codes ili kuongeza menus kwenye blogu hii.

Hapa chini jionee movie ya dakika chache yenye mastar kibao kama vile Mark Zuckerberg na Bill Gates kama nilivyoitambulisha hapo awali.
Share:

USIYOYAJUA KUHUSU FC BARCELONA

Timu ya kwanza (First eleven) ya FC Barcelona inaundwa na zaidi ya 70% ya wachezaji waliokuzwa katika shule ya soka ya timu hiyo maarufu kama La Masia. Hapa ukitaka waweza taja kwa majina РMessi, Fabregas, Xavi, Iniesta, Puyol, Busquets, Vald̩s, Piqu̩, Pedro.

Utegemezi huu wa wahitimu wa La Masia kwa ajili ya First Eleven ni msingi mkubwa katika Falsafa ya Barcelona. Mambo mengine katika falsafa ya FC Barca kama yanavyofafanuliwa na bwana Albert Capellas (Mtaribu Mkuu wa Mafunzo ya soka kwa vijana FC Barca) kama alivyonukuliwa na blogu ya RMC9598.

Uchaguzi bora wa vijana wa kukuza: Barca wanadai wanasaka vipaji vikiwa ‘vibichi’ kabisa toka nchi mbalimbali duniani. Kisha wanawagawa katika makundi ya umri husika halafu kazi ya kuwapika vema inaanzia hapo. Kwa mtindo huu ndipo waliweza kukusanya vipaji kama Messi.


Kujali wachezaji: Katika falsafa ya Barca, kujali wachezaji inamaanisha kuhakikisha wanapata viwanja vizuri vya mazoezi, huduma bora kabisa za matibabu, mawasiliano, na kuwajenga kisaikolojia kuwa Barca ni zaidi ya soka, bali ni sehemu ya wao kuuishi utu wao na kuonyesha thamani ya uhai na maisha kwa ujumla.
Jionee hapa video ya Messi akiwa Mdogo, mechi yake ya kwanza Barcelona.

Muundo wa kitaalamu na shule ya soka ya La Masia: Barca inasisitiza sana mambo ya msingi katika soka kama vile pasi na kumiliki mpira. Mambo mengine yanayosimamiwa ni uwezo wa mchezaji kushambulia, kufunga, na kulinda. Bila shaka ndio maana watu wengi husikika wakisema Barca haina ‘namba’ kwani wachezaji wote huweza kucheza namba zote.
Kwa kusisitiza mambo haya ya msingi kwa wachezaji wote, iwe timu za watoto, hadi timu kubwa Barca imejenga mfumo mmoja tuu wa uchezaji wake. Pasi fupi, wanasonga mbele, pasi wanasonga mbele. Baadhi ya wadau wasoka wameipa jina staili hii ya uchezaji kuwa ‘tik tak’

Staili hii ya ‘tik tak’ ni ya msingi sana kwa Barca na ndiyo staili pekee ambayo Barca nzima iwe ya watoto au ya wakubwa wanajifunza. Ni maamuzi makubwa ya kuamua kutumia staili moja ili kuweza kuboresha mchezo wao. Hata wawe wanaongoza magoli 8-0 au wamefungwa magoli 0-8 Barca wataendelea kutumia staili yao hiyo hiyo.

Falsafa ya Barca inaelezwa katika mambo makuu

Falsafa Namba 1: Timu
Timu nzima inahusishwa katika maamuzi

Falsafa Namba 2: Mafunzo
Kama ilivyoelezwa hapo awali timu zote za Barca zinafuata mfumo mmoja wa mafunzo.
Jionee hapa jinsi walivyo na mfumo mmoja wa uchezaji na ufungaji-  toka under 14.


Falsafa Namba 3: Bwana Mkubwa anajua yote
Kocha mkuu wa Barca ya wakubwa –kwa sasa ni Guadiola na wasaidizi wake wote wanafuatilia muundo na uendelezwaji wa La Masia.

Falsafa Namba 4: Soka Moja
Timu zote zinafuata mfumo mmoja wa uchezaji soka toka U7 hadi timu za wakubwa.

Falsafa Namba 5: Wasifu wa Mchezaji Kwanza
Kabla mchezaji hajachezea timu ya wakubwa ya Barca au kuingia katika shule ya soka ya La Masia ni lazima atambulike kuwa anaweza kufikia viwango vilivyowekwa vya mchezaji wa Barca kwa madaraja mbalimbali.

Falsafa Namba 6: Upokeaji wa wachezaji ulio murua
Kila mchezaji anayepokewa na Barca iwe anaingia timu kubwa moja kwa moja au anaingia kwanza La Masia, ni lazima ahakikishiwe mahitaji yake yote ya msingi kama vile shule, nyumba na mengine ya kifedha yametimizwa. Hii inahusu pia hata familia yake na ndugu zake wa karibu. Mfano mzuri ni kwa Messi, alipochukuliwa na Barca, timu hiyo iliingia gharama zote za matibabu ya gharama kubwa kwa ajili ya Messi, pia timu hiyo inalipia gharama za makazi za familia yake Messi ambapo familia hiyo imehamishiwa Hispania toka Argentina. FC Barcelona pia ilikubali kulipa matibabu ya ugonjwa wa kudumu wa Messi ambapo kila mwezi inagharimu $900 sawa na TZS 1,440,000/=. Messi aliingia FC Barca akiwa na umri wa miaka 11.

Falsafa Namba 7: Kupima wachezaji wadogo
Wachezaji wa timu za vijana/watoto wanapewa nafasi ya kucheza katika timu ya kubwa hata hivyo nafasi hii mwamuzi wa mwisho ni kocha mkuu wa timu ya wakubwa endapo anaona inafaa. Mfano mzuri wa wachezaji waliopewa nafasi hii ni Messi ambaye alipata nafasi ya kuchezea timu ya wakubwa akiwa na umri wa miaka 16 chini ya kocha Frank Rijkaard.

Maelezo Haya kwa Uchambuzi toka: 
www.fcbarcelona.com
www.wikipedia.com 
www.rmc9598.blogspot.com
Share:

UNAPOHISI KUKATA TAMAA YA MAISHA FANYA HIVI

Je, umeshahisi mtu anayehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela anajisikiaje? Je mtu anayefeli mitihani yake ya form 4 ambapo alijituma kwa bidii miaka yote 4 lakini akajikuta anafeli ? Je, umewahi kukata tamaa na kuona maisha ndio yamefika mwisho?. Makala hii inachambua namna ya kuishi kwa matumaini na kushinda hali ya kukata tamaa. 

Niliwahi kuwa jela/gerezani na wafungwa waliokuwa wakitumikia vifungo vyao kwa miaka kadhaa. Ninaposema jela, namaanisha ndani kabisa ya jela, sio nje kama vile kumtembelea mfungwa. Nilikuwa gerezani ila sio kama mfungwa bali kama mwalimu maalum wa wafungwa. Nilistaajabishwa kwa jinsi wanafunzi wangu wafungwa walivyokuwa na matumaini ya maisha. Kwa jinsi ambavyo wanafunzi wangu ambao ni wafungwa walivyokuwa wakijituma waelewe nilichofundisha na jinsi walivyokuwa na hamu ya kupata ujuzi ingawa wengi wao walikuwa bado wanatumikia vifungo kwa miaka mingine zaidi ya mitano.

Novemba 2012, nilipata nafasi ya kuenda kufundisha wafungwa wakiwa gerezani katika gereza moja hapa Afrika Kusini. Ilikuwa ni kuwafundisha jinsi ya kutumia program ya uhasibu iitwayo Pastel. Kwa makubaliano ya gereza hilo na chuo ambacho nimeajiriwa, ilinipasa kutoa masomo kwa wiki nne mfululizo, mara mbili kwa wiki, na kwa siku  ni masaa 2, ambapo nilieleza nadharia ya Pastel Parter V11 na kusimamia matumizi kwa vitendo ya hiyo program. 

Nilitoa mafunzo ndani ya gereza katika chumba maalum chenye ulinzi mkali. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuingia gerezani , niliwahi kuona tuu jinsi ulinzi mkali ulivyo gerezani, ila safari hii nilishuhudia ‘live’. Kuingia huko gerezani ilibidi kupitishwa kwenye mageti sita, ambayo yote yalikuwa yana walinzi waliojizaziti. Baada ya kumaliza somo la siku , nilisindikizwa mpaka nje ya gereza na kuondoka, kesho yake nilifuatwa chuoni  kwa gari maalum la gereza na kuenda kufundisha , mpaka muda wa mkataba ulipoisha nikaacha kuenda gerezani.

Habari ya kuwa gerezani  , uzoefu wa maisha na kujifunza kwa makala na vitabu mbalimbali kumeniweza kutambua mambo yafuatayo kuwa ni ya msingi kwa mtu ambaye anajihisi kukata tamaa. 
Ni muhimu sana kushinda hali ya kukata tamaa kwani ina madhara ya kiafya, kiakili na hata wengine huamua kujiua.

Soma  mbinu zifuatazo za kushinda hali ya kujihisi kukata tamaa:-

Nafasi yako katika kuleta matumaini ya maisha: 
Pamoja na kuwa unahitaji watu wengine kukupa msaada na kushirikiana nao katika mambo kadhaa , wewe kama wewe una nafasi kubwa zaidi ya hao wote ukiwajumlisha. Mfano katika hali hiyo ya kukata tamaa, wewe ndie pekee mwenye uwezo wa kuamua kuwa sasa kukata tamaa basi, na badala yake utafute suluhu ya hilo linalokuumiza, na kama suluhu haiji haraka basi ni bora kulipuuzia jambo husika, kwani kama hauwezi jambo usiloweza kulipatia ufumbuzi , hata ukihuzunika, haisaidii kwani wakati huu unapokuwa umekata tamaa, jambo kubwa unalolihitaji ni ufumbuzi wa hilo tatizo. Hivyo kama ufumbuzi wa tatizo haupo kwa mujibu wa ufahamu wako, basi ni bora kuangalia njia nyingine kuliko kuendelea kuhuzunika.

Tengeneza picha kubwa ya maisha: 
Unapokata tamaa unaweza kujikuta ukichukulia kuwa jambo hilo moja linalokufanya ukate tamaa ndio jambo pekee maishani mwako, na kwakuwa halijaenda vile unavyoona lilitakiwa liende basi maisha yako hayana thamani tena. 
Hata hivyo, fikiria hivi haujui umri wako hasa wa kuishi duniani kikomo chake ni kipi, pengine maisha yako ni miaka 20 au 30 ijayo , hivyo kukata tamaa kwa jambo hili moja hakufai kwani bado una miaka mingine mingi ya kuishi na kurekebisha mambo. 
Pengine ni jambo moja au mawili tuu ndio yanakukatisha tamaa ya maisha, mfano ajira, hasara ya biashara, au kuachwa na mpenzi, hata hivyo ukitengeneza picha kubwa ya maisha utagundua kuwa maisha yako yanaundwa na mambo mengi sana zaidi ya hiyo ajira inayokukatisha tamaa, au huyo mpenzi anayekuumiza kichwa, au wateja/wapinzani wanaofanya biashara yako isiende vyema. 
Utagundua kuwa una muda mwingi wa kurekebisha mambo na kwamba una mambo mengine mengi tuu ya kufanya  na maisha yako ukayaendeleza.

Usijilinganishe:   
Katikahali uliyonayo ya kukata tamaa, kujilinganisha na watu wengi kunaweza kuchochea kukata tamaa zaidi kwani siku zote wapo watu walio na uwezo au nafasi kubwa kuliko wewe, au wenye furaha zaidi kuliko wewe. 
Kumbuka kukata kwako tamaa ni jambo lako binafsi hivyo inabidi utafute ufumbuzi binafsi na sio kujidimiza kwa kujilinganisha na walio na hali nzuri zaidi kuliko wewe. 
Isitoshe maisha ni safari ndefu , hao unaodhani walio bora pengine siku si chache watakuwa wapo chini kimaisha kuliko ulivyo wewe,na zaidi sana kumbuka furaha ni jambo binafsi unaweza kudhani fulani anafuraha kwa kumtazama kwa nje, au kwa vitu alivyo navyo, ila kumbe kiukweli, ana huzuni na pengine anakaribia kukata tamaa.

Kumbuka uwezo wako na sio mapungufu yako:   
Unajpojisikia  kukata tamaa , kumbuka wewe mwenywe ndio ndio msaada mkubwa katika kukabiliana na hali hiyo, na njia kubwa zaidi ya kufanikiwa ni kukumbuka mambo makubwa unayoweza kufanya, na sio madhaifu yako.

Tafuta chanzo (Usijidanganye wala Usijilaumu):   
Kulalamika, kujilaumu hakusaidii kutatua tatizo linalokukabili, au hilo jambo  linalokukwaza. Badala yake tafakari kwa umakini na kwakuwa mkweli wa nafsi yako ili kujua kwanini hasa tatizo ulilo nalo lipo.

Hali ngumu = Fursa ya kuwa bora zaidi: 
Fikiria tatizo lako kama changamoto ambayo inakupa   somo la nini cha kufanya zaidi  ili kurekebisha hali uliyo nayo. Na zaidi sana, utakapoweza kuondokana na hali husika ya kukata tamaa, utaweza kuwa na uzoefu ambao utakusaidia katika siku zijazo.  La msingi fanya utafiti wa makini wa jinsi ya kutatua hali husika, na uchukue uamuzi mapema.                                  

Kumbuka fadhila na mafanikio:   
Katika hali ya kukata tamaa unawezakujikuta unasahau mazuri yote yaliyowahi kukutokea katika maisha yako, na kusahau pia mafanikio ambayo ulikwisha wahi kuyapata katika maisha yako.  Tambua kuwa bado una nafasi ya kuendelea kupata fadhila na mafanikio, kwani uwepo wa tatizo ulilo nalo haimaanishi kuwa milango yote ya fadhila na mafanikio ndio imefungwa.

Zungumza/Omba msaada: 
Usikae kimya na hali yako  inayokukatisha tamaa. Tafuta msaada kwa watu sahihi. Jitahidi kutambua aina sahihi ya watu wa kuwa nao karibu hasa unapokuwa katika hali ngumu ya kukata tamaa kwani baadhi ya watu watakuongezea kukata tamaa.
Share:

JINSI ULIVYO KATIKA HATARI NA VIRUSI VYA KOMPYUTA

Virusi vya kompyuta au tuite Computer Virus, ni program ambazo zimetengenezwa kwa madhumuni ambayo wewe mtumiaji wa kompyuta hauyahitaji ndio maana hata jinsi vinavyoingia kwa kompyuta ni kwa kuvizia kutokufahamu kwako kuwa program hizo zinafanya nini na kwamba zinaingia humo kwa kompyuta. Virusi huingia kwa kompyuta fulani kwa njia mbalimbali mfano kwa kusambazwa kwa email, kwa kusambazwa kwa kutumia flash disk, CD,DVD, au kwa kubofya ‘link’ yenye kubeba kirusi husika kwa kompyuta iliyounganishwa na internet.

Kwanini virusi vipo?
Kuna sababu kadhaa kwanini watu watengeneze Virusi;

Sababu za kibiashara: Baadhi hutengeneza virusi ili waweze kuuza dawa za virusi hivyo (Anti virus), na wengine hutengeneza virusi ili waweze kuua biashara za washindani wao.

Wizi: Baadhi ya watu hutengeneza virusi ili waweze kuiba taarifa fulani fulani za wengine, ikiwemo  password, taarifa za mbinu za kibiashara, taarifa nyingine za kiutendaji na kimaendeleo n.k

Burudani: Wapo baadhi ya watu ambao hutengeneza virusi kama njia ya kujiburudisha , pale wanapoona kuwa ujuzi wao unaweza kutengeneza kitu fulani halisi na kikasumbua watu wengine basi hujisikia raha, na kujiaminisha kuwa wamefanya jambo kubwa.

Uadui:  Baadhi ya virusi hutengenezwa kama njia ya kumuadhibu mtu fulani , hata hivyo kwakuwa virusi husambaa, unaweza kukutwa hata wasio husika na ugomvi au kutokuelewana nao wanajikuta wavipata virusi hivyo. Mfano mie nimekasirishana na ndugu X, nikamtumia email yenye kirusi ndani yake, yeye bila kujua , akaituma kwa rafiki zake, basi rafiki zake wataiona.

Na sasa tambua aina mbalimbali za virusi vya Kompyuta:-

Virus: Jina hili (Virus)  hutumika kueleza aina zote za program zinazosambaa kutoka kompyuta moja kwenda kompyuta nyingine na kuacha madhara toka kompyuta hadi kompyuta. Hata hivyo , virus havisambai peke yake, vinategemea binadamu kuvisadia kusambaa kwa  kupitia njia kama vile kutuma email, kusave files kwa flash disk , au CD na kuenda kutumia kuhamishia mafaili hayo kompyuta nyingine.

Worm:  Hii ni aina ya kipekee ya virusi ambavyo hujizalisha vyenyewe hivyo kuongeza idadi na madhara yake kwa kompyuta.  Kingine kinachoitambulisha Worm ni uwezo wake wwa kusambaa bila msaada wa binadamu. Uwepo wa files au taarifa fulani unatosha kabisa kufanikisha virusi hivi kusambaa. Kwakuwa worm hujizalisha yenyewe hufanya kazi ya kujaza kompyuta , na pia inaweza kuathiri hata usambazi wa taarifa kwa network fulani.

Trojans:  Hii ni aina maalum ya virusi ambayo tofauti na worm, vyenyewe havizaliani, ila huingia kwa kompyuta kwa njia ya kumlaghai mtumiaji wa kompyuta kwa kumfanya adhani kuwa anakubaliana na program nzuri kumbe ndani ya program hiyo kuna hicho kirusi ambacho kinakuja kuleta madhara kwa kompyuta. Hivyo unaweza kujikuta umeingiza program moja nzuri tuu unayoifahamu ila ndani yake kuna hicho kirusi ambacho kinasubiri tuu ubofye sehemu ambayo itakiruhusu kianze kazi zake.

Je, Madhara ya Virusi vya Kompyuta ni yapi ?

Madhara ya virusi vya kompyuta yanategemea na aina ya kirusi husika, yaani madhumuni ya kuundwa kwa hiyo program tunayoiita virus. Mfano:

  • Virusi huiba taarifa fulani fulani na kupatia watu wengine
  • Virusi husababisha usumbufu kwa mtumiaji wa kompyuta kwa kuifanya kompyuta iwe slow,
  • Virusi husababisha files na folders kufichwa au kupotea hivyo kuleta usumbufu kwa mtumiaji
  • Virusi husababisha kompyuta kujaa hivyo kuathiri ufanisi wa kompyuta
  • Virusi husababisha kompyuta kutokufanya kazi kwa sababu zipo program (virus) ambazo huondoa uwezo wa operating system kufanya kazi kwa kufuta mafaili muhimu ya utendaji wa system.
Share:

MAMBO YA MSINGI KUMSAIDIA KIJANA ALIYEFELI FORM 4

Matokeo ya kidato cha nne (form 4) kwa wanafunzi waliofanya mitihani hiyo mwaka 2012 yameishtua jamii ya watanzania waliopo nchini na waliopo nje ya nchi kwa jinsi ambavyo idadi kubwa ya wanafunzi kufeli ambapo zaidi ya 60% ya watahiniwa walipata divisheni sifuli.
Makala hii inachambua nini kifanyike ili kumsaidia kijana mmoja mmoja aliyefeli :

Tulirahisishe tatizo:
Katika maisha yetu kama binadamu tunapitia magumu mengi na mazuri pia. Magumu kama vile kufeli ni sehemu ya maisha , ingawaje huwa yanatuumiza na wakati mwingine tunakata tamaa. Waswahili wanasema maji yakishamwagika hayazoleki,  hivyo basi kwasasa usiumie kichwa  kwa kuwa umefeli badala yake chukulia hiyo ni changamoto ya kutambua udhaifu wako uliokufanya ufeli, au mapungufu mengine ya kifamilia na kijamii. Kumbuka pia maisha ni zaidi ya kufaulu au kufeli mitihani ingawaje kufaulu kunaweza kukaharakisha kufanya mambo fulani, lakini hakumaanishi wala hakukupi uhakika wa furaha na mafanikio ya maisha. Jambo la msingi ni kwa mtu binafsi kutambua kuwa kushindwa jambo fulani hakumaanisha kuwa jambo hilo haliwezekani . Kijana aliyeshindwa kufaulu mitihani ya mwaka jana, haimaanishi kuwa amefeli maisha. Anayo nafasi ya kujijenga sasa, akafanyia marekebisho yale mapungufu aliyo nayo kwani bado umri unadai, maisha hayajaisha bado, anayo miaka zaidi 20 ijayo kuishi hivyo ajipange na kuandaa maisha yake kwa msaada wa familia, jamaa na marafiki.

Nini cha kufanya sasa:

Kuwa mkweli  : Ni muhimu kwa kijana mwenyewe binafsi kutambua mapungufu yaliyosababisha kutokufaulu mitihani husika. Pengine ni kweli kuna magumu ya kijamii kama vile uhaba wa walimu, au magumu ya kifamilia kama vile hali ngumu ya kifedha, ila hizi ni changamoto tuu ambazo zinaweza kutatuliwa ili kuleta utulivu kwa mwanafunzi. Madhaifu kama vile kutokuwa na bidii ya kusoma, kutafuta misaada zaidi, na kujituma hata pale masomo yanapokuwa magumu.

Kujiboresha  katika English:  Somo la English ni kati ya masomo ambayo ni LAZIMA mwanafunzi alimudu vyema  sio tuu kwa sababu inabidi alifaulu ila English ndio msingi wa kuelewa masomo mengine, kwani mwanafunzi ataweza kujisomea vitabu mwenyewe, na pia kuwa na uwezo wa kuandika majibu kwa ufasaha.

Kujiboresha katika Hesabu:  Kujiboresha katika hesabu ni muhimu , sio tuu kwa sababu hesabu ni somo bali kujiboresha katika hesabu kunamfanya mwanafunzi kuwa hodari katika kufikiria, na kuchanganua mambo. Uwezo wa kufikiria na kuchanganua mambo ni muhimu katika kumuwezesha mwanafunzi kuelewa masomo mengine na hata katika kujieleza.

Kujiboresha katika uwezo wa kutafakari (reasoning):  Hii inawezekana kwa mwanafunzi kujihimiza kusoma kwa umakini na kuelewa, kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kutambua mbinu za ziada za maswali na jinsi ya ujibuji.

Kuamua kusoma kwa ufahamu:  Mwanafunzi anatakiwa aamue kwanza kusoma na kwamba adhamirie kuelewa anachokisoma.Maamuzi haya yanasaidia kumfanya awe na usikivu na kujituma hata pale masomo yanapoonekana kuwa magumu.  Waswahili husema: “huwezi kumlazimisha ng’ombe kunywa maji”.

Hitimisho ni kuwa pamoja na kuwa wengi tunaliangalia tatizo la kufeli kwa wanafunzi kama tatizo la kijamii, makala hii inapendekeza kuwa pamoja na juhudi za jumla za kutatua tatizo hili, kuna haja ya kutafuta njia za kumsaidia mwanafunzi mmoja mmoja. Wazazi na walezi ni muhimu wakae na wanafunzi na kutambua changamoto walizonazo, kuwasaidia mara kwa mara, kwani kufaulu au kufeli mitihani ni matokeo ya maandalizi ya muda mrefu, na kwamba familia, ndugu na jamaa wana mchango mkubwa katika kufanya maandalizi ya mwanafunzi yawe bora.
Share:

INTERNET KUWA KWA KILA KITU, KILA MAHALI

Ndio, wanasayansi na wataalamu wa mambo ya mtandao usiotumia nyaya – wireless network wapo mbioni kuhakikisha ndoto ya kufanya vifaa vingi viwe na uwezo wa kuwasiliana vyenyewe kwa wenyewe. Hapo kabla ni computer tuu ndio ziliweza kufanya mawasiliano kwa internet,  lakini miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia hata simu zikitumika kufanya mawasiliano kwa njia ya internet.

Nyuma ya pazia katika mawasiliano haya ya internet, kuna teknolojia zinazofanya tuweze kufanya mawasiliano haya – teknolojia ambazo zimepewa majina tofauti kuendana na toleo husika, na kila toleo la teknolojia ya wireless inaitwa Generation (kizazi) . 
Mfano kuna 1G (1st Generation), 2G ( 2nd Generation), 3G ( 3rd Generation), na hivi karibuni tumeshuhudia kuibuka kwa teknolojia yenye kasi zaidi ya 4G (4th Generation). 

Teknolojia ya 4G, huitwa pia LTE ( Long Term Evolution) ndio inayoelezwa kuwa tegemeo la kuifanya dunia iwe na mawasiliano ya kasi kubwa zaidi na kutokana na uwezo huo, basi vifaa vingi vitaweza kuunganishwa kupitia internet, kitu ambacho watabiri wanakiita “ Internet of Things”.

Zipo tayari simu zenye uwezo wa kuunganishwa na kasi hii ya ajabu ya 4G au LTE, na kama unawaza kununua smartphone, basi wahi fasta smartphone yenye uwezo wa 4G.

Nokia na Siemens kwa mfano wanatabiri kuwa vifaa vingi kama vile magari  na birika za kuchemshia maji/kahawa vitaunganishwa kwa internet. Jionee hapa video ya maelezo kwa ufupi kuhusu LTE:

Share:

BEKA NA MWAJEI: NO. 1

Beka: Hivi Mwaje we fomfoo ulipata divishen gani vile ?

Mwajei: Sisi shule yetu ilifutiwaga matokeo, sijui kwanini, hivi na we ulipata ngapi?.

Beka: Wani ya Saba

Mwajei: Iyo ndo inakuwa ina "A" Ngapi?

Beka: Zamani sana nshasahau "A" ngapi, ila kibao tu! We cha msingi jua mie ndo naleta Ugali hapa home, "A" haziongezagi hata mchuzi kwenye mboga!

          --------------------------------------------------------------------------

Hapo kazi ipo....! 
Share:

MAMBO YALIYOJIFICHA NDANI YA WIMBO 'LEKA DUTIGITE'

Hakika wimbo wa Leka Dutigite, ulioimbwa na wasanii wa bongo fleva, mahiri kabisa nchini Tanzania, ni moja ya nyimbo chache ambazo ukiisikia kwa mara ya kwanza tuu unaupenda. Wimbo huo ni zao la ushirikiano wakali wa bongo fleva wenye asili ya mkoa wa Kigoma, mkoa ambao kiukweli umajaaliwa neema zote kubwa kubwa na ndogo ndogo.   
Kama haujaona basi chungulia fasta video hii hapa chini toka Youtube (hapo chini), utajionea jinsi wakali wa bongo fleva kama vile Diamond, Banana, Chege, wakiporomosha mashairi ambayo kwa hakika utakubali kuwa mzigo huo wa Leka Dutigite kweli umesimama.

Baadhi ya mambo yanayosemwa mitaani kuhusiana na wimbo huo, ambayo kwakweli mengine yana point sana ni kama yafuatayo:


Kabla sijakushushia udaku wa mtaani, kwanza nikudokeze tuu maana ya jina la  wimbo huo. Kwa maana ya mtaani –  jina Leka Dutigite laweza kuwa “ Acha Tule Bata”. Ukiacha  maana hiyo ya kitaa, jina la wimbo huo linaweza maanisha ‘Acha tucheze’, au ‘Acha Tujidai’ au ‘Acha Tujivunie’.


Turudi mtaani, huko mitaani wachambuzi wanasema hivi:


Mosi:

Wimbo umeweza kueleza kwanini Tanzania ni Masikini: Kuna wanaodai eti hata baadhi ya viongozi serikalini hawaelewi kwanini Tanzania ni Maskini,  hata hivyo wasaani wetu wa bongo fleva kupitia wimbo huo wameweza kutupa bonge la dokezo kuwa kwanini Tanzania ni Masikini. 
Wimbo mzima umejaa mashairi ya kuisifu Kigoma, ikionyesha rasilimali kibao zilizopo humo mkoani.  Pamoja na kuwepo na Mbuga, Ziwa refu kabisa kuliko yote Afrika, madini, na hata rasilimali watu ambao wame prove kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa –mfano Miss Tanzania, bingwa wa ngumi, wanamuziki mashuhuri, wachezaji mpira mashuhuri, na hata wanasiasa hodari kabisa, maendeleo ya mkoa huo hayaendani na utajiri uliopo. Hii ni taswira halisi ya nchi yetu Tanzania. 
Kinachosemwa mtaani ni kuwa kumbe tatizo lipo ni katika matumizi ya hizi rasilimali na sio rasilimali. Tumsitafute mchawi.  
Watu wangu wa Kitaa wangependa kusikia katika wimbo huo, au achilia mbali kusikia basi waone hata picha za matunda yanayoendana na hizo rasilimali zinazotajwa na kusherehekewa katika wimbo huo. 
Rasilimali watu ziwekeze kweli huko mkoani kwao, na hizo rasilimali asilia kama madini na ardhi yenye rutuba vitumike vya kutosha kuleta maendeleo.

Si wanasema upendo ni matendo, basi kwa wapenda Tanzania nchi yetu , kila mmoja wetu ajitahidi kufanya kwa vitendo jambo linalowezesha kweli kuboresha hali za maisha ya watu wa Tanzania.

Pili:

Chege kapiga dongo la wazi wazi kwa wanaojifanya si watanzania ili hali ni watanzania. Kuna aina nyingi za kuwa mzalendo, sio tuu kuwa mzalendo kwa nchi yako, pia unatakiwa kuwa mzalendo kwa mkoa wako. Hii iende mbali hata kwa kijiji chako, na familia yako. 
Chege ananukuu maneno ya mama yake kuwa mkataa kwao ni mtumwa. Hata kuenzi basi lugha ya kwenu nalo jambo jema si ndio maana wimbo huu una jina la kilugha – Leka Dutigite! 
Hii ni bonge la hongera kwa chege kugusa swala hili kwani kuna baadhi yetu kwa kuenda nje ya nchi kidogo tuu basi, wanajidai wao si wabongo tena. 

Tatu:

Pamoja na mambo mengi mazuri ya kujifunza kutoka katika wimbo huo, usichukulia kila jambo kwa undani na ukataka kuiga mfano pale Diamond anaposema migebuka na ugali wa muhogo ndio umemfanya yeye kuwa Diamond, usidhani na wewe ukila ugali wa muhogo na migebuka basi kipaji cha kuimba cha Diamond  utakuwa nacho. 
Hizo zilikuwa ni ‘porojo’ tuu za Diamond,  pengine ni kuunganisha vina kama Peter Msechu naye alivyoweka porojo kuwa ‘Kigoma haijagoma, Kigoma yasonga mbele’, usiwazie sana haya maneno mfano ukajiuliza Kigoma ingegomaje ?
Share:

SIFA ZA KUWA MBONGO MZAMIAJI HUKO UGHAIBUNI

Kwa watu wengi , mpango wa kuishi nje ya nchi una maana ya ‘Kuzamia’. Yawezekana neno kuzamia linatumika sivyo ndivyo kwani asili yake ilikuwa haswa miaka ya nyuma sana , ambapo wengi walienda  nje ya Tanzania kwa kupitia meli ambapo walijificha baada ya kuzamia meli, na kuondoka na meli husika mpaka huko ughaibuni ambako wakifika huko hujichanganya na wenyeji na kuanza ‘kutafuta’ maisha. 
Pengine mtindo huu wa kuenda ughaibuni kwa kuzamia meli unatumika bado ila haujashamiri sana siku za hivi karibuni.

Badala ya kuondoka kwa mtindo huu wa kuzamia meli ambapo wazamiaji hao hawakuwa na hata vibali halali vya kuingia nchi husika, achilia mbali kuwa na hata Passport ya Tanzania, siku hizi, wabongo hawatumii meli kuzamia,  ‘wazamiaji’ wengi wa siku hizi huwa na vibali halali vya kusafiria na hata kupanda ndege au mabasi halali kabisa na kuingia nchi husika hata hivyo wanapofika huko hupitiliza muda halali wa kukaa huko nchi husika, na hivyo hiyo kuonekana kama na wao ‘walizamia’.

Kwahiyo neno kuzamia siku hizi halitumiki kama zamani kueleza taswira ya aina ya usafiri mtu aliotumia kusafiria – yaani kuzamia meli, badala yake neno kuzamia limekumbwa na utata wa maana tofauti. Kwa wengine neno ‘kuzamia’ linamaanisha aina yoyote ile ya kuishi ughaibuni zaidi ya shughuli halali iliyompeleka mtu kwa mara ya kwanza. 

Katika maana hii ya pili , kuna mgongano mwingine wa maana ya kuzamia. Je, wewe unaonaje:
1. Je  kila mtu anayeishi ughaibuni zaidi ya shughuli yake ya awali iliyompeleka huko ni mzamiaji hata kama anacho kibali halali cha kuishi huko ?

2. Au mzamiaji ni yule mbongo anayeishi ughaibuni pasipo kuwa na kibali halali cha kuishi huko ughaibuni ?
Share:

LAPTOP KALI YA AINA YAKE

Kompyuta mpakato, kama unavyoweza kusema Laptop kwa kiswahili kisicho rasmi, ni moja ya ndoto ya kila kijana au tuseme kila mtu mwenye matumizi ya kila ya kompyuta au mtandao (internet). 

Dunia itashuhudia laptop ya aina yake ambaye wahandisi wake wanaiita rolltop, kwani itakuwa na muundo wa roller, kama vile ile roller inayotumika kupaka rangi kuta za nyumba.

Mbali na umbo kama la roller, laptonga hiyo itakuwa inauwezo wa kufunga na kufunga ikawa na umbo la kama laptop za kawaida, na pia ukiamua unaweza kuifanya ikawa kama ‘ipad’. 
Mbali na hivyo laptop hiyo ya aina yake itakuwa na speakers ambazo zitakuwa nje ya laptop hiyo, na mziki wa laptonga hiyo utakuwa ni mzito sana- kama wakichina.

Laptop hii mpya iliyopewa jina la rolltop, imebuniwa na Orkin Design, kampuni ya Kijerumani yenye makao yake makuu huko Munich.

Jionee video ya jinsi laptop hiyo itakavyokuwa:
Share:

MAANA HALISI YA KULA BATA

Kila kukicha tunaona mitandaoni au mitaani watu wakizungumzia 'kula bata'. Je, ni kweli kula bata ndio uthibitisho wa mafanikio ya kimaisha ? Je, kula bata ni sawa na kupumzika na kuburudika ? Je, ni kweli kuna maana tofauti za kula bata ?
Msikilize kijana huyu wa kibongo akielezea jinsi alivyo na maendeleo na anavyo kula bata !

“Mie, aah we acha kabisa, Mungu kanijalia neema, nina laptop, nina blackberry, nina badilisha club ninavyotaka, hizo Lounge ndio usiseme sijui Savannah, Nyumbani Lounge , huko kote mie nyumbani. 
Yaani mademu wanavyo ni shobokea, halafu mie hata si wamandai, nimepoa zangu na mademu watatu tuu. 
Yaani swaga ninazotoa Facebook, nina rafiki kibao, nakaribia kufikisha elfu nne. Mie si mkali bwana.

Dunia hii raha ujipe mwenyewe. Nijipe shida ya nini, wakati nakaa kwa wazee (wazazi), halafu naingiza kitu kama elfu ishirini kila siku. 
Kwani nikitumia elfu 15 kwa siku, ikabaki  5 inalinda mfuko, hata ikibaki buku ya vocha poa tuu, kuna shida gani?. Hela utumiavyo, ndivyo zinavyokuzoea”.


Kama kujipa raha kwenyewe ndio hivi, basi kazi ipo ! Maisha bora kwa kila mtanzania kweli yanawezekana!

Je, wewe maana yako ya kula bata ni ipi ?

Picha: via freephoto.com 
Share:

UKWELI KUHUSU RANKING ZA FIFA


Umewahi kujiuliza jinsi ambavyo timu zinapanda na kushuka kwenye rank za timu bora za FIFA ? Basi tulia na ujisomee ufafanuzi uliotulia kabisa. Mambo ya msingi ya haraka haraka kufahamu kuhusu FIFA Ranking ni rank (nafasi) huchanganuliwa kwa mahesabu maalum ambayo hufanywa kila mwezi. 
Hivyo basi matokeo ya nafasi hizo hutolewa kila mwezi.

Na ujue pia kuwa hata timu ishinde Mechi vipi, sio kwamba ndio kigezo pekee kwa nchi kupanda nafasi. FIFA wanacheki pia na hizo timu unazozifunga zipo katika rank gani, umuhimu wa mechi, na historia yako kwa ujumla kwa miezi 48 iliyopita (miaka 4). Hivyo sio tuu Mmeshinda vimechi viwili vitatu basi mnataka muwe kwenye 2O bora.
 

Hivyo basi utaweza kujionea kuwa pamoja na kutolewa kwenye robo fainali ya AFCON 2013 IVORY COAST ndio timu namba 1 Afrika (ya 12 duniani),ikifuatiwa na GHANA (ya pili Afrika na ya 19 duniani), iliyotolewa kwenye Nusu Fainali.
Mali imekuwa ya Tatu kwa Afrika na ya 25 duniani wakati Mabingwa wa Africa Nigeria wameshika nafasi ya 30 duniani na kwa afrika nafasi ya 4.
 

Nchi yetu Tanzania  imeporomoka kwa nafasi 3 toka nafasi ya 130 duniani hadi nafasi ya 127. Kwa matokeo haya ya Februari 2013, Tanzania imekuwa ya 36 kwa ubora Afrika kwa kupanda nafasi 6 toka nafasi ya 42 iliyokuwa inashirikia mwezi Januari 2013.

Nafasi 10 bora kwa Afrika ni kama ifuatavyo:-


-----Kwa mujibu wa The FIFA/Coca-cola World Ranking kwa mwezi huu wa Feb.2013. Iliyotelewa Feb.14, 2013.
Share: